Ajali ya ndege Ziwa Victoria: Mamlaka zinavyobebeshwa mzigo wa lawama

Na Yusuph Mazimu, BBC Swahili

Kumekuwa na maoni tofauti kuhusu ajali ya ndege ya Precision Air iliyotokea Jumapili asubuhi ya Novemba 6, 2022 huko Bukoba, magharibi mwa Tanzania.

Ndege hiyo ATR 42-500 yenye namba PW 494 ilianguka kwenye ziwa Victoria mita chache kutoka uwanja wa ndege wa Bukoba, ikijiandaa kutua ikitokea jijini Dar es Salaam kupitia Mwanza.

Ajali hiyo imeua watu 19 kati ya 43 waliokuwemo akiwemo rubani na msaidizi wake.

Vyombo vingi vya Habari na mitandaoni kumekuwa na maoni mengi kuhusu namna wengi wasivyoridhishwa na shughuli ya uokoaji. Baadhi wakionyesha hasira na kutaka uwajibikaji zaidi wa mamlaka wakiinyooshea kidolea kwa uzembe. 

Maoni ya wadau ni yapi?

Chama cha ACT Wazalendo chenyewe kimemtaka Waziri mkuu, Kassim Majaliwa kujiuzulu kutokana na udhaifu wa kitengo cha uokoaji kilicho chini ya ofisi yake.

Katika taarifa yao iliyosainiwa na Philbert Macheyeki, Msemaji wa sekta ya mawasiliano ya chama hicho kimetaka pia waziri wa uchukuzi na waziri wa mambo ya ndani, kuwajibika huku kikimtaka Rais Samia Suluhu kumfuta kazi mkuu wa mkoa wa Kagera, Albert Chalamila kwa kuchelewa kwa shughuli za uokoaji kwa ngazi ya mkoa.

BBC imezungumza na Mwanasiasa mkongwe na mtaalam wa majanga, James Mbatia, akisema kilichotokea ni sawa na mauaji. Akiitupia lawama serikali kwa kutoanzishwa kwa wakala wa majanga, licha ya bunge kupitisha sheria namba 7 ya mwaka 2015 kuruhusu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo ya usimamizi wa majanga.

'Chombo hichi kingekuwepo leo hii tungekuwa tunakiuliza kulikoni, tungepata mtu wa kumuwajibisha moja kwa moja kwa mujibu wa sheria', alisema.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) chenyewe kupitia kwa mkurugenzi wake wa mawasiliano, kimesema kwamba, tukio la ajali hiyo limeonyesha namna taifa hilo lisivyo na uwezo wa kukabiliana na majanga na kwamba kama lingekuwa limejiandaa madhara ya ajali hiyo yasingekuwa makubwa.

Baadhi ya wananchi wengine waliozungumza na BBC, pamoja na kushtushwa na tukio hilo, na kumpongeza kijana aliyejitolea kuokoa manusura, wanaona lawama kwa sasa si mahala pake.

'Ajali haina kinga, ni mipango ya Mungu, hata ukimlaumu mtu sasa hivi haisaiidi kitu, uwezo wa kuwa na teknolojia za kisasa za uokoaji ni gharama sana kwa nchi maskini kama Tanzania, sio rahisi, juhudi zimefanyika kwa kiwango chetu, tuwapongeze walioshiriki, tusiwakatishe tamaa', alisema Seif Shangali, mkazi wa Dar es Salaam.

Ni kweli kilichotokea ni Uzembe?

Hakuna anayeweza kuthibitisha kwa sasa kuhusu hili. Lakini wanaoamini uwepo wa uzembe wanasisitiza kwenye eneo la kuchelewa kwa zoezi la uokoaji, utaalamu, nguvu kazi na vifaa vilivyotumika.

James Mbatia, anashangazwa kutumika kwa teknolojia dunia ya uokoaji, licha ya kukua kwa teknolojia ulinganisha na miaka 26 iliyopita ilipotokea ajali kubwa ya meli ya MV Bukoba, akigusia teknolojia ya kutumia kamba kuivuta ndege kutoka kwenye ziwa.

'Yaani unavuta ndege kana kwamba ndoano unavua samaki kwenye bahari, ni jambo la fedheha sana' alisema Mbatia na kuongeza 'wale wavuvi wao ndio wanafanya kazi hiyo (uokoaji) wakati vikosi vipo , hakujawa na utashi wa kisiasa wa kufanya kazi hiyo'.

Msemaji wa serikali, Gerson Msigwa akizungumza na waandishi wa habari leo, alisema serikali haiwezi kuwa na dhamira ya kuacha watanzania waangamie yanapotokea majanga, na kwamba serikali imejitahidi kuhakikisha madhara ya ajali yanapunguza.

Mara baada ya ajali kutokea, wavuvi waliokuwa karibu akiwemo mchuuzi wa dagaa katika mwalo Nyamkazi, Bukoba, Jackson Majaliwa, ndio waliokuwa wa kwanza kufika eneo la tukio kuokoa watu 24.

Majaliwa akitambuliwa kama shujaa kwa kufanikiwa kuvunja mlango wa dharura na kwa ujasiri huo, ameweza kupongezwa kwa kupatiwa fedha na serikali huku akihaidiwa kuingizwa kwenye jeshi la uokoaji la nchi hiyo.

Kwa maoni mengi, kitendo kile kimechukuliwa kwa ukubwa huo, kwa sababu ya wahusika wa masuala ya uokoaji kutowajibika kwa wakati na uduni wa teknolojia ya vifaa.

'Serikali itaanza mara moja kununua vifaa na kuvipeleka maeneo mbalimbali ambapo majanga yanaweza kutokea, tutafundisha wataalam na jamii juu ya namna bora ya kukabiliana na majanga', alisema Msigwa.

Kauli ya serikali

Kwa kuwa kitengo kinachoshughulikia majanga kiko chini yake, muda mfupi baada ya ajali hiyo kutokea, Waziri Mkuu, Majaliwa , alifika katika eneo la tukio, akiwa na viongozi wengine akiwemo waziri wa uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa , Waziri wa mambo ya ndani, Hamad Masauni na Waziri wa ulinzi na Jeshi la Kujenga taifa, Innocent Bashungwa.

Waziri mkuu akizungumza na wananchi alisema ’uchunguzi wa chanzo cha ajali hii utafanyika na vyombo husika ili tupate taarifa kamili ya nini kilitokea’.

Kwa kauli hii ya waziri mkuu ni kwamba, ni dhahiri kama kulikuwa na uzembe ama lolote kuhusu tukio zima, yatabainika kupitia kwa ripoti ya uchunguzi huo. Hata hivyo haiko wazi uchunguzi huo utachukua muda gani na linii wannachi wanategemea ripoti yake.

Kwa upande wake Waziri Bashungwa, akizungumza kwenye uwanja wa Kaitaba wakati wa kuaga miili ya watu 19 waliofariki kwenye ajali hiyo alihaidi kwamba serikali imesikia na itafanyia kazi maoni ya wananchi ya kuboresha vifaa vya uokoaji.

‘Katika janga hili lenye majonzi makubwa pia tumepokea maoni ya wananchi ya namna tunavyohitaji kujipanga vyema zaidi katika kuboresha mifumo ya uokoaji na kwa serikali hii sikivu inayoongozwa na rais wetu mpendwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na tunakwenda kuyafanyia kazi’, alisema Bashungwa. 

Pamoja na hayo Msemaji wa Serikali, amesema wataalam kutoka ATR nchini Ufaransa ambao ndio watengenezaji wa ndege iliyopata ajali wanawasili leo ili kuungana na timu ya wataalam waliopo nchini Tanzania, pamoja na timu ya watengenezaji wa injini watafika kwa ajili ya uchunguzi zaidi.