Nagorno Karabakh: Mambo 5 ya kuyajua kuhusu mgogoro wa tangu enzi ya Soviet

fdvc

Chanzo cha picha, REUTERS

Baada ya saaa 24 tangu jeshi la Azerbaijan kuanzisha mashambulizi huko Nagorno-Karabakh, wapiganaji wanaotaka kujitenga wa Armenia wamekubali masharti ya usitishaji mapigano yaliyopendekezwa na Urusi.

Kwa miaka mingi eneo limekuwa na mvutano na katika miezi ya hivi karibuni mvutano umeongezeka juu ya udhibiti wa eneo linalotaka kujitenga, linalotambulika kimataifa kama sehemu ya Azabajani na nyumbani kwa takriban watu 120,000 wanaojitambulisha kuwa Waarmenia.

Usitishaji wa mapigano kati ya pande hizo mbili ulivunjwa Jumanne hii, na Wizara ya Ulinzi ya Azerbaijan kuanzisha operesheni za "kupambana na ugaidi" katika maeneo ya mkoa huo na kuwataka viongozi wa Armenia wanaotaka kujitenga kujisalimisha.

"Ili operesheni za kupambana na ugaidi zikome, makundi haramu ya kijeshi ya Armenia lazima yanyanyue bendera nyeupe, silaha zote lazima zisalimishwe na utawala haramu lazima uvunjwe," Wizara ya Ulinzi ilisema. "Vinginevyo, hatua za kupambana na ugaidi zitaendelea hadi mwisho."

Azerbaijan ilisema kuwa imeanzisha operesheni hiyo baada ya vifo vya watu sita, wakiwemo maafisa wanne wa polisi, katika milipuko miwili ya mabomu ya ardhini Jumanne asubuhi.

Katika jiji kuu la Karabakh, Khankendi (unaojulika kama Stepanakert kwa Waarmenia), ving'ora vya ulinzi wa anga na mabomu vilisikika.

Wawakilishi wa Armenia walisema mashambulizi makubwa ya kijeshi yalisababisha vifo kadhaa, ikiwa ni pamoja na wanawake na watoto, ingawa Azerbaijan ilikanusha kuwa iliwalenga raia.

Azerbaijan na Armenia zimeingia vitani mara mbili juu ya mzozo wa Nagorno-Karabakh. Mara ya kwanza ni mapema 1990, baada ya kuanguka kwa Umoja wa Kisovieti. Mara ya pili ni 2020.

Miaka mitatu iliyopita, Azerbaijan ilinyakua maeneo mengine ndani na karibu na Karabakh ambayo yalikuwa yakishikiliwa na Armenia tangu 1994.

Yote yalianzaje?

dxs

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Wakaazi wa eneo hilo wameathirika sana na mgogoro huo kwa kukosa huduma za msingi kama chakula
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Eneo la milima la Nagorno Karabakh, ni la takriban kilomita za mraba 11,500 lenye wakaazi wengi wa Waarmenia ambao wanaungwa mkono na Armenia. Ni eneo lenye mzozo kwa miongo kadhaa.

1988, kuelekea mwisho wa utawala wa Kisovieti, vikosi vya Azerbaijani na waasi wa Armenia walianza vita vya umwagaji damu - kati ya watu 20,000 na 30,000 walifariki, baada ya bunge la mkoa wa Nagorno-Karabakh kupiga kura ya kuwa sehemu ya Armenia.

Kisha Azerbaijan ilijaribu kukandamiza harakati ya kujitenga, wakati Waarmenia ikiziunga mkono. Hii ilizua mapigano ya kikabila na baada ya Armenia na Azerbaijan kutangaza uhuru kutoka Moscow, vita kamili vikaanza.

Vita vya kwanza vilimalizika kwa usitishaji mapigano uliosimamiwa na Urusi 1994, baada ya vikosi vya Armenia kuchukua udhibiti wa eneo hilo na maeneo ya karibu.

Chini ya makubaliano hayo, eneo hilo lilibakia kuwa sehemu ya Azabajani, lakini tangu wakati huo limekuwa likitawaliwa na makundi ya wanaotaka kujitenga kutoka jamii ya Waarmenia na kuungwa mkono na serikali ya Armenia.

Sovieti ilivyoweka mipaka

az\

Chanzo cha picha, ICTIMAI TV

Maelezo ya picha, Ni vigumu kwa vyombo vya habari kufika eneo hilo jambo linalofanya ukweli wa kinachoendelea kutojuulikana kwa undani

Armenia na Azabajani ya kisasa tunayoijua leo iliunganishwa katika Muungano wa Jamhuri za Kisoshalisti za Kisovieti (USSR) ilipoanzishwa mwaka wa 1920.

Nagorno Karabakh, pia inajulikana kama Upper Karabakh, ni eneo lenye watu wengi wa kabila la Waarmenia, lakini 1923 Wasovieti walikabidhi udhibiti wake kwa mamlaka ya Kiazabajani na ikaundwa kama eneo linalojitawala ndani ya Jamhuri ya Kisovieti ya Azabajani.

Nogorno Karabakh inakaliwa na makumi ya maelfu ya Waarmenia. Kwao, eneo hili ni sehemu ya Armenia.

Kwa mujibu wa na Paulo Botta, mtaalam wa Mashariki ya Kati katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Argentina, aina hii ya mpaka ilikuwa ni kawaida katika USSR ili kueka usawa katika jamhuri zake zote.

Wazo hili linaelezwa na wachambuzi kama vile mwanahistoria wa Uingereza Simon Sebag Montefiore, ambaye katika makala ya The New York Times wakati huo alisema, "Stalin alianzisha mishei ya ufalme wa watu wa Kirusi na kuunda USSR kwa kutumia ujuzi wake wa migogoro ya kikabila katika ili kuunda jamhuri ndani ya jamhuri."

Mtindo huu wa mipaka umeleta migogoro kadhaa ya kikabila na kisiasa ambayo ilitokea baada ya kuvunjika kwa USSR, kama vile vita vya Chechen vya miaka ya 1990, vita vya Georgia 2008 na vile vya Armenia na Azabajani.

Mtaalamu wa siasa za kimataifa Dahlia Scheindlin anaeleza:

"Wakati wa kuvunjika kwa USSR, kulikuwa na migogoro kadhaa ya kikabila na hiyo ilitokana na kwamba ilikuwa himaya kubwa na yenye kupanuka, yenye makundi mengi ya makabila mbalimbali.

USSR ilikuwa na sera ya kujaribu kubadilisha idadi ya watu wa eneo fulani kwa kupeleka watu wa makabila ya Kirusi kuishi huko," anaeleza.

"Majaribio haya yote ya kuunda utambulisho wa kitaifa kwa miaka mingi yalisababisha uasi mara tu USSR ilipoanguka."

Nini kilitokea 2020?

ewsd

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Mvutano wa Armeni na Azerbaijani umesababisha vifo vya maelfu ya watu

Hali imekuwa tete kwa miaka mingi, huku matukio ya mapigano yakitokea hapa na pale. Mapigano makubwa zaidi ya kijeshi tangu mwanzoni mwa miaka ya 1990 yalitokea miaka mitatu iliyopita, wiki sita za mapigano makali.

Azerbaijan ilirejesha eneo lake na pande zote mbili zilikubali kutia saini mkataba wa amani uliosimamiwa na Urusi Novemba 2020. Azerbaijan iliteka tena maeneo yote yanayozunguka Nagorno -Karabakh.

Chini ya makubaliano hayo, vikosi vya Armenia vililazimika kuondoka katika maeneo hayo na tangu wakati huo vimabaki katika sehemu ndogo ya eneo hilo.

Jukumu la Urusi na Türkiye

dx

Mamlaka za kikanda zimehusika sana katika mzozo kwa miaka mingi. Mwanachama wa NATO Uturuki ilikuwa taifa la kwanza kutambua uhuru wa Azerbaijan mwaka 1991 na imesalia kuwa muungaji mkono mkubwa wa nchi hiyo.

Ndege zisizo na rubani za Bayraktar zilizotengenezwa Uturuki zinasemekana kuwa na jukumu muhimu katika mapigano ya 2020, kuruhusu Azerbaijan kutwaa eneo hilo.

Armenia kwa upande wake kwa jadi imedumisha uhusiano mzuri na Urusi. Kuna kambi ya kijeshi ya Urusi nchini Armenia, na wote wawili ni wanachama wa Muungano wa Kijeshi wa mataifa sita ya zamani ya Soviet (CSTO).

Lakini uhusiano kati ya Armenia na Urusi umedorora tangu Nikol Pashinyan, ambaye aliongoza maandamano makubwa dhidi ya serikali 2018, kuwa waziri mkuu wa Armenia.

Hivi karibuni alisema kuwa utegemezi wa Armenia kwa Urusi kama chanzo cha usalama ulikuwa "kosa la kimkakati."

Armenia ilitangaza mwezi huu kwamba itakuwa mwenyeji wa mazoezi ya pamoja na vikosi vya Marekani, ambavyo vilikosolewa na Moscow kama "hatua zisizo za kirafiki."

Rais Vladimir Putin alikanusha kuwa Armenia imevunja muungano wake na Urusi, lakini akatangaza kwamba Yerevan, mji mkuu wa Armenia, kimsingi umetambua mamlaka ya Azerbaijan juu ya eneo la Nagorno-Karabakh.

"Ikiwa Armenia yenyewe imetambua kwamba Karabakh ni sehemu ya Azerbaijan, tufanye nini?" Putin alisema wakati wa kongamano la kiuchumi huko Vladivostok.

Kipi kifuatacho?

wsqx

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Mgogoro kati ya Armenia and Azerbaijani ulishika kasi mwishoni mwa miaka 1980

Rais wa Azerbaijan Ilham Aliyev ametishia mara kwa mara katika siku za nyuma kutwaa tena eneo lote la Nagorno-Karabakh kwa nguvu, ikiwa itabidi.

Mwaka 2019, Pashinyan aliambia umati wa Waarmenia waliokusanyika katika jiji kuu la Karabakh kwamba "Artsakh ni Armenia." Artsakh ni jina la Kiarmenia la Nagorno Karabakh.

Mataifa mengi yanaangalia eneo hili kwa woga kwamba vita vingine vinaweza kutokea kwenye eneo la zamani la Soviet pamoja na vile vya Ukraine.

Ulaya inataka kudumisha amani nchini Azerbaijan, ambapo inasafirisha gesi ya mita za ujazo bilioni 8 kwa mwaka baada ya kupata hasara ya usambazaji wa gesi kutoka Urusi kutokana na mzozo na Ukraine.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ilisema Jumanne kwamba ilikuwa imearifiwa kuhusu mashambulizi ya Azerbaijan dakika chache kabla na kuzitaka nchi zote mbili kuheshimu usitishaji vita uliotiwa saini baada ya vita mwaka 2020.

Mwakilishi maalum wa kikand wa Umoja wa Ulaya, Toivo Klaar alisema kuna "haja ya dharura ya kusitishwa kwa mapigano mara moja."