Priscillah Ruzibuka: Kijana wa Kinyarwanda aliyeamua kujiajiri kutumia fasheni

Priscilla Ruzibuka akiwa akinadi nguo za watoto chini ya nembo Ki-pepeo Kids

Chanzo cha picha, Pricilla Ruzibuka

    • Author, Na Dinah Gahamanyi
    • Nafasi, BBC Swahili

Baada ya kufuzu masomo ya Chuo Kikuu, Priscilla Umutashya Ruzibuka hakusubiri kuajiriwa.

Aliamua kuanzisha kampuni yake ya mitindo ya mavazi chini ya nembo Ki-pepeo Kids mjini Kigali.

Aliweza kufungua mradi huo wa kushona nguo za vitenge za watoto wadogo, na alianza kwa kushona nguo za watoto wa marafiki zake.

Alifanya kazi na kuwa na mikataba ya muda mfupi na mafundi wa kushona nguo, huku akichunguza ubora wa kazi zao,na baadae alibaini wale ambao angefanya nao kazi mara baada ya kukamilisha mchakato wa usajiri wa biashara yake.

Alikuaje mwanamitindo?

Priscilla alianza kupenda fasheni na uanamitindo tangu alipokuwa mtoto.

Alikuwa akimuona msichana wa kazi wa nyumbani kwao aliyekuwa akimlea akishona nguo kwa ajili ya wateja wao, kisha anajaribu na kumuigiza anavyoshona, na kutengeneza nguo kwa ajili ya mwanasesere.

Mlezi wake alikuwa mfano mwema kwake. ''Alikua mfano mwema kwangu kwani alikuwa mtu anayetoka katika familia ambayo haikuwa na uwezo mkubwa, lakini alikuwa mchapakazi ambapo alijifunza ujuzi mdogo wa kushona nguo na kujaribu kubuni mitindo mpya''. Alisema Priscilla.

Penye nia pana njia

Mafundi wa nguo wakiendelea kushona nguo za watoto za Ki-pepeo Kids mjini kigali

Chanzo cha picha, Priscilla Ruzibuka

Maelezo ya picha, Priscilla huwaajiri mafundi wanawake kutoka katika familia maskini

Priscilla alisomea Uhandisi wa mifumo ya taarifa - (Information Systems Engineering) chuo kikuu. Baada ya masomo yake alipata mwamko wa kuanzisha biashara ya mitindo ya mavazi ya watoto kwa kuwa hakutaka kusubiri kuajiriwa.

Kwa kuwa hakujua mengi kuhusu uendeshaji wa biashara, aliamua kurudi tena shuleni kusomea shahada ya juu katika Uongozaji wa miradi (Masters in Project Management).

Baada ya kufuzu masomo, alitumia pesa kidogo za akiba alizokuwa nazo na wazazi wakamsaidia na hapo ndipo alipoanza kushona nguo za watoto wadogo kwa ajili ya watoto wa marafiki zake na familia. ''Nilianza kwa kuwapatia mikataba mifupi mifupi ya kazi mafundi wa nguo huku nikipima ujuzi wao wa kazi, na baadae niikawatambua wale ambao ningefanya nao kazi baada ya kukamilisha mchakato wa usajili wa biashara'' anasema Bi.Priscillah.

Kushuhudia maisha ya wanawake aliowapa mafunzo ya ushonaji yakibadilika kutokana na ujuzi pamoja na mapato ndio kinachomtia Priscillah msukumo zaidi Priscilla. ''Kuona mitindo niliyoibuni na kushonwa na mafundi ikivaliwa na kupendwa na wateja wanaofurahia ubora wake kupitia kampuni yangu Kipepeo ni jambo linalonifurahisa''. Anasema Priscillah.

Nguo za watoto zikiuzwa mjini Kigali Rwanda

Chanzo cha picha, PA

Ushauri wa Priscilla kwa vijana wenzake wanaotaka kuanzisha biashara ya kudumu

  • Chukua muda kutambu aina ya biashara unayotaka kuifanya .
  • Usianze tu biashara kwasababu kila mtu anaifanya.
  • Uwe wazi biashara yako inawalenga wateja gani na ni vipi watafaidika kutokana na bidhaa yako au huduma utakayoitoa.
  • Kama unataka kuisaidia jamii yako, chukua muda kuelewa ni nini unachotaka kuisaidia jamii yako, na fikiria ni vipi utatekeleza.
  • Usikate tamaa, fanya kazi kwa bidii mpaka ufikie malengo yako ya kibiashara

Changamoto na mafanikio

kama mjasiliamali , Priscilla anathibitisha kuwa - "Ujasiliamali ni safari yenye upweke." Alikabiliana na shinikizo la kuhakikisha biashara yake inasimama, huku akifanya kazi muda mrefu kuhakikisha wateja wake wanapata nguzo zao kwa wakatina ameweza kupata mafanikio kwa hilo.

Anasema: ''Kwasababu biashara yangu inakuwa, wakati mwingine ninakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa pesa, na pia suala la mikataba ya ajira anayoifanya na wafanyakazi wake inayomlazimu kuwalipa mshahara katika kipindi fulani ni changamoto''.

Priscilla akitunukiwa tuzo la Queens Young Leaders kutoka kwa Malkia Elizabeth wa Uingereza kwa ajili ya vijana kwa mchango wake wa kutoa ajira kwa wanawake wasiojiweza. mwaka jana

Chanzo cha picha, Priscilla Ruzibuka

Maelezo ya picha, Priscilla akitunukiwa tuzo la Queens Young Leaders kutoka kwa Malkia Elizabeth wa Uingereza kwa ajili ya vijana kwa mchango wake wa kutoa ajira kwa wanawake wasiojiweza, mwaka jana

Priscilla ameweza kupata mafanikio mengi ya kibiashara chini ya nembo yake Kipepeo.

Priscilla pia alitunukiwa tuzo ya Queens Young Leaders, inayotolewa na Malkia Elizabeth wa Uingereza kwa ajili ya vijana. Alipokea tuzo hilo mwaka jana mjini London Uingereza kutokana na mchango wake wa kuwaajiri wanawake wasiojiweza kupitia nembo yake -Kipepeo Kids.

Kipepeo imepokea ufadhili wa mradi wake kutoka kwa Pollination Project wa kiasi cha dola $1000 , ambazo alizitumia kununua mashine bora zaidi za ushonaji na vitambaa na hivyo kupanua zaidi biashara yake.

Akiwa mwanachama wa wahitimua wa taasisi ya Uongozi Afrika Mashariki-YALI, Priscilla alituma maombi ya ufadhili wa maendeleo wa Marekani kwa ajili ya Afrika wa $10,000 ambapo alichaguliwa kupokea pesa hizo. Anatumia fedha hizo kupanua zaidi biashara yake katika mataifa ya kigeni yenye nguo za watoto zenye ubora kutoka Afrika mashariki.

Mwezi Agosti mwaka jana , Priscilla aliweza kupeleka Kipepeo's Kids Clothing katika klabu ya nguo za watoto kwenye maonyesho ya kimataifa mjini New York City. Aliweza kuanzoisha ushirikiano na wafanyabiashara kadhaa na kupata idadi kubwa ya watu waliotaka bidhaa za Ki-pepeo kids.

Priscilla anawaasa vijana wenzake kufanya kazi wanayoipenda kwa bidii. ''Ukifanya kazi unayoipenda na kwa bidii bila shaka utapata mafanikio'' anasema Priscilla.