Kiongozi wa ngome ya vijana upinzani Tanzania adai 'watekaji' wametishia kumuua iwapo atazungumza

    • Author, Alfred Lasteck
    • Nafasi, BBC Dar es Salaam
  • Muda wa kusoma: Dakika 3

“Ukitoka hapa nenda moja kwa moja nyumbani kwako. Tunapajua vizuri na usizungumze kokote juu ya kilichotokea, pia tusikuone ukizungumza na vyombo vya habari. Ukifanya hivyo tutakuchukua na raundi hii tutakuua,” Mwanasiasa wa upinzani, Abdul Nondo ameieleza BBC huku akisema watekaji walikuwa wakimpa vitisho kila mara.

Nondo ambaye ni Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya ACT Wazalengo, amedai kuwa alikamatwa na kuchukuliwa kwa nguvu na watu sita dakika chache baada ya kuwasili katika eneo la Stendi Kuu ya Mabasi jijini Dar es Salaam akitokea Kigoma alipokuwepo kikazi.

Nondo alisema, baada ya kunaswa, waliohusika na tukio hilo walikuwa wakimueleza mara kadha kuwa kuzungumza kwake kumemponza na kwamba huo ndio mwisho wake.

“Wakati wakinipiga waliniambia ‘wewe si cha mdomo’ endelea leo tunakuua,” alisema na kuongeza kuwa waliomteka walimuumiza vibaya kwenye maeneo mbalimbali ya mgongo, mikono na miguu.

Jinsi alivyochukuliwa

Mwanasiasa huyo, anadai kuwa alipowasili katika jiji la Dar es salaam, alishtuka baada ya watu sita kumkaba na kumchukua kwa nguvu katika eneo hilo la stendi ya mabasi.

Anasema, “Watekaji walinichukua kwa nguvu, licha ya kelele na vuta nikuvute. sikusaidika na kulikuwa na bodaboda moja na watu wengine wakiangalia tukio lile likiendelea lakini hawakunisaidia.”

Nondo anaongeza kuwa walimuingiza kwenye gari na kuondoka naye. “Walinifunga kitambaa cheusi kwenye macho, kamba mikononi … walinisafirisha kwa mwendo huku nikipigwa na baadaye walininginiza mahali, miguu juu huku wakinipiga kwenye unyao wa miguu, walinipiga mgongo na mikononi,” anasimulia.

Aokotwa pembeni katika fukwe

Nondo anasema, “Nilitolewa na kubadilishwa kwenye gari nyingine… wakanifungua pingu, wakanifunga kamba na kuniingiza kwenye gari ndogo kutoka ‘hardtop’ kisha kunisukumiza kwenye fukwe hizo…Nilihisi upepo na mawimbi ya bahari.”

Anasema wakaondoka na ndipo alipopata msaada wa kwenda katika ofisi za chama hicho zilizopo Magomeni jijini Dar es salaam.

“Nilikuwa na hali mbaya, sikuweza kwenda nyumbani maana naishi mwenyewe hivyo salama yangu ilikuwa ni kwenda ofisini na ndipo nilipoletwa hospitalini,” anaeleza Nondo.

Aendelea kupata tiba

Watu wa karibu wa mwanasiasa huyo wameeleza kuwa atamlazimika kuendelea kupata huduma katika hospitali mpaka pale wataalamu watakapomruhusu kurejea nyumbani na kuendelea na shughuli zake.

ACT wataka haki kwa wale wanaodaiwa kutekwa

Chama cha ACT Wazalendo walizitaka mamlaka za Tanzania kuhakikisha wote waliotekwa wanaachiwa wakiwa salama

Akizungumza na vyombo vya habari jana jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu wa ngome ya vijana wa chama hicho, Ruqayya Nassir, "Tunataka watu wote waliotekwa na jeshi la polisi warudishwe salama na haya matukio yanayoendelea ya uvunjifu wa haki za binadamu yakome mara moja."

Ruqayya aliwataja na kusema, “ Tunataka majibu kamili kuhusu hatma ya vijana na wapambanaji wenzetu; ambao ni Deusdedit Soka, Adinan Hussein Mbezi, ⁠Dioniz Kipanya, Mlay, Mbise na wengine wengi ambao hatma zao hazifahamiki mpaka sasa."

Polisi waendelea na uchunguzi

Siku ya jana, jeshi la Polisi lilitoa taarifa ya tukio la kutekwa kwa Nondo na kwamba walikuwa wanachunguza kubaini wahusika kisha kuwachukulia hatua za kisheria.