Afungwa kifungo cha maisha mara mbili kwa kumuua mke wake kwa nyoka aina ya cobra

Mwanaume mmoja nchini India, ameshtakiwa kumuua mke wake na kumuwekea nyoka aina ya 'cobra amng'ate, na kuhukumiwa kifungo cha maisha mara mbili.

Sooraj Kumar alikamatwa mwaka jana baada ya mke wake Uthra, kufariki na kukutwa na alama ya kung'atwa na nyoka.

Polisi walianza kufanya uchunguzi baada ya familia yake kutoa shutuma za mauaji na kusema Sooraj alikuwa akiwanyanyasa kwasababu ya mahari.

Jumatatu , mahakama ilimkuta Sooraj na hatia ya kumuachia cobra atembee kwenye kitanda chao wakati Uthra akiwa amelala.

Bi. Uthra mwenye umri wa miaka 25- alikutwa amekufa nyumbani kwake mnamo Mei Mosi mwaka jana.

Familia yake ilishuku tukio hilo baada ya kukuta Uthra akiwa na alama ya kung'atwa na aina nyingine ya nyoka ,wiki moja kabla ya kung'atwa na cobra.

Polisi wamesema uchunguzi umebaini kuwa bwana Sooraj alikuwa anahusika na majaribio mawili ya mashambulio ya nyoka wote wawili . Aidha wamemkamata pia mwanaume aliyemsaidia kupata nyoka hao - ingawa alisaidia polisi kutoa ushahidi dhidi ya kesi hiyo.

Kwa mujibu wa sheria ya India , polisi wamemshikilia baada ya ya kubaini njama walizotumia kufanya uhalifu.

Mwendesha mashtaka amesema kesi hii ni miongoni mwa kesi za nadra sana ambazo zinahitajika hukumu ya kifo kutolewa kwa mtu anayehusika.

Mahakama imekubali kuwa kesi hii ya nadra inapaswa kupata adhabu mara mbili ya kifungo cha maisha.

Hivyo Sooraj amehukumiwa kifungo cha maisha na kutakiwa kulipa dola $6,635.