Je, Ufaransa ndio wa kulaumiwa kwa mapinduzi ya kijeshi Afrika Magharibi?

A man holds up a placard during a march in Niamey

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, "Kwaheri Ufaransa," ndivyo linavyosomeka bango lililokuwa limeshikwa na wafuasi wanaounga mkono mapindu

Niger limekuwa taifa la tano katika ukanda wa Afrika Magharibi kufanya mapinduzi ya kijeshi katika siku za hivi karibuni ikizifuatia nchi za Burkina Faso, Guinea, Mali na Chad. Nchi zote hizo ni makoloni ya zamani ya Ufaransa.

Kutoka mwaka 1990, asilimia 78 ya mapinduzi yote 27 yaliyoshuhudiwa katika nchi za kusini mwa jangwa la Sahara yamefanyika katika nchi ambazo ni makoloni ya zamani ya Ufaransa, hali inayofanya baadhi ya wachambuzi kujiuliza ikiwa Ufaransa – ama urithi wa ukoloni wake – ndio wa kulaumiwa kwa kuchochea mapinduzi hayo?

Watekelezaji wa mapinduzi hayo bila shaka wanataka watu waamini kuwa kuna mkono wa Ufaransa. Kanali Abdoulaye Maiga, ambaye alitangazwa kuwa waziri mkuu wa mpito wa Mali baada ya jeshi kuwa madaraka Septemba 2022 alianza kazi kwa kutoa shutuma kali dhidi ya Ufaransa.

Kanali maiga aliishutumu Ufaransa kwa kutekeleza “sera za ukoloni mamboleo, kushusha hadhi (ya nchi za Kiafrika) na visasi,” na kuongeza kuwa nchi hiyo imeusaliti ulimwengu kwa tokuwa waadilifu na “imeichoma nchi ya Mali kisu mgongoni.”

Kashfa na kejeli dhidi ya Ufaransa pia vimepemba moto katika nchi ya Burkina Faso, ambako mwezi Februari mwaka huu serikali ya kijeshi ilivunja makubaliano ya muda mrefu ambayo yaliruhusu wanajeshi wa Ufaransa kuendesha operesheni zao nchini humo. Jeshi la Ufaransa lilipewa mwezi mmoja tu kufungasha virago.

Katika nchi ya Niger, ambayo inapakana na Mali na Burkina Faso madai kuwa Rais Mohamed Bazoum alikuwa ni kibaraka wa Ufaransa yametumika kuhalalisha mapinduzi ya kijeshi dhidi ya utawala wake.

Mikataba mitano ya kijeshi baina ya Niger na Ufaransa tayari imeshavunjwa na kiongozi wa mapinduzi hayo ya juma lililopita, Jenerali Abdourahmane Tchiani. Maandamano ya kuunga mkono mapinduzi hayo yameshuhudia ubalozi wa Ufaransa nchini humo ukishambuliwa na waandamanaji.

Kwa kiasi fulani ushahidi wa kihistoria unaunga mkono baadhi ya madai haya. Utawala wa kikoloni wa Ufaransa ulitengeneza mifumo ya kisiasa ya kuiwezesha kunyakua rasilimali muhimu kutoka kwenye makoloni yake na nchi hiyo imetumia sera kandamizi kuendeleza udhibiti rasilimali hizo.

Hata utawala wa kikoloni wa Uingereza ulitekeleza sera kama hizo. Lakini kinachowatofautisha wakoloni hao wawili, ni namna gani Ufaransa imekita mizizi na kuendelea kuwa na mkono wake barani Afrika – wakosoaji wake wanasema inaingilia moja kwa moja – uendeshaji wa siasa na uchumi wa makoloni yake ya zamani hata baada ya uhuru.

Nchi saba kati ya tisa zilizotawaliwa na Ufaransa katika ukanda wa Afrika Magharibi bado zinatumia sarafu ya CFA fanc, ambayo mdhamini wake mkuu ni Ufaransa, hii ni sera ya kurithi ya moja kwa moja kiuchumi ya nchi hiyo kwa makoloni yake.

Ufaransa pia iliingia mikataba kadhaa ya kijeshi na makoloni yake ya zamani ambayo iliilazimu nchi hiyo kuingilia kati kijeshi na kuwahakikishia usalama wao watawala wa nchi hizo pale walipotaka kung’olewa mamlakani na raia wasiounga mkono tawala hizo.

.

Chanzo cha picha, EPA

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kwa kiasi kikubwa, ufadhili na ulinzi wa Ufaransa uliwapa nguvu viongozi mafisadi na madikteta kama rais wa zamani wa Chad' Idriss Déby na rais wa zamani wa Burkina Fasobe Blaise Compaoré, hali ambayo ilifanya mapambano ya kuleta demokrasia katika mataifa hayo kuwa magumu na hatari zaidi.

Ijapokuwa Ufaransa haikuingia mstari wa kati kuwarejesha mamlakani viongozi waliopinduliwa katika siku za hivi karibuni, marais wote waliopinduliwa wamekuwa wakionekana kama wanaunga mkono sera za Ufaransa.

Kibaya zaidi, mahusiano baina ya viongozi wa kisiasa wa Ufaransa na washirika wao barani Afrika umekuwa ukihusisha rushwa na ufisadi na kusababisha kuibuka kwa tabaka la watawala wenye nguvu na utajiri katika nchi ambazo raia wengi wanaishi katika lindi la umasikini.

Mchumi maarufu kutoka Ufaransa, François-Xavier Verschave ndiye mtunzi wa neno Françafrique akielezea mahusiano ya ukoloni mamboleo yaliyojificha katika “siri za kijinai katika ngazi za juu kabisa katika uongozi wa kisiasa na kiuchumi wa Ufaransa. Mahusiano hayo, kwa mujibu wa Verschave, yamesababisha kiwango kikubwa cha fedha "kutwaliwa kifisadi."

Ijapokuwa serekali za Ufaransa za miaka ya karibuni zimekuwa zikijitahidi kujitenga na sera ya Françafrique, kumekuwa na ukumbusho wa mara kwa mara wa uhusiano wa mashaka baina ya Ufaransa, maslahi yake ya kibiashara dhidi maslahi ya bara la Afrika, ikiwemo msururu wa kesi za rushwa na ufisadi.

Hivyo si jambo gumu kuelewa kwanini raia mmoja wa Niger aliiambia BBC kuwa: "Toka utotoni mwangu nimekuwa nikiipinga Ufaransa… Wamepora utajiri wote wa nchi yetu kama madini ya urani, dhahabu na mafuta.”

Kashfa kama hizo zimekuwa zikifichwa nyuma ya pazia wakati viongozi madikteta na washirika wa Ufaransa walipokuwa madarakani, na msaada wa kijeshi wa Ufaransa uliwapa madikteta hao nguvu ya kutuliza mambo.

Katika miaka ya hivi karibuni, uwezo na ushawishi wa Ufaransa pamoja na mataifa mengine ya Magharibi umezorota, hali inayowezesha nchi hizo kushambuliwa na kulaumiwa barani Afrika.

Hali hiyo imedhihiri zaidi pale ambapo viongozi wa kiraia walipong’olewa madarakani na jeshi katika nchi za Burkina Faso na Mali. Kushindwa kwa viongozi hao kuwalinda raia wao dhidi ya tishio la wapiganaji wa kijihadi ikatengeneza taswira kuwa ushirikiano na Ufaransa ni kikwazo na si faida.

Kiwango cha juu juu cha hasira na kukata tamaa cha raia kikawafanya viongozi wa kijeshi kuamini kuwa mapinduzi yatapokelewa kwa shangwe na wananchi.

Hata hivyo, pamoja na makosa yote ambayo Wafaransa wamewatendea makoloni yao barani Afrika kwa miaka yote hiyo, kuzorota kwa amani na demokrasia kunakoendelea kushuhudiwa katika makoloni ya zamani ya Ufaransa haiwezi kulaumiwa Ufaransa pekee kwa kusababisha hali hiyo.

Haikuwa Ufaransa pekee dola yenye nguvu iliyotengeneza na kuwalinda madikteta kuongoza nchi za ughaibuni.

.

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Baadhi ya wale wanaopinga ushiriki wa Ufaransa nchini Niger wameonyesha uungaji mkono wao kwa Urusi badala yake

Katika kipindi cha Vita Baridi, Uingereza na Marekani walisaidia kuwaingiza madarakani na kuwalinda madikteta katika nchi kadhaa, kitu cha pekee ambacho walitakiwa kufanya madikteta hao ni kuwa watiifu kwa Marekani na Uingereza. Kuanzia Daniel arap Moi nchini Kenya mpaka Mobutu Sese Seko wa Zaire (sasa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo).

Uhusiano wa karibu baina ya mapinduzi na athari za ukoloni haukonekana katika zama zilizopita. Nchi nne zilizopitia mapinduzi mengi zaidi ya kijeshi barani Afrika toka mwaka 1952 ni Nigeria (8), Ghana (10), Sierra Leone (10) na Sudan (17), zote zilitawaliwa na Uingereza.

Japo msururu wa mapinduzi ya sasa katika makoloni ya zamani ya Ufaransa unaashiria kuwa historia na athari ya sera ya Françafrique inadhihirika, lakini pia mapinduzi hayo yanachochewa na hali isiyomithilika ya kukithiri kwa upotevu wa usalama katika maeneo kadhaa ya Afrika Magharibi na ukanda wa Sahel, ambapo kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa “makundi ya wanamgambo wenye silaha na wenye msimamo mkali,” yanafanya wananchi kupoteza imani na serikali za kiraia.

Kila mapinduzi katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita yamechochewa na sababu za kipekee katika mifumo ya kisiasa ya nchi husika. Ni sababu hizo ndizo zilizowagombanisha viongozi wa kiraia na jeshi, na kuwawachochea wanajeshi kupoka madaraka pale walipopata upenyo.

Nchini Mali, mazingira yaliyochochea mapinduzi yalianza kujitengeneza baada ya kushamiri kwa wapiganaji wenye msimamo mkali wa kidini baada ya kuanguka kwa serikali ya Libya mwaka 2011, pamoja na madai kuwa rais aliyekuwa madarakani alichakachua uchaguzi na kukua kwa maandamano dhidi ya serikali yaliyoongozwa na vyama vya upinzani katika mji mkuu wa nchi hiyo.

Duru zinaarifu kuwa kilichochochea mapinduzi ya wiki iliyopita nchini Niger ni mipango ya Bazoum kutaka kufumua uongozi wa juu wa jeshi na kumng’oa Jenerali Tchiani kutoka katika wadhfa wake wa mkuu wa majeshi.

Hiyo ni alama tosha kuwa mapinduzi hayo wala hayakuwa na nia ya kuirejeshea Niger mamlaka yake kamili ya kujitawala ama kuwakwamua wananchi kutoka kwenye umasikini bali kulinda maslahi ya maafande wakuu wa jeshi.

Sababu mseto zilizochochea mapinduzi ya miaka ya hivi karibuni pia zinapimika katika kasi ya serikali mpya za kijeshi katika kubadili mahusiano na ushirikiano na dola za kigeni zenye utata.

Katika mkutano wa hivi karibuni wa ushirikiano wa Urusi na nchi za Afrika, viongozi wa Burkina Faso na Mali wote walitangaza kumuunga mkono Rais Vladimir Putin na uvamizi wake nchini Ukraine.

Kama ilivyokuwa katika miongo iliyopita, wanufaika wakuu wa mahusiano haya ya kimataifa ni viongozi wakuu wa nchi na si wananchi wa kawaida. Tayari kuna ripoti zinazoonyesha kuwa vikosi vya mamluki vya Wagner vimekuwa vikitekeleza ukatili na mauaji ya mamia ya wananchi nchini Mali kama sehemu ya operesheni yake dhidi ya wanamgambo wa kijihadi.

Hivyo, kupunguza ushawishi wa Ufaransa katika makoloni yake ya zamani hakuwezi kuwa ni mwarobaini wa kuleta utulivu wa kisiasa, na katika miongo kadhaa ijayo tunaweza kushuhudia kizazi kipya cha wanajeshi ambacho kitafanya mapinduzi na kutoa sababu ya kutaka minyororo ya ushawishi wa Urusi katika nchi zao.

Leonard Mbulle-Nziege mchambuzi mtafiti kutoka shirika la Africa Risk Consulting (ARC) na Profesa Nic Cheeseman ni mhadhiri mwandamizi wa siasa za Afrika katika Chuo Kikuu cha Birmingham.