Afcon 2021: Idadi ya wanaohudhuria mechi za Afcon yawekwa kuwa kati ya 60-80% Cameroon

Chanzo cha picha, Getty Images
Idadi ya wanaohudhuria mechi za Kombe la Mataifa ya Afrika litafikia asilimia 80 ya uwezo wa mechi itakayohusisha wenyeji Cameroon, na 60% kwa mechi nyingine zote kwenye mashindano hayo.
Hatua hiyo ya waandaaji wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf) inakuja kufuatia mashauriano na serikali ya Cameroon kuhusu janga la coronavirus linaloendelea.
Watazamaji lazima wapewe chanjo kamili na wawasilishe matokeo ya vipimo hasi ili kuhudhuria michezo.
Ni asilimia 2 tu ya watu nchini Cameroon wamechanjwa kikamilifu , kwa mujibu wa takwimu kutoka Our World in Data, lakini ripoti zinaonyesha kuwa kumekuwa na ongezeko la watu nchini humo wanaojaribu kupata chanjo ili waweze kununua tiketi za Kombe la Mataifa ya Afrika. .
"Caf itaendelea kufuatilia hali na mabadiliko ya hali ya afya na kurekebisha hatua kama itahitajika," ilisema taarifa ya shirikisho la soka barani Afrika.
Cameroon itafungua dimba dhidi ya Burkina Faso kwenye Uwanja wa Olembe mjini Yaounde, ambao una uwezo wa kuchukua watu 60,000, siku ya Jumapili (16:00 GMT).
Visa zaidi vya Covid vimerekodiwa katika vikosi
Huku janga la Coronavirus likionekana kuwa na athari kwenye Kombe la Mataifa kwenye uwanja na hata nje yake.
Wapinzani wa Kundi A la Cameroon, Cape Verde wameripoti kesi kadhaa kwenye kambi yao ya mazoezi ya kabla ya mechi, huku kocha Bubista akibainika kuwa miongoni mwa waliopatikana na virusi hivyo.
Blue Sharks ina wachezaji sita - wakiwemo makipa wawili - wanaojitenga kabla ya mechi yao dhidi ya Ethiopia Jumapili.
Senegal, washindi wa pili mwaka wa 2019, walichelewesha kuondoka kwa dimba hilo baada ya Saliou Ciss, Mamadou Loum na Habib Diallo kukutwa na virusi, huku kesi zingine zikishukiwa.
Fowadi wa Tunisia Seifeddine Jaziri na winga Youssef Msakni pia wamepimwa na kukutwa na virusi wiki hii.
Jaziri alikuwa mfungaji bora wa Fifa Arab Cup nchini Qatar mwezi uliopita, akifunga mabao manne Tunisia ilipotinga fainali ambapo walifungwa 2-0 na Algeria huku Msakni akipangwa kufuzu kwa mara ya saba mfululizo ya Kombe la Mataifa ya Afrika.














