Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kifo kwenye kivuko cha kuingia Uingereza - ni nini kilisababisha mvulana wa miaka 14 kufanya safari ya kifo?
Na Andrew Harding
BBC News
Usiku aliozama, Obada Abd Rabbo mwenye umri wa miaka 14 alikuwa na mashaka kwa mara nyingine tena.
“Siwezi kuogelea,” aliendelea kuwaambia wanaume waliokuwa karibu naye, huku wakijisogeza kwenye barabara yenye unyevunyevu kwenye giza nene, kuelekea kwenye mawimbi ya barafu.
Kaka mkubwa wa Obada, Ayser, 24, alimshika mkono wake.
Hii ilikuwa ni mara ya tatu tangu waondoke Syria miezi tisa iliyopita ambapo walikuwa wameelekea baharini, na kila mara Obada alikua akielezea wasi wasi ule ule - kwamba alikuwa na hofu, kwamba hajui kuogelea, na kwamba hakuwa na uhakika kuhusu safari.
Obada na Ayser walikuwa miongoni mwa watu watano waliozama, mita chache kutoka ufukweni, kwenye pwani ya kaskazini mwa Ufaransa usiku huo - wa kwanza kufa wakati wakijaribu kuvuka kwenda Uingereza kwa boti ndogo mnamo 2024, wiki mbili baada ya mwaka mpya. .
Ili kujaribu kuelewa jinsi mtoto anavyoweza kuwekwa katika hali hii, BBC ilifuatilia upya safari ya Obada kutoka Syria - kwa kutumia video, jumbe na mahojiano na jamaa za ndugu na wengine walioandamana naye. Lengo letu lilikuwa ni kuchunguza maamuzi magumu yanayohusika katika kila hatua.
Tuligundua shinikizo la ajabu ambalo baadhi ya watoto wanaonekana kuwekewa - na wazazi, jamaa na wasafirishaji haramu. Na tulipata hadithi pana kuhusu nia na mikakati ya wale wanaotaka kufika Uingereza, na athari za vizuizi ambavyo Uingereza na serikali nyingine zimeanzisha.
Katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita, wanaume ambao sasa wanamzunguka Obada kwenye kivuko - karibu kumi na mbili kati yao kutoka kitongoji kimoja huko Daraa, kilichopo katika jiji la kusini mwa Syria - walikuwa wakijaribu kumshinikiza mvulana huyo, wakimwambia awe jasiri, kajitunze na awe mwanaume , lakini haikusaidia.
Ni kawaida kwa wanaume kujaribu safari hiyo, ikizingatiwa kwamba wanawake huchuchukuliwa kuwa wanyonge zaidi, si haba kwani wangepitia Libya iliyokumbwa na vita. Lakini pia kulikuwa na akina mama wawili wenye watoto wenye umri wa balekhe waliokuwa wakijaribu kuvuka usiku huo.
Boti ilikuwa tayari ndani ya maji, na baadhi ya watu walikuwa wakipanda. Kwa jumla likuwa na zaidi ya watu 60 katika umati uliowazunguka wakitarajia kupata nafasi – na kufika salama.
Mawimbi ya maji yakaanza kuivuta boti kwa haraka na kuiondoa kwenye ufukweni na kuelekea kwenye kina kirefu cha maji. Ilikuwa mapema Jumapili Januari 14 na upepo ulikuwa umepungua vya kutosha kuyawezesha makundi ya wasafirishaji haramu wa binadamu kujaribu kuzindua safari zao za kwanza mwaka 2024.
Muda si muda kulikuwa na vurugu huku watu wakikimbilia baharini wakijaribu kuingia kwenye mashua hiyo ilipokuwa ikiyumba kutoka ufukweni ambazo zilisababisha hisia ya kuchanganyikiwa miongoni mwa watu waliokuwemo ndani ya boti.
Huu haukuwa ufuo mpana wa kawaida ambao wote walikuwa wameuona kando ya pwani ya kaskazini mwa Ufaransa. Badala yake, wasafirishaji haramu walikuwa wamewaleta katikati ya Wimereux, mji mdogo wa mapumziko ulio kaskazini mwa bandari ya Boulogne, na kwenye njia panda katikati ya ukuta mkubwa wa bahari, kwenye mawimbi makubwa ya maji.
Hakukuwa njia salama wakati walipokuwa wakitaka kupanda mashua iliyokuwa ikirudi nyuma, bali kulikuwa na maji ya kina kirefu kuanzia ufukweni hadi kwenye eneo lilipokuwa boti.
"Sivyo tulivyotarajia," mmoja wa walionusurika alisema.
Akiwa katika kitandani magharibi mwa London, kaka mwingine wa Obada, Nada, 25, aliendelea kuitazama simu yake. Ilikuwa saba kwa saa za London, sawa na saa nane mchana huko Ufaransa.
Saa chache mapema, Nada alikuwa ameita kundi zima walipokuwa wameketi wakiota moto kwenye kambi yao ya muda chini ya daraja la kivuko huko Calais. Walionekana kujiamini katika safari iliyo mbele yao.
Hata Obada, akiwa amevalia kofia nyeusi na skafu ya bluu, alikuwa mwenye tabasamu na kuinua vidole viwili kwenye kamera kwa ishara ya ushindi. Safari yao ndefu na ngumu ilikuwa karibu kuisha.
Nada alikuwa amevuka kivuko kile kile cha hatari miaka miwili iliyopita, akimpuuza baba yake, nyumbani huko Daraa, ambaye hapo awali alimsihi awe na subira, akisema vita vya Syria vinaweza kuisha hivi karibuni.
"Lakini tumengoja kwa miaka 12, na havijakamilika. Hakuna usalama. Hakukuwa na njia (nyingine) ya kuomba hifadhi," Nada anakumbuka alimwambia baba yake. Nada ni mtu mwenye ndevu, mwenye saut ya upole, na mrefu, kama ndugu zake wote.
Nada alikuwa amechagua kwenda Uingereza kwa sababu mjomba alikuwa tayari amefanya safari hiyo karibu miaka kumi kabls na akapewa ruhusa ya kubaki huko.
Wanaume wote wawili walikuja kinyume cha sheria kwa sababu, Nada alisema, hapakuwa na njia mbadala.
Kulingana na Asylum Aid, shirika la usaidizi linalotoa ushauri wa kitaalam wa kisheria kwa watu wanaotafuta hifadhi, hakuna njia yoyote kwa raia wa Syria kuomba hifadhi bila kusafiri kibinafsi hadi Uingereza.
Wengi hujaribu kuvuka mpaka kinyume cha sheria kwani hakuna viza ya kuomba hifadhi. Muungano wa familia - mojawapo ya njia chache za kisheria - umefafanuliwa kwa ufupi na viza mara nyingi hukataliwa, lakini baadhi hufaulu.
Idadi ndogo pia inaruhusiwa kuingia kupitia mipango ya makazi mapya na takwimu za Wizara ya Mambo ya Ndani zinaonyesha kwamba, katika mwaka jana kufikia mwezi wa Septemba 2023, Wasyria wapatao 325 waliruhusiwa kuingia kwa njia hii. Zaidi ya 90% ya Wasyria wanaoomba hifadhi nchini Uingereza wamefanikiwa, kwa sababu ya mzozo ambao bado unaendelea nchini mwao.
Alipofika Uingereza, Nada alikuwa amewaambia maafisa kwamba alipokea vitisho vya kuuawa katika chuo kikuu chake huko Damascus baada ya kushutumiwa kwa kukosa uaminifu kwa serikali na kwamba alitaka kuepuka kuandikishwa jeshini.
"Haikuwa salama. Unaenda jeshini na kuushi huko miaka 10. Unahitaji kuua, au ufe. Hatutaki hii."
Oktoba mwaka jana, Nada alipewa hadhi ya ukimbizi na ruhusa ya kusalia nchini Uingereza kwa miaka mitano. Hivi majuzi alipata kazi katika ghala moja karibu na Wembley. Sasa anasoma lugha ya Kiingereza na anatumai kumleta mke wake kutoka Syria hivi karibuni - jambo ambalo anaruhusiwa kuomba kama mkimbizi - na hatimaye kurejea masomoni kusomea shahada yake ya sheria nchini Uingereza.
Mara tu baada ya kuwasili Uingereza, Nada alikuwa amewahimiza kaka zake, ambao bado wako nyumbani Daraa, wajiunge naye.
"Wewe bado ni mdogo, unaweza kusoma hapa," alisema alimwambia Obada kwa simu.
Binamu kadhaa pia walikuwa wamefika Uingereza tangu kuanza kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria. Kulikuwa na mtandao mzima hapa wa watu kutoka Daraa, jiji lenye sifa ya kuwa chimbuko la mapinduzi dhidi ya utawala wa Assad.
"Unaweza kuanza maisha mapya hapa," Nada alifurahi.
_______________________________________________________________________
Huko Daraa, Obada alikuwa anasoma shule. Kaka zake walidhani alikuwa "mwema sana na mwerevu sana", na walitumaini angetaka kuwa daktari. Alikuwa mchezaji mahiri wa soka na alizungumza kwa furaha na Nada alipenda kuzungumzia na na kuitazama Manchester City ikicheza nchini Uingereza. Alikuwa ni "Mtoto tu," rafiki aliyemfahamu huko Syria alisema.
Lakini kuna dalili kwamba Obada pia alikuwa akihimizwa, au pengine hata kushinikizwa, kusafiri na wazazi wake waliozidi kukata tamaa. Baba yake, Abu Ayeser, alikuwa na matatizo mengi ya kiafya na alitarajia matibabu nchini Uingereza.
Mama yake, Um Ayeser, alituthibitishia katika ujumbe wa video kwamba "mwanangu mdogo alienda ili aweze kuungana nasi katika siku zijazo". Jirani kutoka Daraa, ambaye alikuwa na Obada usiku wa kuzama majini, aliunga mkono kauli hiyo
"Angefika Uingereza na kuungana na kaka yake na baada ya muda mfupi angemleta mama na baba yake. Hiyo ndiyo ilikuwa sababu ya wao kuondoka, ili baba yake apate matibabu nje ya nchi," alisema mtu huyo ambaye alitutaka tusitangaze jina.
Kwa kweli, mpango huo ulikuwa na dosari tangu mwanzo. Ikizingatiwa kuwa tayari alikuwa na kaka yake mtu mzima huko London, Obada hangekuwa katika nafasi, kama mtoto, kupanga wazazi wake wamfuate kihalali.
Obada bado alikuwa na umri wa miaka 13 wakati yeye na kaka yake Ayser walipopanda ndege kutoka Damascus hadi katika mji wa Benghazi nchini Libya, Mei mwaka jana.
Viza hazihitajiki kwa Wasyria wanaosafiri kwenda Libya na mjomba wake anayefanya kazi Dubai alikuwa amewasaidia kwa pesa, lakini kujiunga naye katika Ghuba halikuwa chaguo. Dubai haina mfumo wa hifadhi. Obada hangeweza kuhudhuria shule huko, na familia ilionekana kudhamiria kulenga Uingereza.
Mnamo Oktoba 2023, baada ya miezi kadhaa ya kusubiri nchini Libya, ndugu walijaribu kuvuka Bahari ya Mediterania kwa mashua ya magendo, wakitoka katika mji mkuu, Tripoli. Lakini walikamatwa na boti ya doria ya Tunisia na kurudishwa Libya, ambapo waliangukia mikononi mwa wanamgambo wa ndani.
"Tulifungwa na kuteswa kwa mwezi mmoja," alisema kijana mwenye umri wa miaka 23 anayejulikana kama Faris, jirani kutoka Daraa, ambaye alikuwa nao mara kwa mara katika safari kutoka Syria.
Walilala kwenye sakafu tupu, na mara nyingi walilishwa mlo mmoja tu kwa siku, na walipewa bakuli dogo la tambi pekee. Hatimaye, kwa usaidizi zaidi wa kifedha kutoka kwa mjomba wao huko Dubai, ndugu hao wawili waliweza kununua uhuru wao kwa $900 (£707) kila mmoja.
Katika hatua hii, bila ya kushangaza, Obada alianza kutoa mashaka makubwa juu ya kuendelea na safari.
"Aliogopa. Tulikuwa tunazungumza naye ili kumfanya awe na nguvu zaidi na kumwambia asiwe na wasiwasi juu ya chochote. Lakini alihitaji mtu wa kumtunza," anakumbuka Faris.
Tuliushika mkono wake tukamwambia, ''tuko nawe, haupaswi kuogopa''-rafiki wa Faris.
Wakati kundi hilo lilipotangaza kupata mlanguzi mwingine aliye tayari kuwapeleka Italia, Obada aliwapigia simu wazazi wake na kuwaambia hili lingekuwa jaribio lake la mwisho kuvuka bahari ya Mediterani na kwamba kama asingefanikiwa angerudi nyumbani.
"Tulimshika mkono. Tulimwambia, 'Tuko pamoja nawe, hakuna haja ya kuwa na hofu," alisema Faris, wakati kikundi hicho kilipopanda kwenye mashua nyingine mwezi Desemba.
Na wakati huu, walifanikiwa, baada ya saa 22 baharini, waliokolewa na walinzi wa pwani wa Italia karibu na kisiwa cha Lampedusa. Walisajiliwa na mamlaka za mitaa, ambayo ingefanya iwe vigumu kwao kuomba hifadhi katika nchi nyingine yoyote ya Umoja wa Ulaya isipokuwa Italia. Hata hivyo, mara tu waliporuhusiwa kuwa huru walianza safari kutoka Bologna ufukweni mwa Italia, wakenda hadi Milan, na kisha kuvuka mpaka na kuingia Ufaransa.
Nada, wakati huo huo, alianza kuwa na mashaka yake mwenyewe. Sheria za wanaotafuta hifadhi zilikuwa zikizidi kuwa kali nchini Uingereza. Akawapigia tena simu ndugu zake.
"Niliwaambia [wao] kwenda Ujerumani, au Italia. Kwa sababu hapa, [kuna] sheria ngumu. Sheria mpya ni ngumu sana kwa wanaotafuta hifadhi." Lakini ndugu zake walikataa.
Kinadharia, Sheria mpya ya Uhamiaji Haramu ya Uingereza, ambayo ilianza kutumika Julai iliyopita, sasa ingemnyima Obada haki yoyote ya kudai hifadhi na kusalia Uingereza. Lakini katika hali halisi, bila makubaliano bado juu ya wapi pa kuwapeleka wale wanaowasili kwa boti ndogo, Obada angeishia kuungana na makumi ya maelfu ya watu wengine wanaotoka katika kile Baraza la Wakimbizi limekielezea kama "hali ya kutokuwa na utulivu wa kudumu" - wanaoishi Uingereza, lakini bila mustakabali ulio wazi.
Ndugu za Nada walisafiri kwa gari moshi hadi Paris. Hawakujua mtu yeyote katika bara la Ulaya. Na Nada alikuwa Uingereza, kama vile jamaa wengine wengi. Isitoshe, sehemu ngumu zaidi ya safari hakika ilikuwa imekwisha.
"Nataka kuja hapa [Uingereza] kwa sababu uko hapo," Nada anakumbuka Obada alimwambia.
Na kwa hivyo, mapema Januari, Obada, Ayser na marafiki zake sita wa Syria walifika Calais. Walipiga hema chini ya daraja, wakijaribu kuwaepuka polisi wa Ufaransa ambao wakati mwingine wangechukua mahema na kuwaamuru "kusonga mbele".
BBC imezungumza na shirika la kutoa misaada la ndani ambalo lilitaka kusaidia kundi hilo huko Calais. Obada alipewa hifadhi, kama mtoto, lakini alisema alitaka kukaa na kaka yake. Shirika hilo, ambalo halijatajwa kwa sababu ya umuhimu wa kazi yake, pia liliwasiliana na angalau wavulana wengine wawili ambao walipanda mashua ambayo Obada alijaribu kuipanda.
Mwakilishi wa shirika la hisani aliwatuambia wasafirishaji haramu huko Calais waliwazuia baadhi ya wavulana hawa "kujiamulia wenyewe", na kwamba pia walihisi "kushinikizwa na familia zao".
Akizungumza kuhusu mmoja wa wavulana wengine, mwakilishi huyo alisema: "Alitupigia simu na kutuambia anaogopa. Alituambia kwamba ni wazazi wake waliomlazimisha (kujaribu kuvuka)."
Baada ya zaidi ya wiki moja, kundi hilo liliambiwa kujitayarisha na wasafirishaji haramu wa Syria ambao walikuwa wamewalipa Euro 2,000 kila mmoja ili kuwapeleka Uingereza. Utabiri ulikuwa mzuri. Wangeondoka Jumamosi usiku.
Upepo ulikuwa umepungua kando ya pwani. Lakini halijoto ilikuwa juu tu ya kipimo cha barafu, na bahari labda ilikuwa 7C.
Akiwa gizani Wimereux, Obada alijaribu kuungana na watu waliokuwa wakijaribu kupanda boti iliyokuwa ikiondoka kwenye ufuko. Lakini mara moja, yeye na Ayser waligundua kuwa walikuwa wametoka kwenye boti na kurushwa kwenye bahari yenye barafu.
"Walianza kupiga kelele na kuomba msaada," alisema Faris, ambaye alifanikiwa kunyata na kurudi kwenye boti na tayari alikuwa akisaidia kuwatoa watu nje ya maji. Lakini gizani, hakuweza kujua Obada alikuwa wapi.
"Sikuweza kuwaona tena. Walitoweka ndani ya maji. Maji yaliwavuta, na sikuweza kuwafikia. Hatukujua ikulikuwa [na kina kirefu] hivi," alisema.
Polisi wa Ufaransa walikuwa wakishika doria karibu na hapo. Ufadhili wa ziada kutoka Uingereza umewezesha Ufaransa kuongeza idadi ya maafisa katika eneo hilo, lakini bado haitoshi kufuatilia kila sehemu ya takriban kilomita 150 (maili 93) ya ufuo ambayo sasa inatumiwa na wasafirishaji haramu.
Helikopta ya jeshi la wanamaji na boti ya doria ilifika eneo la tukio saa 02:15. Wafanyakazi wa uokoaji walisaidia kuwatibu wahamiaji 20 wameugua kutokana na baridi. Lakini Obada hakuwa miongoni mwao.
"Bado nayasikia kichwani mwangu, mayowe, mayowe yakipiga hadi kufa, naweza kusema," alikumbuka Sgt Maj Maxime Menu, ambaye alikuwa amejitumbukiza kwenye maji yaliyokuwa yameganda alipokuwa katika kazi ya uokoaji katika eneo hilo usiku huo.
Dakika chache baadaye, Nada alipokea simu akiwa London…"Wote wawili wamefariki’’.
Alipoulizwa ''Je ungejua unachokijua sasa ungebaki nchini Syria?''...''Ndio'' alisema kaka wa Obada, Nada
Alikuwa ni mtu mwingine mmoja wa Wasyria katika kundi hilo akipiga simu. Alikuwa amefaulu kumtoa Ayser nje ya maji kwanza, lakini akiwa amechelewa. Na kisha mwili wa Obada ulivutwa ufukweni. Hawakuweza kuogelea, wote wawili walikuwa wamezama maji labda mita 10 kutoka kwenye ufukweni.
Katika kitanda chake, Nada alilia machozi. Alianza kulia huku akipumua kwa haraka, kisha akafuta macho yake.
Ikiwa ungejua wakati huo unachojua sasa, ungebaki Syria? Nilimuuliza.
"Ndiyo. Baada ya kile kilichotokea kwa Ayser na Obada, ningebaki Syria," alijibu.
Je, ungependa Obada angebaki Syria pia?
"Ndiyo."
Je, unahisikia hatia kwa kumtia moyo kufanya safari.
"Ndiyo. Ndiyo," alisema.
Jioni iliyofuata, wenyeji wapatao 100 kutoka Calais na wahamiaji wachache walikusanyika katikati mwa jiji ili kukaa kimwa kwa dakika moja kuwakumbuka watu watano waliofariki na kuongeza majina ya Obada na Ayser kwenye orodha nefu ya wale waliokufa wakijaribu kuvuka kivuko cha Ufaransa kuelekea Uingereza miaka ya hivi karibuni.
Watu wengi watakuwa na mwelekeo wa kuwakosoa wazazi na familia yake kwa kuhatarisha maisha ya mtoto katika safari hiyo hatari. Wengine, haswa wale walio na uzoefu wa moja kwa moja wa maisha katika maeneo ya vita kama Syria, wanaweza kusema kwamba ni kitendo cha kusikitisha na kukatisha tamaa kwa familia kwamba walichukua hatua kama hiyo.
Inaonekana kuna uwezekano kuwa mwili wa Obada, pamoja na wa kaka yake, utazikwa huko Calais katika siku zijazo. Mamlaka ya Ufaransa ilisema haitawezekana kuwasafirisha hadi Uingereza, na gharama zinazohusika katika usafirishaji wa kurudi Syria, kulingana na Nada, ni za juu sana kutafakari.
Utafiti wa ziada umefanywa na Kathy Long, Feras Kawaf na Marianne Baisnee; muundo wa Lilly Huynh, Matt Thomas na Kate Gaynor; uzalishaji na James Percy na Dominic Bailey
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi