Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, utumiaji wa pilipili kali unaweza kuleta madhara kwa afya?
- Author, Jessica Brown
- Nafasi, BBC
Tambi za Asia Mashariki zimepigwa marufuku katika baadhi ya nchi za Ulaya kwa kuwa na pilipili nyingi. Je, chakula hicho kinaweza kuwa na hatari kwa afya?
Tambi kutoka Korea Kusini ziligonga vichwa vya habari hivi karibuni, wakati mamlaka ya chakula ya Denmark, ilipoeleza hatari inayoweza kusababishwa na chakula hicho.
Habari nyingine iliyozua vichwa vya habari ni kisa cha kijana mmoja nchini Marekani, ambaye alikufa baada ya kushiriki katika shindano la kula chakula chenye pilipili kali.
Mamlaka ya Viwango vya Chakula nchini Uingereza hauruhusu wazalishaji wa chakula kuongeza pilipili halisi kwenye vyakula, kwani huchukuliwa kuwa si salama.
Ingawa hakuna kikomo juu ya kiasi cha kutumia, inapokuwa kwenye mkebe kutoka kiwandani.
Pilipili inaweza kuleta madhara gani?
Denmark sio nchi ya kwanza kuonya dhidi ya kula chakula kilicho na viwango vya juu vya pilipili. Taasisi ya Kutathmini Hatari nchini Ujerumani (BfR), pia imeonya dhidi ya matumizi ya kupindukia ya pilipili.
“Tafiti zinaonyesha ulaji mwingi wa pilipili unaweza kusababisha kiungulia, tumbo kuchoma, kichefuchefu, kuhara na maumivu kwenye tumbo na kifua,” inasema taasisi ya BfR.
“Inaweza pia kusababisha joto na baridi kwa wakati mmoja, mabadiliko ya shinikizo la damu au kizunguzungu. Lakini bado hakuna taarifa za kutosha kufafanua ni kiwango gani hasa cha matumizi ya pilipili kinaweza kusababisha hayo kutokea.”
"Kwa sababu athari ya pilipili inaweza kutokea kwa viwango tofauti vya matumizi, kutoka mtu mmoja na mwingine, hivyo hakuna kipimo cha uhakika cha kujua ni kiwango gani kina athari kwa afya kwa watu wasio na uzio," anasema msemaji wa BfR.
Ila kulingana na taarifa kutoka BfR, makadirio ya ulaji unaoweza kuleta athari ni miligramu 0.5 hadi 1 au zaidi, inaweza kusababisha athari, kama vile hisia ya joto, shinikizo kwenye tumbo au kiungulia.
Na makadirio mengine yanaweka kiwango hatari cha pilipili kwa binadamu ni miligramu 500-5,000 kwa kila kilo ya uzito wa mwili. Hii ni sawa na karibu miligramu 35,000 za pilipili kwa mtu mwenye uzani wa kilogramu 70.
"Ulaji wa kuanzia miligramu 170, kuna athari mbaya zinaweza kutokea. Kuna kesi ya mtu kulazwa hospitalini baada ya kumeza takribani miligramu 600 za pilipili," BfR inasema.
Mtu huyo mwenye umri wa miaka 27, alikuwa akishiriki shindano la kula pilipili huko Berlin, Ujerumani, alikula pilipili hoho nne na vyakula vingine vyenye pilipili.
Saa mbili na nusu baada ya kula chakula, alianza kuhisi maumivu makali ya tumbo na uvimbe kwenye tumbo, na jioni alikwenda katika Hospitali ya Helios Berlin-Buch.
Madaktari walimnywesha dawa za kutuliza maumivu. Baada ya saa 12 tangu ale pilipili, alitapika na hali yake ikaanza kukaa sawa.
Pilipili inaweza kuuwa?
"Pilipili inaweza kusababisha muwasho, usumbufu na maumivu," anasema Christian Moro, profesa wa sayansi ya dawa katika Chuo Kikuu cha Bond huko Australia.
"Ikiingia kwenye jicho, inaweza kuuma sana, na kusababisha uoni hafifu. Ukipaaliwa, inaweza kusababisha kukohoa kwa muda mrefu, na hata kuchochea magonjwa kama vile pumu."
“Lakini athari ndogo ndogo za pilipili, kama kuwasha hazipaswi kuleta wasiwasi,” anasema Moro.
"Pilipili huamsha mishipa yetu na hii ndiyo sababu ya kuhisi kama mwili wako unaungua, lakini ni hisia tu, na haituletei madhara yoyote," anafafanua.
"Nimeulizwa mara nyingi: Je, kula pilipili kunauwa?' Jibu, ni 'ndiyo na hapana'," anasema Paul Bosland, profesa wa sayansi ya mimea na mazingira chuo Kikuu cha New Mexico.
"Pilipili inaweza kusababisha kifo, lakini miili ya watu wengi itadhoofika sana kabla ya kufikia hatua hiyo. Kwa maneno mengine, miili yetu itatoa chakula chenye pilipili kabla hatujatumia kiasi cha kutosha cha kutuuwa.
"Utalazimika kuendelea kula pilipili mara nyingi, kupita kiwango cha kutokwa na jasho, kutetemeka, kutapika, na kuhisi kuzimia. Kwa hivyo, pilipili haiuwi," anasema.
Baadhi yetu wana kinga dhidi ya hatari hizo?
Kama ilivyo kwa vyakula na vinywaji vyote, mwili wa mtu mmoja hutofautiana na mwili wa mtu mwingine katika kujibu, na hilo linaweza kusababishwa na mambo kadhaa.
“Kutumia pilipili kunaweza kusababisha majibu tofauti kwa watu tofauti,” BfR inasema – “kwa mfano, watoto au watu ambao mara chache hula chakula chenye pilipili, wanaweza kuwa hatarini zaidi kuliko watu wanaotumia pilipili mara kwa mara.”
Utafiti mmoja uligundua pilipili inaweza kuleta shida kwa watu walio na shida ya tumbo. Watafiti waliwalisha watu 20 wenye shida ya tumbo, na watu 38 wenye afya nzuri bila shida yoyote ya tumbo, chakula cha kawaida, chakula chenye pilipili, au mlo wa kawaida na gramu 2 za pilipili za vidonge.
Watu wenye afya njema, milo ya pilipili na milo yenye vidonge vya pilipili ilisababisha usumbufu mdogo tu wa tumbo, lakini ilisababisha kiwango kikubwa cha maumivu ya tumbo na kuungua, kwa wale walio na matatizo mbalimbai ya tumbo.
BfR inasema, pilipili inaweza pia kuwa hatari kwa watu walio na magonjwa ya moyo, kwa sababu ya kuathiri mzunguko wa damu, ikiwa utaila kupita kiasi.
“Madhara ya kula pilipili pia yanaweza kuathiriwa na jinsi mtu anavyozoea kula vyakula vya pilipili,” anasema Bosland.
"Kila binadamu ana kiwango tofauti cha uvumilivu wa pilipili, kiwango kinachoweza kuonekana kikubwa kwa mtu mmoja, kinaweza kuonekana cha wastani kwa mwingine," anasema Bosland.
Faida za kiafya
Utafiti mmoja nchini Tawain, uligundua kutumia pilipili mara kwa mara kunaweza kupunguza hatari ya kupata kiungulia kadiri mwili unavyostahimili zaidi.
Katika historia, pilipili zimetumika kama tiba ya afya, na dawa ya kisasa zina tumia pilipili pia. Pilipili hutumiwa katika uundaji wa dawa nyingi, pamoja na bidhaa za kutuliza maumivu, kipandauso, maumivu ya kichwa na matatizo ya ngozi.
Fauka ya hayo, pilipili imependekezwa na watafiti kama dawa ya kuzuia na kutibu saratani ya tumbo.
Pamoja na wasiwasi kuhusu athari mbaya za pilipili, tafiti nyingi zimegundua utumiaji wa pilipili mara kwa mara, una faida kiafya, kutokana na misombo yake ya kupambana na magonjwa na kuboresha afya.
Uchunguzi kuhusu matumizi ya mara kwa mara ya pilipili, unasema huchangia kupunguza shinikizo la damu, ugonjwa wa moyo na unene.
Ingawa wakati mwingine hufikiriwa kusababisha vidonda vya tumbo, kuna ushahidi kuwa matumizi ya pilipili yanaweza kusaidia kuvizuia na kuponya.
Hakuna ushahidi kwamba kiasi kinachofaa cha pilipili katika mlo wetu kitatuletea madhara yoyote zaidi ya hisia ya kawaida ya kuwasha.
Lakini swali moja limebaki: Je, ni China au India ambayo ina chakula chenye pilipili zaidi? Jibu, litaendelea kuwa mjadala.
End of Pia unaweza kusoma
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah