R. Kelly: Nyota aliyehukumiwa kwa kuwanyanyasa kingono wasichana

Chanzo cha picha, Getty Images
''Msanii huyu 'mnyama' ametumia usanii wake kwa kunyanyasa wasichana wadogo wasiokuwa na uwezo wa kujitetea''.
''Alitumia watu wake wa karibu katika kutafutiwa wasichana hao na kuwanyanyasa kingono''.
Maneno ya wakili wa Marekani jimbo la mashariki la New York ,J acquelin Kasulis, baada ya mwimbaji wa R&B R. Kelly kuhukumiwa kwa biashara ya ngono.
Mashahidi kumi na moja - wanawake tisa na wanaume wawili - walichukua maamuzi ya kuelezea yale waliokuwa wametendewa hasa udhalilishaji.
Baada ya siku mbili za majadiliano, hakimu alimpata Kelly na hatia kwa mashtaka yote tisa aliyokabiliwa nayo. Anatarajiwa kuhukumiwa tarehe 4 Mei na anaweza kutumia maisha yake yote kifungoni.
Kelly ambaye jina lake kamili ni Robert Sylvester Kelly, alipatikana na hatia ya kutumia umaarufu wake na utajiri kushawishi wasichana wadogo kwa kuwapa ahadi za kuwasaidia katika kazi zao za muziki.
Wengi wao walioshuhudia vitendo hivyo wanasema waathirika walinyanyaswa kingono.
Kelly amekuwa akikanusha madai hayo dhidi yake.
Msanii huyo alijizolea umaarufu miaka ya 1990 na nyimbo kama "Bump and Grind" na "Ignition". Moja ya nyimbo zake zinazojulikana ni wimbo wa mwaka 2004 "I believe I can fly".

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika tawasifu yake, R Kelly anasema kwamba yeye mwenyewe alikuwa mwathirika wa unyanyasaji wa kijinsia akiwa mtoto.
Kelly pia alihukumiwa kwa kukiuka sheria ya Mann, sheria ambayo inaangalia uhalifu wa kushiriki katika biashara ya ngono katika maeneo yote Marekani.
Pia alipatikana na hatia kwa masuala ya ulaghai, katika muktadha huu, majaji walimchukulia kama kiongozi wa mpango wa kiovu wa kulazimisha kwa kuwapa maisha mazuri wanawake na watoto ili awanyanyase kingono.
Kesi ikiwa inaendelea , waendesha mashtaka walifafanua jinsi mameneja wake, walinda usalama na watu wengine katika msafara wake walivyomsaidia katika kufanya jinai hizo.
Majaji pia walisikia jinsi Kelly alivyokuwa amepata hati kinyume cha sheria kumuoa mwimbaji Aaliyah wakati akiwa na miaka 15 tu na kuchukuliwa kuwa bado ni binti mdogo. Aaliyah aliaga dunia mwaka 2001 kwa ajali ya ndege.

Chanzo cha picha, Getty Images
Wakati wa kesi hiyo, mashuhuda walielezea jinsi mwanamuziki huyo alivyoyadhibiti maisha ya waathirika, akiangalia kila hatua ya maisha yao kwa kuwanyima haki zao za msingi kama kumiliki mali pamoja na kuwasiliana na watu.
Kwa ujumla walikuwa vijana wenye matamanio ya kuwa watu wakubwa kwenye tasnia ya muziki.
Ripoti kutoka tovuti ya Buzzfeed 2017 ilidai kwamba wanawake waliowasili kwenye kikundi cha Kelly waliandaliwa na mwanamke wa miaka 31 aliyejulikana kama "den mother" kujua msanii huyo alipendelea nini kwenye tendo la ndoa.
Kelly aliwaita wasichana hao "babies" na aliwalazimisha wamuite "Daddy".
Waathirika walilazimika kuomba ruhusa kuondoka katika nyumba walizopewa na msanii huyo na Kelly alikuwa anaamua juu ya mavazi yao na kutaifisha simu zao za mkononi. Wasipomtii waliadhibiwa kwa maneno au vitendo.
Kesi ya awali
Kesi hii ilikuwa sio mara ya kwanza R.Kelly alihusika na tuhuma za unyanyasaji wa kijinsia. Kipindi kilichopita alikabiliwa na tuhuma za unyanyasaji wa wasichana kati ya umri wa miaka 13-19.
Mwaka 1994 Msanii R.Kelly alipokuwa na miaka 27, alifunga ndoa na msanii chipukizi wa R&B Aaliyah.

Chanzo cha picha, Getty Images
Muda mfupi baada ya kufunga ndoa, ndoa hiyo ilifutwa baada kutambulika kwamba Aaliyah hakuwa na umri wa miaka 18 kama ilivyokuwa imeandikwa kwenye cheti cha ndoa bali alikuwa na miaka 15.
R.Kelly aliweza pia kukwepa mashtaka mbali mbali yaliyomkabili.
Mmoja wa wanawake waliomshtaki alikuwa Tiffany Kawkins, aliyedai kuathirika na 'unyanyasaji wa kihisia na kimwili' katika kipindi cha miaka mitatu ya mahusiano na msanii huyo yaliyoanza alipokuwa na miaka 15 wakati Kelly akiwa na miaka 24.
Mwanamke mwingine alikuwa Tracy Sampson, aliyemshitaki Kelly kumhusisha na mahusiano yasiyo na maadili pindi allipokuwa na miaka 17.
Mwaka 2002, Kelly alishutumiwa na polisi wa Chicago kutengeneza picha za ngono na watoto.

Chanzo cha picha, Getty Images
Rekodi, ambazo zilijumuisha video na picha za ngono, zilivuja na ndizo zilizotumika dhidi yake kama sehemu ya ushahidi mahakamani dhidi yake. Polisi walimshtaki mwanamuziki huyo kwa kupiga picha na wasichana wadogo.
Lakini aliachiliwa kwa mashtaka yote miaka sita iliyopita: majaji walihitimisha kwa kudai kuwa hawawezi kuthibitisha kuwa wasichana waliopo kwenye video ni wenye umri mdogo.
Akizungumza baada ya hukumu hiyo siku ya Jumatatu ,wakili Jacquelin Kasulis, alisema, "Kwa upande wa waathiriwa wa vitendo viovu juu yao ndani ya kesi hii, sauti zao zimesikilizwa na haki imetendeka."
Gloria Allred, mwanasheria aliyewawakilisha waathirika,alizungumza kwa niaba ya mwathirika mmoja aliyesema "nilikuwa nikijificha kwasababu ya uwoga na kupokea vitisho kutoka kwa Robert Kelly. Sasa niko tayari kuanza kuishi maisha yangu bila uoga na kuanza kupona".








