Israel yashambulia Rafah licha ya Marekani kupinga hatua hiyo
Mashambuzi makali ya makombora yameripotiwa katika mji huo hata baada ya Rais Biden kuonya Marekani itasitisha kuipa silaha Israel itakapoanzisha operesheni ya ardhini.
Moja kwa moja
Asha Juma and Ambia Hirsi
Polisi wa Israel wavamia studio inayohusishwa na Al Jazeera

Chanzo cha picha, Shlomo Karhi
Israel inasema imevamia studio inayotumiwa Al Jazeera huko Nazareth, katika mzozo wa hivi punde kati ya nchi hiyo na kituo shirika hilo la utangazaji.
Waziri wa Mawasiliano Shlomo Karhi alihusisha shirika hilo la habari na kundi la Hamas na kusema vifaa vilikuwa vikichukuliwa katika mji wa kaskazini mwa Israel siku ya Alhamisi asubuhi.
Al Jazeera hapo awali ilitaja madai kuwa kituo chake ni tishio kwa usalama wa Israel kuwa "uongo na kichekesho".
Tukio hilo linakuja baada ya polisi wa Israel kulenga ofisi ya Al Jazeera huko Jerusalem Mashariki katika eneo inayokaliwa kimabavu Jumapili iliyopita.
Uhusiano kati ya shirika hilo la utangazaji na serikali ya Israel umekuwa wa wasiwasi kwa muda mrefu lakini umezidi kuwa mbaya kufuatia kuzuka kwa vita huko Gaza.
Haaland ajumuishwa kwenye orodha ya mchezaji bora wa Ligi Kuu ya England

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Mshambuliaji wa Manchester City Erling Haaland Mshambuliaji wa Manchester City Erling Haaland huenda akachaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya England kwa mwaka wa pili mfululizo.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Norway mwenye umri wa miaka 23 ameteuliwa kuwania tuzo hiyo pamoja na mchezaji mwenzake wa City Phil Foden
Viungo wa Arsenal Martin Odegaard na Declan Rice, mshambuliaji wa Chelsea Cole Palmer, mshambuliaji wa Newcastle Alexander Isak, mshambuliaji wa Aston Villa Ollie Watkins na mlinzi wa Liverpool Virgil van Dijk pia wamejumuishwa kwenye orodha hiyo.
Mshindi, ataamuliwa kwa kura ya umma na jopo la Ligi Kuu, atatangazwa tarehe 18 Mei.
Kocha wa City Pep Guardiola, mshindi mara nne wa tuzo ya kocha bora wa msimu, ameorodheshwa tena, pamoja na Mikel Arteta wa Arsenal, Jurgen Klopp wa Liverpool, Unai Emery wa Villa na Andoni Iraola wa Bournemouth.
Mwaka jana Haaland alikua mchezaji wa kwanza kushinda tuzo ya mchezaji bora wa msimu na tuzo ya mchezaji aliye na umri mdogo baada ya kufunga mabao 36 katika mechi 35 za Ligi Kuu ya England.
Mashambulizi ya Rafah: Ni nini kinachoendelea?
Mashambulizi makali ya makombora yameripotiwa mjini Rafah, huku waliyoshuhudia wakielezea "msururu" wa mashambulizi ya usiku kucha.
Haya ndio matukio ya hivi punde kwa mukhtasari:
- Rais wa Marekani Joe Biden ameonya Israel dhidi ya kushambulia mji wa Rafah, akisema yuko tayari kusitisha usambazaji wa silaha ikiwa wanajeshi wa Israel watavamia mji huo.
- Balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa Gilad Erdan, ameelezea onyo la Biden kama la "kuvunja moyo sana"
- Scott Anderson, kutoka UNRWA, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina, ameambia BBC kuwa mapigano yanaelekea katikati mwa jiji.
- Takriban watu 80,000 wameukimbia mji huo tangu Jumatatu,UNRWA inasema
- Mazungumzo ya kusitisha mapigano yanaanza tena mjini Cairo, huku wajumbe kutoka Israel, Hamas na Marekani wakikutana na wapatanishi wa Misri na Qatar.
Somalia yaomba ujumbe wa Umoja wa Mataifa kuondoka nchini humo,
Somalia inasema haitaongeza tena mamlaka ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo.
Waziri wa Mambo ya Nje ameliambia Baraza la Usalama kwamba serikali yake ina imani katika juhudi zake za kudumisha amani na ustawi kufuatia miongo kadhaa ya ukosefu wa utulivu kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe na mashambulizi yanayohusiana na ugaidi.
Ujumbe huo sasa unatarajiwa kumaliza muda wake mwezi Oktoba kwa ombi la nchi hiyo.
Katika barua kwa baraza la usalama, Waziri wa Mashauri ya Kigeni Mohamed Fiqi anasema uamuzi huo umeafikiwa baada ya kuzingatia kwa kina vipaumbele vya serikali yake.
Bw.Fiqi anasema ujumbe huo umekuwa na mchango mkubwa kueleka upatikanaji wa amani, utulivu na maendeleo nchini.
Pia ameutaka ujumbe huo kuanza taratibu za kusitisha shughuli zake.
Serikali ya Rais Hassan Sheikh imekuwa katika harakati ya kuifanya Somalia kuwa taifa lenye utulivu na amani baada ya miaka mingi ya ukosefu wa utulivu.
Ndege aina ya Boeing 737 yaanguka wakati wa kupaa nchini Senegal

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Picha ya Boeing 737-300 ikiwa Hangzhou, China. Ndege aina ya Boeing 737-300 imeanguka wakati ikipaa nchini Senegal na kujeruhi watu 11, wanne kati yao vibaya.
Ndege ya Air Senegal HC 301 iliyokuwa ikielekea mji mkuu wa Mali Bamako ilitoka kwenye njia ya kurukia ndege mapema Alhamisi, Mamlaka ya uwanja wa ndege wa Dakar wa Blaise Diagne ulisema katika taarifa.
Rubani alijeruhiwa kidogo, lakini idadi kubwa ya abiria 78 waliokuwemo hawakujeruhiwa katika tukio hilo.
Shughuli zimesitishwa katika uwanja wa ndege.
Huduma za dharura katika uwanja wa ndege zimasaidia kuwaondoa abiria, taarifa ya uwanja huo wa ndege ilisema.
Uchunguzi umeanzishwa kubaini chanzo cha ajali.
Boeing haijazungumzia tukio hilo wala Transair, kampuni ya kibinafsi ambayo Air Senegal ilikodisha ndege hiyo
Ingawa bado haijajulikana ni nini kilisababisha ajali hiyo, inakuja wakati shirika la Boeing anakabiliwa na changamoto kubwa kuhusu usalama wa ndege zake.
Wanachama wanne wa Hezbollah wauawa Lebanon katika shambulizi la Israel- chanzo cha usalama
Mamlaka ya Ulinzi wa raia wa Lebanon unasema watu wanne wameuawa katika shambulizi la Israel dhidi ya gari kusini mwa Lebanon, huku chanzo cha usalama kikiambia AFP kuwa walikuwa wanachama wa Hezbollah - kundi la Kishia linaloungwa mkono na Iran.
Israel imekuwa ikifanya mashambulizi kusini mwa Lebanon karibu kila siku tangu Hezbollah iliporusha makombora dhidi ya Israel tarehe 8 Oktoba ili kuunga mkono Hamas huko Gaza, na hivyo kusababisha mfululizo wa mashambulizi ya kukabiliana nayo.
Jeshi la Israel limeliambia shirika la habari la AFP kwamba halitoi maoni yoyote kuhusu ripoti katika vyombo vya habari vya kigeni.
Jeshi la Israel linasema linalenga wanachama na miundombinu ya Hezbollah, na kulipiza kisasi mashambulizi dhidi ya kambi za jeshi la Israel kaskazini mwa Israel.
Soma pia:
Katika Picha: Wapalestina wakimbia baada ya Israel kushambulia Rafah
Mashambuzi makali ya makombora yameripotiwa katika mji huo huku Rais Biden kuonya kuwa Marekani itasitisha kusambaza silaha kwa Israel itakapoanzisha operesheni ya ardhini.
"Walianza kutushambulia kwa makombora: watoto, wanawake na wazee," mmoja wa wakazi Khaled Taweel aliambia BBC.

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Shirika la Umoja wa Mataifa linasema watu 80,000 wameukimbia mji huo wiki hii huku mapigano yakiendelea viunga mwake. 
Chanzo cha picha, ABIR SULTAN/EPA-EFE/REX/Shutterstock
Maelezo ya picha, Wanajeshi wa Israel wakiwa na magari ya kijeshi wanaonekana wakiwa wamekusanyika katika eneo lisilojulikana karibu na uzio wa mpaka na Ukanda wa Gaza, kusini mwa Israel. 
Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Mwanamke wa Kipalestina akishuka kwenye ngazi ya nyumba iliyobomoka baada ya shambulizi. 
Chanzo cha picha, Reuters
Mafuriko Kenya: Serikali inatathmini hali kabla shule kufunguliwa tena

Chanzo cha picha, Getty Images
Kenya inafuatilia kwa makini hali katika shule zote nchini kuhakikisha usalama wa wanafunzi kabla ya shule kufunguliwa tena kwa muhula wa pili wiki ijayo baada ya kuahirishwa kufuatia mvua kubwa na mafuriko.
Kulingana na taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani, Mpango huo unaongozwa na Utawala wa Serikali ya Kitaifa Maafisa (NGAOs) kwa ushirikiano na Wakurugenzi wa Elimu wa Mikoa na Kaunti.
“Wanafunzi hasa wa shule za bweni wataanza kurejea kati ya Ijumaa na Jumatatu. Licha ya changamoto kadhaa, tumeweka mikakati ya kuhakikisha usalama wa wanafunzi," alisema Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani na Usalama wa Kitaifa Dk. Raymond Omoll.
Huku hayo yakijiri Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu ametangaza kwamba serikali itaongeza muhula wa pili ili kufidia muda uliopotea baada ya muda wa kufungua shule kuahirishwa kwa wiki mbili kutokana na mafuriko.
Shule zilipaswa kufunguliwa Aprili 29 lakini serikali iliahirishwa kufuatia mvua kubwa na mafuriko ambayo kufikia sasa yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 257.
Wiki iliyopita Rais William Ruto alitangaza kuwa wanafunzi watarejea shuleni Jumatatu, Mei 13, baada ya utabiri wa mamlaka ya utabiri wa hali ya hewa kuoonyesha kupungua kwa mvua kuanzia wikendi hii.
Soma pia:
Rafah imekumbwa na mashambulizi makali zaidi kuliko wiki mbili zilizopita - Afisa wa UN
Mji wa Rafah umekumbwa na mashambulizi makali zaidi ya mabomu katika muda wa saa 24 zilizopita ikilinganishwa na wiki mbili zilizopita, mfanyakazi wa shirika la kutoa misaada katika eneo hilo ameiambia BBC.
Louise Waterridge, afisa wa mawasiliano katika shirika la Umoja wa Mataifa la misaada kwa wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, anasema mashambulizi hayo yameendelea hadi "asubuhi ya leo umbali wa maili kadhaa mashariki mwa Rafah".
Waterridge anasema jengo alilomo, magharibi mwa Rafah, "linatikiswa mara kwa mara kutokana na milipuko ya mabomu iliyo karibu" na kwamba anaweza kuona magari yakiondoka eneo hilo kutoka kwa dirisha lake, yakiwa yamebeba familia zilizohamishwa.
Kuna watu huko Rafah ambao "hawawezi kuhamia mbali sana kwa sababu ya wazazi wazee au watoto wadogo", anasema.
"Nafasi inayopatikana mahali pengine ni ndogo sana, miundombinu imeharibiwa sawa kila mahali katika Ukanda wa Gaza na hakuna uhakika wa usalama wowote", Waterridge anaongeza.
'Kila wakati ninapoona madaktari wakiandamana nakumbuka jinsi mtoto wangu alivyofariki'
Maelezo ya video, 'Kila wakati ninapoona madaktari wakiandamana, nakumbuka jinsi mtoto wangu alivyofariki' Madaktari nchini Kenya wamesitisha mgomo ambao ulikuwa umelemaza mfumo wa huduma za afya nchini kwa siku 56.
Muungano wa madaktari na serikali walifikia makubaliano baada ya mazungumzo makali. Moja ya masuala yenye utata bado hayajatatuliwa.
Madaktari huo sasa wanatarajiwa kurejea kazini ndani ya saa 24 zijazo.
Zaidi ya mwezi mmoja baada ya mgomo huo, familia zilizotegemea taasisi za afya za umma kwa ajili ya huduma za matibabu ziliathirika sana.
Kassim na Rophine walipoteza mtoto wao. Hii ni hadithi yao.
Imetayarishwa na Carolyne Kiambo na Dorcas Wangira
Mhariri wa video- Jeff Sauke
'Inasikitisha sana': Afisa wa Israel asema juu ya tishio la Biden la kuinyima silaha

Chanzo cha picha, Reuters
Tishio la Joe Biden la kukata usambazaji zaidi wa silaha kwa Israel katika tukio la shambulio kamili dhidi ya Rafah "ni la kukatisha tamaa sana", balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa anasema.
"Hii ni kauli ngumu na ya kukatisha tamaa sana kusikia kutoka kwa rais ambaye tumekuwa tukimshukuru tangu mwanzo wa vita," Gilad Erdan anaiambia redio ya umma ya Israel Kan.
"Ikiwa Israel imezuiwa kuingia katika eneo muhimu na la kati kama Rafah ambako kuna maelfu ya magaidi, mateka na viongozi wa Hamas, ni jinsi gani hasa tunapaswa kufikia malengo yetu?"
Soma zaidi:
Afisa wa UN asema hali huko Rafah 'inazidi kutia wasiwasi'

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Hali ilivyo huko Rafah asubuhi ya leo Afisa wa Umoja wa Mataifa, wa masuala ya wakimbizi wa Kipalestina huko Gaza Scott Anderson, amesema hali nayoendelea huko Gaza "imezidi kutia wasiwasi".
Wiki hii, Israel ilitoa maagizo ya kuhama katika maeneo ya mashariki ya Rafah. Anderson anasema mara moja kulikuwa na mapigano upande wa magharibi -"kuelekea katikati ya Rafah yenyewe" - na baadhi ya watu 80,000 sasa wameyahama makazi yao zaidi.
"Labda jambo la kuhuzunisha zaidi, kwa sababu maeneo ya kuingia Kerem Shalom na Rafah [ndani ya Gaza] yamefungwa... tunaanza kukosa mafuta," Anderson amezungumza katika kipindi cha Today kwenye Radio 4.
Anderson ameongeza kuwa ingawa kivuko cha Erez kaskazini bado kiko wazi, kazi zinazoendeshwa huko ni kidogo kwa idadi kubwa ya watu - milioni 1.9 - ambao wako sehemu ya kusini ya Ukanda huo.
"Tunahitaji sana vivuko kufunguliwa tena ili misaada iendelee kuingia, kwani hivi karibuni tutaona Umoja wa Mataifa na washirika wetu wa kibinadamu wakianza kukosa chakula hata kuanzia kesho," Anderson anasema.
Soma zaidi:
Human Rights Watch yadai vikosi vya RSF nchini Sudan vilitekeleza mauaji ya halaiki Darfur,

Chanzo cha picha, Reuters
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch linasema wanajeshi wa Rapid Support Forces wa Sudan na washirika wake wa Kiarabu huenda walifanya mauaji ya halaiki katika mji wa Darfur Magharibi wa El Geneina.
Pia linawatambua makamanda watatu wa RSF waliohusika na ukatili huo, akiwemo kiongozi wa kundi hilo, Mohammed Hamdan Dagalo, maarufu kwa jina la Hemedti.
Vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya RSF na jeshi vimezua mzozo mkubwa wa kibinadamu na uhamishaji makazi inapoingia mwaka wake wa pili.
Mengi yameripotiwa kuhusu mawimbi ya mashambulizi dhidi ya wakazi wa El Geneina ambao wengi wao si Waarabu mwaka jana.
Lakini hii ni moja ya uchunguzi wa kina zaidi hadi sasa.
Inahitimisha kuwa RSF na washirika wake wa Kiarabu walifanya uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita kwa kuwalenga Massalit.
Na inazua uwezekano kwamba wanaweza kuwa na nia ya kuharibu jamii ya Darfur Magharibi, ambayo ingeashiria mauaji ya halaiki.
Kiongozi wa RSF Jenerali Hemedti amekanusha wapiganaji wake kuwashambulia raia kimakusudi.
Lakini Human Rights Watch inasema yeye ni miongoni mwa wale walio na jukumu la amri juu ya vikosi vilivyofanya ukatili huo.
Marekani na mwendesha mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wamezungumza kuhusu uhalifu wa kivita kwa pande zote mbili, lakini hawajataja hasa mauaji ya halaiki.
Soma zaidi:
Watu 81 ndio waliokuwa katika eneo la jengo lililoporomoka Afrika Kusini

Chanzo cha picha, FB/GEORGE MUNICIPALITY
Wafanyakazi 81 sasa wamethibitishwa kuwa walikuwa kwenye eneo wakati jengo katika mji wa George wa Afrika Kusini linapoporomoka.
Mamlaka ya eneo hilo ilithibitisha takwimu mpya ikitoa uhakiki wa rekodi za usalama za mwanakandarasi.
Idadi hiyo inatolewa wakati waokoaji wakipambana dhidi ya muda muhimu katika uokoaji wa saa 72 kutafuta manusura.
Shughuli za uokoaji ziliendelea nyakati za usiku kwa kutumia vivunja zege pamoja na lori kuondoa vifusi.
Katika taarifa iliyotolewa Alhamisi asubuhi mamlaka ya eneo hilo ilisema jumla ya watu 37 hadi sasa wamepatikana, na vifo vinane na watu 44 bado hawajulikani waliko.

Soma zaidi:
Mfichuzi: Mzambazaji wa Boeing alituma vifaa vyenye kasoro

Chanzo cha picha, Getty Images
Sehemu kuu za ndege zilizotengenezwa na msambazaji mkuu wa Boeing mara kwa mara zilitoka kiwandani zikiwa na kasoro kubwa, kulingana na mkaguzi wa zamani wa ubora katika kampuni hiyo.
Santiago Paredes ambaye alifanya kazi na Spirit AeroSystems huko Kansas, aliiambia BBC mara nyingi alipata hadi kasoro 200 kwenye sehemu zilizokuwa zikitayarishwa kusafirishwa kwa Boeing.
Alipewa jina la utani la "showstopper" kwa kupunguza kasi ya utengenezaji alipojaribu kushughulikia wasiwasi wake, alidai.
Hata hivyo, kampuni ya Spirit ilisema "haikubaliani" na madai hayo.
"Tunajitetea kwa nguvu dhidi ya madai yake," alisema msemaji wa shirika la Spirit, ambalo linasalia kuwa msambazaji mkuu wa Boeing.
Bw Paredes alitoa madai hayo dhidi ya Spirit katika mahojiano ya kipekee na BBC na mtandao wa Marekani wa CBS, ambapo alieleza kile alichosema alipitia alipokuwa akifanya kazi katika kampuni hiyo kati ya 2010 na 2022.
Alikuwa na mazoea ya kupata "kuanzia kasoro 50, 100 hadi 200" kwenye sehemu kuu za ndege - ambazo zilipaswa kusafirishwa kwa Boeing, alisema.
"Nilikuwa nikipata sehemu nyingi zenye kasoro, sehemu nyingi zilizopinda, wakati mwingine hata sehemu ambazo haziko kabisa."
Hata hivyo, Boeing ilikataa kutoa maoni yake juu ya hilo.
Kampuni za Spirit AeroSystems na Boeing zote zimechunguzwa vikali baada ya mlango ambao haujatumika kufunguka kwenye ndege ya 737 Max muda mfupi baada ya kupaa mnamo mwezi Januari, na kuacha pengo ubavuni mwa ndege.
Kulingana na wachunguzi, mlango huo hapo awali ulikuwa umewekwa na kampuni ya Spirit, lakini baadaye uliondolewa na mafundi wa Boeing ili kurekebisha utelezi mbovu.
Tukio hilo lilisababisha mdhibiti wa Marekani, Shirika la Usimamizi wa Safari za Ndege, kuzindua ukaguzi wa mazoea ya utengenezaji katika kampuni zote mbili. Ilipata matukio mengi ambapo kampuni hizo zilishindwa kuzingatia mazoea ya udhibiti wa utengenezaji.
Bw Paredes aliambia BBC kwamba baadhi ya kasoro alizozitambua alipokuwa Spirit zilikuwa ndogo - lakini nyingine zilikuwa mbaya zaidi.
Soma zaidi:
Mwanamume akiri kuwaua watalii watatu waliotoweka Mexico

Chanzo cha picha, Instagram@Callum10Robinson
Mwanamume aliyeshtakiwa kwa kutoweka kwa watalii watatu katika safari ya kuteleza kwenye mawimbi nchini Mexico alikiri kuwaua, mahakama imesikiliza ushahidi huo.
Ndugu wa Australia Jake na Callum Robinson na rafiki yao Mmarekani Jack Carter Rhoad walitoweka tarehe 27 Aprili karibu na Ensenada.
Jesús Gerardo Jumatano alikabiliwa na mahakama kwa makosa ya utekaji nyara, lakini maafisa wanasema mashtaka ya mauaji yatafunguliwa hivi karibuni.
Pia anajulikana kama "El Kekas", bado hajawasilisha ombi.
Maafisa wa jimbo la Baja California wamesema watalii hao watatu - wote wakiwa na umri wa miaka ya 30 - huenda waliuawa walipokuwa wakijaribu kuzuia wizi wa matairi ya lori lao la kubebea mizigo.
Miili yao ilipatikana ikiwa imetupwa kwenye kisima cha miamba siku sita baada ya kutoweka, kila mmoja akiwa na risasi kichwani, kulingana na mamlaka za eneo hilo. Mwili wa nne pia ulipatikana kwenye kisima hicho lakini ulikuwa hapo kwa muda mrefu na haukujumuishwa kwenye kesi hiyo, waliongeza.
Jesús ameshtakiwa kwa "kutoweka kwa lazima" na mpenzi wake Ari Gisel na mwanamume mwingine wamezuiliwa kwa kushukiwa kuhusika. Majina yao ya ukoo yamefichwa na mahakama.
Wakati wa kufikishwa mahakamani Jumatano, waendesha mashtaka walimtaja Ari - ambaye hajafunguliwa mashtaka kuhusu kutoweka kwao - kama mmoja wa mashahidi wao.
Mahakama iliambiwa kijana huyo mwenye umri wa miaka 23 aliwaambia wachunguzi kwamba Jesús alifika nyumbani kwake tarehe 28 Aprili, na kumwambia kuwa alikuwa amefanya kitu kwa watu watatu.
Alimuuliza anamaanisha nini, naye akajibu "nimewaua", kikao kiliambiwa.
Soma zaidi:
Jeshi la Saudia 'liliruhusiwa kuua' kwa ajili ya mji mpya wa kisasa wa kimazingira

Chanzo cha picha, Shutterstock
Mamlaka ya Saudia imeruhusu matumizi ya nguvu kupita kiasi kuwafurusha raia kwa ajili ya mradi wa mji wa jangwani wa siku zijazo unaojengwa na makumi ya makampuni ya Magharibi, afisa wa zamani wa ujasusi ameiambia BBC.
Kanali Rabih Alenezi anasema aliamriwa kuwafurusha wanakijiji kutoka kabila moja katika jimbo la Ghuba ili kutoa nafasi kwa ‘The Line’, sehemu ya mradi wa mazingira wa eneo la Neom.
Mmoja wao alipigwa risasi na kuuawa kwa kupinga kufurushwa kwake.
Serikali ya Saudia na usimamizi wa eneo la Neom walikataa kutoa maoni.
Neom, eneo la ekolojia la Saudi Arabia la $500bn (£399bn), ni sehemu ya mkakati wake wa Saudi Vision 2030 ambao unalenga kuleta mseto wa uchumi wa ufalme huo mbali na mafuta.
Kampuni nyingi za kimataifa, zikiwemo za Uingereza, zinahusika katika ujenzi wa eneo la Neom.
Eneo hilo ambalo linajengwa limefafanuliwa kama "turubai tupu" na kiongozi wa Saudi Mrithi wa Kifalme Mohamed bin Salman. Lakini zaidi ya watu 6,000 wamehamishwa kwa ajili ya mradi huo kulingana na serikali yake - na shirika la haki za binadamu lenye makao yake nchini Uingereza ALQST linakadiria kuwa idadi hiyo ni kubwa zaidi.
BBC imechambua picha za satelaiti za vijiji vitatu vilivyobomolewa - al-Khuraybah, Sharma na Gayal.
Nyumba, shule na hospitali zimefutwa kabisa kwenye ramani.
Marekani kusitisha usambazaji wa baadhi ya silaha kwa Israel iwapo itaendelea na uvamizi Rafah

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais Biden anaonya kuwa ataacha kusambaza baadhi ya silaha iwapo Israel itaanzisha operesheni ya ardhini.
Rais Joe Biden ameionya Israel kwamba Marekani itaacha kusambaza baadhi ya silaha iwapo itaanzisha operesheni kubwa ya ardhini katika mji wa Rafah wa Gaza.
"Ikiwa wataingia Rafah, sitoi silaha ambazo zimetumika kihistoria kukabiliana na Rafah," alisema wakati wa mahojiano na CNN.
Aliongeza kuwa "ataendelea kuhakikisha Israel iko salama".
Licha ya upinzani mkali wa Marekani, Israel inaonekana iko tayari kufanya uvamizi mkubwa huko Rafah.
Sehemu iliyosongamana ya kusini mwa Gaza ndiyo ngome kuu ya mwisho ya Hamas katika eneo hilo. Maafisa wa Marekani wameonya kwamba operesheni katika mji huo - ambapo idadi ya watu imeongezeka na wakimbizi kutoka maeneo mengine ya Gaza - inaweza kusababisha hasara kubwa ya raia.
"Hatutasambaza silaha na makombora ya mizinga," Bw Biden alisema katika mahojiano hayo yaliyopeperushwa Jumatano.
Alisema Marekani haikufafanua hali ya sasa ya Rafah kama operesheni ya chinichini. "Hawajaingia katika maeneo yenye watu. Walichokifanya ni kufika mpakani," alisema.
"Lakini nimeweka wazi kwa [Waziri Mkuu wa Israel Netanyahu] na baraza la mawaziri la vita, hawatapata uungwaji mkono wetu, kama kweli wataenda katika maeneo yenye watu."
Bw Biden alikiri kwamba silaha za Marekani zilitumiwa na Israel kuwaua raia huko Gaza.
Alipoulizwa kama Israel imevuka "mpaka", rais wa Marekani alijibu "bado".
Soma zaidi:
Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 09/05/2024

