'Tusaidieni': Vilio vya mamia ya wahamiaji waliotolewa Marekani na kushikiliwa katika hoteli ya Panama

Muda wa kusoma: Dakika 5

Katika chumba cha Hoteli ya kifahari ya Decápolis huko Jiji la Panama, wasichana wawili wanashikilia kipande cha karatasi kwenye dirisha chenye ujumbe ulioandikwa. "Tafadhali tusaidieni," unasema ujumbe huo.

Hoteli hiyo inawapa wateja wake vyumba vinavyoelekea bahari, ina migahawa miwili ya kipekee, bwawa la kuogelea, spa na usafiri wa binafsi. Lakini sasa imegeuka kuwa "kituo cha muda cha kutunza wahamiaji" kinachohifadhi wahamiaji 299 wasio na hati za uraia waliotolewa Marekani, serikali ya Panama ilisema Jumanne.

Baadhi ya wahamiaji wanainua mikono yao na kuiweka katika ishara ya msalaba kuonesha kuwa wamenyimwa uhuru wao. Wengine wanaonesha alama zenye ujumbe mwingine kama: "Hatuwezi kuwa salama katika nchi yetu."

Utawala wa Trump uliahidi kuwafukuza mamilioni ya watu waliovuka kinyume cha sheria kuingia Marekani. Wale walioko katika hoteli ya Jiji la Panama walifika kwa ndege tatu wiki iliyopita, baada ya Rais José Raúl Mulino kukubaliana kwamba Panama itakuwa nchi ya "daraja" kwa wahamiaji walioondolewa.

Hata hivyo, kati ya wahamiaji 299 wasio na hati za uraia, kutoka India, China, Uzbekistan, Iran, Vietnam, Uturuki, Nepal, Pakistan, Afghanistan na Sri Lanka, ni 171 pekee waliokubali kurejea katika nchi zao za asili.

Wale waliobaki sasa wanakutana na mustakabali usio na uhakika, na ni mamlaka za Panama zinazodhibiti kile kitakachotokea baadaye.

Kwa mujibu wa serikali, kundi hili litahamishiwa kambini katika jimbo la Darién, ambalo limekuwa likihifadhi wahamiaji wanaovuka msitu wakielekea Marekani.

Katika siku za kawaida, watalii wanaweza kuingia na kutoka kwa urahisi katika Hoteli ya Decápolis, lakini sasa wanajeshi wa Panama waliobeba silaha nzito wanatekeleza hatua kali za usalama ndani na nje ya jengo hilo.

Kutoka mtaani, nguo zilizofuliwa zinaonekana zikining'inia dirishani. Moja ya vitu hivyo ni jezi ya mpira wa kikapu ya Los Angeles Lakers ya rangi ya manjano na nambari 24, aliyovaa mchezaji maarufu Kobe Bryant.

Katika dirisha jingine, kundi la watu wazima na watoto watatu wanainua mikono yao kwa ishara ya kimataifa kwa wale wanaohitaji msaada. "Tusaidieni," imeandikwa kwa herufi nyekundu kwenye kioo.

Na watoto wawili wenye nyuso zao zilizofichwa wanashikilia karatasi kwenye kioo zikiwa na ujumbe: "Tafadhali waokoe wasichana wa Afghanistan."

Mwanamke Muirani ambaye ameishi Panama kwa miaka kadhaa aliiambia BBC kwamba alikuwa katika mawasiliano na mmoja wa wahamiaji walioko ndani ya hoteli. Alisema walikuwa "wakiogopa" uwezekano wa kurudishwa Iran.

Mwanamke huyo, ambaye aliiomba BBC isimtaje jina, alisema alikwenda katika hoteli kutoa msaada wake kama mfasiri wa Kifarsi lakini alielezwa kwamba tayari walikuwa na mfasiri.

Hata hivyo, aliongeza kuwa watu ndani ya hoteli walisema hiyo haikuwa kweli.

Kwa kutumia simu ya mkononi iliyofichwa, kwani inaaminika kuwa mawasiliano na wale walioko nje ya Hoteli ya Decápolis hayaruhusiwi, mwanamke Muirani alisema mhamiaji huyo alimwambia kuwa kulikuwa na watoto kadhaa katika hoteli, ambao wamekataliwa kuwa na wakili na kwamba hawaruhusiwi kutoka kwenye vyumba vyao hata kwenda kula.

Baada ya habari kuhusu wahamiaji waliotolewa na kuwekwa ndani ya hoteli hiyo kutangazwa kwa mara ya kwanza Jumanne, hatua za usalama zilizowekwa ziliongezewa nguvu na upatikanaji wa wahamiaji kwenye intaneti ukakatwa, alisema mwanamke huyo.

BBC iliwasiliana na Hoteli ya Decápolis na serikali ya Panama kuuliza kuhusu yanayojiri ndani ya jengo, lakini haikupata majibu.

Hata hivyo, Waziri wa Usalama wa Umma wa Panama, Frank Ábrego, alisema wahamiaji hawaruhusiwi kutoka katika hoteli kwa sababu serikali yake inapaswa kuhakikisha usalama na amani ya Wapanama.

Video iliyowekwa kwenye mitandao ya kijamii wikiendi iliyopita ilionesha mhamiaji mmoja akielezea kwa Kifarsi jinsi walivyoshikiliwa baada ya kuvuka mpaka kuingia Marekani na kuambiwa wangepelekwa Texas, lakini waliishia Panama.

Mwanamke katika video alisema maisha yake yatakuwa hatarini ikiwa atarudi Iran kutokana na uwezekano wa kulipizwa kisasi na serikali.

Alisema azma yake ni kuomba hifadhi ya kisiasa.

Wachambuzi wanasema kufanikisha hili ni vigumu bila kuwa na wakili, zaidi sana wakati serikali ya Panama ilitangaza kuwa uhuru huo hautapatikana kwa wahamiaji walioondolewa.

Waziri Ábrego alisema Jumanne kwamba wahamiaji wataendelea kubaki kwa muda nchini Panama chini ya ulinzi wa mamlaka za nchi hiyo.

"Kilichokubaliwa na serikali ya Marekani ni kwamba wako hapa na watabaki chini ya uangalizi wa muda wa mamlaka zetu kwa usalama wao," alisema.

Pia alionya kwamba wahamiaji ambao hawataki kurudi katika nchi zao za asili watapaswa kuchagua nchi ya tatu.

Katika hali hiyo, alisema, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) na Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Wakimbizi (UNHCR) watakuwa na jukumu la kuwarudisha kwao.

Msemaji wa IOM aliiambia BBC kwamba shirika hilo linahusika na "kutoa msaada muhimu" kwa watu waliotolewa Marekani.

"Tunafanya kazi na maafisa wa hapa nchini kusaidia wale walioathirika, tunasaidia kurudi kwa hiari kwa wale wanaoomba na kutambua mbadala salama kwa wengine," alisema.

"Ingawa hatuna ushiriki wa moja kwa moja katika kuzuiliwa au kuzuia harakati za watu, tumejitolea kuhakikisha kuwa wahamiaji wote wanatendewa kwa heshima na kulingana na viwango vya kimataifa," alisema.

Ábrego pia alisema wahamiaji wanahifadhiwa katika Hoteli ya Decápolis kutokana na uwezo wake wa kuwahifadhi.

Afisa mwingine wa ngazi ya juu alisema "hakutegemewi kuja kwa wahamiaji zaidi" kwa sababu hakuna ndege zaidi za aina hii ambazo zimekubaliwa na Marekani.

Panama ilikubali kuwa nchi ya "daraja" kwa waliondolewa Marekani, baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, kutembelea nchi hiyo wakati hali ya mvutano ilipokuwa inatokea kutokana na vitisho vya Trump vya "kurudisha" mamlaka ya mfereji wa Panama

Muzaffar Chishti, mtafiti mkuu katika Taasisi ya Sera ya Uhamiaji, taasisi ya utafiti nchini Marekani, alisema wengi wa waliotolewa wanatoka katika mataifa ambayo hawapokei watu waliotolewa Marekani.

"Hii inahitaji majadiliano ya kidiplomasia ya mara kwa mara na serikali hizo," aliiambia BBC.

"Kwa kuwapeleka Panama, Marekani inajiondoa katika picha," aliongeza. "Ni mzigo kwa Panama kuchukua jukumu la majadiliano hayo na kuona jinsi ya kufanya mataifa hayo kukubaliana kuwapokea tena."

Wiki hii, ndege inayobeba wahamiaji waliotolewa Marekani inatarajiwa kufika Costa Rica, nchi nyingine ya Amerika ya Kati ambayo imekubaliana na Washington kuwa nchi ya "daraja" kwa wahamiaji walioondolewa.

Imetafsiriwa na Lizzy Masinga