Video ya ngono yasababisha maafisa wa Umoja wa Mataifa kusimamishwa kazi bila malipo

Vehicles of a convoy United Nations Interim Forces in Lebanon (UNIFIL) ride on a road along the border between Lebanon and Israel

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Umoja wa mataifa umekuwa na kashfa nyingi kuhusu ngono katika miaka ya hivi karibuni

Umoja wa Mataifa (UN) umewapeleka likizo bila malipo wafanyakazi wake wawili ambao wanakabiliwa na kashfa ya kufanya vitendo vya ngono katika gari ya kazini nchini Israel.

Maafisa hao walipigwa picha ya video katika gari ambayo ilikuwa ina nembo ya UN- katika mji wa Tel Aviv katika mtaa wa ufukweni mwa bahari.

Katika video hiyo, mwanamke alikuwa amevalia gauni jekundu alionekana akiwa amemkalia mwanaume katika kiti cha nyuma cha gari.

UN imeanza kufanya uchunguzi wa video hiyo ya sekunde 18 ambayo imesambaa katika mitandao ya kijamii toka mwezi uliopita.

Stéphane Dujarric, msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, alikitaja kitendo hicho kinachoonekana katika kanda ya video kuwa kimemshtua na kimemchukiza.

Kufikia sasa UN imebaini kuwa wanaume hao ni waajiririwa katika taasisi yake ya Kusimamia Kusitishwa kwa Mapigano yaani Truce Supervision Organization (UNTSO).

Wawili hao wamesimamishwa kazi bila malipo yoyote mpaka uchunguzi kuhusu madai dhidi yao ukamilike.

Bwana Dujarric aliiambia BBC siku ya Alhamisi kuwa kusimamishwa kazi kwa muda kwa wafanyakazi hao ilikuwa ni hatua sahihi kutokana na ukubwa wa madai hayo ambayo ni kinyume cha utaratibu wa kazi katika kiwango cha kimataifa.

"UNTSO imeanza kampeni za kuwakumbusha wafanyakazi wake majukumu na wajibu wao kulingana na kanuni ambazo Umoja wa Mataifa umeziweka," bwana Dujarric alisema.

UN ina sera kali dhdi ya madai ya kingono kwa wafanyakazi wake.

Wafanyakazi wanaweza kuwajibishwa kwa kukiuka sheria ambazo zimewekwa.

Wanaweza kufukuzwa hata kazi katika operesheni za ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa lakini ni jukumu la nchi zao kuchukua hatua zaidi au hatua za kisheria.

United Nations Interim Forces in Lebanon (UNIFIL) patrol the area around the southern Lebanese town of Kfar Kila on the border with Israel

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Umoja wa mataifa umedai kuwa hautavumilia vitendo vyovyote vya madai ya kingono katika operesheni zake

Je rekodi ya UN kuhusu masuala ya ngono ni ipi?

Heather Barr, mwanaharakati wa masuala ya haki za kibinadamu katika shirika la Human Rights Watch alisema, ''sikushangazwa na kanda hiyo kutoka Israel''.

Bi Bar, ambaye alifanya kazi na UN nchini Burundi na Afghanistan , alisema ''ni vyema wanachunguza," lakini akaongezea kwamba "UN ina matatizo makubwa zaidi ya kanda hiyo".

''Tatizo ni kuhusu madai ya unyanyasaji wa kingono unaotekelezwa na wafanykazi wa UN'', alisema bi Barr.

Mwaka 2019, kulikuwa na madai 175 ya unyanyasaji wa kingono dhidi ya wafanyakazi wa UN, ripoti moja ilisema.

Kati ya madai hayo, 16 yalikuwa na ushahidi, 15 yalikosa ushahidi na mengine yote yaliosalia yanafanyiwa uchunguzi.