Miji ya Ulaya inayogawa kuku bure kwa wananchi

trfgv

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 5

Miji nchini Ufaransa na Ubelgiji imekuwa ikitoa kuku bure kwa miaka mingi ili kukabiliana na upotevu wa chakula. Karibu na Pasaka mwaka 2015, mji wa Ufaransa wa Colmar ulianza kutoa kuku bure kwa wakaazi wake.

Lengo la mpango huu uliokuwa wa majaribio, uliozinduliwa na idara ya ukusanyaji taka katika mji wa kaskazini mashariki mwa Ufaransa, ilikuwa kupunguza upotevu wa chakula.

Mradi huo umefanya kazi. Meya wa wakati huo wa mji wa Colmar Agglomération, Gilbert Meyer, alikuwa amechaguliwa tena mwaka 2014 chini ya kauli mbiu "familia moja, kuku mmoja."

Mwaka uliofuata operesheni hiyo ilianzishwa, kwa ushirikiano na mashamba mawili ya ufugaji kuku yaliyo karibu. Zaidi ya nyumba 200 katika manispaa nne zilijiandikisha na kupewa kuku wawili kila moja.

Kila kaya ilitia saini ahadi ya ufugaji wa kuku, kwa maelewano kwamba idara ya taka inaweza kufanya ukaguzi wa maeneo ya kuku hao wakati wowote. Vibanda vya kuku havikutolewa, ilikuwa juu ya wakazi kujenga au kununua. Idara ilihakikisha kila kibanda kina nafasi ya kutosha kwa kuku - kati ya 8 na 10 sq m (86 na 108 sq ft).

"Mpango huo ulifanikiwa - na bado unaendelea. Manispaa nyingine zilijiunga na mpango huo 2022. Na kwa sasa manispaa zote 20 za mji huo zinashiriki," anasema Eric Straumann, meya wa sasa wa Colmar Agglomération.

Kufikia sasa, kuku 5,282 wamesambazwa kwa wakazi wa eneo hilo, na maombi yamefunguliwa kwa awamu inayofuata ya usambazaji kuku kuanzia Juni 2025. Sio tu kwamba wakazi wamepata mayai ya bure, pia taka za chakula zimepungua katika dampo kwani kuku wanalishwa mabaki ya jikoni ya chakula ambayo yangetupwa.

"Kuku ana wastani wa umri wa kuishi wa miaka minne na hula kwa wastani wa gramu 150 (5.3oz) kwa siku, tunakadiria kuwa tumeepuka tani 273.35 za takataka [tangu 2015]," anasema Straumann.

Pia unaweza kusoma

Athari ya taka za chakula

df

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mji wa Ufaransa wa Colmar umekuwa ukitoa kuku bure kwa wakaazi wake tangu 2015
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Taka za chakula huchangia uzalishaji zaidi wa methane kwenye angahewa kuliko taka nyingine yoyote inayotupwa, kutokana na kasi yake ya kuoza. Nchini Marekani, karibu 58% ya uzalishaji wa gesi ya methane kwenye angahewa ni kutoka kwenye dampo za taka za chakula.

Ingawa gesi hiyo hubaki kwa muda mfupi katika angahewa kuliko kaboni dioksidi (CO2), lakini imekuwa na athari ya kuongeza joto duniani kwa zaidi ya mara 80 kuliko CO2 katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.

Takribani theluthi moja ya chakula kinachozalishwa kwa ajili ya binadamu kinapotea duniani kote, kiasi cha tani bilioni 1.3 kwa mwaka. Taka za chakula husababisha 8-10% ya uzalishaji wa kila mwaka wa gesi chafu duniani - ambayo ni karibu mara tano ya uzalishaji jumla kwa sekta ya anga.

Ingawa wamiliki wa kuku nchini Uingereza wameshauriwa kuepuka kuwalisha mabaki ya chakula cha jikoni kutokana na wasiwasi kuhusu kueneza magonjwa, ni halali kabisa kufanya hivyo mahali pengine duniani, na hilo linaweza kupunguza upotevu wa chakula.

Colmar sio mji pekee uliosambaza kuku bure - wala haukuwa wa kwanza kufanya hivyo. Mwaka 2012 katika mji mwingine mdogo wa kaskazini-magharibi wa Ufaransa unaoitwa Pincé, kuku wawili walitolewa kwa kila kaya ili kusaidia kupunguza taka. Jumla ya familia 31 zilipewa kuku, pamoja na mfuko wa chakula cha kuku.

Nchini Ubelgiji, kuku wa bure wametolewa katika miji ya Mouscron na Antwerp na jimbo la Limburg. Zaidi ya familia 2,500 zilikubali kupokea kuku katika mwaka mmoja pekee huko Limburg, kulingana na ripoti.

Huko Mouscron, jozi 50 za kuku zilitolewa katika duru ya pili ya mpango huo, baada ya mpango wa awali kufanikiwa. Wakazi ambao walipaswa kuthibitisha kuwa wana eneo la kutosha katika bustani zao ili kufuga kuku, walipewa mafunzo juu ya ufugaji wa kuku.

Mpango huo unaonekana kuwa wazo zuri, haswa katika sehemu ambazo mayai ni haba au ghali sana. Mfano California au New York, dazeni ya mayai hugharimu karibu dola za kimarekani 9 (£7). Kwa vile baadhi ya kuku wanaweza kutaga hadi mayai 300 kila mwaka, kuku mmoja anaweza kutaga hadi mayai yenye thamani ya dola 225 (£178) kila mwaka.

Mashaka kwa baadhi

erdf

Chanzo cha picha, Alamy

Maelezo ya picha, Mpango huo umewafanya wakazi wa Colmar kuwa na mayai ya kutosha tangu 2015

Lakini Paul Behrens, profesa katika Chuo Kikuu cha Oxford anasema kuna changamoto: "Nina uhakika mpango huo unaweza kufanywa nchini Uingereza lakini sina uhakika ikiwa ni wazo zuri," anasema. "Homa ya mafua ya ndege ni wasiwasi unaoendelea kila wakati."

"Mpango huu hauwezi kufanya kazi vizuri nchini Marekani pia," anasema Mark Bomford, mkurugenzi wa mpango endelevu wa chakula katika Chuo Kikuu cha Yale.

Marekani kwa sasa inakabiliwa na uhaba wa mayai kutokana na mlipuko wa homa ya mafua ya ndege - na kwa sababu hiyo bei ya mayai imepanda kwa asilimia 36 ikilinganishwa na 2023.

"Lakini kutoa kuku bure halitokuwa jibu linalofaa," anasema Bomford.

"Mfumuko mkali wa bei kwa bidhaa kama mayai unawaumiza maskini zaidi kuliko kuwaumiza matajiri. Ili kutunza kuku unahitaji chakula, maji, nyumba, nafasi na muda wa ziada," anasema.

"Watu wengi wenye kipato cha chini hawana uwezo wa kupata vitu hivi. Ukizingatia gharama zote hizo, kuku hawezi tena kuwa bure," anahitimisha.