Utafiti: Omicron inaonekana kuwa dhaifu lakini wasiwasi bado upo

m

Chanzo cha picha, Getty Images

Kwa mujibu wa tafiti za awali zilizochapishwa nchini Uingereza na Afrka ya kusini zinaonesha kuwa wimbi la kirusi cha corona aina ya Omicroni si kali kulinganisha na aina nyingine ya virusi vilivyopita.

Ushahidi wa awali unaonesha kuwa watu wachache wanahitaji matibabu ya hospitali kuliko aina zingine ambapo makadirio yamepungua kati ya asilimia 30 hadi asilimia 70.

Lakini wasiwasi unabaki palepale hata kama wimbi hili si kali kwani hospitali zinaweza kuzidiwa na idadi kubwa ya watu wenye kesi za omicroni.

Kwa mara kwanza, zaidi ya kesi 100,000 zimeripotiwa nchini Uingereza ndani ya siku moja.

m

Chanzo cha picha, Getty Images

Uelewa wa kina juu ya makali ya omicron, kutasaidia nchi kuamua namna ya kukabiliana na virusi hivyo.

Utafiti unasema kuwa endapo Omicron ingekuwa na tabia kama za Delta, wangetarajia takribani watu 47 wawe wamelazwa hospitalini tayari. Kwa sasa ni watu 15 tu waliolazwa.

Watafiti wanasema wanaona kupungua kwa takriban theluthi mbili kwa idadi inayohitaji huduma za hospitali, lakini katika utafiti huo kulikuwa na visa vichache na wazee wachache walio hatarini.

Mkurugenzi mkuu anayehusika na covid 19 katika hospitali ya umma nchini Scotland ameelezea hali hiyo kuwa ni habari nzuri iliyothibitishwa. Kirusi aina ya Omicron kinasambaa kwa haraka sana na idadi kubwa ya kesi inaweza kufuta faida yoyote ya kuwa ni dhaifu.

Profesa Mark Woolhouse, kutoka Chuo Kikuu cha Edinburgh, anasema "Maambukizi ya mtu binafsi yanaweza kuwa si makali kwa watu wengi, lakini uwezekano wa maambukizo haya yote kuja mara moja na kuleta mzigo mkubwa katika huduma za afya kitaifa bado upo.

Wakati huo huo, utafiti mwingine nchini Afrika Kusini pia unaonyesha kuwa wimbi la Omicron ni dhaifu zaidi.

Unaonesha kuwa kulikuwa na uwezekano mdogo wa watu kuhitaji matibabu ya hospitali kwa asilimia 70 mpaka 80 ukilinganisha na mawimbi ya awali au aina nyingine za virusi vya corona .

Hata hivyo, inapendekeza hakukuwa na tofauti katika matokeo kwa wagonjwa wachache ambao waliishia hospitalini na Omicron.

"Lakini, kwa pamoja data zetu zinapendekeza habari chanya juu ya kupungua kwa ukali wa Omicron ikilinganishwa na aina nyingine," alisema Prof Cheryl Cohen wa Taasisi ya Kitaifa ya Magonjwa ya Kuambukiza, nchini Afrika Kusini.

Kwanini Dhaifu

Kupungua kwa ukali kunadhaniwa kuwa ni mchanganyiko wa sifa za msingi za Omicron pamoja na viwango vya juu vya kinga dhidi ya chanjo na maambukizi ya awali.

Uchambuzi wa Omicron uliofanywa na chuo cha Imperial College mjini London unapendekeza mabadiliko ya Omicron yameifanya kuwa virusi hafifu kuliko Delta.

Watafiti wanasema uwezekano wa wagonjwa katika idara ya dharula imeshuka kwa 11% kwa upande wa Omicron kuliko Delta ikiwa huna kinga ya hapo awali.

Hata hivyo, kwa sasa inatumika kwa watu wachache nchini Uingereza kutokana na viwango vya juu vya chanjo na maambukizi.

Mmoja wa watafiti Profesa Neil Ferguson, alisema: "Ni wazi kuwa ni habari njema, kwa kiwango fulani."

Lakini alionya kupungua hakutoshi kubadilisha muundo na kasi ambayo Omicron inaeneza akimaanisha kuna uwezekano wa kulazwa hospitalini kwa idadi ambayo inaweza kuziweka huduma za hospitali katika hali ngumu".

Mtaalam wa chanjo wa Chuo cha Imperial profes Peter Openshaw ambaye hakuwa mmoja wa waandishi wa utafiti huo alisema dalili za mapema.

Zilionyesha kuwa hali inaweza kuwa mbaya zaidi lakini akasema kuwa tafiti hizo zinaonyesha imebadilika na kuwa homa ya kawaida .

Uchunguzi wa maabara umeelezea sababu zinazofanya Omicron kuwa dhaifu.

Chuo Kikuu cha Hong Kong kiligundua kuwa Omicron alikuwa bora zaidi katika kuambukiza njia za hewa, lakini mbaya zaidi katika kuingia kwenye tishu za kina za mapafu, ambapo inaweza kufanya uharibifu zaidi.

Chuo Kikuu cha Cambridge kilisema aina hiyo ya corona haikuwa nzuri katika kuunganisha seli za mapafu, ambayo hutokea kwenye mapafu ya watu na kufanya mtu kuwa mgonjwa sana.

Shirika la Usalama wa Afya la Uingereza linatarajiwa kuchapisha takwimu za awali juu ya hali halisi kuhusu Omicron hivi karibuni, ambayo inaweza ikatoa dalili kali zaidi za aina hii ya corona.