Matokeo ya uchaguzi tanzania 2020: Je Kassim Majaliwa kurejea katika wadhifa wa Waziri Mkuu?

Kassim majaliwa
Maelezo ya picha, Waziri mkuu wa Tanzania Kassim majaliwa
    • Author, Na Ezekiel Kamwaga
    • Nafasi, Mchambuzi

KAMA ningekuwa mcheza kamari, leo ningeweka kete zangu mezani kwamba Rais John Magufuli atamteua tena, Kassim Majaliwa, kuendelea kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika historia ya Tanzania, ni Waziri Mkuu mmoja tu, Frederick Sumaye, ndiye aliyefanikiwa kukaa madarakani kwa kipindi cha miaka 10; ikimaanisha katika muda wote wa urais wa hayati Rais Benjamin Mkapa.

Kwa hiyo si kazi rahisi sana kubashiri moja kwa moja kwamba Majaliwa; ambaye hakupewa nafasi na wengi ya kushika wadhifa huo miaka mitano iliyopita, ataendelea na Magufuli hadi mwisho na hivyo kufikia rekodi iliyowekwa na Sumaye.

Hata hivyo, kuna mambo makubwa matatu ambayo yananipa picha kwamba mwelekeo ni kwa Majaliwa ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Ruangwa kuwa ataendelea na wadhifa wake huo.

Kauli na matendo ya Rais Magufuli kwake

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Rais Magufuli alizungumza wakati wa tukio la kuapishwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Adelardus Kilangi, kwamba viongozi wa serikali hawatakiwi kuwa na hofu ya nafasi zao kwa sababu mafanikio yaliyopatikana katika miaka mitano iliyopita yalitokana na ufanisi wao pia.

Ingawa alisema kutakuwa na mabadiliko makubwa katika baraza jipya la mawaziri, ni vigumu kutenganisha mafanikio ya utawala wa Awamu ya Tano na utendaji wa Waziri Mkuu. Katika mawaziri wote wa serikali ya Rais Magufuli, Majaliwa - kama kiranja wa mawaziri wengine, ndiye pekee ambaye nafasi yake inafungamanishwa moja kwa moja na Rais katika utendaji.

Rais Magufuli na waziri mkuu Kassim Majaliwa
Maelezo ya picha, Rais Magufuli na waziri mkuu Kassim Majaliwa

Kama Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa na Wakurugenzi wanapongezwa kwa kazi nzuri, ni vigumu kumwondoa Waziri Mkuu katika kundi hilo - ingawa ni muhimu pia kufahamu kwamba katika awamu hii ya uongozi, Ofisi ya Rais na si Waziri Mkuu, ndiyo iliyokuwa ikisimamia masuala ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Jambo lingine ambalo limenifanya niweke kete zangu kwa Majaliwa ni suala la kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28 mwaka huu. Hakuna kiongozi wa serikali aliyezunguka katika mikoa mingi kumuombea kura Rais Magufuli kuliko Majaliwa. Kimsingi, ingawa hakuwa mgombea urais katika kampeni hizo, Majaliwa alizunguka katika mikoa mingi kuliko hata Rais mwenyewe.

Jambo la kufahamu kuhusu kampeni za uchaguzi wa mwaka 2020 ni kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kiliendesha kampeni tofauti na ilivyozoeleka miaka ya nyuma. Hakukuwa na viongozi wengi waliokuwa wakizunguka kumwombea kura Magufuli na ni kama vile chama kiliamua hivyo.

Ni Majaliwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan - aliyekuwa mgombea mwenza, ndiyo waliozunguka nchi nzima kuomba kura za wagombea wa CCM katika uchaguzi huo. Hii ndiyo kusema, Rais Magufuli alikuwa na imani na Majaliwa kwa sababu kama isingekuwa hivyo, angeweza kumwambia abaki jimboni kama walivyobaki wanasiasa wengine waliotaka kuingia kwenye kampeni za kumsaidia Magufuli lakini wakatakiwa kubaki majimboni mwao.

Jambo hilo pekee limeonyesha imani ambayo Rais Magufuli anayo kwa Majaliwa na ni imani hiyo ambayo inamfanya Majaliwa awe mstari wa mbele miongoni mwa wale ambao Rais anaweza kuamua kumpa nafasi mmoja wao.

Ingawa anafikisha miaka 60 mwezi ujao, Majaliwa anaonekana bado ana nguvu ya kufanya kazi na kwa serikali ambayo inafanya jitihada kubwa ya kubana matumizi, kuchagua mtu mwingine kuwa Waziri Mkuu itamaanisha kuongeza gharama nyingine kwa serikali kumhudumia kiongozi mstaafu wa kitaifa.

Kwanini asiwe Majaliwa?

Katika historia ya Tanzania, ni watu 10 tu - kabla ya Majaliwa, wamewahi kushika wadhifa wa Waziri Mkuu wa taifa hili. Watu hao ni Julius Nyerere (wakati huo Tanzania ikijulikana kama Tanganyika), Rashid Kawawa, Edward Sokoine, Cleopa Msuya, Dk. Salim Ahmed Salim, Joseph Warioba, John Malecela, Sumaye, Edward Lowassa na Mizengo Pinda.

Miongoni mwa wote hao, ni mmoja tu; Sumaye, ndiye aliyekaa madarakani kwa vipindi viwili vya bosi wake. Hiyo maana yake ni kwamba katika wastani wa kawaida, nafasi yake ni ndogo kurejea kwenye nafasi hiyo.

Katika kitabu ninachoandika cha Waziri Mkuu, kinachotazama cheo, wasifu na uzoefu wa mawaziri wakuu waliowahi kuongoza Tanzania, nimejifunza jambo moja kuhusu wadhifa huu.

Katika mahojiano yangu na Sumaye, alinieleza wazi kwamba kihistoria, nafasi ya Waziri Mkuu hapa Tanzania inafaa kwa mtu anayeweza kutumika kama begi la kufanyia mazoezi la mabondia (punching bag) kumkinga Rais.

" Waziri Mkuu mzuri ni yule ambaye ataruhusu lawama zote ambazo zingeweza kwenda kwa Rais zipitie kwake kwanza. Kama ukiona Rais anapata lawama zote na Waziri Mkuu anaonekana mzuri, ujue hapo kuna tatizo ama la utendaji au kwenye mfumo," alinieleza Sumaye.

Wakati wa utawala wa Mkapa, Sumaye alipachikwa majina mengi yaliyomwonyesha kama mtu asiye na maarifa na anayefanya mambo kwa mtulinga. Huko nyuma zaidi, swahiba wa Nyerere, Mzee Kawawa, alitungiwa hadi michapo ya kwenye vijiwe vya kahawa iliyoonyesha kama mtu asiyejua hata vitu vidogo tu vya kiitifaki.

Miongoni mwa mawaziri wakuu wote waliotangulia, ni Sokoine pekee ambaye Watanzania walimchukulia kwa heshima kubwa hadi alipofariki dunia kwa ajali ya gari iliyotokea mkoani Morogoro mwaka 1984.

Hata hivyo, staili ya utawala ya Magufuli ni tofauti na watangulizi wake wote. Yeye ni kiongozi ambaye anaongoza kwa mfano na hivyo anashindwa kuepuka lawama za moja kwa moja kwenye utawala wake.

Staili hii ya Magufuli imemfanya Majaliwa akwepe mishale mingi ambayo ingeelekezwa kwake kama utendaji wa Rais wa sasa ungefanana na wa watangulizi wake. Kwa sababu hii, kuna wanaoamini kwamba Majaliwa hakufanya kazi nzuri ya kuhakikisha lawama za Rais zinaelekezwa kwake.

Kwa miaka hii mitano ya kwanza, Rais ndiye amekuwa punching bag ingawa hilo linaweza lisiwe tatizo la Majaliwa moja kwa moja bali la staili ya utendaji ya bosi wake.

Nini changamoto za Waziri Mkuu ajaye?

Waziri Mkuu ana kazi kubwa mbili; kusimamia shughuli za kila siku za serikali na kuwasimamia wabunge wa chama chake wanapokuwa bungeni. Yeye ndiye Mkuu wa Shughuli za Serikali Bungeni.

Matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, yatalifanya Bunge la 12 kuwa tofauti na mabunge karibu yote yaliyotangulia kuanzia mwaka 2000. Kwa kiasi kikubwa, Bunge hili litakuwa kama la chama kimoja.

Waziri Mkuu atakayeteuliwa na Rais Magufuli atakuwa na kazi kubwa mbili bungeni; mosi kuhakikisha linatengeneza taswira nzuri kwa serikali na chama chake na pili kuhakikisha anaongoza vema makundi tofauti yatakayojitokeza miongoni mwa wabunge wa CCM.

Ni jambo lisilo la siri kwamba CCM -kwa miaka yote, kimekuwa chama cha makundi yenye maslahi tofauti ambayo yanaunganishwa na jambo tu la kuhakikisha chama hicho kinabaki madarakani.

Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, makundi haya ya ndani ya CCM yatajidhihirisha zaidi wakati chama hicho kikijiandaa kupata mtu atakayerithi nafasi ya Magufuli katika uchaguzi ujao. Waziri Mkuu ajaye anatakiwa kuwa mtu ambaye atajua namna ya kudhibiti makundi maslahi haya ya ndani ya CCM.

Kuna uwezekano mkubwa kwamba mbadala wa Rais Magufuli atakuwa miongoni mwa watu watakaokuwa ndani ya Bunge la 12 - naye na wengine watakaowania nafasi hiyo watataka kutanua misuli yao ya kisiasa bungeni.

Ni wazi kwamba Waziri Mkuu ajaye pia atataka kuwa sehemu ya mafanikio ya utawala wa Awamu ya Tano. Kihistoria, kuondoa Sokoine ambaye alifariki mapema kabla ya kuonyesha nia ya kutaka urais, mawaziri wakuu wote waliotangulia wamewahi kuwania nafasi hiyo ya juu ya uongozi.

Ni jambo linalotarajiwa kwamba Waziri Mkuu ajaye naye atakuwa mstarini kuomba nafasi ya kumrithi Magufuli wakati utakapofika. Namna pekee ya kupata nafasi hiyo ni kuhakikisha anakuwa sehemu ya mafanikio ya utawala huu ili kwamba wakati utakapofika, sifa zake zijiuze zenyewe kama ilivyokuwa kwa Rais wa sasa miaka mitano iliyopita.

Waziri Mkuu ajaye ataanza kazi katika nchi ambayo inapitia katika wakati mgumu wa mgawanyiko uliosababishwa na uchaguzi wa mwaka huu. Tofauti na Rais Magufuli ambaye ana miaka mitano tu ya kutumikia Watanzania kwa mujibu wa Katiba, Waziri Mkuu mpya anatarajiwa kuwa na maisha mengine ya kisiasa baada ya awamu ya tano.

Kwa sababu hiyo, yeyote atakayepewa nafasi hiyo anatakiwa kuwa mtu ambaye maneno na matendo yake yanatakiwa kuonyesha maridhiano na mapatano katika kujenga Tanzania yenye amani na maelewano kuanzia wakati huu na kuendelea.

Bahati moja mbaya kwa wanaoshika nafasi hii ni kwamba kuondoa Nyerere, hakuna mtu aliyewahi kuwa Waziri Mkuu na kuja kuwa Rais hata kama huwa wanajitosa katika kinyang'anyiro hicho. Tatizo lao kubwa huwa ni kwamba utendaji wao huwa umejifungamanisha na utawala unaoondoka madarakani kiasi kwamba nao hujikuta wamechokwa na wapiga kura.

Jambo moja ambalo Waziri Mkuu ajaye anapaswa kulifanya ni kufanya au kutengeneza jambo litakalomfanya aonekane tofauti au kuwa na sifa ya utendaji kazi wa jambo fulani kama vile ujenzi wa barabara ulivyohusishwa na Magufuli miaka mitano iliyopita.

Si jambo rahisi sana lakini Waswahili wana msemo; Penye Nia, Pana Njia.