Je, maandamano ya Chadema yatazaa mageuzi ya kisiasa Tanzania?

Na Sammy Awami
Aliyekuwa mbunge wa Chadema Upendo Peneza alisema katika mkutano wa kujitambulisha rasmi kwenye chama chake kipya kwamba wito wa waandamano ya Chadema ilikuwa ni mbinu ya chama hicho cha upinzani kukagua wanakubalika kiasi gani kwa wananchi. Kwa sehemu, ni mawazo ambayo wafuatiliaji wengi wa siasa nchini walikuwanayo, wakiaimini kulikuwa na matumaini kidogo sana kwa maandamano yale kufanyika.
Baada ya kufanikiwa, wengi sasa wanaamini maandamano yale yamethibitisha mambo kadhaa: Mosi, dhana ya maandamano huhatarisha amani na usalama wa mali za watu haina mashiko. Pili, wapo wafuasi wengi wa vyama vya upinzani ambao bado wana shauku ya kushiriki katika shughuli za kisiasa pale wanapohakikishiwa usalama wao.
Mchambbuzi wa siasa na mwanaharakati Dkt. Thabit Jacob anasema Chadema hawakuwa na budi bali kufanya maandamano haya kama sehemu kuthibitisha kwamba mazungumo ambayo chama hicho imekuwa ikiyafanya kwa si chini ya muda wa mwaka mmoja sasa hayajamdhoofisha mwenyekiti wake Freeman Mbowe wala agenda za chama.
“Kumbuka Mbowe alikuwa anashutumiwa kwa kulamba asali, shutuma ambazo hazikuwa na msingi. Wito wa maandamano ulilenga kutuma ujumbe mzito kwamba hajanunuliwa. Lakini wamefanya jambo la msingi pia, kufanya msingi wa maandamano haya kutokuwa juu ya tume huru ya uchaguzi na katiba mpya pekee bali pia kupanda kwa gharama za maisha,” anasema Jacob.
Chadema kilitangaza maandamano kupinga mabadiliko yanayopendekezwa kwenye sheria za uchaguzi wakati wabunge wanajiandaa kuyajadili mapendekezo hayo mapema mwezi ujao.
Miswada yenye utata

Chanzo cha picha, IKULU TANZANIA
Baadhi ya mabadiliko yanayopingwa katika miswada hiyo ni pamoja na muundo wa kamati inayochagua makaminishna wa tume ya uchaguzi na uteuzi wa mwenyekiti na makamu wa mwenyekiti wa tume ya uchaguzi kufanywa na Rais, ambaye pia ni mwenyekiti wa chama tawala. Vyama vya upinzani wanataka mwenyekiti na makamu wa mwenyekiti wa tume wachujwe na kuchaguliwa na kamati huru pia.
Chadema inadai kuwa miswada hiyo ni mibaya sana kuweza kufanyiwa marekebisho. Wanataka miswada hiyo iondolewe na iandikwe upya kabisa.
Kwa sasa, chama hicho kinataka serikali iwasilishe muswada wa kuanzishwa kwa kutengenezwa kwa katiba mpya na mwingine kwa marekebisho ya katiba ya sasa ya mwaka 1977 ili kuruhusu sheria za uchaguzi za muda kufikiria uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwezi Oktoba na uchaguzi mkuu mwakani.
“Inawezekana kwamba maandamano haya yaliitishwa ili kuwaacha watu wapumue ili serikali iendelee na mambo yake bila kufanya mabadiliko yoyote yale ya maana,” anasema Deus Rweyemamu, mwanaharakati wa haki za binadamu na mchambuzi wa haki za binaadamu.
Viongozi wa Chadema wamedhamiria kuendelea na maandamano hayo nchi nzima kuishinikiza serikali kuandika upya miswaada ya sheria za uchaguzi zinazoakisi matakwa yao pia. Kufanikiwa kwa dhamira hiyo kunaangaliwa kama kipimo kingine cha nia ya Rais Samia Suluhu Hassan kutimiza ahadi yake ya kuleta mageuzi ya kidemokrasia nchini Tanzania.
Je, kuna matumaini ?

Chanzo cha picha, IKULU TANZANIA
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
“Tofauti ya sasa na wakati ule wa zama za Rais John Magufuli ni kwamba utawala ule haukujali kuufungamanisha uhalali wa serikali yake katika mageuzi ya kidemokrasia. Kitu ambacho serikali ya Samia inajali hilo,” anasema Dr Dan Paget, mhadhiri wa masuala ya siasa za Afrika katika Chuo Kikuu cha Sussex nchini Uingereza.
Ikiwa maandamano haya yatafanikiwa kuishinikiza serikali kushughulikia matakwa ya Chadema ama la ni jambo ambalo wachambuzi wengi wanasita kulithibitisha kwa wakati huu
“Ni mapema sana kusema hilo litawezekana kwa kiasi gani. Hasa ukizingatia kwamba Samia na serikali wapo katika majadiliano na Mfuko wa Maendeleo ya Milenia wa Marekani, hivyo wanacheza karata zao kwa umakini sana” anasema Rweyemamu.
Iwe ni katika uteuzi wa watumishi serikalini au katika chama chake Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia amefanikiwa kuvuruga utabiri wa nini hasa dhamira yake ama hatua yake inayofata itakuwa na uelekeo gani. Uteuzi mkubwa wa hivi karibuni wa Katibu Mkuu wa CCM Dkt Emmanuel Nchimbi ni kielelezo kimojawapo
Wakati Dkt Nchimbi anafahamika kwa misimamo yake, hasa ule ambao hata ulikwenda kinyume na maamuzi ya kamati kuu ya chama chake katika uteuzi wa mgombea wa urais wa chama hicho mwaka 2015, hotuba zake za hivi karibuni, hasa ile aliyoitoa mjini Dodoma wakati wa mapokezi yake ilikuwa na vionjo na viashiria vya maridhiano baina ya chama tawala na vyama vya upinzani
'Uzalendo'

“Pamoja na maendeleo yote tuliyonayo (kama chama), pamoja na mafanikio yote tuliyonayo, pamoja na ukweli kwamba tutashinda kwa kishindo, lakini hatukubali kuwa na kiburi. Bado tutaendelea kuwa wanyenyekevu. Tunapowaambia wapinzani kwamba tunawaomba jamani tukae tuzungumze, sio maana yake kwamba wana nafasi ya kushinda, hawana. Ni uungwana wetu, tunajua wajibu wetu ni kutumikia nchi yetu. Tunajua pia kwamba wapinzani nao wanayo nafasi ya kikatiba ya kushiriki kuijenga nchi. Ndio maana tunawabembeleza ‘jamani tukae tuzungumze’” alisema Nchimbi
Mchambuzi wa siasa na mfuatiliaji wa karibu wa harakati za Chadema, Dkt Aikande Kwayu anasema hataki kuwa na matumaini makubwa sana kwamba serikali itafanya mabadiliko ya msingi kulingana na matakwa ya Chadema.
“Samia alikuwa anazungumzia maridhiano, lakini yakashindikana, akazungumzia mageuzi lakini tunaona hicho walichokipeleka bungeni kwenye hii miswada. Ningetamani kuwa na matumaini makubwa, lakini naona kuna nguvu kubwa sana anayopambana nayo ndani ya chama chake mwenyewe” anasema Dkt Kwayu.














