Wanawake wawili wapelelezi wa Urusi wamefuatiliwa na kutajwa na BBC

Cvetelina Gencheva na Tsvetanka Doncheva

Chanzo cha picha, Facebook

Maelezo ya picha, Cvetelina Gencheva (kushoto) na Tsvetanka Doncheva (kulia)
    • Author, Daniel De Simone, Chris Bell, Tom Beal na Nikolai Atefie
    • Nafasi, BBC News Investigations
  • Muda wa kusoma: Dakika 8

Wanawake wawili ambao walikuwa sehemu ya kundi la kijasusi la Urusi lililokuwa Uingereza wametambulishwa kwa mara ya kwanza hii leo baada ya BBC kufanya uchunguzi.

Raia hawa wa Bulgaria Cvetelina Gencheva na Tsvetanka Doncheva walishiriki katika operesheni ya kuchunguza watu ambao walikuwa walengwa wa kundi la kijasusi.

Wote wawili hawakujibu maswali walioulizwa baada ya kupigiwa simu na BBC kupata upande wao wa maoni.

Bi Gencheva, mfanyakazi wa uwanja wa ndege, alikata simu alipopigiwa, na kusema hakutaka kuzungumzia kisa hicho kufuatia barua ya kumtaka aelezee upande wake.

Naye Bi Doncheva alikana kuwa ndiye anafahamika kwa hilo jina na kuondoka baada ya kutafutwa karibu na nyumbani kwake huko Vienna, Austria.

Wabulgaria wengine sita wanasubiri kuhukumiwa huko London kwa majukumu yao ya kusaidia Urusi kupeleleza walengwa walioko Uingereza.

Maafisa wa polisi walitaja kikosi hicho kama operesheni "ya hali ya juu" ambayo ilitishia maisha.

Watu watatu walikiri mashtaka dhidi yao, wakikubali walijua walikuwa wanafanyia kazi Urusi, huku wengine watatu wakihukumiwa mwezi huu baada ya kesi iliyokuwa ikisikilizwa Old Bailey na kushindwa kuwashawishi waamuzi kwamba hawakuhusika na kundi hilo la kijasusi.

Kikosi hicho kiliongozwa kutoka nje ya nchi na Jan Marsalek, aliyetoka Austria, ambaye alikuwa mfanyibiashara mkuu nchini Ujerumani na kugeukia kuwa jasusi wa Urusi.

Walengwa wa kikosi hicho ilikuwa ni pamoja na waandishi wa habari ambao wamechunguza ujasusi wa Urusi.

Mmoja wa kati ya walengwa, Roman Dobrokhotov, aliambia BBC kuwa anaamini Vladimir Putin ndiye aliyehusika.

Mahakama ilijua kuhusu wanawake wawili wasiojulikana ambao walishiriki katika shughuli za uchunguzi barani Ulaya.

BBC ilifuatilia na kuthibitisha utambulisho wa wanawake wote wawili kupitia utafiti wa wazi wa kidijitali na kuzungumza na vyanzo.

Mfanyakazi katika uwanja wa ndege

Cvetelina Gencheva

Chanzo cha picha, Cvetelina Gencheva/Facebook

Maelezo ya picha, Cvetelina Gencheva
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Bi Gencheva, ambaye anaishi katika mji mkuu wa Bulgaria unaojulikana kama Sofia, alitumia mamlaka alikuwa nayo katika sekta ya usafiri wa ndege kufuatilia na kupata maelezo ya kibinafsi ya watu waliolengwa na kikosi hicho cha ujasusi wa Urusi.

Majasusi wangetumia maelezo hayo na kuwafatilia watu hao hadi wanapoabiri ndege na walikuwa wanahakikisha wamekaa karibu yao ili kujua ni kipi wanachofanya katika simu za mikononi za walengwa wao na hata katika hatua moja walitambua nambari ya siri ya simu ya mwandishi wa habari Roman Dobrokhotov.

Bi Gencheva alikuwa sehemu ya timu iliyotumwa Berlin kumpeleleza Bwana Dobrokhotov, na alikuwa mwanachama wa vikundi vya mazungumzo vya mitandao na watatu kati ya wale waliopatikana na hatia ya ujasusi katika kesi ya Uingereza - kiongozi wa kikosi Orlin Roussev, Biser Dzhambazov na Katrin Ivanova - ambayo ilitumiwa kuratibu upelelezi.

Pia alitoa maelezo ya safari ya ndege ya mwandishi wa habari Christo Grozev, na alipewa jukumu la kukusanya habari nyingi za kusafiri iwezekanavyo juu ya mlengwa mwingine wa kikosi hicho cha ujasusi, mpinzani wa Kirusi Kirill Kachur.

Wakati wa kesi ya Old Bailey, mfanyakazi huyo wa shirika la ndege alijulikana kama "Cvetka" au "Sveti".

BBC ilimtambua Bi Gencheva kwa mara ya kwanza kupitia wasifu wake kwenye mitandao ya kijamii.

Kwenye Facebook, alikuwa ametangamana na Katrin Ivanova na Biser Dzhambazov.

Kisha tukagundua alikuwa mfanyakazi wa shirika la ndege.

Kulingana na wasifu wake wa Linkedin, ameshikilia nyadhifa katika mauzo ya tikiti kwa kampuni za usafiri.

Jalada za kampuni ya Bulgaria zinasema yeye ndiye mmiliki wa taasisi ya kimataifa ya kushauri masuala ya sayansi na vyombo vya anga.

Picha za skrini za data ya usafiri iliyopatikana kwenye diski kuu ya kiongozi wa kikosi hicho cha ujasusi Roussev zilitoka kwenye programu ya sekta ya ndege inayojulikana kama "Amadeus".

Kwenye wasifu wake wa LinkedIn, tulimpata Bi Gencheva alibainisha ustadi wake na programu.

Baada ya utafiti uliofanywa na BBC ulimtambua Bi Gencheva, na chanzo kilichokuwa kikishirikiana na BBC kilithibitisha kuwa mwanamke huyo alikuwa akijulikana na idara ya usalama ya Bulgaria kuwa anahusika na kikosi cha ujasusi cha Urusi, hata hivyo hajafunguliwa mashtaka.

Tulimpigia simu Gencheva kupitia namba ya simu anayoitumia huko Bulgaria katika sekta yake ya ujenzi.

Alikata simu kwa haraka alipojulishwa ni BBC na ilikuwa inarekodiwa, hata hakutaka kusubiri kusikiliza ni kipi angeulizwa au angeongelelea.

Na kuhusu barua ambayo tulimtumia ikieleza ushahidi tuliokuwa nayo alijibu kuwa hayuko tayari kugusia ''kesi hiyo'' na pia hakuridhia jina lake litajwe.

Akiandika kwa lugha rasmi ya Bulgaria pia alieleza hana uelewa kamili wa kuongea lugha ya kiingereza.

Hata hivyo, katika akaunti yake ya mtandao wa Linkedln imeeleza ana uwezo wa kiingereza ''anajua kuzungumza na kuelewa'' na kusema kuwa amesomea shahada yake kwa lugha ya kiingereza.

Mwanamke anayeishi Vienna

Tsvetanka Doncheva

Chanzo cha picha, Tsveti Doncheva/Facebook

Maelezo ya picha, Tsvetanka Doncheva

Bi Doncheva alisaidia kupeleleza mwandishi wa habari za uchunguzi Christo Grozev huko Vienna, akikaa orofa mkabala na alipokuwa akiishi na kuendesha kamera iliyopiga picha za nyumba yake.

Alilipwa kuendesha kampeni ya uenezi dhidi ya Ukrainia, ambayo ni pamoja na kuweka vibandiko kwenye maeneo yakiwemo kumbukumbu ya vita vya Sovieti ya Vienna na ilikusudiwa kuwafanya wafuasi wa Ukraine waonekane kama Wanazi mamboleo.

BBC ilimtambua Bi Doncheva kupitia wasifu wake kwenye mitandao ya kijamii baada ya kesi ya Old Bailey kusikia kuhusu "Tsveti" ambaye alifanya kazi na kikosi hicho cha ujasusi cha Urusi.

Vyanzo vya Austria pia vilithibitisha utambulisho wake.

Huko Vienna, alikutana na angalau watu watatu wa wale waliopatikana na hatia ya upelelezi katika kesi ya Uingereza - Vanya Gaberova, Biser Dzhambazov na Katrin Ivanova.

Maafisa wakuu wa Austria, akiwemo mkuu wa Huduma ya Siri Omar Haijawi-Pirchner, walikuwa miongoni mwa waliochaguliwa kuchunguzwa na Bi Doncheva, pamoja na mwandishi wa habari wa uchunguzi wa Austria Anna Thalhammer, ambaye ameandika kuhusu ujasusi wa Urusi.

Bi Doncheva, ambaye hana kazi, alikamatwa na polisi wa Austria mnamo Disemba.

Nyaraka za mahakama zilizoripotiwa kwa mara ya kwanza na magazeti ya Austria ya Profil na Falter, na baadaye kuonekana na BBC, zinaonyesha kuwa "anashukiwa vikali kutenda uhalifu wa upelelezi wa siri kwa madhara ya Austria".

Aliwaambia wachunguzi kwamba alifanya uchunguzi baada ya kuulizwa na rafiki wa muda mrefu Vanya Gaberova - mmoja wa Wabulgaria sita waliokuwa wakisubiri hukumu.

Alisema Gaberova alimpa orodha ya majina, anwani na picha.

Awali aliwaambia polisi kwamba alikuwa amepotoshwa na wengine, ambao kwanza walimwambia walikuwa wakiendesha "mradi wa wanafunzi" na baadaye kwamba walikuwa wakifanya kazi kwa Interpol.

Lakini wachunguzi wa Austria wamerekodiwa wakisema "haieleweki" kwamba Bi Doncheva aliamini "hadithi zenye kutia shaka".

Kulingana na nyaraka hizo zinasema kikosi cha kijasusi ambacho Doncheva alifanyia kazi kilikuwa kikiongozwa na Jan Marsalek kutoka Moscow kwa niaba ya ujasusi wa Urusi na ushahidi uliopatikana ulionyesha aliajiriwa na Marsalek na kiongozi wa kikosi cha Ujasusi kilichoko Uingereza bwana Orlin Roussev.

Anna Thalhammer pichani akiwa ofisini mwake

Chanzo cha picha, Adam Walker/BBC

Maelezo ya picha, Mhariri wa sura Anna Thalhammer alilengwa na kikosi cha ujasusi

Hati hizo zinasema Marsalek aliagiza Anna Thalhammer afuatiliwe na kuchunguzwa.

Bi Doncheva alikiri kwa polisi kuwa alikuwa amepiga picha mahali pa kazi pa mwanahabari huyo wakati huo na kutaka kumwangalia kutoka kwenye mkahawa wa karibu.

Bi Thalhammer, ambaye sasa ni mhariri wa jarida la habari la Austria la Profil, aliambia BBC kwamba aliambiwa mara ya kwanza kuhusu kupeleleza mwaka jana na polisi, na sasa anafahamu kuwa anatazamwa kwa muda.

"Ni wazi aliketi mbele ya ofisi katika mkahawa wa samaki. Kwa kweli naweza kuupendekeza. Alilalamika kuwa ni ghali sana kukidhi gharama , kwamba anahitaji pesa zaidi. Baadaye alipata pesa hizo."

Anasema "mwanamke huyo" pia alipeleleza idadi ya "watu wa vyeo vya juu".

Bi Thalhammer hajui mahali pengine alipofuatwa, lakini kwamba baadhi ya vyanzo vyake alivyovitumia katika kazi zake vilitambuliwa na majaribio yalifanywa kuvamia nyumba zao.

Anasema "Vienna ni mji mkuu wa wapelelezi" lakini hakuna mtu aliyehukumiwa katika jiji hilo kwa ujasusi na "sheria hapa ni nzuri kwa wapelelezi".

"Nimechanganyikiwa na pia kwa uaminifu ninaogopa kidogo," aliongeza. "Ninaishi peke yangu na binti yangu. Haipendezi sana kujua kwamba serikali haijali kama mtu anawatishia waandishi wa habari, wanasiasa au mtu mwingine yeyote."

Tsvetanka Doncheva akiwa amevalia shati iliyochorwa Vladimir Putin

Chanzo cha picha, Tsveti Doncheva/Facebook

Maelezo ya picha, Tsvetanka Doncheva akiwa amevalia shati iliyochorwa Vladimir Putin ikiwa imeandikwa maandishi: ''nina uwezo wa kusoma akili zenu''

Mtumiaji mahiri wa mitandao ya kijamii - hata paka wake ana akaunti ya TikTok - Bi Doncheva alichapisha picha yake kwenye Facebook akiwa amevalia fulana ya Vladimir Putin mwaka wa 2022 na 2023.

Mtu alipotoa maoni kwamba nchini Urusi asilimia kubwa ya wanawake wanataka kupata mtoto na Putin, Bi Doncheva alijibu akisema si tu nchini Urusi, ikifuatiwa na emoji ya kulamba midomo.

Bi Doncheva alikanusha kuwa ni yeye anafahamika kwa jina hiloalipofuatwa na BBC katika mtaa wa Vienna na kukataa kujibu maswali, lakini tumethibitisha kwamba mwanamke huyo alikuwa Bi Doncheva.

Maelezo ya video, Tazama: Tsvetanka Doncheva akifuatwa na BBC akiwa nyumbani kwake Vienna

Alipofikiwa, alikuwa amevalia nguo na kubeba vitu vilivyoonekana kwenye mitandao ya kijamii ya Bi Doncheva: suti ya kipekee ya rangi ya samawati, miwani, na kipochi chenye muundo wa simu ya mkononi.

Pia tulimwona akiingiza anwani ya nyumba ya Bi Doncheva iliyosajiliwa chini ya dakika 20 baada ya kukana kuwa Bi Doncheva.

Hajajibu barua inayompa nafasi ya kutoa maoni yake.

Wanawake hao wawili walifanya kazi pamoja na Wabulgaria sita waliopatikana na hatia ya kula njama ya kufanya ujasusi wa Urusi.

Picha ya pamoja ya raia sita wa Bulgaria wanaoshutumiwa kwa kuifayia kazi Urusi upelelezi

Chanzo cha picha, Metropolitan Police handout and social media

Maelezo ya picha, Kuanzia kushoto kutoka juu: Orlin Roussev, Katrin Ivanova, Ivan Stoyanov, Tihomir Ivanchev, Vanya Gaberova na Biser Dzhambazov

Hifadhi ya karibu jumbe 80,000 za Telegram kati ya Roussev na bosi wake Marsalek zilipatikana na polisi wa Uingereza.

Jumbe hizo zilifichua oparesheni nyingi zilizofanywa na kikosi hicho cha ujasusi katika miaka ya tangu mwezi Februari 2023, wakati shughuli zao zilitatizwa na polisi.

Majasusi hao wa Uingereza hata waliwalenga wanajeshi wa Ukraine wanaodhaniwa kuwa wanafanya mafunzo katika kambi ya kijeshi ya Marekani nchini Ujerumani.

Roussev na Marsalek walijadili utekaji nyara na kuua waandishi wa habari Christo Grozev na Roman Dobrokhotov.

Tofauti na majasusi sita waliohukumiwa nchini Uingereza, Bi Doncheva na Bi Gencheva hawako rumande na hawajahukumiwa kwa kosa lolote.

Ombi la mwendesha mashtaka wa umma wa Austria la kuzuiliwa kabla ya kusikilizwa kwa Bi Doncheva lilikataliwa na akaachiliwa.

Nyaraka za mahakama ya Austria zinasema "hakuna hatari" ya Bi Doncheva kutoroka kwa sababu "ameunganishwa na jamii" nchini humo na anamjali mama yake, na kwamba hatari ya uhalifu zaidi sio juu hasa kutokana na kufungwa nchini Uingereza kwa wengine waliohusika,

Bi Thalhammer aliambia BBC kuwa "haelewi" kwa nini mtu aliyempeleleza aliachiliwa huru.

"Labda [hawapaswi] kuamini kila kitu anachosema jasusi."

Alisema idara ya siri ya Austria inadhani kuna kesi kingine cha kijasusi na kwamba shughuli zao zimeendelea baada ya kukamatwa kwa Wabulgaria sita nchini Uingereza.

Bi Gencheva amesalia huru nchini Bulgaria, akijionyesha hadharani kama mtaalamu wa tasnia ya usafiri wa anga na usafiri kwa ujumla.

Baada ya kuwasiliana na BBC, Bi Gencheva alibadilisha jina lake la wasifu kwenye Facebook na LinkedIn.

Anaendelea kuorodhesha ujuzi wake na programu ya shirika la ndege la Amadeus.

Ikiwa una habari kuhusu taarifa hii au nyingine kama hiyo ambayo ungependa kushiriki na timu ya Uchunguzi wa Habari za BBC tafadhali wasiliana. Tafadhali jumuisha nambari ya mawasiliano ikiwa uko tayari kuzungumza na mwandishi wa habari wa BBC. Unaweza kuwasiliana nasi kwa njia zifuatazo:

Barua pepe: [email protected]

Signal: +447811921399

Bonyeza hapa ukiwa unataka kujifunza namna yakutumia mtandao huu ili upatiane taarifa bila kujulikana na ufuate maagizo hadi tamati.