Je hizi ndizo siasa wanazozitaka Tanzania?

mm
    • Author, Yusuph Mazimu
    • Nafasi, BBC Swahili

Rais Samia Suluhu Hassan, ametimiza mwaka mmoja madarakani, baada ya kuwa mwanamke wa kwanza katika historia ya taifa hilo kushika nafasi hiyo ya juu kabisa ya uongozi akimrithi John Magufuli, aliyefariki dunia mwezi Machi mwaka 2021.

Tangu aingine madarakani mwezi Machi 2021 kumekuwa na mabadiliko kadhaa ya kimtazamo yanayoanza kuonekana kuhusu siasa, vyama vya siasa, wanasiasa na demokrasia kwa ujumla ya nchi hiyo.

m

Kakutana na wanasiasa wa upinzani, karuhusu maoni ya kuboresha kanuni za mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, uhuru kiasi wa habari, uhuru kiasi wa kukosoa na mengine kwenye uga wa siasa na demokrasia ya nchi hiyo.

Kwa muelekeo huo huo alipozungumza na BBC katika mahojiano maalumu yaliyorushwa leo, ameyagusia pia mambo kadhaa yanayoashiria uelekeo tofauti wa kisiasa na demokrasia nchini humo.

Lakini Je, huu ndio muelekeo na siasa wanayoitaka watanzania? Maelezo afuatayo yatakupeleka kwenye hoja zilizopo juu ya swali hili.

Alichoiambia BBC Rais Samia na alichokifanya katika mwaka mmoja uliopita .

Akizungumza na BBC Rais Samia amesisitiza kwa mara nyingine kwamba yeye na mtangulizi wake Magufuli "walikuwa kitu kimoja'' akibainisha kwamba tangu aingie madarakani amekuwa akifuata nyayo za mtangulizi wake huyo.

m

"nilisema katika majukwaa tofauti, kwamba mimi na Magufuli ni kitu kimoja, kwa sababu wote tumetokana na CCM, wote tulifanya kazi miaka mitano, tulipanga wote mipango", alisema Samia katika mahojiano maalumu na BBC kuhusu mwaka wake mmoja madarakani na Kuongeza "lakini nikasema nitaendeleza mema yaliyopita na kuleta mema mapya na kwa hiyo watu watarajie mabadiliko'.

Pengine kauli hii inathibitishwa na aliyoyafanya katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita kwenye eneo la siasa na demokrasia.

Katika kipindi hicho Rais Samia amezungumza mara kadhaa nia yake ya kukutana na wapinzani, licha ya kuchukua muda mrefu kukutana na baadhi yao hasa kutoka chama kikuu cha Upinzani, CHADEMA, lakini amefanya hivyo.

mm

Amekutana nchini Ubelgiji na Mgombea urais wa CHADEMA katika uchaguzi uliopita wa 2020, Tundu Lissu ambaye pia makamu mwenyekiti kabla ya juma lililopita kukutana na mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, aliyekuwa gerezani kwa karibu miezi nane, akituhumiwa kwa makosa ya ugaidi. Mwendesha mashitaka wa kesi ya Mbowe aliiondoa kesi hiyo kwa kuieleza Mahakama hana nia ya kuendelea nayo, na mara baada ya kuachiwa akakutana na Rais Samia Ikulu Dar es Salaam.

Amemteua mgombea urais wa upinzani katika uchaguzi mkuu uliopita, naibu katibu mkuu wa chama cha ADC, Queen Sendiga kuwa mkuu wa mkoa wa Iringa, moja ya mikoa inayosifika kwa uzalishaji wa chakula Tanzania.

Hivi karibuni yeye na Rais wa Zanzibar walishiriki mkutano wa wadau wa siasa unaoangalia hali ya demokrasia ya vyama vingi nchini humo, licha ya awali mkutano huo kususiwa na baadhi ya vyama kikiwemo CHADEMA.

Akaunda Kikosi kazi cha kuratibu maoni ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa, chini ya uenyekiti wa Profesa Rwekaza Mukandala. Kama haitoshi juma lililopita alimuagiza Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge kuandaa kanuni zitakazoelekeza jinsi ya kufanya mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa.

Hata hivyo John Heche, mbunge wa zamani wa bunge la Tanzania, na mjumbe wa kamati kuu ya CHADEMA, kupitia mtandao wake wa twitter leo ameonyesha wasiwasi wake, hasa baada ya Baraza la vyama vya siasa Tanzania kueleza kuridhia kwa kauli moja vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu kuwasilisha mapendekezo ya kuboresha kanuni za mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa.

Hisia mseto kuhusu kauli za Samia, matendo na muelekeo wa siasa Tanzania

Hisia tofauti zimeendelea kutawala, kuhusu hatua, kauli na mienendo ya Rais Samia kuhusu siasa na demomkrasia ya vyama vingi nchini Tanzania, hasa baada ya kuieleza BBC kuhusu mabadiliko na hatua alizoanza kuchukua.

'nimemsikiliza mama (Samia) BBC leo na nimemfuatilia toka ameingia madarakani, ukweli kuna utofauti mkubwa na mtangulizi wake kwenye siasa, hatujafika kuwa kama wenzetu Kenya, lakini muelekeo unatoa picha ya siasa tunazotaka", anasema Innocent Mushi wa Moshi.

Kwa hatua kadhaa anazochukua kama zilivyotajwa awali, Raia anaonyesha dhamira na nia yake kwenye eneo hili la siasa na demokrasia Tanzania.

m

Chanzo cha picha, Getty Images

"Kuna dalili nzuri. Rais Samia amejipambanua kuwa tofauti na Mtangulizi wake Rais Magufuli. Hatua yake ya kukutana na viongozi wa Vyama vya Siasa na kauli zake za kuwa tayari kufungua ukurasa wa kisiasa zinatia moyo. Muhimu ni kwamba ni lazima tuguse kiini cha tatizo ambacho ni Katiba mbovu tuliyonayo', Ado Shaibu, katibu mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo ameiambia BBC.

Muda mfupi baada ya kuingia madarakani kupitia uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa Tanzania ilipigwa marufuku akitaka watu 'kuchapa' kazi kwanza. Marufuku hiyo iliendelea kwa zaidi ya miaka 6 mpaka awamu hii.

Uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2019 na chaguzi ndogo katika majimbo na kata kati ya mwaka 2015 mpaka 2020 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 ulilalamikiwa kuwa na mapungufu na udanganyifu mkubwa. Licha ya utata wake, Tume ya taifa ya Uchaguzi ya Tanzania ilieleza mara kadhaa kwamba chaguzi zote zilikuwa zilizofanyika zilikuwa huru na haki kwa mujibu wa sheria.

Mikutano ya ndani pia ya vyama vya upinzani ilikutana na 'misukosuko' ya kunyimwa vibali kwa kile jeshi la Polisi kusema mingine ina viashiria va uvunjifu wa Amani kutokana na uchunguzi wao wa kiintelijensia.

m

Kama ataruhusu mikutano ya hadhara, ataruhusu katiba mpya, vyombo va habari na watu wakawa huru kusema na kueleza, tukakosoana kwa staha kama wakenya tunavyowasikia na uchaguzi wao, basi siasa zitakuwa nzuri, na zitavutia hata sie wanawake kushiriki kwa wingi', alisema Rosemary Macha, binti mwenye ndoto ya kuwa mbunge.

Kauli za Rais Samia, Mbowe na uelekeo wa siasa za kesho

Akizungumza na waandishi wa habari mchana wa leo, Mwenyekiti wa CHADEMA, Mbowe amewataka wafuasi wa chama hicho kusamehe yaliyotokea nyuma kwneye harakati za siasa na demokrasia.

"tumeumizwa sana, nawaomba wanachedema wenzangu, tusamehe, lakini katika kusamehe kwetu tusitoke nje ya ajenda yetu (katiba mpya), tuzungumze kutafuta suluhu, milango iliyofunguliwa tutaingia tujadili, lakini tunapoona kinachojadiliwa ni tofauti na tunachokiamini tutatoka, na tutatoka kwa haraka na tutauamia umma wa watanzania na dunia', alisema Mbowe.

M

Chanzo cha picha, IKULU

Beatrice Kimaro, mchambuzi wa siasa Tanzania, anasema kauli za Rais Samia katika mahojiano na BBC na kauli kama hii ya Mbowe ni dalili nzuri ya namna siasa za Tanzania zinavyopaswa kujielekeza, kwenye kuaminiana, kusikilizana, kuambiana ukweli, na kwenye makosa kusameheana',

Katibu mkuu wa ACT Wazalendo, Shaibu aliunga mkono uelekeo wa siasa za mazungumzo na maridhiano kuliko uhasama.

"ACT Wazalendo tunaamini katika siasa za kushindana kwa hoja badala ya uhasama. Tulikotoka tulianza kubaguana kiitikadi. Ni lazima tuchore mstari na kufungua ukurasa Mpya wa Siasa za kistaarabu', alisema Shaibu.

Katika mwaka mmoja uliopita Rais Samia, ambaye ni mwenyekiti wa chama tawala, CCM, amekuwa kiongozi aliyejinasibu kutaka kurejesha imani kwenye siasa na demokrasia ya taifa hilo, ambayo ilikutana na 'dhoruba' katika utawala wa awamu ya tano chini ya Magufuli.

"Rais ameonyesha nia njema, Rais amesimama mbele ya kamera na amesema tutakutana mbele ya haki, ni kauli kubwa kutolewa na kiongozi wa nchi', alisema Mbowe.

Maelezo ya video, Mwaka mmoja tangu achukue mamlaka, Je Rais Samia amefuata nyayo za Magufuli?

Pamoja na hayo, Kauli za Rais na mitazamo ya baadhi ya watu waliotoa maoni yao wakiwemo wanasiasa, na wananchi wa kawaida yapo matumaini ya baadaye ya uwepo wa siasa na demokrasia yenye matumaini, swali kubwa la kuangaziwa ni je siasa na demokrasia wanayoitaka watanzania itafikiwa lini na kwa haraka kiasi gani?