Mapinduzi ya Niger: Wagner inatumia fursa ya ukosefu wa utulivu - Antony Blinken

Chanzo cha picha, Getty Images
Kundi la mamluki la Urusi la Wagner "linatumia fursa" ya ukosefu wa utulivu nchini Niger, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken ameiambia BBC.
Nchi hiyo imetawaliwa na utawala wa kijeshi baada ya kuondolewa madarakani kwa Rais Mohamed Bazoum zaidi ya wiki mbili zilizopita.
Kumekuwa na mapendekezo ambayo viongozi wa mapinduzi wameomba msaada kutoka kwa Wagner, ambao wanajulikana kuwepo katika nchi jirani ya Mali.
Bw Blinken alisema hafikirii Urusi au Wagner ndiyo zilizochochea mapinduzi ya Niger.
Hata hivyo Marekani ilikuwa na wasiwasi kuhusu kundi hilo "labda kujidhihirisha" katika sehemu za ukanda wa Sahel, alikiambia kipindi cha BBC Focus on Africa.
"Nadhani kilichotokea, na kinachoendelea kutokea Niger hakikuchochewa na Urusi au na Wagner, lakini...walijaribu kutumia fursa hiyo."
"Kila mahali ambapo kundi hili la Wagner limepita, vifo, uharibifu na unyonyaji vimefuata," alisema Bw Blinken.
"Ukosefu wa usalama umeongezeka, si kushuka".
Aliongeza kuwa kulikuwa na "marudio ya kile kilichotokea katika nchi nyingine, ambapo hawakuleta chochote isipokuwa mambo mabaya''

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wagner inaaminika kuwa na maelfu ya wapiganaji katika nchi zikiwemo Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) na Mali, ambako ina maslahi ya kibiashara lakini pia inaimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi wa Urusi.
Wapiganaji wa kundi hilo wameshutumiwa kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu katika nchi kadhaa za Afrika.
Licha ya hayo, kumekuwa na uvumi kuwa jeshi la Niger limeiomba Wagner msaada huku nchi hiyo ikikabiliwa na uwezekano wa kuiingilia kijeshi.
Ecowas, jumuiya ya kiuchumi ya mataifa 15 ya Afrika Magharibi ilitoa makataa ya Jumapili kwa viongozi wa serikali ya Niger kujiuzulu na kumrejesha Rais Bazoum.
Tarehe hii ya mwisho ilipuuzwa na Ecowas inatazamiwa kufanya mkutano siku ya Alhamisi ili kuamua nini cha kufanya baadaye.
Siku ya Jumatatu, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Victoria Nuland, alifanya kile alichokitaja kuwa "mazungumzo magumu na ya wazi" na viongozi wa mapinduzi, ambao alisema wanaelewa hatari ya kufanya kazi na mamluki.
Bw Bazoum, ambaye kwa sasa yuko kifungoni, pia amezungumzia wasiwasi wake kuhusu ushawishi wa Wagner barani Afrika.
"Kwa mwaliko wa wazi kutoka kwa wapanga mapinduzi na washirika wao wa kikanda, eneo lote la Sahel ya kati linaweza kuanguka kwa ushawishi wa Urusi kupitia Kundi la Wagner, ambalo ugaidi wao wa kikatili umeoneshwa kikamilifu nchini Ukraine," aliandika katika safu ya maoni ya Washington Post. Chapisho lililochapishwa wiki iliyopita.
Kwa sasa haijulikani kama wapiganaji wa Wagner wameingia nchini lakini kituo maarufu cha Telegram kinachohusishwa na Wagner, Gray Zone kilisema Jumatatu kwamba wapiganaji wake 1,500 hivi karibuni walitumwa Afrika.
Haikueleza ni wapi walikodaiwa kupelekwa barani.
Kiongozi wa Wagner, Yevgeny Prigozhin amewataka watawala "tupigie simu" katika ujumbe wa sauti uliopakiwa kwenye Telegram siku ya Jumanne.
"Siku zote tuko upande wa wema, upande wa haki, na upande wa wale wanaopigania uhuru wao na haki za watu wao," alisema.

Chanzo cha picha, Reuters
Niger ni koloni la zamani la Ufaransa na mapinduzi hayo yamesababisha wimbi la chuki dhidi ya Ufaransa na Urusi nchini humo, sawa na hali ya majirani wa Mali na Burkina Faso, ambazo zote zimeegemea Moscow tangu mapinduzi yao wenyewe.
Nchi hizo mbili, ambazo ni wanachama wa Ecowas, zimetuma ujumbe katika mji mkuu wa Niger, Niamey, kuwahakikishia viongozi wa mapinduzi kuwa watajitetea dhidi ya mataifa mengine ya Afrika Magharibi na washirika wao wa Magharibi ikiwa itahitajika.
Wakati huo huo, serikali ya kijeshi imemteua aliyekuwa waziri wa fedha wa nchi hiyo, Ali Mahaman Lamine Zeine, kuwa waziri mkuu mpya wa nchi hiyo kufuatia mapinduzi hayo.
Bw Zeine anachukua nafasi ya Mahamadou Ouhoumoudou, ambaye alikuwa Ulaya wakati wa mapinduzi.















