Bidhaa 10 mwiba kwa watanzania

- Author, Beatrice Kimaro
- Nafasi, Mchambuzi, Tanzania
Septemba 10, 2021, wakati wa kuahirisha Mkutano wa nne wa Bunge la 12 jijini Dodoma, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema Serikali imeunda timu maalumu ili kuchunguza kupanda kwa bei ya mafuta kwa kuwa kitendo hicho kinawaumiza wananchi hususan wale wa hali ya chini.
Pia, Novemba 24, 2021 Waziri wa Viwanda na Biashara nchini Tanzania, Profesa Kitila Mkumbo wakati akizungumzia hatua wanazochukua baada ya kupanda kwa bei ya vifaa vya ujenzi nchini, aliiagiza Tume ya Ushindani wa Biashara nchini (FCC) kufanya uchunguzi kuhusiana na kupanda kwa bei ya saruji nchini humo.
Kauli hizi za vingozi waandamizi wa Serikali zinakupa picha kubwa kwamba tatizo la kupanda kwa bei ya baadhi ya bidhaa nchini humo sio la kuchukulia mzaha.
Inaona bila hatua kuchukuliwa, kupanda huko kutaendelea kutikisa maisha ya watu wa kipato cha chini ambao wanategemewa kuwa na mchango katika ujenzi na ukuzaji wa uchumi mdogo wa taifa.
Katika kipindi cha hivi karibuni bidhaa hizi zimeonekana kuwa mwiba kwa bei yake kupanda. Mfano wa bidhaa hizo ni pamoja na;
1: Mafuta ya kupikia, mafuta ya Petrol, dizeli na mafuta ya taa

Kupanda kwa bei ya mafuta ghafi sokoni ilianza kushuhudiwa mwezi Aprili 2020.
Kupanda kwa bei hii kukaathiri bidhaa karibu zote kwenye soko, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) linaonyesha sababu kubwa ni kuongezeka kwa gharama za uzalishaji na usafirishaji.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) bei ya mafuta ghafi nchini Tanzania imekuwa ikiongezeka tangu mwezi Mei, 2020 ambapo bei imeongezeka zaidi mara mbili kutoka wastani wa dola za Marekani 32 kwa pipa mwezi Mei, 2020 hadi kufikia dola za Marekani 86 kwa pipa mwishoni mwa mwezi wa Oktoba.
Pia mwanzoni mwa Novemba, 2021, EWURA ilitangaza kushuka kwa bei ya kikomo ya mafuta kwa asilimia 18, isipokuwa mafuta ya Dizeli yaliyopokewa katika bandari ya Dar es Salaam na kukiri bila jitihada za Serikali, bei za rejareja za bidhaa za mafuta zimeongezeka maradufu.
Septemba mosi, 2021, Serikali ilisitisha bei mpya zilizotangazwa na EWURA ili kufanya uchunguzi kwa nini bei ya mafuta imekuwa ikipanda mara kwa mara hasa mafuta ya petroli, dizeli, mafuta ya taa na mafuta ya ndege.
Mafuta ya kupikia nayo yamepanda katika kipindi kifupi kilichopita. Kwenye baadhi ya maeneo ya nchi, lita moja ya mafuta ya kupikia kwa sasa ni wastani wa shilingi 4,400 mpaka 4,700 kutoka wastani wa shilingi 3,000 mpaka 3,700 kwa lita moja, miezi michache iliyopita.
2: Vyakula kama nyama, unga wa ngano na viungo

Kama kuna eneo ambalo limekuwa likigusa wengi, ni eneo la chakula. Kila binadamu ili aishi lazima ale, na uchumi unamtaka mtu mwenye afya njema, ili kuujenga uchumi wa mtu binafsi na uchumi wa taifa lake, chakula ni msingi.
Kwa mfano, mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia Julai, 2021 uliongezeka hadi kufikia asilimia 5.1 kutoka asilimia 4.7 kulinganisha na kipindi kilichopita.
Takwimu za Agosti, 2021 za Shirika la takwimu nchini Tanzania, NBS zinaonyesha bei ya ngano nchini humo iliongezeka karibu kwa asilimia 6.8 na nyama ya ng'ombe iliongezeka kwa asilimia 3.4, huku mfumuko wa bei ukiongezeka na kufikia asilimia 4 kwa mwezi Septemba kutoka asilimia 3.8 ya mwezi Agosti.
Kuongezeka kwa mfumuko wa bei kumechangiwa na kuongezeka kwa mfumuko wa bei za bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula kwa Septemba 2021 ikilingnishwa na Septemba mwaka jana" alisema Ruth Minja, Kaimu Mkurugenzi wa Sensa ya watu na takwimu za jamii.
Kwa mwezi Novemba kwenye mabucha mengi ya nyama ya ng'ombe, nyama iliyokuwa inauzwa kati ya shilingi 6,500 mpaka 7,500 imepanda na kufikia kati ya shilingi 7,500 mpaka 9,000.
Fungu la samaki la kawaida mfano kibua wanaoliwa sana eneo la pwani ya nchi hiyo, limepanda mpaka shilingi10,000 kutoka wastani wa shilingi 6,500 na 7,500.
Kitunguu kwenye masoko mbalimbali mfano mabibo mwezi Oktoba kilipatikana kwa shilingi 1,000 kwa kilo sasa ni Tsh 1,300.
Viazi vitamu na viazi mviringo pia vimekumbana na mfumuko wa bei.
Sababu ya kupanda kwa bei za bidhaa
Zipo sababu nyingi, zinazoweza kuhusianishwa na kupanda kwa bei ya bidhaa kwa mfano vyakula nchini Tanzania.
Mabadiliko ya tabia nchi ni sababu inayofahamika zaidi, hata kama athari zake unaziona kwa jicho la pembeni.
„Tumeanza kushuhudia maeneo mengi yakikumbwa na ukame, ama mafuriko, joto kali na mvua zisizotabirika, hii huathiri kilimo na kilimo ndio chanzo kikuu cha chakula', alisema (Dokta. Rashidi Chikoyo)
Sababu nyingine kubwa ni mfumuko wa bei ya vyakula kwenye soko la dunia. Bei ya vyakula duniani mwaka huu imefikia kiwango kilichoweka rekodi.
Bei hiyo imekuwa ikipanda kwa asilimia 3 tangu mwezi Julai mwaka huu na kufikia kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa tangu mwaka 2011.
Hali ilikuwa mbaya zaidi mwezi Septemba, bei ya vyakula duniani ikipanda kwa asilimia 33, ukilinganisha na kipindi kama hicho mwaka uliopita.
Kwa mujibu wa FAO, bidhaa za chakula zilizoguswa ni pamoja na mafuta ya kula, nafaka, nyama na sukari. Kupanda huko hakuwezi kuiacha salama Tanzania ambao inategemea pia hali ya soko, kwenye viwango na vipimo vya mfumuko wa bei kidunia.
Ugonjwa wa COVID-19 nao umetikisa bei ya bidhaa mbalimbali duniani, nguvu kazi nyingi ilisamama kuzalisha, ama inazalisha kwa viwango vya kawaida. Wapo waliofariki, wapo waliougua na wapo walioguza, ambao muda wa kutumia kuzalisha ulitumika kushugulikia ugonjwa huu hatari.
Hali hiyo imesababisha kuwa na upungufu wa nguvukazi za uzalishaji mali na chakula (kupanda, kuvuna, kuchakata na kusambaza chakula), ukilinganisha na miaka miwili ya nyuma kabla ya Covid.
3: Vifaa vya ujenzi; saruji, nondo na mabati
Wizara ya Viwanda na Biashara ilifanya tathimini ya bei ya bidhaa za saruji, mabati na nondo kati ya mwezi Septemba hadi Novemba mwaka huu katika mikoa mbalimbali nchini ikiwemo Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Kilimanjaro, Mbeya, Mwanza, Pwani, Shinyanga na Ruvuma na kubaini kuwa bei ya saruji ilipanda kwa wastani wa shilingi 1000 kwa kila mfuko wa kilo 50.
Kwa upande wa mabati tathimini hiyo ilionyesha kuwa imepanda kwa wastani wa asilimia 5.5 kwa mabati ya gauge 28. Kwa upande wa nondo zimepanda kwa wastani wa asilimia sita katika kipindi hicho.
Sababu kubwa inayotajwa kwa bei ya bidhaa hizi kwa mfano saruji kulisababishwa na kupanda kwa gharama za uzalishaji viwandani.
Mchumi (Dokta Barnos Willium) anasema; 'suala la umeme kukatikakatika imekuwa msalaba pia kwa wazalishaji wa vifaa vye ujenzi, gharama za uzalishaji zinaongezeka, huku kunaongeza pia bei ya vifaa hivi'.
Nini cha kufanya sasa?

Mchumi Walter Nguma kutoka Tanzania amesema huenda hali ya uchumi na bei ikaendelea kuwa hivi kwa muda.
"Sioni dalili ya bei ya bidhaa kushuka, kwasababu hali ya uchumi haijawa vizuri kabisa. Ukigusa petroli, mafuta ya kupikia na miamala, moja kwa moja hauwezi ukazuia mfumuko wa bei, lazima utaongezeka. Kitakachoweza kupunguza bei ni pale ambapo miamala hii itapunguzwa na gharama ya mafuta kushuka," anasema Walter.
Unapokutana na mfumuko wa bei, kiasi cha bei kuonekana ni mwiba kwa wananchi, njia inayoweza kutumika haraka kuondoa makali hayo ni kuongeza uwezo wa ununuaji wa mtu wa kawaida.
'Hakuna njia ya mkato, ni lazima watu wawe na (income) kipato, bila kipato, ni ngumu kwa mtu kuweza kununua bidhaa hasa ikipanda bei', alisema Dkt. Barnos Willium.
Zitto Kabwe, mwanasiasa na mchumi kutoka Tanzania aliwahi kusema ili kukabiliana na kupanda kwa bei za bidhaa serikali inapaswa kuingiza fedha kwenye uchumi.
Njia rahisi kubwa ya kufanya ni kwa serikali kulipa madeni ya wakandarasi wa ndani, kuendesha miradi mikubwa ya maendeleo inayotumia malighafi za ndani na serikali kutumia huduma na bidhaa za ndani.
'kwangu muhimu serikali isiwe na mwelekeo wa kubana matumizi, ukibana matumizi, unapunguza mzunguko wa fedha, ukifunika mzunguko unapunguza uwezo wa watu kununua, lazima walie na bei za bidhaa', alisema Dkt. Willium
Hizi ni hatua za kiuchumi ambazo ni muhimu kuzifuata, hauna namna ya kukwepa kwenye kuweka fedha kwenye mzunguko watu waweze kuwa na uwezo wa kununua bidhaa mbalimbali.














