Baada ya Rais Rajapaksa kukimbia, Ikulu ya Sri Lanka yageuka kivutio kisicho na mwenyewe cha utalii wa bure kwa Wasrilanka

Sri lanka

Rashmi Kavindhya anasema hakuwahi kuwa na ndoto ya kuingia ndani ya makazi rasmi ya rais wa Sri Lanka huko Colombo katika maisha yake.

Siku moja baada ya umati mkubwa wa watu kuingia katika moja ya majengo yaliyolindwa zaidi nchini humo, maelfu ya watu kama Bi Kavindhya wamejazana kama 'watalii' kuona jumba hilo ambalo picha zake zimesambaa sana kwenye mitandao.

Ni jumba lenye usanifu wa aina ya ukoloni ambalo kuna varanda kadhaa, vyumba vya mikutano na maeneo ya kuishi na bwawa kubwa la kuogelea.

Matukio makubwa ya Jumamosi yalimlazimu Rais Gotabaya Rajapaksa kukimbia.

"Angalia utajiri na utajiri wa mahali hapa," alisema Bi Kavindhya, ambaye alikuja na watoto wake wanne kwenye makazi ya rais.

"Tunaishi kijijini na nyumba yetu ni ndogo. Ikulu hii ni ya wananchi na imejengwa kwa fedha za watu."

Maelfu ya wanaume, wanawake na watoto walikuwa wakijaribu kuingia ndani ya boma na baadhi ya waandalizi wa maandamano hayo walikuwa wakidhibiti umati huo.

Polisi wa Sri Lanka na askari maalum walisimama tu kwenye kona na kutazama yote yanayoendelea kimya kimya.

Watu walipokuwa wakirandaranda kutoka chumba hadi chumba, kila mtu alitaka kujonea na wakati huo kupiga picha za 'selfie', mbele ya samani zilizonakshiwa kwa michoro mizuri za mbao, katika maeneo ya sebuleni.

Viti vilivyovunjwa, vioo vilivyovunjwa kutoka madirishani na vyungu vilikuwa vimetapakaa katika baadhi ya sehemu za majengo, kutokana na fujo na mkanganyiko huo mara baada ya umati wa watu kuingia ndani ya boma.

Sri lanka

"Ni ndoto kwangu kuona jumba kama hili," alisema AL Premawardene ambaye anafanya kazi katika bustani ya watoto katika mji wa Ganeamulla.

"Tunasubiri kwenye foleni ndefu kutafuta mafuta ya taa, gesi na chakula, lakini Rajapaksas walikuwa wakiishi maisha tofauti."

Viongozi wa waandamanaji tayari wamesema hawataondoka katika makazi rasmi ya Rais Rajapaksa na Waziri Mkuu Ranil Wickremesinghe hadi watakaondoka reasmi madarakani.

Sri lanka
Maelezo ya picha, Msururu wa umati wa watu wakijipanga kuingia Ikulu 'kushangaa'

Licha ya hatari ya mkanyagano huku umati wa watu ukisonga mbele kulitazama jengo hilo, askari waliokuwa na silaha nzito na maafisa maalum wa polisi walisimama nyuma huku watu waliojitolea kutoka katika vuguvugu la maandamano wakiwadhibiti wageni.

Bwawa la kuogelea lilivutia watu wengi. Familia kadhaa zilikuwa zimesimama karibu na bwawa lililojaa maji ya kahawia. Watazamaji walipiga makofi na kupiga kelele za shangwe wakati kijana mmoja aliporuka ndani ya maji ambapo waandamanaji walikuwa wamerekodiwa wakiogelea Jumamosi.

Sri lanka
Maelezo ya picha, Kila kona ya Ikulu kulionekana watu wakipiga picha za kumbukumbu

"Nina huzuni," alisema Nirosha Sudarshini Hutchinson, ambaye alikuwa akitembelea boma hilo pamoja na binti zake wawili matineja.

"Mtu aliyechaguliwa kuwa rais kwa njia ya kidemokrasia alilazimika kuondoka kwa njia ya aibu. Sasa tuna aibu kumpigia kura. Watu wanataka warudishe pesa walizoiba nchini."

Sri lanka

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Vijana wakufurahia kulala kwenye moja ya vitanda vya Ikulu

Moja ya sehemu maarufu zaidi ilionekana kuwa kivutio kwa wengi ni kitanda cha ambapo kundi la vijana walionekana kulala na kukikalia kwa shangwe.

Lugha kuu za kisiwa hicho, Kisinhala na Kitamil, pamoja na Kiingereza zilisikika kwenye korido za Ikulu.

Wengi walionekana kuwa na msisimko. Nje ya jumba hilo la kifahari lililopambwa, mamia ya watu - Wabudha, Wahindu na Wakristo - walikuwa wakizungukazunguka huku na huko.

Familia moja ilikuwa na sherehe yao ya kawaida waliifanyia Ikulu, ambapo isingewezekana wao kufanya hivyo saa 24 zilizopita.

Raia wa Sri Lanka wanahisi maandamano yao ya miezi kadhaa hatimaye yamesababisha kujizulu kwa viongozi wa nchi yao, ambao wanawalaumu kwa kuzorota kwa uchumi.

Mtazamo wa maisha ya viongozi wao unawafanya kuwa na hasira zaidi.