Hakainde Hichilema:Tundu Lissu,Raila Odinga na Bobi Wine wanaweza kujifunza yapi kutoka kwake?

Chanzo cha picha, Getty Images
Historia ya upinzani katika bara la Afrika, haijaanza jana wala juzi, ni ya muda mrefu, imedumu miongo na miongo, ukianzia tangu wakati wa ukoloni mpaka sasa nchi za bara hilo zikiwa huru.
Upinzani wa wakati huo ulijiegemeza zaidi kwenye kuutafuta uhuru wa bendera ama uhuru wa nchi ili ijiamulie mambo yake yenyewe na kujitawala, lakini upinzani wa sasa ni wa tofauti kiasi: Upo upinzani katika ataifa unaona vyama vya ukombozi vimepitwa na wakati, lazima kufanyika mabadiliko, wapinzani wengine katika mataifa mengine yanaona watawala wameshindwa kukidhi matakwa na mahitaji ya wananchi huku vyama vingine tawala vikidaiwa kukiuka misingi ya utu, haki za binadamu na kutojali ya maisha ya watu, hivyo sera mbadala ama mtazamo mbadala ukihitajika.
Pamoja na yote sio rahisi, kwa Afrika mpinzani kuingia madarakani. Vyama upinzani na viongozi wao wamekuwa wakipitia tanuri la moto, wakati wa wa harakati zao wa kuwania kiti cha urais; kufungwa au kuwekwa mahabusu, kunyanyaswa, kunyima haki, kupigwa na kuteswa ni matukio ya kawaida sana kwa viongozi wa upinzani katika nchi za Afrika.
Je,ushindi wa Hichilema unawapa fuzo gani viongozi wengine wa upinzani barani Afrika
"Inatia moyo sana," alisema kiongozi wa upinzaji wa Tanzania Tundu Lissu ambaye alinusurika jaribio la mauaji mnamo 2017 baada ya kupigwa risasi mara 16 na watu anaoamini walikuwa maajenti wa serikali.
"Wazambia wametuonyesha inaweza kufanyika, bila kujali vikwazo walivyotuwekea , bila kujali hali mbaya," ameongeza.
Bwana Lissu alishindwa katika uchaguzi wa mwaka jana na Rais John Magufuli, aliyeaga dunia ambao anadai kuwa uliibiwa.
Baadaye alikimbia nchini wakati maafisa wa usalama walipopanga kumkamata.

Chanzo cha picha, AFP
Baadhi ya wenzake katika chama cha Chadema, akiwemo mwenyekiti Freeman Mbowe, walizuiliwa kwa muda mfupi.
Mnamo Mei, Bw Mbowe alishtakiwa kwa makosa yanayohusiana na ugaidi. Wafuasi wake wanasema anakabiliwa na "mateso ya kisiasa" kwa kampeni ya katiba mpya.
Kulingana na mwanasiasa wa upinzani nchini Tanzania Zitto Kabwe, ni katiba mpya tu ambayo itahakikisha uhuru wa tume ya uchaguzi ili kuipa upinzani nafasi nzuri katika kura ijayo.
Rais mteule wa Zambia kutoka chama cha upinzani cha UPND, Hakainde Hichilema, katika hotuba yake mara baada ya kutangazwa kumshinda rais Edgar Lungu, alisema kabla ya kushinda uchaguzi mkuu uliofanyika wiki hii, aliwahi kuwekwa ndani mara 15.
Ukiacha Hichilema anayeapishwa leo na aliyewania urais mara tano kabla ya kuupata, wafuatao ni baadhi tu ya viongozi wa Afrika kutoka vyama vya upinzani waliowahi kushinda Urais ingawa kwa mbinde.
1: Frederick Jacob Titus Chiluba - Zambia

Chanzo cha picha, Getty Images
Fredrick Chiluba, alikuwa kiongozi wa chama cha Upinzani cha Movement for Multi-party Democracy (MMD), aliyekianzisha mwaka 1990 ili kumuondoa Keneth Kaunda wa chama tawala cha United National Independence Party (UNIP), aliyekuwa muasisi na kiongozi aliyekaa madarakani kwa miaka 27.
Chiluba alikuwa rais wa pili wa Zambia akiongoza taifa hilo kwa miaka 11 kati ya mwaka 1991 mpaka 2002. Chiluba, aliyekuwa kiongozi wa chama cha wafanyakazi, alishinda katika uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi uliofanyika mwaka 1991 akimwanga Kaunda, aliyeonekana ngumu kumshinda.
Katika chaguzi huo Chiluba alishinda kwa kupata asilimia 75% ya kura dhidi ya 25% alizopata Kaunda. Wanasema ushindi huo ilikuwa vigumu kuupindua kwa njia yoyote ya hila, Kaunda maarufu kama KK' akakubali kushindwa, na hapo ukawa mwanzo wa upinzani kuingia madarakani.
Chiluba alichaguliwa tena mwaka 1996 kabla ya kumpisha makamu wa Rais wa zamani, Levy Mwanawasa aliyepeperusha bendera ya MMD katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2002 na kuwa rais wa tatu wa nchi hiyo.
Wakati wa utawala wake, aliifungua nchi hiyo na kuruhusu uhuru wa vyama vingi, uhuru wa kujieleza, uhuru wa habari na akabadilisha katiba ambayo inaonekana kuwa msingi wa demokrasia iliyopo leo nchini humo.
2: Michael Sata - Zambia

Chanzo cha picha, Getty Images
Sata alikuwa rais wa tano wa Zambia kuanzia Septemba 2011 mpaka kifo chake oktoba 2014
Sata alikuwa sehemu ya chama cha MMD kilichosika hatamu chini ya utawala wa Rais Fredrick Chiluba, na aliwahi mpaka kushika nafasi ya uwaziri. Alifahamika zaidi kama 'King Cobra', akijitokeza kupambana na Levy Mwanawasa katika uchaguzi mkuu wa 2006, bahati mbaya akashindwa.
Kufuatia kifo cha Rais Levy Mwanawasa, Rupia Banda aliyekuwa makamu wa Rais akashika madaraka kikatiba mpaka 2008. Katika uchaguzi mkuu wa 2008, Sata akawania tena nafasi hiyo, akipambana na Rupia Banda akashindwa tena. Baad ya miaka 10 ya kuwa upinzani Sata akaingia tena kwenye uchaguzi mkuu wa Septemba 2011 safari hii akashinda dhidi ya Banda na kuwa rais wa tano wa taifa hilo.
Alifariki jijini London oktoba 28, 2014, na kuacha makamu wake wa rais Guy Scott kushika usukukani kwa miezi mitatu mpaka uchaguzi ulipofanyika Januari 20, 2015.
3: Lazarus Chakwera - Malawi

Chanzo cha picha, Getty Images
Kiongozi wa upinzani wa Malawi Lazarus Chakwera sasa ni rais wan chi hiyo kufuatia ushindi wake wa jasho alioupata mwaka 2020.
Chakwera alimwaga aliyekuw arais wa nchi hiyo Peter Mutharika kwa kupata asilimia 58.57% za kura zote zilizopigwa katika uchaguzi huo.
Awali Mahakama ya nchi hiyo ilisema uchaguzi wa Mei 2019 haukuwa halali na kumpa fursa marejeo yaliyompa ushindi Chakwera.
Chakwera aliongoza muungano wa vyama tisa vya upinzani kumuondoa Mutharika akiungwa mkono na rais wa zamani wa taifa hilo Joyce Banda pamoja na makamu wa Rais Saulos Chilima, aliyekuwa mgombea mwenza.
Katika chaguzi wa mwaka 2019 Chilima alikuwa watatu , na kuna wakati alimuunga mkono Mutharika, ingawa baada ya uchaguzi huo, alibadili muelekeo na kumuunga mkono Chakwera.
4: Félix Tshisekedi Tshilombo - DRC

Chanzo cha picha, Reuters
Akitumia kivuli cha baba yake aliyekuwa waziri mkuu wa zamani wa DRC wakati huo ikiitwa zaire, kujitengeneza kisiasa na kuutwaa urais Januari 2019 akitokea upinzani.
Tshisekedi ni kiongozi wa chama cha UDPS, moja ya vyama vikongwe vya uda mrefu vya upinzani nchini DRC, akimrithi baba yake Étienne Tshisekedi aliyekuwa mpinzani mkuwa wa Rais wa wakati huo, Mobutu Sese Seko.
Tshisekedi alishinda uchaguzi mku wa Disemba 2018, unaotajwa kuwa wa kwanza wa mani kfanyika nchini humo, akiwabwaga Martin Fayulu, na Emmanuel Shadary aliyekuwa anaungwa mkono na rais Joseph Kabila na utawala wake.
Ushindi wake uliashiria angalau kuimarika kiasi kwa demokrasia nchini humo tangu ipate uhuru kutoka kwa wabelgiji mwaka 1960. Licha ya kukosolewa kuhusu masuala ya rushwa lakini pia kla njama na rais aliyekuwa madarakani Kabila kwa lengo la kumuangusha mpinzani mwingine aliyekuwa na nguvu Fayulu.
Mahakama iliamua tofauti lakini pia mara kadhaa Kabila na Tshisekedi wenyewe walikana kuhusika na hujuma zozote kwenye uchaguzi huo.
5: Mwai Kibaki - Kenya

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwai Kibaki alikuwa rais wa tatu wa Kenya 931 akiongoza taifa hilo kati ya Disemba 2002 mpaka April 2013.
Haikuwa rais kwa Mwa Kiaki kuukwaa kwa sababu alikuwaanatokeo upinzani ilibdi apigane vya kutosha kuingia Ikulu.
Kabla ya kuingia upinzani, Kibaki alikuwa makamu wa Rais wa Kenya kwa miaka 10 chini ya utawala wa Rais Daniel arap Moi kuanzia kati ya 1978 to 1988
Moi alipomrithi Jomo Kenyatta kama rais mwaka 1978, akamchagua Kibaki kuwa makamu wake wa rais, lakini mwezi Machi 1988, 'uswahiba' wao ukaanz akuyumba baada ya Moi kumuondoa Kibaki kwenye nafasi ya makamu wa rais na kumpeleka kuwa waziri wa afya.
Hilo lilikuwa kama pigo kwake, akiamini ameshushwa cheo, lakini ikawa mwanzo wake wa kuutafuta urai. Akajiuzulu nafasi yake siku ya krismasi, Disemba 1991 na siku chache baada ya mfumo wa vyama vingi kuingia nchini humo mwaka 1992, Kibaki akaanzisha chama cha Democratic Party (DP) na kuingia katika uchaguzi mkuu wa mwaka huo akashika nafasi ya tatu. Moi na chama chake cha KANU alishinda uchaguzi huo.
Mwaka 1997 akashinda tena uchaguzi wa mwaka 1997, safari hii Kibaki akishika nafasi ya pili. Januari 1998 akawa kiongozi wa upinzani na chama chake kikwa chama kikuu cha upinzani bungeni.
Kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2002, Kibaki akakubali chama chake cha DP kuungana na vyama vingine na kutengeneza muungano wa NARC, uliofanikiwa kumuingiza madarakani kwa kumshinda mgombea wa KANU, Uhuru Kenyatta, mtoto wa rais wa kwanza wa taifa hio, Jomo Kenyatta, aliyekuwa anaungwa mkono na Moi. Kenyatta ni rais wa sasa na wanne wa taifa hilo akimrithi Kibaki.












