Mbwana Samatta: Mshambuliaji kinara wa Tanzania afunga bao la kufutia machozi Genk ikilazwa 2-1 na Liverpool

Mbwana Samatta, Mshambuliahi wa KRC Genk

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 2

Mshambuliaji kinara wa klabu bingwa ya Ubelgiji KRC Genk na nahodha wa Tanzania, Mbwana Samatta, hatimaye amepachika goli dhidi ya vigogo wa England klabu ya Liverpool jana usiku.

Goli hilo lilikuwa likisubiriwa kwa hamu na mashabiki wa mpira wa miguu nchini Tanzania.

Hata hivyo, matokeo ya mwisho ya mchezo huo wa Klabu Bingwa Ulaya yalikuwa mabaya kwa Genk kwa kulazwa kwa goli 2-1.

Samatta, aliunganisha kwa kichwa mpira wa kona mpaka wavuni katika dakika ya 40 ya mchezo.

Mshambuliaji huyo ambaye ameweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza michuano hiyo mikubwa zaidi ya vilabu barani Ulaya tayari ameshapachika magoli mawili katika mechi nne.

Katika mechi ya mkondo wa kwanza dhidi ya Liverpool, Samatta pia alipachika bao la kichwa ambalo hata hivyo lilikataliwa baada ya kumchezea rafu mchezaji wa Liverpool kabla ya kupachika bao.

Goli la kwanza la Liverpool katika mchezo huo lilifungwa na Georginio Wijnaldum katika dakika ya 14 baada ya safu ya ulinzi ya Genk kufanya uzembe wa kuondosha krosi iliyochingwa na winga wa Liverpool James Milner.

Ruka X ujumbe
Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

Onyo: Imetoka kwingine na inaweza kuwa na matangazo

Mwisho wa X ujumbe

Samatta aliirejesha Genk mchezoni kwa kombora la kichwa dakika tano kabla ya mapumziko, hata hivyo Alex Oxlade-Chamberlain aliiandikia Liverpool bao la ushindi katika dakika ya 53.

Kwa matokeo hayo, Liverpool imepanda mpaka kileleni mwa kundi E kwa kufikisha alama tisa baada ya michezo minne. Napoli imeshuka mpaka nafasi ya pili baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na RB Salzburg. Genk inashika mkia kwa kusalia na alama moja.

Genk haina historia nzuri kwenye michuano hii, ikiwa hii ni mara ya tatu kwa klabu hiyo kucheza hatua ya makundi ya Champions League. Haijawahi kupata ushindi hata mmoja kwenye mechi 16 sasa.

Katika misimu hiyo ya 2002-03 na 2011-12 Genk ilimaliza mkiani kwenye makundi iliyopangiwa, kama ilivyo mpaka sasa kwenye msimu huu ikisalia na mechi mbili tu kujikomboa na 'nuksi' hiyo.

Matokeo ya mechi za Novemba 5, 2019

  • Barcelona 0-0 Slavia Prague
  • Zenit 0- RB Leipzig
  • Liverpool 2-1 KRC Genk
  • Napoli 1-1 RB Salzburg
  • B Dortmund 3-2 Inter Milan
  • Lyon 3-1 Benfica
  • Chelsea 4-4 Ajax
  • Valencia 4-1 Lille