Kombe la Dunia Urusi 2018: Nyota wa Manchester City Leroy Sane aachwa nje kikosi cha Ujerumani

Winga wa Manchester City Leroy Sane ameachwa nje ya kikosi cha mwisho cha Ujerumani ambacho kitawakilisha mabingwa hao watetezi Kombe la Dunia baadaye mwezi huu.

Sane, wachezaji wa Bayer Leverkusen Bernd Leno na Jonathan Tah na mshambuliaji wa Freiburg Nils Petersen wote wameachwa nje Joachim Low alipopunguza kikosi chake kutoka wachezaji 27 hadi 23.

Kipa Manuel Neuer, aliyerejea kucheza baada ya kukaa nje miezi tisa wakati wa mechi ambayo walilazwa na Austria 2-1 Jumamosi, yumo kwenye kikosi.

Kuna wachezaji watatu wa Ligi ya Premia.

Beki wa Chelsea Antonio Rudiger, kiungo wa kati wa City Ilkay Gundogan na kiungo wa Arsenal Mesut Ozil wamo kikosini.

Ujerumani wamo Kundi F na Mexico, Sweden na Korea Kusini, na watacheza mechi yao ya kwanza mnamo Jumapili 17 Juni.

Sane alikuwa ameng'aa sana akichezea Manchester City kiasi kwamba alitawazwa mchezaji bora chipukizi wa mwaka Ligi ya Premia.

Alifungia City magoli 14 na kusaidia ufungaji wa mabao mengine 19.

Kiungo wa kati Ozil alifunga mabao matano na kusaidia ufungaji wa mabao 14 akichezea Arsenal msimu uliopita. Hata hivyo aliunda nafasi 84 za ufungaji Ligi ya Premia akilinganishwa na Sane aliyetengeneza nafasi 58.

Low amesema kulikuwa na ushindani mkali kati ya Sane na Julian Brandt, aliyefunga mabao 12 na kusaidia ufungaji wa mengine saba akichezea Bayer Leverkusen.

Sane amechezea Ujerumani mechi sita kati ya saba za karibuni. Alianza kikosi Jumamosi dhidi ya Austria.

Kikosi cha Ujerumani cha wachezaji 23

Walinda lango: Manuel Neuer (Bayern Munich), Marc-Andre ter Stegen (Barcelona), Kevin Trapp (Paris St-Germain)

Mabeki: Jerome Boateng (Bayern Munich), Matthias Ginter (Borussia Monchengladbach), Jonas Hector (Cologne), Mats Hummels (Bayern Munich), Joshua Kimmich (Bayern Munich), Marvin Plattenhardt (Hertha Berlin), Antonio Rudiger (Chelsea), Niklas Sule (Bayern Munich)

Viungo wa kati: Julian Brandt (Bayer Leverkusen), Julian Draxler (Paris St-Germain), Leon Goretska (Schalke), Ilkay Gundogan (Manchester City), Sami Khedira (Juventus), Toni Kroos (Real Madrid), Mesut Ozil (Arsenal), Sebastian Rudy (Bayern Munich)

Washambuliaji: Mario Gomez (Stuttgart), Thomas Muller (Bayern Munich), Marco Reus (Borussia Dortmund), Timo Werner (RB Leipzig)