Ghetto Kids: Nini kilicho nyuma ya harakati zao kinazowafanya watambe dunia nzima?
The Conversation

Chanzo cha picha, Britain's Got Talent
Kundi la wacheza au muziki la watoto wadogo kutoka Uganda, linaloitwa Ghetto Kids, walivuma kote ulimwenguni walipopata "Golden buzzer" katikati ya onyesho lao la kucheza kwenye kipindi maarufu cha televisheni cha Britain's Got Talent.
"Golden buzzer" ni kitu kinachobonyezwa kama kengere ambacho hutuoa vitu vya rangi ya dhahabu kutoka juu vinavyosambaa jukwaani zima kuashiria kwamba onyesho lako ni zuri sana na lenye thamani ya dhahabu.
Na hiyo inamaanisha washiriki hao wanaingia moja kwa moja kwenye raundi za mwisho za onyesho - hapo awali, haikuwahi kutokea kubonyezwa "Golden buzzer" katikati ya onyesho.
Kwa kweli, kikundi hiki cha kucheza muziki kimekuwa mitandaoni kwa miaka kadhaa tayari. Wanacheza nyimbo mbalimbali na kutoa video kwenye mitandao ya YouTube, Instagram na TikTok.
Kama mtaalam wa jinsi mitindo ya dansi ya Kiafrika inavyosambaa ulimwenguni kote, nimekuwa nikivutiwa na jinsi maonyesho yao ya kipekee yanavyotokana na nyimbo maarufu za Kiafrika na aina za uchezaji za kitamaduni za Kiafrika - zikiendana na mabadiliko ya kisasa. Ghetto Kids ni uthibitisho wa namna kucheza muziki kunavyoweza kubadilisha maisha.
Je! Ghetto Kids ni akina nani?

Chanzo cha picha, Ghetto Kids
Ghetto Kids ni sehemu ya familia ya watoto 30 wanaolelewa na Kavuma Dauda. Taasisi yake inatoa malazi, chakula na elimu kwa watoto kutoka mitaa ya Kampala tangu 2007. Triplets Ghetto Kids ilisajiliwa kama shirika lisilo la kiserikali mwaka wa 2013 kufuatia mafanikio yasiyotarajiwa ya kikundi cha kucheza muziki na video ya dansi iliyotengenezewa nyumbani ya Sitya Loss na mwimbaji na msanii maarufu wa Uganda Eddy Kenzo. Taasisi hiyo hutumia muziki, kucheza au kudansi na maigizo kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu kupata maisha bora.
Wameshinda tuzo nyingi za kucheza muziki kimataifa tangu 2015, zikiwemo Tuzo la Afrimma, tuzo kutoka kwa Muungano wa Sekta ya Kurekodi Marekani na Tuzo ya Watayarishi wa YouTube. Walicheza pia kwenye mahsindano ya Kombe la Dunia la mpira wa miguu kwa wanaume mwaka 2022.
Kukua kwa umaarufu wao

Chanzo cha picha, Ghetto Kids
Ghetto Kids kwa mara ya kwanza walipata kutambulika duniani kote mwaka wa 2017 kwa video yao wimbo wa Afro house unaoitwa Marimba Rija wa mwanamuziki wa Angola Dotorado Pro. Video hiyo ilitazamwa na watu milioni 25 wakati huo.
Marimba Rija ilikuwa chaguo bora kuwaelezea Ghetto Kids. Wimbo huu ulitayarishwa na mwanamuziki mashuhuri wa Afro house na nyota wa kuduro - kuduro ni aina ya muziki na dansi uliokuwa unatengenezwa Luanda, Angola mwishoni mwa miaka ya 1980. Video hiyo ilihusisha vipengele mahususi vya kucheza kitamaduni na kuongeza miondoko ya asili iliyotokana na ubunifu na mtindo wa kikundi hicho.
Ni nini kinachowafanya kuwa wa kipekee

Chanzo cha picha, Ghetto Kids
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mchanganyiko wa mila na ubunifu unasimamiwa kikamilifu na Ghetto Kids. Hatua zao za kimaadili zinaonyesha ushawishi wa kisanii na kitamaduni uliopo kati ya nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Kundi hili pia linafahamu uwezo wa kuonyesha na kuondoa taswira potofu za Afrika kupitia tafsiri za kushangaza na za kuchekesha zitokanazo na ushawishi wao. Picha ya kijiji cha jadi cha Kiafrika, mandhari ya vijijini na hata ya mitindo ya Kiafrika (kuvaa kofia na koti za kifahari) hutumiwa kuonyesha muonekano wao na mtazamo wao kwenye maisha.
Kujiamini, mbwembwe na matumaini yenye furaha hujionyesha kwenye video na maonyesho yao yote. Wanajikubali jinsi walivyo na wako tayari kushiriki furaha yao pamoja.
Mwanzilishi wa Ghetto Kids, Dauda mara nyingi amezungumza kuwa yeye mwenyewe ni mtoto wa mitaani, asiye na uwezo wa kwenda shule. Raia wa kigeni alifadhili elimu yake na akajiwekea ahidi kwamba na yeye atasaidia wengine; alianza kutengeneza msingi huo baada ya kuhitimu mafunzo ya ualimu (mwalimu wa hisabati).

Chanzo cha picha, Ghetto Kids
Ujumbe wa Dauda unachukua umuhimu wa kipekee nchini Uganda, nchi ambayo imekuwa na matatizo mengi kwa miongo kadhaa na vita vya wenyewe kwa wenyewe ambapo watoto wamekuwa wahanga wa hali mbaya ya kisiasa pamoja na kutekwa nyara na kunyanyaswa na vikundi vya wanamgambo kama Lord's Resistance Army. Pia magonjwa ya malaria, magonjwa ya kupumua na Ukimwi yamemaliza maisha ya vijana wengi.
Katika hali hii, kuwaweka watoto waonekane pia ni mkakati wa kulinda maisha yao na kuwafanya waonekane kuchochea ukuaji na elimu yao, kukabiliana na ukatili wa siku za nyuma katika kijamii.
Triplets Ghetto Kids ni kielelezo cha haja ya kubadilisha udhaifu wa kihistoria kuwa nguvu kwa jamii nzima. Wanacheza kwa ajili ya elimu na kuendelea kuishi, na watafanikiwa.












