Biden akubali kuipa Ukraine mabomu ya kutegwa ardhini

th

Chanzo cha picha, Reuters

Muda wa kusoma: Dakika 3

Rais wa Marekani Joe Biden amekubali kuipa Ukraine mabomu ya kutegwa ardhini, afisa wa Marekani ameiambia BBC.

Afisa huyo ambaye alizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, anasema mabomu ya aina hiyo yatapelekwa hivi karibuni na Washington inatarajia yatatumika katika eneo la Ukraine.

Kyiv pia imeahidi kutotumia mabomu hayo katika maeneo yenye raia wa Ukraine, afisa huyo amesema.

Hatua hiyo inaonekana kama jaribio la kupunguza kasi ya wanajeshi wa Urusi ambao wamekuwa wakisonga mbele kwa kasi mashariki mwa Ukraine katika miezi ya hivi karibuni.

Unaweza Pia Kusoma

Utoaji wa mabomu ya ardhini ni hatua ya hivi punde zaidi ya utawala wa Marekani unaomaliza muda wake wa kuimarisha juhudi za vita vya Ukraine kabla ya Donald Trump kurejea Ikulu ya White House tarehe 20 Januari.

Urusi imeyatumiwa mabomu ya ardhini tangu kuanza kwa uvamizi wake kamili wa Ukraine mnamo Februari 2022 lakini pingamizi za kimataifa za utumiaji wa silaha hizo kwa misingi kwamba zinahatarisha raia zilizuia utawala wa Biden kuruhusu matumizi yake.

Afisa huyo wa ulinzi wa Marekani aliithibitishia BBC kwamba Ukraine iliahidi kutumia mabomu hayo kwa muda mfupi tu.

Hapo awali, ilithibitishwa kuwa makombora ya masafa marefu ya Mfumo wa Makombora ya Kijeshi (Atacms) yaliyotengenezwa na Marekani yalilenga shabaha ndani ya Urusi siku chache tu baada ya ripoti kuibuka kuwa Ikulu ya Marekani imetoa kibali cha matumizi yake.

TH

Chanzo cha picha, EPA

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wizara ya ulinzi ya Urusi ilisema kuwa shambulio hilo lilikuwa limelenga eneo la Bryansk linalopakana na Ukraine kaskazini siku ya Jumanne asubuhi.

Ilisema kuwa makombora matano yamedunguliwa na moja kusababisha uharibifu - huku vipande vyake vikiwasha moto katika kituo cha kijeshi.

Lakini maafisa wawili wa Marekani walisema dalili za awali zilionyesha kuwa Urusi ilinasa makombora mawili tu kati ya takriban manane yaliyorushwa na Ukraine.

BBC haijaweza kuthibitisha kwa njia huru takwimu zinazokinzana.

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov aliishutumu Washington kwa kujaribu kuzidisha mzozo huo.

Ikulu ya Kremlin imeapa kulipiza kisasi.

Siku ya Jumanne, Rais wa Urusi Vladimir Putin aliidhinisha mabadiliko katika sera za nyuklia ya Urusi, na kuweka masharti mapya ambayo nchi hiyo itazingatia kutumia silaha zake.

Sasa inasema shambulio kutoka kwa taifa lisilo la kinyuklia, ikiwa litaungwa mkono na nchi yenye nguvu za nyuklia, litachukuliwa kama shambulio la pamoja dhidi ya Urusi.

Akizungumzia mabadiliko hayo, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Matthew Miller alisema: "Tangu kuanza kwa vita vyake vya uchokozi dhidi ya Ukraine, [Urusi] imejaribu kuwalazimisha na kuwatia hofu Ukraine na nchi nyingine duniani kote kupitia matamshi na mienendo kuhusu matumizi ya silaha za nyuklia kwa njia isiyowajibika."