Kwanini uhusiano wa Kabila na Tschisekedi unaendelea kuzorota?

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, Dinah Gahamanyi
- Nafasi, BBC Swahili News
- Akiripoti kutoka,
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Uhusiano wa Kabila na mrithi wake Felix Tchisekedi umekuwa ukiendelea kudorora huku pande mbili zikirushiana cheche za maneno, kila mmoja akimlaumu mwenzake kusababisha ukosefu wa usalama DRC.
Alhamisi Bunge la Seneti la DRC lilimeondoa kinga ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Joseph Kabila, na hivyo kumtengenezea njia ya kufunguliwa mashitaka, hatua iliyomkera Bw Kabila.
Kwa jumla, Maseneta 88 walipiga kura ya kuunga mkono kuondolewa kwake kwa kinga hiyo ili aweze kushitakiwa, ni watano pekee waliopiga kura kupinga hilo, huku kura nyingine tatu zikiharibika.
Kabila sasa anakuwa mkuu wa nchi wa kwanza wa zamani kuondolewa kinga hiyo na kushtakiwa kwa uhaini, uhalifu wa kivita na mashtaka yanayohusiana nayo nchini DRC.
Hatua ya kuondolewa kinga ya kutoshitakiwa kama rais wa zamani kwa Kabila ambaye amekuwa Seneta wa maisha, imekuja baada ya mrithi wake Rais wa Felix Tschisekedi kumtuhumu kwa uhaini, uhalifu wa kivita, na kuunga mkono kundi la waasi la M23 ambalo liliteka miji mikubwa Mashariki mwa Congo mapema mwaka huu.
Joseph Kabila ambaye aliondoka nchini DRC mwaka 2023 hakufika mbele ya Bunge hilo la Seneti kujitetea kabla ya kura hiyo kupigwa. Lakini je nini kitakachofuata na hatima yake kwa Bwana Kabila baada ya kuondolewa kinga hiyo? Ni swali muhimu kujibiwa na makala hii, lakini pia muhimu kufahamu kauli yake kuhusu sakata hili.
Joseph Kabila anasemaje?
Kabla ya kufahamu ni nini kitakachofuata baada ya kuondolewa kinga kwa Joseph Kabila, ni vyema tukaangalia binafsi amesema nini kuhusiana na hatua hii dhidi yake.
Akijibu hatua za kumuondolea kinga kupitia ukurasa wake wa X, kabila ameonyesha kutofurahishwa na hatua ya kumtolea kinga dhidi yake huku ujumbe ukiashiria kumlenga Rais Tschisekedi moja kwa moja:
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
''Nitafakari uamuzi wa Seneti wa kuondoa kinga zangu. Uamuzi huu uliopangwa kwa haraka na bila kuheshimu taasisi, sio kitendo cha haki. Ni ujanja wa kisiasa wa kukata tamaa, katika muktadha wa hofu iliyoenea juu ya serikali''.
Aliongeza kuwa:''Sijawahi kukwepa majukumu yangu, sio kwa watu, wala kabla ya historia. Sihitaji kinga ili kukabiliana na hali hiyo, lakini wale wanaonilenga leo wanapaswa kuwa tayari kufikiria juu ya kile watakachosema kesho.
Kwasababu nchi hii haina amnesia[haisahau]. Inajua ni nani aliyeijenga, na inajua ni nani anayeiharibu. Kwa wale wanaoamini kuwa kuondoa kinga zangu kutazuia kushindwa kwao: mmekosea. Ukweli hauwezi kupigiwa kura. Ni muhimu. Na itakuja (kujulikana)'', anamaliza kuandika Kabila.
Kabila amekuwa akimshutumu Rais Tshisekedi kwa kushindwa kushughulikia mizozo inayolikumba taifa kwa busara, ukiwemo mzozo wa waasi wa M23 walioyateka maeneo ya mashariki mwa nchi ukiwemo mji muhimu wa Goma. Rais huyo wa zamani amekuwa akilalamika mara kwa mara kwamba Tshisekedi ameegemea upatanishi kutoka nje badala ya kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na waasi, jambo ambalo Tshisekedi amekuwa akilipinga.
Kwanini serikali ya DRC imeondoa kinga ya Kabila?
Waziri wa Sheria wa DRC Constant Mutamba aliwaambia waandishi wa habari Jumatano kwamba serikali imekusanya ushahidi unaomhusisha Kabila katika "uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu na mauaji ya raia na wanajeshi wa amani" mashariki mwa nchi hiyo. Hakutoa maelezo maalum ya uhalifu huu.
Sehemu za mkoa wa mashariki kwa sasa ziko chini ya udhibiti wa kundi la M23, ambalo linatafuta udhibiti wa utajiri wa madini na lina matarajio ya kuchukua madaraka huko Kinshasa. Umoja wa Mataifa na Marekani zinadai kundi hilo linaungwa mkono na nchi jirani ya Rwanda, shutuma ambazo Rwanda imekuwa ikizikana mara kwa mara.
Kuhusiana na hili, Kabila anatuhumiwa kwa ''uhaini, uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu, na kushiriki katika harakati za uasi", waziri wa sheria alisema.
Haijulikani ni lini Seneti itaidhinisha mahitaji ya jeshi, au ni lini kesi inaweza kuanza.
Kuzorota kwa uhusiano baina ya Kabila na Tchisekedi

Chanzo cha picha, AFP
Uhusiano wa Rais Tshisekedi na Joseph Kabila umekuwa wa uhasama hasa kutokana na kutoelewana kuhusu ni nani mwenye kuwateua maafisa gani katika serikali na taasisi za taifa hilo.
Ingawa wawili hao walikubaliana mwaka wa 2019 kuhusu mkataba wa kugawana madaraka ambao ulikiruhusu wanachama wa Chama cha Kabila cha People's Party for Reconstruction and Democracy (PPRD) kushiriki katika serikali mpya, muungano wao ulivunjika mwaka mmoja baadaye, mnamo 2020 kutokana na suala hilo nyeti la uteuzi wa maafisa, ambalo wachambuzi wanasema lingemuwezesha Bw. Kabila kuwa na ''mikono'' katika serikali ya Rais Tschisekedi.
Wakati mmoja Tschisekedi alilalamika kuhusu suala la Kabila kuingilia utendaji wa serikali yake na kumtaka akae mbali nayo.
Mvutano kati ya Kabila na Mrithi wake uliongezeka zaidi kutokana na uasi wa M23 ulioanza mwaka 2012.
Tshisekedi anamlaumu Kabila kwa kudhoofisha serikali yake na kumshutumu kwa kuunga mkono M23, akitoa mfano wa uhusiano wake wa karibu na mwenyekiti wa zamani wa uchaguzi aliyegeuka kuwa kiongozi wa waasi, wa M23 Corneille Nangaa.
Nangaa, ambaye alitangaza muungano wake na waasi mnamo 2023, alikuwa mkuu wa tume ya uchaguzi ya nchi hiyo kutoka 2015 hadi 2021 na alisimamia uchaguzi wa 2018 uliokuwa na utata ambao ulimuweka Tshisekedi madarakani. Wawili hao baadaye walitofautiana juu ya jinsi uchaguzi ulivyoendeshwa, na kusababisha Nangaa kumkosoa hadharani Tshisekedi na hatimaye kujiunga na kundi la waasi.
Mnamo Aprili 20, serikali ya DRC ilisimamisha chama cha Kabila, PPRD, na kuamuru mali zake zikamatwe kwa tuhuma za kuunga mkono M23. Haijulikani ikiwa mali hizo bado ziko chini ya udhibiti wa serikali.
Nangaa, ambaye alitangaza muungano wake na waasi mnamo 2023, alikuwa mkuu wa tume ya uchaguzi ya nchi hiyo kutoka 2015 hadi 2021 na alisimamia uchaguzi wa 2018 uliokuwa na utata ambao ulimleta Tshisekedi madarakani. Wawili hao baadaye walitofautiana juu ya jinsi uchaguzi ulivyoendeshwa, na kusababisha Nangaa kumkosoa hadharani Tshisekedi na hatimaye kujiunga na kundi la waasi.
Mvutano kati ya wawili hao umemweka Kabila mbali na nchi kwa miaka kadhaa, akiishi kwa sehemu kubwa nchini Afrika Kusini. Lakini kuripotiwa kwake kujitokeza tena mwezi uliopita katika eneo linaloshikiliwa na waasi wa M23 la Goma katika eneo la Kivu mashariki mwa DRC kulisababisha uvumi kwamba huenda alishirikiana na kundi hilo la waasi wenye silaha, M23.
Kujitokeza kwake tena nchini DRC kumeonekana pia kuikasirisha serikali, ambayo imekuwa ikipambana na kundi la M23 katika mzozo mbaya mashariki mwa nchi hiyo kwa miezi kadhaa.
Mnamo Aprili 20, Serikali ya DRC ilikisimamisha chama cha Kabila, PPRD, na kuamuru mali zake zikamatwe kwa tuhuma za kuunga mkono M23. Haijulikani ikiwa mali hizo bado ziko chini ya udhibiti wa serikali ama la.
Nini kitakachofuata na ni ipi hatma ya Kabila?
Baada ya kuondolewa kwa kinga ya usalama, Bwana Kabila sasa anakabiliwa na uwezekano wa kukamatwa. ''Kinachofuata sasa ni kwamba jeshi litatoa kibali cha kumkamata ili akabiliwe na mashtaka ya "uhaini, uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu, na kushiriki katika harakati za uasi", anasema Mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini DRC, Ap Jollo Msambya Joseph.
Bwana Apollo anasema, Kabila sasa anatakiwa kuwa mtu mwenye wasiwasi na kudhibiti matembezi yake ambayo amekuwa akiyafanya katika nchi kama Afrika Kusini, Namibia , Zimbabwe na kwingineko ambazo anasema iwapo zitatatekeleza agizo la kukamatwa kwakwe kwa kibali maalumu, anaweza kukamatwa na kurejeshwa Kinshasa. Lakini iwapo hazitatekeleza uamuzi huo, kibali hicho kitasalia kuwepo bila athari yoyote…Hii itatokana uhusiano wake na mataifa hayo''
Kulingana na mchambuzi huyo wa kisiasa , itakua vigumu kwa Kinshasa kumdhibiti Bwana Kabila ambaye binafsi alikuwa mwanajeshi, kwani hakuna uthibitisho wa shutuma dhidi yake ambazo amekwishizitaja kama ni za uongo.
Joseph kabila ni nani katika uongozi wa DRC?
Joseph Kabila, mwenye umri wa miaka 53, ni afisa wa zamani wa kijeshi ambaye alikuwa rais wa nne wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kuuanzia mwaka 2001 hadi 2019. Ingawa muhula wake ulipaswa kumalizika 2016, kwa utata alichelewesha uchaguzi hadi maandamano makubwa yalipozuka.
Marais nchini DRC huchaguliwa kwa muhula wa miaka mitano na wanaruhusiwa kuhudumu mihula miwili pekee (si zaidi ya miaka 10). Katiba mpya, iliyopitishwa mwaka 2006, iliweka upya muhula wa mihula miwili ya Kabila.
Alichukua uongozi wa nchi mwaka 2001 akiwa na umri wa miaka 29 tu, baada ya baba yake na kiongozi wa zamani wa mapinduzi, Rais Laurent Kabila, kuuawa. Marais wa DRC, marais wa zamani na Maseneta hawana kinga dhidi ya kushtakiwa isipokuwa kama watafanya "uovu mkubwa" kulingana na katiba ya nchi hiyo.















