Je, Rais wa Iran Ebrahim Raisi anatafuta nini Afrika?

    • Author, Rashid Abdalla
    • Nafasi, Mchambuzi

Miaka 11 imepita tangu rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kutembelea bara la Afrika. Ziara ya mwisho ilikuwa ni rais wa sita wa nchi hiyo Mahmoud Ahmadinejad, katikati ya Aprili 2013 alipotembelea nchi tatu - Benin, Niger na kumalizia Ghana.

‘Mwanzo mpya wa uhusiano na Afrika,’ ndio kauli ya Rais Ebrahim Raisi alipokuwa akijindaa kuanza ziara ya siku tatu barani Afrika wiki hii. Alianza Kenya, akaelekea Uganda na anahitimisha ziara yake nchini Zimbabwe.

Iran ni nchi ilio katika vikwazo vya Marekani, ziara hii inatazamwa na wengi kama njia ya kujenga washirika wapya wa kisiasa na kibiashara ili kupambana na vikwazo hivyo, ambavyo vimeathiri pakubwa uchumi wa taifa hilo.

Rais Raisi ameongoza ujumbe wa ngazi za juu wa Iran akiwemo Waziri wa Afya, Waziri wa Jihadi ya Kilimo, Waziri wa Mambo ya Nje na maafisa wengine wa ngazi za juu wa sayansi na teknolojia wa nchi hiyo.

Kuipa kisogo Ulaya

Baada ya Urusi kuivamia Ukraine Februari 2022, msururu wa vikwazo kutoka mataifa ya Ulaya dhidi yake ukafuatia. Hilo likapelekea taifa hilo kuanza kusaka washirika wapya. Ziara za Waziri wake wa Mambo ya Nje, Sergey Lavrov ziliongezeka Afrika. Yaonekana Iran nayo imeamua kufuata nyayo hizo.

Iran inasaka washirika wapya kutoka kila pembe. Tangu kuingia madarakani Sayyid Ebrahim Raisolsadati, ameshafanya ziara katika mataifa mbalimbali, yakiwemo yale ambayo ni mahasimu wa mataifa ya magharibi.

Amekuja Afrika ikiwa umepita mwezi mmoja tangu afanye ziara Amerika kusini, kwa siku tano – Venezuela, Cuba na Nicaragua, nchi zote hizo ziko katika vikwazo vya Marekani. Ilikuwa ni ziara yake ya 13 nje ya Iran tangu awe Raisi.

Pia, ameshatembelea Urusi na kukutana na rais wa taifa hilo Vladimir Putin Januari 2022 katika ziara ya siku mbili. Kabla ya kuelekea huko, Raisi alisema, Urusi na Iran zikiwa imara pamoja zitakuzuka biashara na usalama.

Pia, Februari 2023, Rais Raisi alifanya ziara ya siku tatu nchini China kufuatia mwaliko wa Rais wa China, Xi Jinping. Nchi zote mbili zina mivutano ya hapa na pale na mataifa ya magharibi. Ukaribu wa China na Iran unatokana na ile kauli ya,‘adui wa adui yangu ni rafiki yangu.’

Mwezi Mei 2023, rais Raisi alifanya ziara ya siku mbili katika taifa la Waislamu wengi la Indonesia, lengo likiwa ni kuimarisha ushirikiano wa kibiashara. Ziara ya mwisho ya kiongozi wa Iran katika nchi hiyo ilikuwa ni 2015 iliyofanywa na rais mstaafu Hassan Rouhani.

Ziara ya Afrika

Afrika imegeuka kuwa kimbilio la mataifa mengi ambayo yana vuta nikuvute na dunia ya magharibi.

Bara lenye rasilimali na fursa, mataifa yasiyo na mlahaka mzuri na Ulaya huja kutaka kujenga ushawishi, kukukuza biashara na ushiarikiano.

''Rais aliyepita wa Iran aliipa mgongo Afrika na akajaribu kutumia mazungumzo ili kumaliza mkwamo na mataifa ya magharibi - ila hilo halikufanikiwa. Huyu wa sasa anajaribu kubadilisa mbinu ya kushinda vikwazo vya Marekani,’' anasema profesa mshiriki wa kitengo cha siasa na uhusiano wa kimataifa, chuo kikuu cha kimataifa cha Florida, Eric Lob akizungumza na Al-jazeera.

Zimbabwe: Iran na Zimbabwe hazina tofauti na yale mataifa ya Amerika ya Kusini, zote ziko katika kundi la nchi zilizoekewa vikwazo na Magharibi. Vikwazo ambavyo kimsingi vinaumizi chumi na ustawi wa mataifa hayo.

Zimbabwe ndio nchi ya mwisho katika ziara ya Raisi. Nchi hizo zina uhusiano mzuri wa kidiplomasia kwa miaka ming. Ubalozi wa Iran nchini Zimbabwe ulifunguliwa tangu 1982, wakati Ali Khamenei akiwa rais wa Iran.

Zimbabwe kwa upande wake ilifungua ubalozi wake Tehran mwaka 2003, wakati huo hayati Robert Gabriel Mugabe akiwa rais. Huku upande wa Iran, Mohammad Khatami akiwa rais wa wakati huo.

Kenya: Katika ziara yake nchini Kenya, nchi hizo zimetiliana saini ya ushirikiano katika maeneo kadhaa, ikiwemo sekta ya mawasiliano, uvuvi, kilimo, afya, elimu ya ufundi, maarifa na matibabu,

Raisi alifanya uzinduzi wa droni jijini Nairobi alipotembelea Jumba la Ubunifu na Teknolojia la Iran (IHIT). Droni zinazotumika katika shughuli za kilimo, ikiwemo kunyunyizia mashamba na kubaini iwapo kuna wadudu waharibifu wa shambani.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Takwimu nchini Kenya (KNBS), thamani ya biashara kati ya Kenya na Iran ni Ksh bilioni 9.3 kwa mwaka 2022. Kenya ikisafirisha biashara Ksh bilioni 5.9 na kuingiza kutoka Iran ya thamani ya Ksh bilioni 3.4. Kenya hupeleka chai, kahawa, matunda, samaki na kupokea kemikali, mafuta na plastiki.

Uganda: Shirika la Habari la Iran (IRNA) limeripoti kuwa, suala la msamaha wa viza, ushirikiano wa kilimo, uanzishwaji wa kamisheni ya pamoja ya kudumu ni hati za ushirikiano zilizosainiwa kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Uganda.

Katika kile kinachoonekana ni kuunga mkono Uganda, Rais Raisi amekemea vikali mahusiano ya jinsia moja huku akizinyooshea kidole nchi za magharibi. Hii ikiendana kabisa na msimamo wa Uganda ambayo hivi karibuni imepitisha sheria kali iliyokosolewa kimataifa dhidi ya watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja.

Uganda ina historia ya kutembelewa na marais wa Jamhuri hiyo, Mahmoud Ahmadinejad aliitembelea siku mbili mwaka 2010, Mohammad Khatami rais wa tano, alitembelea Uganda 2005 na rais wa nne Akbar Hashemi Rafsanjan – 1996.

Katika ziara hii yaonekana hakuna uhaba wa saini ya hati za ushirikiano kati ya Iran na nchi ilizozitembelea. Ingawa hilo halitoi uhakika ikiwa alilolifuata rais Raisi Afrika limefanikiwa, kwa sababu utilianaji saini ni jambo moja na utekelezwaji wa hayo makubaliano ni kazi nyingine.