'Nilienda nyumbani kwa likizo ya Krismasi, lakini badala yake, 'nikakeketwa'

A photo of Catherine Meng’anyi

Chanzo cha picha, Catherine Meng’anyi

Maelezo ya picha, Catherine Meng'anyi
    • Author, Sandrine Lungumbu
    • Nafasi, BBC World Service
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Catherine Meng'anyi wakati huo akiwa na umri wa miaka kumi na miwili alienda nyumbani kwa likizo ya Krismasi na familia yake, kama ilivyokuwa kila mwaka, lakini safari hii ilibadilisha maisha yake milele.

Bila yeye kujua, wazazi wake walikuwa wamepanga kwamba afanyiwe "ukeketaji" na mhudumu wa afya katika eneo analotokea nchini Kenya.

Onyo: Simulizi hii inazungumzia kwa undani ukeketaji.

Kukua katika mji mkuu, Nairobi, Catherine alidhani alikuwa salama kutokana na baadhi ya mila na desturi za jadi zilizofanywa mijini na vijijini.

Anasema hakuwa anafikiria kwamba angekuwa miongoni mwa wasichana ambao wamepitia ukeketaji; Wazazi wake walikuwa wameelimika vizuri, waliishi na walifanya kazi mjini.

Hicho ndicho kilichotokea miaka 30 iliyopita.

"Wakati tunasafiri kwenda kijijini sikujua kwamba kuna kitu kama hicho kingeweza kutokea hadi nilipofika huko. Nakumbuka kulikuwa na uvumi kwamba kuna tafrija inaandaliwa."

Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef), zaidi ya wasichana na wanawake milioni 230 ulimwenguni kote wamekeketwa.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Umoja wa Mataifa inasema kuwa ingawa desturi hii bado inaendelea kutekelezwa katika nchi 30 za Afrika na Mashariki ya Kati, pia inafanyika katika nchi fulani za Asia na Amerika ya Latini, na miongoni mwa wahamiaji wanaoishi Ulaya Magharibi, Amerika Kaskazini, Australia na New Zealand.

Kinachojulikana kama "ukeketaji unaofanywa hospitalini" kinarejelea kukeketwa kwa kukusudia au kuondolewa kwa sehemu ya juu ya uke, utaratibu unaofanywa na madaktari au mtaalamu wa huduma ya afya.

Mara nyingi huwa ni kuondolewa kidogo au kukatwa kabisa kwa sehemu ya midomo ya shavu la uzazi na kibofu cha uke, na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) hueleza hilo kuwa "utaratibu unaoharibu viungo vya uzazi vya kike kwa sababu zisizo za kitiba".

"Ukeketaji unaofanywa hospitalini" mara nyingi huonekana kama njia salama ya kudumisha mila na desturi, licha ya kuwa hatari kwa afya ya kimwili, kisaikolojia na afya ya uzazi ya msichana, kwa sababu inafanywa na mtaalamu wa matibabu - lakini matumizi ya vifaa vya upasuaji inaweza kufanya uharibifu mkubwa.

''UKEKETAJI WA HOSPITALINI' UNAOFANYWA KOTE DUNIANI

  • Viwango vya juu vya ukeketaji unaofanywa hospitalini katika nchi tano: Misri (38%), Sudan (67%), Guinea (15%), Kenya (15%) na Nigeria (13%)
  • Afrika inachangia idadi kubwa ya visa hivi, na zaidi ya milioni 144.
  • Asia ifuatia na visa zaidi ya milioni 80, na milioni sita zaidi katika Mashariki ya Kati
  • Wanawake wengine milioni moja hadi mbili huathiriwa katika jamii ndogo zinazoendeleza desturi hii na nchi ambazo huingia wahamiaji katika maeneo mengine duniani

Chanzo: Unicef

Wazazi wa Catherine walichagua ukeketaji unaofanywa kitaalamu na walikuwa na mhudumu wa afya tayari.

"Imenichukua muda mrefu sana kupambana na [kumbukumbu] hii na kuwa imara kuzungumza juu ya suala hili kwa sababu inanikumbusha wakati nikiwa na umri wa miaka 12," anasema mwanamke, 42, ambaye kwa sasa ni muuguzi.

Siku kadhaa kabla ya kufanyika kwa utaratibu huo, Catherine aligundua kwamba alikuwa "atakeketwa". Lakini hakuelewa inamaanisha nini.

"Mialiko ilikuwa ikitumwa kwa marafiki na familia kwa sherehe," anakumbuka, "ilikuwa sherehe kubwa."

Siku chache baadaye, mhudumu wa afya alifika nyumbani kwao.

"Niliona wanawake wakinizunguka; wakiimba nyimbo na wenye furaha sana", anakumbuka.

"Kisha akalazimishwa kukaa chini.

"Mhudumu huyu wa afya alivaa glavu, akachukua kisu kinachotumika wakati wa upasuaji hospitalini huku wanawake wengine wakinishika.

"Unalia, unapiga mayowe. Lakini wanajaribu kukuzuia kupiga kelele yoyote kwa sababu wanaamini ukipiga kelele, wewe si mwamke jasiri.

"Nakumbuka vizuri nilitoka damu nyingi sana hadi wakanipaka dawa za kuzuia kutoka damu".

Baadaye, Catherine anakumbuka alikuwa amechanganyikiwa na kuwa "katika hali ya mshtuko".

"Msongo wa mawazo [bado] upo na hali ni mbaya hata kuliko kitu kingine chochote".

'Nilimjua, na nilimchukia'

Kwa Catherine, kuwa muuguzi ilikuwa njia ya kuhakikisha kuwa anachangia athari chanya kwa wasichana wadogo na wanawake katika jamii yake Kaunti ya Migori, kusini-magharibi mwa Kenya.

Sasa amekuwa mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza kwa miaka 20 na anafanya kazi kwa karibu na jamii zinazoshughulikia vurugu za kijinsia, pamoja na ukeketaji.

Pamoja na uuguzi, Catherine anafanya kazi kama mratibu wa masuala ya unyanyasaji wa kijinsia katika kaunti hiyo.

"Nilihisi ninaweza kusaidia kupunguza kile nilichokuwa nikiona katika jamii yangu. Kulikuwa na ujauzito mwingi miongoni mwa vijana, wasichana wadogo sana, na walikuwa wajawazito kwa msingi kwamba 'Wamekeketwa na sasa wako tayari kuwa kina mama"

Kwa miaka mingi, Catherine alikuwa anaenda kumwona mwanamke aliyemkeketa ambaye bado alikuwa akifanya kazi katika mji huohuo.

"Ni mwanamke niliyemjua, na kwa miaka mingi nilimchukia. Alikuwa na kliniki katika mojawapo ya miji hiyo. Kwangu, alikuwa mlinzi, lakini alibadilika kuwa mwenye kunidhuru. Na alijua vizuri sana kwamba hilo halikuwa na manufaa yoyote kwa afya yangu. Lakini bado alitekeleza kitendo hicho.

"Kulikuwa na wakati [ambapo] nilitaka sana kumkabili, lakini baada ya muda nikagundua nilipaswa kutulia kwanza ili moyo wangu upone," anaongeza.

A photo of Catherine Meng’anyi when she was younger with her mum.

Chanzo cha picha, Catherine Meng’anyi

Maelezo ya picha, Catherine (kulia) akiwa msichana mdogo pamoja na mama yake

Catherine anasema hajawahi kujadili kile kilichompata na wazazi wake "kwa sababu sitaki kufufa madonda ya zamani", lakini anasema mama yake sasa ni mmoja wa wafuasi wake wakubwa katika kazi yake ya kupinga ukeketaji.

Kenya ilipiga marufuku ukeketaji mnamo mwaka 2001 na kupigwa marufuku kabisa mnamo mwaka 2011.

Hata hivyo, ukeketaji ambao unahusishwa na desturi na tamaduni za jamii zingine, bado mila hii inaendelezwa.

'Ukeketaji unaofanywa hospitalini kimya kimya'

A street in Migori County, south-western Kenya

Chanzo cha picha, Catherine Meng’anyi

Maelezo ya picha, Katika kipindi cha miaka 30 iliyopita, idadi ya wasichana wenye umri wa kati ya miaka 15 na 19 nchini Kenya ambao wamehatarishwa kwa njia hiyo imepungua kwa zaidi ya nusu

Wakati Kenya imepiga marufuku ukeketaji, Catherine anasema kuna mwenendo ambao umejitokeza wenye kutia wasiwasi kwa sababu wanaokeketa wamegundua njia ambayo inafanya kuwa vigumu kwao kukamatwa.

Kijadi, sherehe za ukeketaji zingefanyika nyakati za asubuhi na kawaida ilikuwa kwa wasichana wenye umri wa miaka 10-12. Lakini sasa wasichana wadogo wenye umri wa miaka kama sita hivi, wanakeketwa tayari ili kuzuia kugunduliwa, anasema.

"[Kukeketwa hospitalini] kuna fanyika kimya kimya," anaelezea. "Inakuwa vigumu kupata data kwa sababu watu hawazungumzi tena kuhusu suala hili.

"Wanafanya ukeketaji na kujificha," anaongeza.

"Jamii zinazoendeleza ukeketaji zimegundua mbinu mpya. Wanawabaini wasichana wa kuwakeketa, lakini sasa wanawaficha.

"Utaratibu huo unafanya kwa haraka sana ili wasikamatwe, hivyo basi, wanaishia kusababisha madhara mengi. Wasichana wanakatwa vibaya, [ukiwachunguza], ni kama mtu aliyekuwa akifanya kitu kwa haraka."

Mnamo mwaka wa 2020, wastani wa wasichana na wanawake milioni 52 walikuwa wamepitia ukeketaji uliotekelezwa na wahudumu wa afya ulimwenguni kote - hiyo ni kwa kisa kimoja kati ya karibu vinne, UNICEF inasema.

Mnamo Aprili, WHO ilisasisha miongozo yake, kufuatia wasiwasi unaozunguka idadi inayoongezeka ya taratibu za matibabu za ukeketaji.

Utafiti unaonyesha kwamba inaweza kuwa hatari zaidi wakati utaratibu wa ukeketaji unafanywa na mhudumu wa afya, kwa sababu ya uwezekano wa kukatwa sana, WHO inasema.