Je, Shirika la ndege Tanzania linatoka Shimoni kwenda gizani?

- Author, Beatrice Kimaro
- Nafasi, Mchambuzi, Tanzania
Serikali ya Tanzania imeendelea kuagiza ndege za aina mbalimbali zikiwemo zingine nne mpya licha ya Shirika lake la ndege (ATCL) kutengeneza hasara ya mamilioni ya dola katika kipindi cha miaka mitano mpaka kumi mfululizo.
Kulingana na Ripoti iliyotolewa mwaka huu na ofisi ya mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG) ilisema ukaguzi wa mwaka mmoja pekee wa 2019/2020 ilibainika Shirika hilo lilitengeneza hasara ya Tsh. Bilioni 60, huku ikiendelea kutengeneza hasara ya shilingi bilioni 150 katika miaka mitano mfululizo.
Mtu mwingine angeweza kujiuliza, kwanini niwekeze kwenye biashara isiyolipa? Au biashara inayokupa hasara? Lakini Serikali ya Tanzania imeendelea kuweka fedha zake kwenye ndege.
Kutoka Shimoni
Unaweza kusema, ATCL ilikuwa shimoni, tena kwenye shimo kubwa hasa kabla ya utawala wa serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani mwaka 2015.
Aliyekuwa Rais wa awamu hiyo, John Magufuli alisukuma uamuzi wa kulifufua Shirika hili, ambapo alisimama kidete hasa mwaka 2016 na kuwekeza mamilioni ya pesa kununua ndege kwa ajili ya Shirika la ndege la Tanzania kama hatua muhimu ya kulipanua shirika hilo katika utoaji wa huduma na kuimarisha sekta ya anga ya nchi hiyo.
Katika kipindi cha miaka 5 iliyopita kutoka kuwa na ndege moja iliyokuwa inasuasua mpaka kuwa na ndege 11, ni hatua kubwa ya kulitoa shimoni Shirika hili. Hatua inayoonekana kuwa na uelekeo fulani wa kulipanua na kulisogeza mbele Shirika hilo.
Mpaka sasa kati ya ndege 11 zilizonunuliwa awali, ndege 9 zimekwishawasili na zinaendelea kutoa huduma, huku ndege mpya ya hivi karibuni aina ya Bombadier Dash 8-Q400 ikipokelewa na Rais Samia Suluhu, ambaye aliwahi kukiri kuhusu ugumu wa biashara ya ndege.
'Sote tunafahamu kuwa biashara ya ndege ni ngumu, tutajitahidi kusoma mwenendo wa biashara hii ulimwenguni na kuepuka mambo yote yasiyo na tija kwa shirika letu', alisema Rais wa Tanzania Samia Suluhu, akilihutubia bunge mapema mwaka huu muda mfupi baada ya kuingia madarakani.
Pamoja na ugumu wa biashara ya anga Serikali ya Tanzania kuendelea kulilea na kununua ndege kwa ajili ya Shirika hili ambalo lilikuwa 'maututi' miaka michache iliyopita, ni dhahiri kuna kitu inataka.
Kwa muktadha wa kawaida inataka kulipa uhai tena, lipumue liweze kukua na kutanua sekta yake ya anga, Lakini mtu wa kawaida anaweza kujiuliza, kwa nini taifa hilo linajiahangaisha sana na Shirika hilo, ama linahaha kulitoa Shimoni Shirika hili licha ya kutengeneza hasara?
Kutoka Shimoni, ATCL ielekee gizani?

Mwekezaji bilionea mkubwa duniani Warren Buffett aliwahi kusema, "kuwekeza kwenye biashara ya ndege ni kubahatisha 'ku-bet. Haijalishi kama Shirika linamilikiwa na Serikali ama makampuni binafsi, soko la ndege halina mwenyewe".
Hakuna asiyeona jitihada za Serikali ya Tanzania na hata viongozi wa ATCL kulitoa Shirika hili kwenye shimo, lakini kutoka shimoni ni jambo moja, baada ya kutoka shimoni uelekeo ni upi? Msingi wa swali hili ni kutokana na namna biashara ya anga ilivyo duniani.
Ni biashara yenye changamoto kubwa na ni biashara rahisi kutengeneza hasara kuliko faida. Changamoto hizo ni sawa na kusema 'gizani', ili kuona njia yako unahitaji kubahatisha pa kukanyaga.
Moja ya changamoto kubwa ni ushindani mkubwa wa soko na gharama kubwa za uendeshaji ikiwemo mafuta ya ndege, ubora wa huduma, usalama na majanga kama haya ya Covid 19.
Tumeshuhudia wakati huu wa Covid kwa mfano, mashirika mengi ya ndege yameingiza hasara kubwa, licha ya jitihada kubwa za serikali nyingi duniani kuyapa uhai kwa kuyapa unafuu wa kibiashara, tozo na kuyapa fedha za kusaidia uendeshaji.
Kwa mujibu wa mtandao wa Flyingmag mashirika 6 ya ndege makubwa duniani ya umma, yametengeneza hasara ya dola bilioni 110 kwa mwaka 2020 tu: Mashirika ya Delta Airlines, American Airlines, Lufthansa Group, United Airlines, Air France-KLM na IAG.
Kwenye eneo la ushindani kibiashara, Shirika kama la America Airlines lina ndege zaidi ya 900, Delta Airlines lina ndege zaidi ya 800 na mengine kama Southwest, United Airlines yana ndege zaidi ya 700 kila mmoja huku mashirika kama Lufthansa, Emirates, Britisha Airways, Turkish Airlines, Ryanair na Easy Jet yana zaidi ya ndege 200 kila mmoja.
Huku sio kurahisi kwa ATCL kupitia ndege zake za Air Tanzania ambazo kwa miaka mitano iliyopita imefanikiwa kununua ndege 11 tu. Sio haba lakini safari ni ndefu.
Hata Ukilingaisha kwa ukaribu na mashirika ya nchi jirani kama Kenya yenye ndege zaidi ya 30, zikiwemo Boeing 787 Dreamliner, Boeing 787- 800s na Boeing 787-700s, ikienda vituo zaidi ya 40 Afrika na 13 nje ya Afrika.
Hata kama baadhi ya ndege ni za kukodishwa, lakini kumiliki ndege 19, hakuwezi kuwa sawa na kumiliki ndege 11, kibiashara tofauti ya ndege moja ni kubwa mno.
Kwa sasa Uganda Airlines inayoringia ndege zake nne za Bombardier CRJ-900 na mbili za Airbus A330-800, nayo inajitoa shimoni kama Tanzania. Shirika la ndege la Rwanda, Rwanda Air licha ya kuwa na ndege 12, linakwenda kwenye vituo zaidi ya 30 kwenye nchi za Afrika, Mashariki ya kati, Asia na Ulaya.
Ni mbali kuifananisha Air Tanzania na Ethiopia Airlines ya Ethiopia kama baba wa anga Afrika, ikitajwa kuwa shirika la ndege la nne duniani kwa kuhudumia nchi nyingi duniani au mashirika kama Egypt Air (Misri), Air Algerie (Algeria), South Africa Airways (Afrika Kusini) au Tunis Air (Tunisia)
Jitihada hizi za kuitoa shimoni ATCL zitalipa?

Chanzo cha picha, IKULU
Ukirejea huko nyuma, tangu Shirika hili lianzishwe mwaka 1979, limekuwa na vipindi tofauti vya kupanda na kushuka. Wakati Air Tanzania inaanzishwa, lilikuwa linadhibiti 2% pekee ya soko la anga Tanzania, lakini mpaka kufikia mwaka 2018, lilikuwa linadhibiti asilimia 75% ya soko la ndani, hatua iliyochangiwa zaidi na ununuzi wa ndege mpya uliofanywa, na uwekezaji wa mamilioni ya fedha kwa rasilimali watu na miundo mbinu ya viwanja vya ndege vya ndani.
Ripoti ya kwanza kabisa ya mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali Tanzania, wakati huo Profesa Assad, ilionyesha hasara ya shirika hilo kwa miaka 10 mfululizo. Inaelezwa Shirika lina madeni ya shilingi bilioni 412, kama tulivyosikia bungeni.
Ama huu uwe ukweli ama uongo, haijalishi, Shirika kama hili hata kama linakuwa na deni hata la bilioni 1, kama halijiendeshi lenyewe kwa faida, bado litaendelea kuwa 'gizani'.
Dr. Isack Kazungu, mmoja wa wabobezi wa masuala ya biashara na mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Ushirika anaamini kuingiza faida inawezekana, lakini sio rahisi na kwa haraka.
'itachukua muda kidogo, lakini inawezekana kupata faida, hata hayo mashirika makubwa yalichukua muda, muhimu ni kuwa na 'mpango biashara' mzuri na unaotekelezeka" alisema Dr. Isack Kazungu.
Halikadhalika taarifa ya Waziri wa Mipango na fedha, Mwigulu Mchemba iliyotajwa bungeni kuhusu usafiri wa anga, kuna kuboreka kwa shughuli za anga, miruko ikiongezeka mpaka 292,105 kutoka 225,000 mwaka 2015 wakati huo Shirika likiwa na ndege moja.
Hata hivyo, wapo wabunge walioona hatua hiyo kama ni ya kawaida
'tulikuwa na ndege moja miruko ya ndege ndani na nje, ilikuwa 225,000 mwaka 2015, tulivyokuwa na ndege 11, miruko imekuwa 292,105 ndani ya miaka 5, umetoka ndege 1 kuja 11 katika miaka 5, tulichofanikiwa ni miruko ya ndege 67,000 tu! Alihoji Halima Mdee, mbunge wa viti maalumu.
Kuwepo kwa ndege 11 za Shirika la ndege la Tanzania, kumeongeza pia idadi ya abiria katika kipindi hicho kutoka 4,207,000 kwenda 4,268,000 hiki ni kitu muhimu zaidi linapokuja suala la uwekezaji kwenye biashara ya ndege. Unaweza kuwavuta abiria kutumia ndege zako? Unaweza kupanua shirika kupokonyana abiria na mashirika mengine yanayotoa huduma hiyo?
Ndio maana yapo mataifa ambayo, yameacha mashirika binafsi yahodhi biashara ya anga, na yenyewe kujielekeza kwenye masuala mengine ikiwemo viwanda, teknolojia na kilimo. Lakini waswaili wanasema kuteleza si kuanguka, ilimradi wajua uendako jipanguse kanyaga twende.
Kupanga ni kuchagua, Tanzania ichague giza ama shamba

Chanzo cha picha, IKULU
Shirika la ndege la Tanzania lina machaguo matatu makuu ya kuyaangalia na baadae kujielekeza kwenye chaguo moja. Kuondoka sokoni moja kwa moja kwa kuuza hisa zote kwa mbia, kuingia ubia na mashirika ama makampuni makubwa na chaguo la tatu ni kufungamanisha sekta ya anga na sekta za kiuchumi, huku nimekuita shambani, sekta kama Utalii, biashara na kilimo ili iweze kuvuna na kujenga uchumi wake na watu wake.
Mwaka 2019 Tanzania iliuza nje ya nchi mazao yenye thamani ya dola milioni 700 na ikitarajiwa kuingiza dola bilioni 2 kufikia mwaka 2025.
Lakini imelenga kuongeza watalii kufikia milioni 5 ifikapo mwaka 2025 kutoka milioni 1.5 mwaka 2019, kwa mujibu wa Rais Samia. Kwa kauli hii hili ndilo linaloonekana chaguo muhimu kwa sasa kwa Tanzania linalopaswa kuangaliwa. Kuangalia sekta nyingine kwa jicho la sekta ya anga. Faida ya nyuma ya pazia ni muelekeo mzuri wa kutoka gizani, kuliko faida ya moja kwa moja ya uuzaji wa tiketi za ndege.
Ripoti nyingi za Shirika linalosimamia mashirika ya ndege duniani, zinaonyesha kazi kubwa ya msingi ya mashirika mengi ya ndege duniani, ni kuchochea uchumi mwingine, si lazima shirika lenyewe kutengeneza faida.
Kenya Airways mwaka 2016/17 ilirekodi hasara ya dola mil 249, mwaka uliofuata wa 2018 hasara ikapungua kwa asilimia 51 zikaenda dola 97mil hasara. Mwaka 2017 Shirika la ndege la Afrika Kusini lilirekodi hasara ya dola mil 153, lakini uchumi mwingine uliendelea kuchochewa'.
Kenya na Afrika Kusini kiuchumi ziko mbali ukilinganisha na Tanzania, kutokana na mchango wa sekta yake ya anga kwenye uchumi wake kwa muda mrefu zaidi.
Wachumi wanasema ili iweze kufikia chaguo hili ni lazima machaguo ya kwanza yasitelekezwe.
'wazo langu ATCL ingeingia ubia wa kibiashara na mashirika ama makampuni mengine makubwa hata matatu, ili isibebe mzigo yenyewe, wabia hawa wawe wazoefu wakubwa wa nga, Shirika litapata nafuu,', alisema Barnos Willium, mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi.
Mwaka 2019 mashirika matatu makubwa Ulaya Wow Air, Germania na British Midland Regional yalisitisha huduma lakini katika miongoni miwili iliyopita mashirika mengi tu yaliondoka sokoni, kwa kufa ama kuunganisha nguvu na mashirika mengine ama kutengeneza mapya kutokana na changamoto za biashara ya anga.
Northwest na Delta zimeunda Delta Air lines, TWA ikanyakuliwa na American Airlines, US Airways ni muunganiko wa America West na US Air zilizo kumbana na changamoto, Canadian Airlines imepotea kibiashara sasa kuna Air Canada. Nchini Brazil kulikuwa na Shirika la Varig limetwaliwa na Gol.
Shirika la ndege la India 9 (Air India) mwezi uliopita tu limeuzwa kwenda kwa Tata group, ambalo liliianzisha shirika hilo mwaka 1932 kabla ya mwaka 1953 Serikali kulichukua na sasa maji yamewafika shingoni baada ya kutengeneza Hasara ya dola bilioni 9.5. Serikali ya India ilikiri kutengeneza hasara ya dola mil 2.6 kila siku kuliendesha Shirika hilo.
Kama mtandao wa theafricalogistics.com ulivyoeleza Kenya Airways kwa sasa linamilikiwa kwa ubia (public-private partnership) Serikali yake ikiwa na hisa 48.9% , 38.1% zikimilikiwa na KQ Leaders Company 2017 Ltd, KLM asilimia 7.8 huku hisa zingine zikimilikiwa na wengine wanaozisaka kwenye masoko ya hisa ya Nairobi, Dar es Salaam na Uganda.
Unaweza kusoma pia:
Licha ya hasara inazorekodi, unafuu unaoipata unabebwa na chaguo la pili la kufanya biashara fungamanishi. Inawezekana chaguo la kuachana na biashara ya ndege moja kwa moja, lisiwe chanya kwa Serikali ya Tanzania, kutokana na dhamira na hatua iliyokwishachukua kwenye kulifufua shirika lake na ndege zake za Air Tanzania, inaweza kukopa mawazo mengine ya chaguo la pili ili kupiga ndege wawili kwa jiwe moja; kupunguza makali ya hasara ikiendelea kuwa sokoni na kufungamanisha sekta ya anga na sekta zingine muhimu za kiuchumi ikiwemo utalii, biashara na kilimo. , pamoja na kugeuza ndege za abiria kuwa za mizigo ili kuitumia fursa iliyopo ya kusafirisha mizigo mbalimbali hapa nchini kwenda nchi za nnje ili kujipatia faida mara dufu.
Kwa kufanya hivi, inaweza kutoka shimoni na kuelekea shambani badala ya gizani, yalipo mashirika mengi hasa ya nchi zinazoendelea.














