Kwa nini Wamarekani weusi wanavutiwa kutafuta uraia Afrika?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Wedaeli Chibelushi
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Ingawa mababu zao walitekwa Afrika Magharibi na Kati karne kadhaa zilizopita, uhusiano kati ya Wamarekani Weusi na ardhi ya mababu zao umebaki imara.
Kwa mfano, Liberia, jamhuri kongwe zaidi barani Afrika, ilianzishwa mwaka 1822 na watumwa Wamarekani Weusi walioachiliwa huru. Baada ya uhuru wa Ghana mwaka 1957, wimbi la wasomi na wasanii waliondoka Marekani na kuishi huko.
Martin Luther King Jr., Malcolm X, na Muhammad Ali nao baadaye walifanya ziara nchini Ghana, huku Guinea ikiwa nyumbani kwa kiongozi wa Black Panther, Stokely Carmichael.
Katika miaka ya hivi karibuni uhusiano wa Wamarekani weusi na Afrika umeongezeka, hasa ukichochewa na matumizi ya vipimo vya DNA.
Watu mashuhuri kutoka Marekani wameomba uraia katika nchi za Kiafrika: mwimbaji Ciara alipata uraia wa Benin, rapa Ludacris na nyota wa filamu Samuel L. Jackson ni raia wa Gabon, waigizaji Meagan Good na Jonathan Majors ni raia wa Guinea, na nyota wa muziki Stevie Wonder ana urai wa Ghana.
Wiki iliyopita, mbunifu maarufu wa maudhui IShowSpeed alipata pasipoti ya Ghana baada ya kuzuru nchini humo wakati wa ziara yake barani Afrika.
Watu mashuhuri husafiri kuhudhuria sherehe za kupata uraia na kutembelea maeneo ya watalii, matukio hayo yote huonekana katika mitandao ya kijamii.
Baada ya kuchapisha picha za sherehe yake ya kupata uraia nchini Guinea, Meagan Good aliwaambia wafuasi wake milioni 7.8 wa Instagram mwezi uliopita: "Hii ni historia inayoendelea kuandikwa."
Good, ambaye ameigiza katika filamu kama vile Think Like A Man na Saw V, na mumewe Majors, aliyeigiza katika Creed na filamu ya Marvel ya Ant-Man and the Wasp, walipata uraia baada ya vipimo vya DNA kugundua asili yao ni Guinea.
"Utambuzi huu…ni kurudi kwenye mizizi yetu na kuungana tena na urithi wetu wa uzao wa Kiafrika," Good alisema.
Sera za kuwakaribisha
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ghana kwa miaka mingi imefungua mikono: Mtu yeyote ambaye mababu zake walitokea Afrika ana haki ya uraia wa Ghana, sera ambayo bila shaka imeihimiza Benin kuanzisha sera kama hiyo.
Ghana pia ilizindua "Mwaka wa Kurudi" mwaka 2019, mpango maarufu unalenga kuwatia moyo Waafrika walioko ughaibuni kuishi nchini humo.
Zaidi ya Wamarekani wenye asili ya Afrika 1,000 wamerudi katika muongo mmoja uliopita, kulingana na Dkt. Erieka Bennet, balozi wa Jukwaa la Waafrika wa Diaspora, ambalo huwasaidia watu kuishi Ghana.
Utalii ni sababu ya nyingine ya sera kama hizi. Serikali zinatumai kwamba machapisho kwenye mitandao ya kijamii kutoka kwa watu mashuhuri yatawatia moyo Wamarekani wengine wenye asili ya Afrika, kutembelea nchi hizo na kuwekeza.
Utangazaji chanya unaotokana na nyota kama vile Ciara unaweza pia kuwatia moyo wanachama wa diaspora kuwekeza au kununua mali isiyohamishika nchini Benin, kama walivyofanya nchini Ghana tangu mwaka wa kurudi kutangazwa.
Kwa kutangaza tamaduni wao na kujenga mtandao imara kote ulimwenguni, nchi kama vile Benin, Guinea, Gabon na Ghana zina kila kitu katika suala la ushawishi wa kimataifa.
Katika misheni hii, raia maarufu huchukua jukumu la kuwa mabalozi, anaelezea Francis Kpatindé, profesa kutoka Benin katika Chuo Kikuu cha Sciences Po nchini Ufaransa.
Faida za kiuchumi

Chanzo cha picha, Getty Images
Wakazi wengi wa nchi husika wanatambua faida za kiuchumi na kisiasa za kuwapa uraia watu mashuhuri kutoka Marekani, lakini wengine wanakosoa.
Kuna hisia kwamba watu mashuhuri hawapitii kile kinachoelezwa na watu waliozaliwa katika nchi hizi; mchakato unaochosha na wa gharama kubwa wa kupata pasipoti.
Taufic Suleman, mchoraji na mpambaji kutoka Ghana, "alikasirika" wakati Waziri wa Mambo ya Nje alipotangaza kwamba IShowSpeed, ambaye alikulia Marekani lakini mama yake ni Mghana, amepewa pasipoti.
Kufuatia tangazo la Waziri wa Mambo ya Nje, Patrick Boamah, mjumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Ghana, alikiambia kituo cha televisheni cha Channel One kwamba IShowSpeed alipaswa kufuata taratibu za kisheria zinazohitajika ili kupata pasipoti, ingawa serikali "inaweza kumpa nafuu fulani."
Sindé Chekete, mkurugenzi wa Ofisi ya Utalii ya Benin, aliiambia BBC "maombi ya uraia hayaathiriwi na hadhi ya mtu" kwani Ciara "alifuata utaratibu sawa na mwombaji mwingine yeyote."
Itachukua muda kwa Ghana, Gabon, Guinea na Benin kutathmini kama mikakati yao imefanikiwa, labda muongo mmoja au miwili baadaye.
Mwanzoni mwa wiki, serikali ya Benin ilitangaza kuundwa kwa shirika la serikali lililojitolea kwa ajili ya kuwapa uraia "watu wenye asili ya Afrika."
Hata hivyo, Ghana imekumbana na kikwazo katika mipango yake, ikitangaza inasimamisha maombi ya uraia ili kufanya mfumo huo upatikane kwa urahisi zaidi na rahisi kutumia.
Kwa vyovyote vile, Kpatindé anaamini kuwakaribisha watu mashuhuri wanaoishi nje ya nchi, nchi za Afrika ziko kwenye njia sahihi.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi












