Virusi vya corona: Jinsi viongozi wa Afrika wanavyojikata mishahara kupambana na corona

Rais wa Rwanda, Paul Kagame
Maelezo ya picha, Rais wa Rwanda, Paul Kagame

Katika mapambano dhidi ya Covid-19, na umoja kwa jamii ya raia wa Rwanda walioathirika zaidi , Serikali ya Rwanda imeamua kuwa mawaziri wote ,Wakuu wa taasisi za Umma na maafisa wakuu wengine watatoa mishahara yao ya mwezi mmoja.

Hatua hiyo ya kukatwa mshahara wa mwezi Aprili ni jitihada za pamoja katika kupambana na virusi vya corona nchini humo.

Maafisa wa serikali wanaoangaliwa na hatua hiyo ni takriban 260, wote kwa ujumla mshahara wao wa mwezi ni takriban dola elfu 74.

Wiki iliyopita mfuko la fedha la kimataifa IMF uliidhinisha mkopo wa dola 109 kwa serikali ya Rwanda kupiga jeki uchumi wa Rwanda unaoyumba kutokana na ugonjwa wa virusi vya Corona.

Mwandishi wa BBC aliyeko mjini Kigali Yves Bucyana anasema hatua hiyo imekuja wakati taifa la Rwanda limetangaza kupona kwa wagonjwa wanne wa corona, ambapo raia wa Rwanda ni watatu na raia mmoja ni kutoka Burundi.

Raia huyo wa Burundi Fabrice Nahimana aligundulika na virusi vya Corona tarehe 18, Machi, kwenye uwanja wa ndege wa Kigali alipokuwa safarini kwenda Burundi akitokea mjini Dubai.

Yeye ameiambia redio ya taifa kilicho moyoni mwake:

''Ujumbe mwingi niliotumiwa na jamaa na marafiki kwanza ndio ulinitia uoga sana. nilipokea ujumbe mwingi, baadhi wakilia, wengine wakiona kwamba mwisho wa maisha yangu umefika,lakini Mungu alionyesha nguvu zake.

Wengi niliwakuta hapa na bado wako hapa ila nina matumaini kwamba watapona. Kinachofuata sasa mimi nina hamu ya kurudi nyumbani Burundi, familia wananisubiri, marafiki zangu, wazazi wote wananisubiri ili tuweze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwamba ameniokoa miongoni mwa wengi walioambukizwa virusi vya corona''

Waliotangazwa kupona wamepewa vyeti vinavyoonyesha kwamba wamepona virusi vya Corona.

Pamoja na hayo wizara ya afya imesema kwamba wataendelea kujitenga kwa kipindi cha siku 14 wakiwa nyumbani na kufwata sheria iliyopo ya kutotoka nyumbani.

Hao ni miongoni mwa wagonjwa waliofikishwa katika kituo cha kutoa matibabu ya virusi vya Corona cha Kanyinya ,nje kidogo ya jiji la Kigali katikati ya mwezi wa tatu mwaka huu ugonjwa huo ulipojitokeza kwa mara ya kwanza nchini Rwanda.

Kituo hicho kilikuwa na jumla ya wagonjwa 75,huku wengine wakitibiwa katika kituo kingine kilichoko katika wilaya ya Bugesera kusini mashariki mwa Rwanda.

Siku ya Jumapili 05,April Wizara ya afya ilithibitisha wagonjwa wengine 2 ambao walitangamana na wagonjwa wa awali na kuifanya idadi ya wagonjwa ambao bado wanapokea matibabu kuwa watu 100.

Wizara imesema kwamba kuna matumaini mengi ya wengine zaidi kupona na kurudi nyumbani mnamo wiki hii.

rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta alitangaza kwamba yeye na makamu wake watapunguziwa asilimia 20%

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta alitangaza kwamba yeye na makamu wake watapunguziwa asilimia 20%

Jitihada kama hizi zilitangazwa kuchukuliwa nchini Kenya vilevile ambapo rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta alitangaza kwamba yeye na makamu wake watapunguziwa asilimia 20% katika mshahara wao.

Alihimiza hatua hiyo ichukuliwe na viongozi wengine serikalini kukatwa 10%.

Bwana Kenyatta na wabunge wa Kenya ni miongoni mwa watu wanaolipwa fedha ningi zaidi barani Afrika.

Kwa sasa Kenya imethibitisha kuwa na wagonjwa 142 wenye maambukizi ya Corona.

Wizara ya afya imeeleza kuwa watu watakaokufa kutokana na virusi vya Corona watazikwa ndani ya saa 24 huku watu wa karibu wa familia wasiozidi 15 wakiruhusiwa kuhudhuria mazishi hayo yatakayoandaliwa na Serikali.

Maelezo zaidi

Aidha, ndege kutoka nchi za kigeni zimeendelea kipigwa marufuku kuingia Kenya kwa siku 30 zaidi.

Hatahivyo, marufuku hii imeondolewa kwa ndege za kigeni zinazokuja kuhamisha raia wa nchi za nje waliokwama ingawa zinatakiwa kutoa taarifa kwa serikali angalau saa 72 kabla.

Ndege zingine ambazo hazitaathirika na marufuku hii ni zile za kubeba mizogo hasa ikizingatiwa kwamba kwa sasa serikali inaagiza vifaa vya wahudumu wa afya kutoka nje.

Sekta ya uchukuzi pia imeagizwa kutekeleza sheria zilizotolewa.

Na kutokana na ongezeko hilo, kuanzia Jumatatu, matatu au daladala pamoja na bodaboda ambazo zitakiuka sheria zilizowekwa zitapokonywa leseni na kufikishwa mahakamani kwa kosa la kusambaza virusi kimaksudi.

Rais wa Malawi, bwana Peter Mutharika

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Rais wa Malawi, bwana Peter Mutharika

Jumapili 05, April, Rais wa Malawi alitangaza kuwa yeye na mawaziri wote nchini humo watakatwa asilimia kumi ya mishahara yao ya miezi mitatu ili kupata fedha za kukabiliana na mlipuko wa virusi vya corona.

Rais Peter Mutharika alitangaza hatua hiyo ili kukabiliana na athari za kiuchumi ambazo zimesababishwa na corona.

Malawi imeripoti kisa cha kwanza cha mgonjwa mwenye virusi vya corona siku ya Alhamisi, na lilikuwa taifa la mwisho kutangaza kuwa na maambukizi.

Bwana Mutharika anapata mshahara unaofikia dola 3,600 kwa mwezi lakini haijawekwa wazi ni kiasi gani cha fedha kitakatwa kutoka katika mishahara ya mawaziri wa nchi hiyo.

Vilevile rais ametaka kodi ipunguzwe katika biashara mbalimbali kama mafuta na kuongeza kipato cha wafanyakazi wa afya ambao wako katika mazingira hatari zaidi ya ugonjwa, Reuters imeripoti.