Waridi wa BBC: 'Wajane sio wale waliofiwa tu bali hata wale walioolewa na walevi'

Mesha
Maelezo ya picha, Mesha Singolyo, mratibu wa wajane kutoka asasi isiyokuwa ya kiserikali ya Global Fund for Widows
    • Author, Esther Namuhisa
    • Nafasi, BBC News Dar es Salaam
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

“Ninajiona napendeza sana kuvaa hivi, ninajivunia kuwa Mmasai” Ni maneno ya Mesha Singolyo, mwanamke aliyeelimishwa na ukoo wake. Baada ya kumaliza shahada yake ya uzamili katika masuala ya maendeleo ya jamii, alirejea kutoa mchango wake kwa jamii yake.

Anafanya harakati za kuwasaidia wajane kujikomboa kiuchumi kupitia vikundi vya akiba vya kijamii. Kutokana na mila za ndoa za mitala na changamoto ya ndoa za utotoni katika jamii yake, wajane si wale tu waliopoteza waume zao bali pia wanawake walioolewa na wanaume waliowazidi umri kwa miaka mingi.

Mesha anaendelea kuvaa mavazi ya kitamaduni ya Kimaasai licha ya kuwa mratibu wa wajane katika jamii hiyo.

“Mimi kama zao la jamii ya kimasai sioni kama nina haja ya kuonekana tofauti na jamii ambayo imenizaa, mara nyingi nikiwa kijijini na akina mama ni muhimu kwangu kuvaa kama wao ili kutoonekana tofauti na jamii. Nataka elimu yangu iisaidie jamii yangu lakini si kunifanya nionekane tofauti.”

Mesha
Maelezo ya picha, Mesha akiwa katika kikao cha mafunzo ya ujasiriamali

Mesha pia ni mwanzilishi wa asasi ya PWDT inafanya kazi ya kuwasaidia wasichana kupata haki ya elimu, kama njia ya kutatua tatizo la ndoa za utotoni na utegemezi miongoni mwa wanawake wa jamii ya wafugaji. Lengo kuu la Mesha ni kuona jamii ikikombolewa kutoka katika ukatili wa kijinsia na wanawake kuwa huru kiuchumi.

Anasema ari yake ya kuisaidia jamii ni jambo ambalo amekuwa nalo na kwa sasa kuona kundi la wanawake linafanikiwa katika maisha yao ni jambo ambalo linampa faraja sana.

”Kuona mama anahangaika na watoto na jitihada ambazo mama yangu alikuwa anazifanya wakati anatulea ni hizi ambazo ninaziona kwa jamii yangu. Mimi ni mwanajamii nimesoma masomo ya kijamii, jambo ambalo nimekuwa nalo. Napenda kuwaona wanawake wanafanikiwa hivyo kwa kutumia nafasi yangu huwa naweka jitihada”

Anaeleza kuwa amepata elimu yake kupitia michango ya jamii na mpaka sasa ana shahada tatu.

Akikumbuka wakati anakua, ndugu zake wote hawakupata nafasi ya kwenda shule, hata wale ambao alisoma nao ambao ni zaidi ya wanafunzi zaidi ya 100, nusu walikuwa wasichana ila hadi anafika chuo kikuu anasema alikuwa amebaki mwanamke pekee kutoka shule aliyosoma.

”Nikizingatia mazingira ya nyumbani na familia, shule na nikiangalia sina hata mtu mmoja ambaye ninaweza kumuuliza stori za zamani nikiwa shule, hii ilikuwa mzigo mkubwa sana kwangu.

Anafafanua: Nilijiona nina sababu za dhati kabisa kutumia elimu yangu, leo tuna wanawake wengi wanapitia ukatili wa kijinsia kwa sababu ni tegemezi, kwa sababu mifumo haikuwapa nafasi ya kujitegemea.

Kusomeshwa kunavyomfanya ajione ana deni la kulilipa

mesha

Chanzo cha picha, Mesha

Maelezo ya picha, Mesha anasema ndoto yake ni kuifanya elimu yake iwe sehemu ya jamii yake
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Anakiri kuwa haikuwa rahisi kwake kufika alipo. “Nikiwa na miaka tisa (9), changamoto za kifamilia baada ya wazazi kufariki dunia yalifanya mazingira kuwa magumu.

Anasema anamshukuru Mungu kuwa taasisi moja ilipita kijijini kwao na akapewa ufadhili wa kwenda kusoma sekondari.

Anaelzeza: Baada ya hapo nilihakikisha kuwa ninafanya vizuri shuleni kwa kuwa niliona kuwa nina deni la kulilipa kwa jamii yangu kusaidia wengine, kwa kuwa wengi wanastahili kupata msaada kama nilioupata mimi ila hawakuupata. Hivyo, nina sababu ya kuhakikisha kuwa watoto na wanawake wanapata haki zao.

Kwa sasa Mesha, ameteuliwa kuwa mratibu mkuu taasisi ya Global Fund for Widows nchini Tanzania, ambapo kazi yake kubwa ni kuhakikisha kuwa anawasaidia wajane wanajikomboa kiuchumi.

Mesha kwa sasa anaratibu mpango wa kuweka fedha na kukopa ambao unatumia sanduku la kuhifadhi fedha na kukopesha.

Mkoa huu ulikuwa unaongoza kwa wanafunzi kuacha shule kutokana na mila kandamizi, watoto wanaachishwa shule kwa ajili ya kwenda kukeketwa au kuchunga ng’ombe na kuolewa jambo ambalo linafifia.

Wajane si wale waliofiwa waume pekee

masai
Maelezo ya picha, Kwa sasa akina mama hawa wajane wana uwezo wa kuweka akiba ya kati ya milioni 60-80 za kitanzania

”Vigezo vya mama kuwa mjane huwa tunaangalia mwanamke yeyote ambaye analea familia kwa mkono wake inawezekana mume wake yupo lakini ni mzee sana, au mume ni mlevi au amefariki, anaeleza.

Katika jamii ya kimasai, mume akifariki dunia hata kama amemwacha mjane mwenye umri wa miaka 20 hawezi kuolewa na mwanaume mwingine, anapaswa kubaki katika boma hilo hilo. Kwa taswira hiyo mwanamke anapambana peke yake katika malezi ya watoto.

Hivyo, anaona ni muhimu kumshika mkono kwa kumpa elimu ya ujasiriamali na mtaji ili aweze kuhakikisha anaitunza familia.

Benki ya kisanduku kijijini

masai
Maelezo ya picha, Funguo za Sanduku lao la benki linahifadhiwa na watu watatu tofauti

Kwa sasa Mesha anaratibu mradi wa benki ya sanduku unaoitwa Sara bank, ambao mpaka sasa wameweza kuwafikia wanawake zaidi ya 8000 katika mkoa wa Arusha.

‘Kazi ninayoifanya naiona inaleta matokeo chanya. Sasa kuna kundi la wamama 25 ambao wengine wana zaidi ya milioni 60 au 80. Mara nyingi wanawake wengi wanakuwa hawana ujuzi wa biashara, hivyo lazima tumpe elimu ya ujasiriamali ili asimamie na kumpa mtaji aanze biashara. Vilevile, hii imekuwa somo kubwa kwa wanaume kuweza kuishi nyumbani kwa amani na upendo.

Mesha

Mila na desturi za kimasai, mke mwenza ni rafiki

m

Mesha anasema: Katika jamii hii unaweza kukuta binti wa miaka 20 anaolewa na mzee wa miaka 90 kwa kuwa baba ndiye ametaka na mahari imetolewa hana uchaguzi, na katika boma unayeolewa unakuwa labda mke wa 9, hivyo tunachofanya ni kumsaidia mke ili aweze kulea watoto na hata mzee aliyemuoa kwa kuwa anakuwa hana nguvu ya kufanya kazi tena.

Kulingana na mila na tamaduni ya jamii hii, mwanaume ana uwezo wa kuoa wake wengi kadiri awezavyo.

Tuna kikundi ambacho kina wanawake 25 ambao wote ni wajane wa mwanaume mmoja ambaye wakati wa uhai wake alifanikiwa kuoa wake zaidi ya 25.

Uzuri wa jamii hii ya kimaasai, tunajivunia kufundisha dunia kuwa uke wenza si uadui, kwa mfano wake hawa wanaweza kufanya kazi kwa pamoja na kuendeleza boma lao.

Katika jamii hii mke mwenza ni rafiki huwa hatuna uadui wa kugombania mume. Binafsi ninajisikia vizuri sana kuwa harakati zangu ziliweza kuonekana.

m

Chanzo cha picha, Mesha

Maelezo ya picha, Mesha akiwa na rafiki yake

Mwaka 2022, nilishangaa sana baada ya kupata tuzo ya kusimamia haki za mtoto kwa sababu ya harakati za kumsaidia mtoto wa kike ambazo nilianza tangu nasoma.

Kuna mradi nilikuwa naufanya unaoitwa ‘Ndoto yangu maisha yangu’ nilikuwa napita kwenye shule na kuwajengea watoto uwezo wa kwanini ni muhimu wao kusoma.

Anaweka bayana: Kiukweli tuzo ilinipa nguvu zaidi katika harakati zangu mpaka nikaweza kuanzisha taasisi inayoitwa Partnership for Women Development (Ubia wa Maendeleo ya Wanamke) ambayo inalenga kuwasaidia watoto wa wajane na wengine ambao wanaishi katika maisha hatarishi. Tunawapa mahitaji ya shule na kusaidia wale ambao nyumbani kwao ni sehemu salama.

Mhariri: Florian Kaijage