Changamoto zinazomkabili Tshisekedi baada ya kujitenga na Kabila

Na Mohammed AbdulRahman

Tangu mwanzoni mwa Desemba 2020, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) inakabiliwa na mtihani mwingine wa kisiasa , baada ya Rais Felix Tshilombo Tshisekedi, kuamua kuuvunja ushirikiano wake na Rais wa zamani Joseph Kabila Kabange. Ushirika wao uliundwa kumuwezesha Tshisekedi kuunda serikali kwa sababu ya kutopata wingi wa wajumbe bungeni kufuatia uchaguzi 2018.

Sasa anakabiliwa na kitandawili , aunde serikali kutokana na muungano mpya au alivunje bunge na kuitisha uchaguzi mwingine.

Ushirikiano baada ya ushindi tata wa Tshisekedi:

Desemba 2018, Felix Tshisekedi Kiongozi wa chama cha upinzani Union for Democracy and Social Progress (UPDS), aliingia madarakani katika mabadiliko ya kihistoria nchini Congo,baada ya kumshinda katika uchaguzi chaguo la Kabila ,waziri wa zamani wa mambo ya ndani Emmanuel Ramazani Shadary.

Kabila hakuwa mgombea ikiwa ni kutokana na makubaliano ya suluhisho la kisiasa baada kuiongoza Congo kwa karibu miaka 18.

Mgombea mwungine wa upinzani Martin Fayulu na chama chake LAMUKA walidai ushindi huo ulipangwa ili Kabila aendelee kuwa na usemi na kwamba mshindi halali alikuwa ni yeye.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida katika siasa za Afrika, wafuasi wa Kabila kutoka muungano uliopewa jina la Common Front for Congo (FCC) walishinda karibu asilimia 70 ya viti bungeni, jumla ya wabunge 350.

UDPS asilimia 36 na mshirika wake Union for the Congolese Nation (UNC) chama cha Vital Kahmere asilimia 17. Kwa pamoja viti 46 pekee. FCC inalidhibiti pia Baraza la Seneti ambapo Kabila ni mjumbe wa kudumu.

Ushirika na UNC ulimfungulia mlango:

Katika uchaguzi huo,Tshisekedi na kiongozi wa Union for the Congolese Nation (UNC) Vital Kamerhe, walikubaliana kushirikiana katika uchaguzi wa Rais na kumuachia Tshisekedi kuwa mgombea wao wa pamoja. Kamehre ni spika wa zamani wa bunge la taifa na mtu wa karibu wa Kabila kabla ya kuhasimiana.

Ushirikiano wa Tshisekedi na Kamerhe, uliwashtuwa wanasiasa wenzao waliokuwa pamoja katika kambi ya upinzani, Jean Pierre Bemba kiongozi wa Movement for the Liberation of Congo (MLC) na Gavana wa zamani wa Katanga Moise Katumbi.

Walipokutana mjini Geneva Uswisi, wote waliafikiana kumuunga mkono Fayulu kuwa mgombea wa upinzani. Lakini ghafla Tshisekedi na Kamerhe walitangaza kujitoa.

Ni miaka miwili tangu Tshisekedi alipoapishwa Januari 2019 na kuanza kuzikabili changamoto kubwa. Wafuasi wa Kabila walisisitiza wapewe wizara kadhaa muhimu na walifanikiwa kwa sababu Tshisekedi hakuwa na chaguo jingine.

Kandoni mwa hayo,Kabila ameendelea kutaka kuwa na ushawishi kwenye uteuzi wa nafasi mbalimbali zikiwemo za uongozi jeshini. Akihisi amefungwa mikono, Tshisekedi sasa ameshindwa kuvumilia zaidi.

Uamuzi wa kutengana na Kabila:

Sasa Tshisekedi maarufu kwa wafuasi wake kwa jina la "Fatchi", ameamua kukabiliana na Kabila. Wiki chache zilizopita alitangaza ameuvunja ushirikiano wao.

Lengo lake ni kuunda Umoja mpya utakaokuwa na wingi bungeni ili taifa hilo liweze kusonga mbele. Ameupa jina "Umoja Mtakatifu".

Tayari ameshaonya ikiwa atashindwa, atalazimika kulivunja bunge na kuitisha uchaguzi mpya. Katika hotuba yake mbele ya mabaraza yote mawili ya bunge Desemba 14 alisema,"Nimeivumilia hali hii, lakini uvumilivu huo haukutosha kuniwezesha kuongoza kwa utulivu".

Awali wabunge 281 kati ya 500 walipiga kura kumuondoa Spika wa bunge Jeanine Mabunda. Wapinzani wa Kabila wamesherehekea kuondolewa Mabunda, rafiki yake wa chanda na pete. Amedaiwa kuendesha shughuli za bunge kwa ukereketwa .

Maafisa wa Tshisekedi wamekuwa mbioni kuwashawishi wanasiasa wa upinzani na wabunge wa FCC kujiunga na Muungano mpya na kuna ishara kwamba mkakati umeanza kuzaa matunda.

Magavana wa mikoa 29 walitangaza kumuunga mkono Tshisekedi na ikidaiwa kuna kiasi ya wabunge 70 kutoka kambi ya Kabila na wanasiasa kadhaa ambao tayari wameashiria kuiacha mkono FCC akiwemo waziri wa zamani wa mawasiliano wa Kabila, Lambert Mende.

Tshisekedi pia aliwakaribisha kwa mazungumzo Bemba na Katumbi , mahasimu wengine wakubwa wa Kabila. Juhudi zake zinaonekana kuanza kuzaa matunda.

Akiukaribisha mwaka mpya 2021 Tshisekedi alichukua hatua isiyotarajiwa, alipotoa msahama kwa watu 23 waliokuwa gerezani, baada ya kuhukumiwa kuhusika katika mauaji ya Rais Laurent Desire Kabila 2001. Miongoni mwao ni aliyekuwa mpambe na mlinzi wa kiongozi huyo Kanali Eddy Kapend na mkuu wa usalama wakati huo Georges Leta.

Wote walihukumiwa na mahakama ya kijeshi ambayo baadaye ilivunjwa. Kuachiwa huru watu hao wawili baada ya kuweko gerezani karibu miaka 20 pamoja wenzao 21 kumepokelewa kwa maoni tafauti. Wengi wamempongeza Tshisekedi, wakiamini wafungwa hao walikuwa ni muhanga wa mchezo wa kisiasa.

Kapend amesisitiza wakati wote kuwa hana hatia na kusema, " Waliohusika na njama hiyo wanajijua na wako nje." Wadadisi wanaamini Tshisekedi amejiongezea turufu kujitenga zaidi na Kabila, ingawa binafsi amesema msamaha huo ni zingatio la kiutu.

Uchaguzi ujao ni 2023 , lakini haijafahamika ikiwa Tshisekedi atagombea muhula wa pili. Lakini haijafahamika msimamo wa UNC utakuwaje ikiwa kiongozi wao Kamerhe ataendelea kubakia gerezani. Ngome ya UNC ni mashariki ya Congo.

Juni 2020, Kamerhe aliyedhaniwa angekuwa Waziri mkuu na badala yake akateuliwa Mkurugenzi wa ofisi ya Rais akiwa na jukumu la kusimamia shughuli za utawala Ikulu, alipatikana na hatia ya ubadhirifu wa mali ya umma na ufisadi. Alihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela na kupigwa marufuku kushika wadhifa wowote wa serikali au utumishi wa umma kwa muda wa miaka 10.

Walipoafikiana kushirikiana, wanasiasa hao wawili walikubaliana kupokezana madaraka,Tshisekedi awe mgombea urais mhula wa kwanza na Kamerhe 2023. Yumkini hukumu hiyo ukawa mwisho wa Kamerhe kisiasa.

Kabila na mpango wa kurudi madarakani:

Inaelekea kiu cha madaraka bado hakijamwisha Kabila. Mwishoni mwa Desemba Kabila aliwasili Lubumbashi mji mkuu wa jimbo la Katanga na kulahikiwa na umati mkubwa wa wafuasi wake, katika kile wadadisi wanachokiona kuwa ni kupima joto la kisiasa likoje, ikizingatiwa mpinzani wake mkubwa jimboni humo ni Moise Katumbi aliyezuiliwa na Kabila kuwa mgombea 2018.

Miaka 60 ya uhuru kutoka kwa Ubeligiji 1960, Congo imepitia vipindi tafauti vya misukosuko ya kisiasa, kiuchumi na vita. Rais wa zamani Sese Seko aliyetawala kwa miaka 32 hadi alipoangushwa Mei 1997 alikuwa na msemo " l état cést moi" (Dola ni mimi).

Baada ya kuongoza kwa miaka 18, pengine Kabila naye anahisi Congo ni yeye. Wapambe wake wameanza kuzungumzia uwezekano wa kurudi na kugombea uchaguzi ujao 2023, wakisema hakuna cha kumzuwia.

Wakati ushirika wa Kabila na Tshisekedi sasa haupo tena, Wakongomani wanamkodolea macho Tshisekedi wakitumai atafanikiwa kuunda muungano mpya ili kama alivyoahidi, aanze safari yake ya kuleta mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi wanayoyasubiri kwa muda mrefu.

Ilimchukua muda wa miezi 8 kuunda serikali ya mseto na FCC ya Kabila. Swali ni je itamchukua muda gani kuweza kupata uungaji mkono mpya na kuunda serikali imara, au kama alivyoonya atalazimika kulivunja bunge na kuitisha uchaguzi mwengine ?