Real Madrid wafikia rekodi ya Barca La Liga

James Rodriguez

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Rodriguez amefunga mabao mengi kutoka nje ya eneo la hatari kushinda kiungo mwingine yeyote wa kati ligi tano kuu za Ulaya tangu 2014-15

Real Madrid wamecharaza Espanyol 2-0 na kufikia rekodi ya Barcelona ya kushinda mechi 16 mfululizo katika ligi kuu ya Uhispania, La Liga.

Ushindi wao mechi hiyo ya Jumapili umewaweka alama tatu mbele kileleni mwa ligi hiyo.

Mabao kutoka kwa James Rodriguez na Karim Benzema yaliwawezesha kufikia rekodi hiyo iliyowekwa na Barcelona walipokuwa chini ya Pep Guardiola msimu wa 2010-11.

Real, walicheza bila nyota wao Gareth Bale na Cristiano Ronaldo ugenini uwanja wa Cornella-El Prat lakini hilo halikuwazuia kuandikisha ushindi wao wa nne kutoka kwa mechi nne walizocheza msimu huu.

Gareth Bale

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Bale aliumia akicheza dhidi ya Sporting Lisbon

Barcelona wanashikilia nafasi ya pili ligini kwa sasa wakiwa na alama tisa, sawa na Las Palmas. Madrid wana alama 12.