'Rafiki yangu alikufa mbele yangu': Mwanafunzi aeleza wakati ndege ya jeshi la anga ilipoanguka shuleni

Mwanafunzi wa mwaka wa 10 Farhan Hasan alikuwa amemaliza mtihani wakati ndege ilipoanguka
Muda wa kusoma: Dakika 4

Farhan Hasan alikuwa amemaliza tu mtihani na alitoka darasani akipiga gumzo na marafiki wakati ndege ya mafunzo ya jeshi la wanahewa la Bangladesh ilipoanguka kwenye chuo chake cha shule na kuua takribani watu 31.

"Ndege iliyoungua ilikuwa ikigonga jengo mbele ya macho yangu," mwanafunzi huyo wa Shule ya Milestone na Chuo aliiambia BBC Bangla.

Picha kutoka shuleni katika kitongoji cha kaskazini mwa mji mkuu, Dhaka zinaonesha moto mkubwa na moshi mkubwa, baada ya ndege hiyo kugonga jengo la orofa mbili.

Zaidi ya watu 160 walijeruhiwa katika ajali hiyo.

Vikosi vya jeshi vilisema kuwa ndege ya F-7 ilipata hitilafu ya kiufundi baada ya kupaa kwa ajili ya mazoezi baada ya saa 13:00 kwa saa za huko (07:00 GMT). Rubani, Luteni wa Ndege Md. Taukir Islam, alikuwa miongoni mwa waliopoteza maisha.

Farhan, ambaye alikuwa akizungumza na BBC Bangla pamoja na mjomba wake na baba yake, aliongeza: "Rafiki yangu mkubwa, ambaye nilikuwa naye kwenye chumba cha mtihani, alikufa mbele ya macho yangu.

"Mbele ya macho yangu ... ndege ilipita juu ya kichwa chake. Na wazazi wengi walikuwa wamesimama ndani kwa sababu watoto wadogo walikuwa wakitoka nje kwakuwa ilikuwa mwisho wa siku ya shule ... ndege ilichukua wazazi pamoja nayo."

Mwalimu katika chuo hicho, Rezaul Islam, aliambia BBC kwamba aliona ndege "moja kwa moja" ikigonga jengo hilo.

Mwalimu mwingine, Masud Tarik, aliiambia Reuters kwamba alisikia mlipuko: "Nilipotazama nyuma, niliona tu moto na moshi ... Kulikuwa na walezi wengi na watoto hapa."

Saa chache baada ya ajali hiyo, katika eneo la makazi ambalo lina watu wengi, umati mkubwa wa watu ulikusanyika na watu walisimama juu ya majengo ili kutazama.

Wakati watu wakikimbia kila upande, ambulensi na watu wa kujitolea walifanya kazi kutafuta njia ya kubeba majeruhi na miili mingi nje ya Shule na Chuo cha Milestone.

Takribani ambulensi 30 zilionekana zikiwaondoa watu nje.

Mwanamke mmoja aliyekuwa akitafuta habari katika eneo la tukio aliiambia BBC kuwa mwanawe alimpigia simu mara tu baada ya ajali hiyo, lakini hajasikia kutoka kwake tangu wakati huo.

Waokoaji

Chanzo cha picha, Nur Photo via Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Zaidi ya watu 50, wakiwemo watoto na watu wazima, walipelekwa hospitalini wakiwa na majeraha ya moto, daktari katika Taasisi ya Kitaifa ya Upasuaji wa majeraha ya Moto na Plastiki alisema.

Familia nyingi na jamaa za waathiriwa walikuwa ndani ya hospitali, ikiwa ni pamoja na Shah Alam, mjomba wa mvulana wa miaka minane, Tanvir Ahmed, ambaye alikufa katika ajali hiyo.

"Mpwa wangu mpendwa yuko katika chumba cha kuhifadhia maiti sasa hivi," Bw Alam alisema akiwa amemshikilia mdogo wake, baba yake Tanvir ambaye hakuweza kuzungumza.

Wengi wa waathiriwa ndani ya hospitali ya walioungua ni watoto, wengi wao ni kati ya umri wa miaka tisa na 14.

Sio hospitali ya walioungua pekee ambayo imepokea majeruhi. Wizara ya afya ya Bangladesh ilisema hospitali saba kote jijini zinawatibu waathiriwa.

Kiwango cha ajali hiyo kimewafanya wananchi kujitokeza na kuchangia damu, pamoja na kuwatembelea majeruhi wakiwemo wanasiasa wanaowakilisha vyama viwili vikubwa nchini humo, Bangladesh Nationalist Party (BNP) na Jamaat-e-Islamim.

Jumanne, wakati huo huo, imetangazwa kuwa siku ya maombolezo, huku bendera ya taifa ikipeperushwa nusu mlingoti.

Muhammad Yunus, kiongozi wa serikali ya mpito ya Bangladesh, alisema "hatua za lazima" zitachukuliwa kuchunguza chanzo cha tukio hilo na "kuhakikisha kila aina ya usaidizi unapatikana".

"Huu ni wakati wa majonzi makubwa kwa taifa. Nawatakia majeruhi ahueni ya haraka na ninaagiza mamlaka zote, ikiwa ni pamoja na hospitali zinazohusika, kushughulikia hali hiyo kwa umuhimu mkubwa," alisema katika chapisho kwenye mtandao wa kijamii wa X.

Kamati ya uchunguzi imeundwa kuchunguza tukio hilo, taarifa hiyo iliongeza.

Kulingana na taarifa ya vikosi vya jeshi, rubani alijaribu kuelekeza ndege hadi eneo lisilo na watu wengi baada ya hitilafu ya kiufundi kutokea. Alikuwa ametoka tu kutoka kituo cha jeshi la anga katika mji mkuu.