Jinsi Urusi inavyojaribu kimya kimya kujishindia ushawishi ulimwenguni zaidi ya Magharibi

Kwa kawaida Javier Gallardo hupenda kuanza asubuhi yake kwa kutazama kipindi cha muziki wa zamani (au zilipendwa) kwenye televisheni , ambao ni sehemu ya utaratibu wake ambao humuweka katika hali nzuri siku moja kabla ya kwenda katika kazi yake kama dereva wa lori.
Lakini Jumatatu moja mnamo mwezi waJuni, alifungua televisheni na, badala ya muziki, skrini ikuwa imejaa picha za eneo la vita. Ripoti ya habari ilikuwa ikicheza kwenye chaneli ambayo hajawahi kuisikia.
"Ni nini kinatokea?" alijiuliza. Baada ya dakika 20, aliizima. "Sikuweza kuielewa."
Nembo ya kijani kwenye kona ya chini ya skrini ilionyesha herufi: "RT". Kutafuta mtandaoni, aligundua kuwa hii ilikuwa chaneli ya televisheni ya Kirusi.
Javier anaishi Chile. Inadaiwa kuwa Telecanal, chaneli ya televisheni inayomilikiwa na watu binafsi nchini humo, imekabidhi mawimbi yake kwa shirika la habari la Urusi RT, lililokuwa Urusi Today.

Chanzo cha picha, YURI KADOBNOV/AFP via Getty ImagesY
Taasisi ya udhibiti wa matangazo na utangazaji nchini amefungua kesi za vikwazo dhidi ya Telecanal kwa uwezekano wa ukiukaji wa sheria ya utangazaji, na anasubiri majibu ya kituo hicho.
Telecanal haikujibu ombi la kutoa maoni kuhusu madai hayo.
Watazamaji, wakati huo huo, waliachwa wamechanganyikiwa.
"Nilikasirika," anasema Javier. "Hawakutangaza chochote kabla, na sikuweza kuelewa ni kwa nini."
Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, chaneli ya habari inayoungwa mkono na serikali ya Urusi RT na wakala wa habari na redio Sputnik, wamepanua uwepo wao kimataifa; kati yao, sasa wanatangaza kote Afrika, Balkan, Mashariki ya Kati, Asia ya Kusini na Amerika Kusini.
Haya yote yanaambatana na umarufuku katika nchi za Magharibi.

Chanzo cha picha, Kirill KUDRYAVTSEV / AFP
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kufuatia uvamizi kamili wa Urusi nchini Ukraine mnamo Februari 2022, vizuizi vikali viliwekwa kwa utangazaji wa RT nchini Marekani, Uingereza, Canada na kote katika Umoja wa Ulaya - pamoja na makampuni makubwa ya teknolojia - kwa kueneza habari zisizofaa kuhusu vita.
Hatua hiyo ilifikia kilele chake mwaka wa 2024, wakati mamlaka ya Marekani ilipowatuhumu watendaji wa RT - ikiwa ni pamoja na mhariri wake mkuu Margarita Simonyan - kwa madai ya majaribio ya kuharibu "imani ya umma" katika taasisi za nchi.
Hii ilikuja huku kukiwa na shutuma za Kremlin kuandaa kampeni iliyoenea ya kuingilia uchaguzi wa rais. RT ilikanusha kuhusika.
Bado mahali pengine, ushawishi wa RT umepanuka tu.
Tangu 2023, RT imefungua ofisi nchini Algeria, ilizindua huduma ya TV katika lugha ya Kiserbia, na kuanzisha programu za mafunzo bila malipo zinazolenga wanahabari kutoka Afrika, Kusini-mashariki mwa Asia, India na Uchina.
Taasisi hiyo ya utangazaji pia imetangaza kuwa itafungua ofisi nchini India. Sputnik, wakati huo huo, ilizindua chumba cha habari nchini Ethiopia mnamo mwezi wa Februari.
Haya yote yanaambatana na kudhoofika kwa vyombo vya habari vya Magharibi katika baadhi ya maeneo ya dunia. Kutokana na kupungua kwa bajeti na kubadilisha vipaumbele vya sera za kigeni, vyombo fulani vimepunguza ukubwa na hata kujiondoa kutoka sehemu za dunia.
Miaka miwili iliyopita, BBC ilifunga huduma yake ya redio ya Kiarabu kwa kupendelea huduma yake ya kidijitali - ambayo hutoa sauti, video na habari zinazotegemea maandishi. Tangu wakati huo imezindua huduma za redio za dharura kwa Gaza na Sudan. Mwaka huo huo Sputnik ya Urusi ilianza huduma ya saa 24 nchini Lebanon, ikichukua mkondo wa matangazo ulioachwa na BBC Arabic.
Wakati huo huo, huduma ya utangazaji ya kimataifa inayofadhiliwa na serikali ya Marekani Sauti ya Amerika imepunguza wafanyakazi wake wengi.
"Urusi ni kama maji: ambapo kuna nyufa kwenye saruji, huingia ndani," anasema Dk Kathryn Stoner, mwanasayansi wa siasa katika Chuo Kikuu cha Stanford.
Swali ambalo linabaki, hata hivyo, ni, ni mwisho wa Urusi ni nini? Na hushawishi huu unaonekana kuenea kwa nguvu ya vyombo vya habari katika maeneo hayo ina maana gani katika enzi yenye mabadiliko ya mamlaka ya dunia?
'Yote haya sio nadharia ya njama ya wazimu'
"[Nchi za nje ya Magharibi] ni eneo lenye rutuba sana kiakili, kitamaduni, na kiitikadi [kwa sababu ya] mabaki ya hisia za kupinga Uamerika, Magharibi, na dhidi ya himaya," asema Stephen Hutchings, profesa wa Masomo ya Kirusi katika Chuo Kikuu cha Manchester.
Propaganda ya Urusi, anasema, pia inaenezwa kwa busara: yaliyomo ndani yake yanarekebishwa ili kukidhi hadhira maalum, hata ikiwa inamaanisha kupitisha misimamo tofauti ya kiitikadi katika maeneo tofauti.

Chanzo cha picha, KIRILL KUDRYAVTSEV/AFP via Getty Images
Chukua mtazamo wa RT. Huko Magharibi mara nyingi huonekana kama "sehemu ya serikali ya Urusi na muenezaji wa habari zisizofaa," anasema. Katika sehemu nyingine za ulimwengu, hata hivyo, mara nyingi huchukuliwa kuwa chombo halali cha utangazaji.
Hili huwafanya watazamaji waweze kuamini - "sio wananadharia wote wa njama wazimu ambao kwa ujinga huangukia kwenye taarifa potofu".
Hivi ndivyo Dk Rhys Crilley anavyoiweka. Yeye ni mhadhiri wa mahusiano ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha Glasgow, na anaamini kwamba utangazaji wa RT kuhusu ulimwengu unaweza kuvutia hadhira pana - "watu ambao wanajali kwa haki kuhusu ukosefu wa haki wa kimataifa, au matukio ambayo wanaona Magharibi kuhusika katika kutekeleza".
'Udanganyifu kwa umakini sana'
Kwa juu juu, tovuti ya kimataifa ya RT inaonekana kama tovuti ya kawaida ya habari na inaripoti baadhi ya hadithi kwa usahihi. "[Ni] ujanja wa uangalifu sana", asema Dk Precious Chatterje-Doody, mhadhiri mkuu wa Siasa na Mafunzo ya Kimataifa katika Chuo Kikuu Huria, ambaye aliandika kitabu kuhusu RT pamoja na Prof Hutchings, Dk Crilley na wengine.
Yeye na wafanyakazi wenzake walichanganua taarifa za habari za kimataifa za RT zinazohusu kipindi cha miaka miwili kati ya Mei 2017 na Mei 2019, na kuhitimisha kuwa mkusanyiko wake wa hadithi (kile ilichochagua kuangazia na ilichoacha) ulilingana na masimulizi fulani.
Kwa mfano, watafiti waligundua kuwa machafuko ya kijamii yalipewa kipaumbele kama mada ya kuripoti wakati yalipotokea katika nchi za Ulaya, ambapo moja ya upendeleo wa mara kwa mara katika uandishi wa mambo ya ndani ya Urusi ni mazoezi ya kijeshi ya nchi hiyo.
Mtangazaji huyo pia anatoa madai ya uongo ya wazi, kama vile kuonyesha unyakuzi wa Urusi wa Crimea mwaka wa 2014 kama "kuungana tena" kwa amani, kukataa ushahidi wa wazi wa kuhusika kijeshi. Imekanusha kimfumo ushahidi wa uhalifu wa kivita wa Urusi uliofanywa nchini Ukraine tangu uvamizi kamili wa 2022.

Chanzo cha picha, SERGEI BOBYLYOV /AFP via Getty
RT pia imechapisha hadithi huku wachambuzi wakiilaumu Ukraine kwa kudungua ndege ya shirika la ndege la Malaysia MH17 mnamo Julai 2014. (Shirika la anga la Umoja wa Mataifa limehitimisha kuwa Shirikisho la Urusi linahusika na udunguaji na wachunguzi wa kimataifa waligundua kuwa mfumo wa makombora uliosafirishwa kutoka Urusi hadi mashariki mwa Ukraine ulitumiwa na Warusi na makundi yanayounga mkono Urusi ).
Cha kushangaza ni idadi ya watazamaji waliofuatilia taarifa hii.
Kati ya 2018 na 2022, watafiti waliwahoji watu 109 ambao walitazama RT nchini Uingereza kabla ya kupata leseni yake ya kutangaza kufutwa na mdhibiti wa media wa Ofcom. Dk Chatterje-Doody anasema aliona kwamba wengi walisema waliona kuwa "RT ina upendeleo" lakini walikuwa na zana za kupambanua kile ambacho kilikuwa cha kweli na kisicho cha kweli.
Hata hivyo, kulingana na utafiti wake, alionya: "[Watazamaji] si lazima wafahamu njia sahihi ambazo RT inaegemea upande mmoja na ambapo ukosefu wa uaminifu wa utangazaji unatoka."
Kwa nini Urusi imerejelea mtazamo mpya kwa Afrika
Upanuzi mkubwa zaidi wa vyombo vya habari vya serikali ya Urusi umedhuhudiwa barani Afrika, kulingana na Prof Hutchings.
Mnamo Februari, mamlaka ya Urusi ilisafiri hadi Ethiopia kwa uzinduzi wa kituo kipya cha wahariri cha Sputnik. Sputnik tayari inatangaza kote Afrika katika lugha za Kiingereza na Kifaransa, na imepanuka na kujumuisha Kiamharic, mojawapo ya lugha rasmi za Ethiopia.
RT pia imeelekeza upya chaneli yake ya lugha ya Kifaransa kulenga mataifa ya Afrika yanayozungumza Kifaransa, pamoja na kuelekeza ufadhili kutoka kwa miradi ya London, Paris, Berlin na Marekani hadi bara, kulingana na mhariri mkuu wa RT.

Chanzo cha picha, MLADEN ANTONOV /AFP via Getty
Mwaka jana vyombo vya habari vya serikali ya Urusi vilidai kuwa RT ilikuwa na ofisi saba barani Afrika, ingawa hii haiwezi kuthibitishwa.
Waafrika wengi tayari wana maoni ya kirafiki kuelekea Urusi - hisia za kupinga ukoloni na ubeberu, pamoja na urithi wa uungaji mkono wa Soviet kwa harakati za ukombozi wakati wa Vita Baridi ilifanya jambo hilo kuwa la kawaida.
Kwa mtazamo huu mpya, Urusi inatarajia kudhoofisha ushawishi wa Magharibi, kujenga uungwaji mkono kwa matendo yake, na kujenga uhusiano wa kiuchumi, anasema Dk Crilley.
Ndani ya lengo la RT kwa waandishi wa Afrika
Wakati RT ilipozindua kozi yake ya kwanza ya mtandaoni iliyolenga waandishi wa habari wa Kiafrika na wanablogu, Kitengo cha BBC cha Global Disinformation Unit kilijiunga nacho ili kujua zaidi.
"Sisi ni moja kati ya wataalam bora katika kuangalia ukweli na hatujawahi kukamatwa tukisambaza habari za uwongo," mkurugenzi mkuu wa RT Alexey Nikolov aliwaambia wanafunzi.
Somo moja lilichunguza jinsi ya kukanusha habari potofu. Mkufunzi huyo alisema shambulio la silaha za kemikali katika mji wa Syria wa Douma mnamo 2018, na serikali ya Assad inayoungwa mkono na Urusi, ilikuwa "mfano wa kweli wa habari za uwongo", akipuuza matokeo ya uchunguzi wa miaka miwili wa Shirika la Kuzuia Silaha za Kemikali kuthibitisha mashambulio hayo yalifanywa na Jeshi la Wanahewa la Syria.
Pia alipuuzilia mbali mauaji makubwa ya raia wa Ukraine yaliyofanywa na vikosi vya Urusi katika mji wa Bucha wa Ukraine mwaka 2022, na kuyataja kuwa ni "feki inayojulikana zaidi". (Hii, licha ya ushahidi mwingi wa UN na huru unaolaumu vikosi vya Urusi.)
Wakizungumza na wale walioshiriki baada ya lengo hilo, wengi walionekana kutokerwa na hili - baadhi waliambia BBC wanaamini RT ilikuwa mtangazaji wa kawaida wa TV wa kimataifa, kulinganishwa na CNN au Al Jazeera.
Tulipomhoji mwandishi wa habari wa Ethiopia mnamo Desemba 2024, waliunga mkono madai ya RT kwa kuyaita mauaji ya Bucha "tukio la jukwaani". Picha yao ya wasifu kwenye mitandao ya kijamii ilikuwa picha ya Putin.
Mwandishi wa habari kutoka Sierra Leone alikiri hatari ya taarifa potofu na disinformation lakini, wakati huo, aliongeza kuwa kila taasisi ya vyombo vya habari ina "thamani ya habari na mtindo" wake.
Kuanzia Mashariki ya Kati hadi Amerika ya Kusini
Katika Mashariki ya Kati, vyombo vya habari vya serikali ya Urusi kama vile RT Arabic na Sputnik Arabic vinarekebisha utangazaji wao wa vita vya Israel-Gaza ili kuvutia watazamaji wanaounga mkono Palestina, kulingana na Prof Hutchings.
RT pia inajaribu kupanua ufikiaji wake mahali pengine, ikiwa ni pamoja na Amerika Kusini,
RT inapatikana bila malipo katika nchi 10 za eneo hilo kulingana na tovuti yake. Argentina, Mexico, na Venezuela ni miongoni mwao. Pia inapatikana kwenye mtandao wa televisheni katika nchi nyingine 10.
Kutoa habari za kimataifa kwa lugha ya Kihispania katika televisheni bila malipo ni "sehemu ya mafanikio yake," anasema Dk Armando Chaguaceda, mwanahistoria na mwanasayansi wa siasa wa Cuba-Meksiko, ambaye ni mtafiti kutoka taasisi ya uchunguzi ya Serikali na Uchambuzi wa Kisiasa (unaolenga elimu ya uraia na kukuza utamaduni wa kidemokrasia).

Chanzo cha picha, REUTERS/Dado Ruvic
Na ingawa RT imepigwa marufuku kwenye YouTube kote ulimwenguni, tangu Machi 2022, bado inaingia kwenye jukwaa katika baadhi ya maeneo.
Nchini Argentina, seremala mwenye umri wa miaka 52 Aníbal Baigorria hurekodi ripoti za TV kutoka RT na kuzipakia kwenye chaneli yake ya YouTube, pamoja na maoni yake.
"Hapa Buenos Aires habari zinaangazia sana jiji," anahoji. "RT inatoa muhtasari wa maeneo yote katika Amerika ya Kusini na, bila shaka, habari za kimataifa."
"Kila mtu ana haki ya kuamua kile anachoamini kuwa ni kweli."
Kuelewa athari
Hatimaye, ni vigumu kukadiria athari za vyombo vya habari vinavyoungwa mkono na serikali ya Urusi kote ulimwenguni.
RT inadai kuwa inapatikana kwa zaidi ya watazamaji milioni 900 wa TV katika zaidi ya nchi 100 na inasema maudhui yake yalivutia maoni bilioni 23 mtandaoni mnamo 2024.
Lakini, kama Dk Rasmus Kleis Nielsen, profesa wa mawasiliano katika Chuo Kikuu cha Copenhagen, anavyoonyesha: "Upatikanaji sio kipimo cha maana cha ukubwa wa watazamaji."
Pia anabisha kuwa idadi ya watazamaji milioni 900 "haiwezekani sana" na anaelezea mitazamo ya mtandaoni kama kipimo kisichoeleweka na kinachobadilishwa kwa urahisi.
Dk Chatterje-Doody anakubali kwamba kutathmini athari ya moja kwa moja ni ngumu. Lakini anaashiria kesi moja ambayo inaweza kupendekeza mafanikio fulani kwa Urusi. Katika eneo la Sahel barani Afrika, ambalo linaenea kutoka Senegal kuelekea mashariki hadi Sudan, Urusi imecheza majukumu makubwa ya kijeshi "pamoja na upinzani mdogo wa umma", hata kwa kuzingatia mazingira yenye changamoto. (Imejiimarisha yenyewe kwa kuunga mkono vikosi vya kijeshi katika nchi kama vile Mali, Burkina Faso, na Niger.)
Hadithi nyingine ambayo imekwama imekuwa uhalali wa Urusi kwa uvamizi wa Ukraine. Kwa muda mrefu Urusi imeanzisha upanuzi wa Nato wa mashariki na kuongezeka kwa uhusiano wa Ukraine na muungano kama sababu kuu ya uvamizi wake kamili, ikidai kuwa ni "tishio la usalama" na kwamba Urusi ilichukua hatua "kujilinda". Ingawa ilikanushwa sana katika nchi za Magharibi, dai hili la uwongo lilidumu kote Kusini mwa Ulimwengu.

Chanzo cha picha, REUTERS/Dado Ruvic
"Wazo… ni simulizi iliyopokelewa vyema, hasa katika duru za kitaaluma, nchini Mexico na Amerika Kusini kwa jumla," anasema Dk Chaguaceda wa hoja ya upanuzi wa Nato.
Baadhi ya viongozi wa Global South wamesita kulaani vita vya Urusi dhidi ya Ukraine. Katika kura ya kwanza ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa baada ya uvamizi kamili mwaka 2022, idadi kubwa ya nchi zililaani vita hivyo, lakini nchi 52 ama zilipiga kura dhidi ya maazimio hayo, ambazo hapo awali zilijiandikisha kutopiga kura, au zilijizuia kupiga kura. Miongoni mwao, Bolivia, Mali, Nicaragua, Afrika Kusini na Uganda.

Chanzo cha picha, RONALDO SCHEMIDT/AFP via Getty Images
Dr Crilley ana maoni yake mwenyewe juu ya nini mwisho wa mchezo wa Urusi ni.
"[Kremlin inajaribu] kupunguza kutengwa kwa Urusi katika jukwaa la dunia kwa kuonyesha Urusi kama mwathirika mwenza wa uchokozi wa 'Magharibi' na mtetezi wa Kusini mwa Ulimwengu."
Hatari, anaonya, "ni kwamba RT na juhudi zingine za upotoshaji za Urusi zinavamia na kutumia udhaifu wa demokrasia ya kiliberali, huku ikirekebisha uchokozi wa Urusi nchini Ukraine, na kuwasilisha Urusi kama serikali ya kimabavu lakini kama aina fulani ya nguvu isiyo na usawa katika siasa za ulimwengu."
Ilipoulizwa jibu la madai yaliyotolewa katika makala haya, RT ilisema: "Kweli tunapanuka kote ulimwenguni."
Walikataa kutoa maoni zaidi juu ya hoja maalum.
Sputnik haikujibu maombi ya maoni.
Hatimaye, Prof Hutchings anaamini kwamba sote tunapaswa kuwa na wasiwasi kuhusu shughuli za serikali ya Urusi - hasa katika muktadha wa mustakabali wa utaratibu wa dunia na demokrasia.
Anaamini kuwa nchi za Magharibi zinaondoa "jicho lake nje ya mpira" kwa kukata ufadhili wa vyombo vya habari na "kuacha uwanja wazi kwa watu kama wa Russia Today."
"Kuna mengi ya kucheza na mengi ya kupoteza... Na Urusi inashinda - lakini vita haijapotea."












