Rais wa zamani wa Zambia Rupiah Banda afariki

m

Chanzo cha picha, AFP

Rupiah Banda, ambaye alikuwa rais wa Zambia kuanzia mwaka 2008 hadi 2011, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 85 baada ya kuugua saratani ya utumbo mpana.

"Maisha yake ya utumishi kwa nchi yetu, na kwa bara letu, yanawakilisha aina ya juu zaidi ya uzalendo," Rais Hakainde Hichilema alisema.

Bw Banda, mwanadiplomasia wa zamani, alikuwa akihudumu kama makamu wa rais mwaka 2008, Rais Levy Mwanawasa alipougua kiharusi na baadaye kufariki.

Kisha alichukua wadhifa huo, na kuwa rais wa nne wa nchi, na akashinda uchaguzi uliofuata.

Lakini alijiuzulu mnamo 2011 baada ya kushindwa katika kura ya maoni ya mwaka huo dhidi ya Michael Sata. Bw Banda alisifiwa sana wakati huo kwa kukubali kushindwa, badala ya kupinga matokeo.

Muda wake madarakani ulitawaliwa na tuhuma za ufisadi na mwaka 2013 alikamatwa baada ya kutuhumiwa kuiba mamilioni ya dola.

Alikanusha mashtaka hayo, akieleza kuwa ni sehemu ya uwindaji wa wakosaji, na hakuwahi kuhukumiwa.