Waasi wa M23 wauteka mji wa mashariki mwa DR Congo

"Sasa tuko Nyanzale, adui amekimbia," msemaji wa waasi Willy Ngoma aliambia BBC Idhaa ya Maziwa Makuu.

Moja kwa moja

Dinah Gahamanyi, Lizzy Masinga and Asha Juma

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo haya ya moja kwa moja. Hadi kesho kwaheri.

  2. Waasi wa M23 wauteka mji wa mashariki mwa DR Congo

    xx

    Chanzo cha picha, AF

    Wapiganaji wa kundi la waasi la M23 wameuteka mji wa Nyanzale kutoka kwa wanajeshi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

    "Sasa tuko Nyanzale, adui amekimbia," msemaji wa waasi Willy Ngoma aliambia BBC Idhaa ya Maziwa Makuu.

    Kamanda wa jeshi Jerome Chico Tshitambwe alithibitisha kwa shirika la habari la Reuters kwamba Nyanzale imetekwa na waasi.

    Nyanzale, ambayo iko kilomita 130 (maili 80) kaskazini mwa mji wa Goma, ilikuwa ni kimbilio la watu waliotoroka makazi yao kutokana na mapigano katika maeneo jirani.

    Lakini mapema wiki hii maelfu ya watu walitoroka tena Nyanzale iliposhutumiwa.

    Bw Ngoma alisema kwa sasa wengi wamerejea mjini.

    Isaac Kibira, naibu wa gavana katika mji wa karibu wa Bambo, alisema M23 walikuwa wakifyatua risasi "kiholela" kabla ya kuuteka Nyanzale.

    "Tulishuhudia kutekwa kwa Nyanzale na M23 tangu asubuhi na idadi ya waliofariki iliongezeka hadi 15," Bw Kibira aliambia Reuters.

    Kundi la M23, lililoundwa kutokana na kundi lingine la waasi lilianza kufanya kazi mwaka 2012 - kwa kiasi kikubwa kulinda wakazi wa eneo la Watutsi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamikia mateso na ubaguzi.

    Wapiganaji wake walichukua silaha tena mwaka wa 2021, wakilalamikia kuvunjwa kwa ahadi katika mkataba wa amani wa awali.

    Wapiganaji wa M23 wana vifaa vya kutosha, lakini kundi hilo linakanusha kuwa wakala wa Rwanda.

    Siku ya Jumatatu, Umoja wa Ulaya ulisema "unasikitishwa sana na kuongezeka kwa ghasia" na kutoa wito wa mazungumzo kati ya DR Congo na Rwanda ili kukabiliana na chanzo cha mzozo huo.

  3. Habari za hivi punde, Haley ajiondoa katika kinyang’anyiro cha urais lakini anasema 'hajutii'

    Nikki Haley ametangaza kusimamisha kampeni yake - lakini anasema "hajutii".

    Anafungua hotuba yake Jumatano kwa kusema: "Zaidi ya mwaka mmoja uliopita nilizindua kampeni yangu ya urais, nilipoanza, nilisema kampeni hiyo ilitokana na mapenzi yangu kwa nchi.

    "Wiki iliyopita tu, mama yangu, mhamiaji wa kizazi cha kwanza, alipata kumpigia kura bintiye kuwa rais. Ni Marekani pekee."

    Haley amesema kwamba alitafuta heshima ya kuwa rais wa nchi.

    Ingawa hatashinda uteuzi huo, anasema, kuwa raia wa Marekani yenyewe tu ni fursa.

    Muda mfupi baadaye, anakubali kwamba Donald Trump anaweza kuwa mgombea wa Republican, na kuongeza: "Nakutakia kila la kheri."

    Hata hivyo, Haley hajatoa ridhaa yake kamili kwa rais huyo wa zamani, jambo ambalo wafuatiliaji wengi wa kisiasa walikuwa wakilifuatilia.

  4. Meli ya mizigo yaharibiwa katika shambulio jipya Yemen

    ,

    Chanzo cha picha, Reuters

    Wafanyakazi wanaokolewa baada ya meli ya mizigo kuharibiwa katika shambulio lililodhamiriwa kwenye Ghuba ya Aden karibu na Yemen, kampuni ya usalama ya baharini ya Ambrey imesema.

    Shambulio hilo linafuatia ripoti za mlipuko kilomita 100 (maili 62) kusini-magharibi mwa Aden.

    Meli zilizo karibu ziliripoti mlio mkubwa na moshi mwingi, kulingana na wakala wa Uendeshaji Biashara wa Bahari wa Uingereza.

    Kundi la Houthi la Yemen, ambalo limekuwa likishambulia meli za kibiashara katika eneo hilo, bado halijatoa maoni yoyote.

    Kundi linaloungwa mkono na Iran linasema kuwa mashambulizi hayo ni ishara ya kuwaunga mkono Wapalestina katika vita kati ya Israel na Hamas katika Ukanda wa Gaza.

    Shughuli za uokoaji zilikuwa zikiendelea na baadhi ya wahudumu wa meli hiyo walikuwa tayari wameingia kwenye boti za kuokoa maisha, kampuni ya Ambrey ilisema huku meli ya jeshi la wanamaji la India ikiwa karibu na eneo hilo.

    Ilikuwa imebeba shehena ya tani 21 za mbolea ya ammonium nitrate, ambayo jeshi la Marekani lilisema ilihatarisha mazingira katika Bahari ya Shamu.

    Vikosi vya Marekani na Uingereza vimejibu mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na makombora dhidi ya meli za wafanyabiashara zinazopitia Bahari ya Shamu na Ghuba ya Aden kwa kulenga silaha na miundombinu ya Houthi magharibi mwa Yemen.

    Soma zaidi:

  5. Israel yaidhinisha mipango ya nyumba mpya 3,400 katika makazi ya Ukingo wa Magharibi

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Mipango ya zaidi ya nyumba 2,500 katika makazi ya Maale Adumim iliripotiwa kuendelezwa.

    Serikali ya Israel imeendeleza mipango ya nyumba mpya 3,400 katika makazi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa.

    Takriban 70% ya nyumba zitajengwa huko Maale Adumim, mashariki mwa Yerusalemu, na zingine zitajengwa karibu na Kedar na Efrati, kusini mwa Bethlehemu.

    Waziri mmoja amesema ujenzi huo ni jibu la shambulio baya la Wapalestina karibu na Maale Adumim wiki mbili zilizopita.

    Mamlaka ya Palestina ililaani mipango hiyo, ambayo inaripotiwa kuwa ya kwanza kuidhinishwa tangu Juni.

    Israel imejenga takriban makazi 160 ya Wayahudi 700,000 tangu ilipokalia Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki - ardhi ambayo Wapalestina wanataka kama sehemu ya taifa la baadaye - katika vita vya Mashariki ya Kati vya 1967.

    Idadi kubwa ya jumuiya ya kimataifa inachukulia makaazi hayo kuwa haramu chini ya sheria za kimataifa, ingawa Israel inapinga hili.

    Soma zaidi:

  6. Urusi yapuuza vibali vya ICC vya kukamatwa kwa makamanda wa Putin

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Urusi imesema haitambui vibali vya kukamatwa vilivyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa makamanda wawili wakuu wa Urusi kwa tuhuma za uhalifu wa kivita nchini Ukraine.

    Mahakama iliwataja Sergei Kobylash na Viktor Sokolov siku ya Jumanne.

    "Sisi si washiriki wa sheria ya [Roma] - hatutambui hili," msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alisema.

    Hii ni mara ya pili kwa waranti kutolewa kwa Warusi kuhusu vita nchini Ukraine.

    Ya kwanza ilikuwa ya Rais Vladimir Putin na mjumbe wake wa haki za watoto.

    Akizungumza na wanahabari siku ya Jumatano, Bw Peskov alisema: "Huu si uamuzi wa kwanza. Pia tunajua kwamba kuna michakato mbalimbali inayoendelea huko, ambayo ni siri, na tunashughulikia maamuzi hayo ipasavyo."

    It is unlikely Russian nationals will be extradited to face charges.

    Bw Peskov alisema ukweli kwamba Urusi haikutia saini Mkataba wa Roma, mkataba wa kimataifa uliounda ICC, inamaanisha kuwa Urusi haitambui vibali hivyo.

    Soma zaidi:

  7. Mwanamume wa Ujerumani apewa chanjo ya Covid mara 217

    xx

    Chanzo cha picha, PA MEDIA

    Mwanamume wa miaka 62 kutoka Ujerumani, amepewa chanjo dhidi ya Covid, mara 217 kinyume na ushauri wa kimatibabu, madaktari wanaripoti.

    Kesi hiyo ya ajabu imeandikwa katika jarida la Lancet la magonjwa ya kuambukiza

    Chanjo hizo zilinunuliwa na kutolewa kwa faragha kwa muda wa miezi 29.

    Mwanamume huyo anaonekana hakupata madhara yoyote, watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Erlangen-Nuremberg wanasema.

    "Tulipata taarifa hizo kupitia makala za magazeti," Dkt Kilian Schober, kutoka idara ya biolojia ya chuo kikuu, alisema.

    "Kisha tukawasiliana naye na kumuomba afanyiwe majaribio ya uchunguzi mbalimbali huko Erlangen. Alifurahia sana kufanya hivyo."

    Mwanamume huyo alitoa sampuli za damu na mate.

    Watafiti pia walifanyia uchunguzi baadhi ya sampuli za damu zilizoganda ambazo zilikuwa zimehifadhiwa katika miaka ya hivi karibuni.

    Dk Schober alisema: "Tuliweza kuchukua sampuli za damu wenyewe wakati mwanamume huyo alipopata chanjo zaidi wakati wa utafiti kwa ridhaa yake mwenyewe.

    "Tuliweza kutumia sampuli hizi ili kubaini jinsi mfumo wa kinga unavyoathiriwa na chanjo."

    Chanjo za Covid haziwezi kusababisha maambukizi lakini zinaweza kusaidia mwili jinsi ya kupambana na ugonjwa huo.

  8. Mswada wa kudhibiti mama kubeba ujauzito kwa niaba ya mwingine wawasilishwa katika bunge la Uganda

    .

    Chanzo cha picha, Sarah Opendi/X

    Maelezo ya picha, Mbunge anayewasilisha mswada huo, Sarah Opendi, anasema Uganda itakuwa mfano kimataifa katika kutunga sheria ya kusaidiwa katika uzazi iwapo itapitishwa

    Mswada huo unaokusudiwa kudhibiti utumiaji wa njia ya mzazi kumbebea mwingine ujauzito kwa walio na utasa au changamoto za kiafya zinazowazuia kuzaliana kwa njia asilia uliwasilishwa Jumanne katika bunge la Uganda.

    Mswada huo pia unalenga kuweka kuweka umri chini kwa wanaobebea wengine mimba kuwa miaka 18.

    Madaktari wanaokaidi masharti haya wanaweza kufungwa jela kwa hadi miaka mitano ikiwa mswada huo utapita.

    Madaktari pia wanaweza kufungwa jela maisha ikiwa watatumia chembechembe zao za mimba au viinitete au zile ambazo hazijachaguliwa na wateja wao.

    Wafadhili lazima pia wasiwe na magonjwa ya kijeni.

    Mswada wa Teknolojia ya Uzazi unaosaidiwa na Binadamu uliwasilishwa na Mbunge wa Uganda Sarah Opendi na kupendekeza kanuni zaidi za vipengele vingine vya uzazi wa kusaidiwa na binadamu.

    Mswada huo pia unalenga kutoa leseni kwa vituo vya uzazi na kudhibiti uchangiaji na uhifadhi wa manii, yai na viinitete.

    Mswada huo pia unalenga kuanzisha ulinzi kwa watoto wanaozaliwa kupitia njia hii.

    Mbunge anayewasilisha mswada huo, Sarah Opendi, anasema Uganda itakuwa mfano kimataifa katika kutunga sheria ya kusaidiwa katika uzazi iwapo itapitishwa, Bi Opendi alinukuliwa akizungumza na gazeti la kibinafsi la Daily Monitor.

    Soma zaidi:

  9. Kiongozi wa genge la Haiti atishia 'vita vya wenyewe kwa wenyewe' ikiwa Waziri Mkuu hatajiuzulu

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Kiongozi wa genge lililosababisha ghasia zinazokumba mji mkuu wa Haiti ameonya kuwa kutakuwa na "vita vya wenyewe kwa wenyewe" ikiwa waziri mkuu wa Haiti, Ariel Henry, hatajiuzulu.

    Jimmy "Barbecue" Chérizier alitoa tishio hilo huku wanachama wa genge lake wakijaribu kuuteka uwanja wa ndege wa mji mkuu ili kumzuia Bw Henry asirudi kutoka nje ya nchi.

    Machafuko yameenea katika miji mingine huku ghasia katika magereza zikiripotiwa huko Jacmel.

    Maelfu wamekimbia makazi yao kutokana na ghasia hizo.

    Bw Henry alikuwa analenga kukubaliana na Kenya kuongoza operesheni ya polisi wa kimataifa ili kukomesha ghasia nchini Haiti.

    Barbeque anahofia kuwa Bw Henry angetumia majeshi kusalia madarakani.

    Kiongozi huyo wa genge amekuwa akimpinga waziri mkuu tangu achukue madaraka muda mfupi baada ya kuuawa kwa Rais Jovenel Moïse mnamo Julai 2021, bila uchaguzi.

    Hata hivyo wakosoaji wa Bw Henry wanasema kuwa utawala wake si halali.

    Pia wanaelezea ukweli kwamba miaka miwili na nusu baada ya kuingia madarakani bado hajaandaa uchaguzi wa rais, kama alivyoahidi hapo awali.

    Soma zaidi:

  10. Vita vya Sudan vinaweza kusababisha mzozo mkubwa zaidi wa njaa duniani - WFP

    ,

    Chanzo cha picha, AFP

    Maelezo ya picha, Zaidi ya miezi 10 ya mapigano kati ya vikosi vinavyohasimiana yamesababisha karibu watu 14,000 kupoteza maisha

    Vita nchini Sudan vinaweza kusababisha janga kubwa zaidi la njaa duniani, isipokuwa mapigano yasitishwe, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limeonya.

    Zaidi ya miezi 10 ya mapigano kati ya vikosi vinavyohasimiana yamesababisha karibu watu 14,000 kupoteza maisha, zaidi ya milioni nane kuyahama makazi yao na idadi kubwa ya watu nchini humo kukatishwa tamaa na kukabiliwa na njaa.

    Wakati vita vikiendelea, familia za Sudan zinaendelea kukimbilia nchi jirani.

    Wengi wamehamishwa mara kadhaa. Wanafika kwenye kambi za usafiri wakiwa hawana chochote, wakiwa na njaa na wakihitaji msaada.

    Katika ziara yake katika kambi nchi jirani ya Sudan Kusini, mkuu wa WFP, Cindy McCain, alisema waathirika wa vita hivyo wamesahaulika.

    Alisema mashirika ya misaada yalipaswa kupewa fursa kwa wale wanaokabiliwa na viwango vya dharura vya njaa ambao wamekwama katika maeneo yaliyokatishwa na ghasia.

    Soma zaidi:

  11. Umoja wa Mataifa walaani mauaji ya wafanyakazi wake nchini Sudan Kusini

    Charles Kiir Gone alikuwa akihudumu na misheni ya kulinda amani huko Wau

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS umelaani mauaji ya mmoja wa wafanyakazi wake nchini humo.

    Charles Kiir Gone alikuwa akihudumu na misheni ya kulinda amani huko Wau, kaskazini-magharibi.

    Inasemekana aliuawa wakati wa shambulio la watu wenye silaha katika nyumba ya jamaa, ambapo alikuwa akiishi.

    Bw Gone alikuwa likizoni kutoka kazini wakati wa shambulio hilo ambalo limehusishwa na wizi wa mifugo, kulingana na tovuti ya habari inayomilikiwa na kibinafsi ya Eye Radio.

    UNMISS imetoa pole kwa familia na imezitaka mamlaka kuchunguza mara moja tukio hilo.

    Katika taarifa, mkuu wa UNMISS Nicholas Haysom alisema shambulio hilo "linaonyesha tishio halisi na linaloendelea kwa maisha ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanaoiunga mkono Sudan Kusini katika safari yake ya kuelekea amani".

    Mzunguko mbaya wa uvamizi wa mifugo na mashambulizi ya kulipiza kisasi umekumba Sudan Kusini, huku maelfu wakiuawa katika miaka ya hivi karibuni.

  12. Wakimbizi wa ndani watekwa nyara nchini Nigeria

    xx

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Makumi ya wakimbizi wa ndani walitekwa nyara mwishoni mwa juma na Boko Haram karibu na kambi ya Ngala, kaskazini mashariki mwa jimbo la Borno.

    Idadi kamili ya waathiriwa haijabainika, lakini baadhi ya ripoti za vyombo vya habari nchini humo zinasema kuwa huenda ikafikia 319, na hivyo kufanya kuwa utekaji nyara mkubwa zaidi wa raia katika jimbo la Borno tangu kutekwa nyara kwa wasichana 276 kutoka Chibok mwaka wa 2014.

    Kuna ripoti nyingi zinazokinzana kuhusu ni nini hasa kilitokea Ngala wikendi hii.

    Hata siku ambayo waathiriwa walichukuliwa inabishaniwa, na vyanzo vya habari katika eneo hilo kutokubaliana ikiwa ilifanyika Ijumaa, Jumamosi au Jumapili.

    Tunachojua ni kwamba wakimbizi wa ndani kutoka kambi ya Ngala, karibu na mpaka na Cameroon walitekwa nyara.

    Wengi wanakadiriwa kuwa wanawake na wasichana ambao walikuwa wakiokota kuni ili kuuza na kutumia kupikia.

    Viongozi wa wanamgambo wa eneo hilo wameliambia shirika la habari la AFP ni wanawake 47 pekee ambao bado hawajapatikana.

    Mamlaka katika jimbo la Borno bado haijathibitisha idadi ya watu waliotekwa nyara.

    Tukio hilo linakuja wakati serikali ya Borno kaskazini mashariki mwa Nigeria, ilisema kuwa 95% ya wapiganaji wa Boko Haram walikuwa wamekufa au wamejisalimisha kwa mamlaka.

    Kwa zaidi ya muongo mmoja, wapiganaji wa Kiislamu wamekuwa wakifanya mashambulizi na utekaji nyara wa watu wengi kaskazini mwa Nigeria, na kuua zaidi ya watu 40,000 na milioni mbili kuyahama makazi yao.

    Maelezo zaidi:

  13. Msanii nyota wa Tanzania Zuchu aomba radhi kwa onyesho 'lisilofaa'

    ,

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 30 ni mmoja wa wanamuziki wakubwa Afrika Mashariki

    Mwimbaji maarufu wa Tanzania Zuchu ameomba radhi baada ya mamlaka visiwani Zanzibar kumsimamisha kwa muda wa miezi sita kujihusisha na shughuli zote za kisanii katika visiwa hivyo kutokana na onyesho ambalo waliona kuwa halifai kimaadili ya eneo hilo.

    Onyesho la Zuchu katika kisiwa cha Kendwa cha Zanzibar mwezi uliopita lilijumuisha lugha na ishara za ngono.

    Taasisi ya Sanaa, Sensa, Filamu na Utamaduni Zanzibar Jumanne ilisema kuwa maonyesho hayo yalikwenda kinyume na mila, desturi na utamaduni wa visiwa hivyo.

    Pia ilimtaka Zuchu kuomba msamaha wa maandishi.

    Katika video iliyosambazwa kwenye Instagram yake Jumanne jioni, mwanamuziki huyo aliomba msamaha kwa kosa lolote lililosababishwa na uchezaji wake.

    "Lengo lilikuwa kuburudisha na sio kupotosha," alisema.

    Mwimbaji huyo pia amesimamishwa "kujishughulisha na shughuli zozote za kisanii" Zanzibar kwa muda wa miezi sita ijayo na baraza la utamaduni la eneo hilo.

    Zuchu, jina halisi Zuhura Othman Soud, ni mmoja wa wanamuziki waliofanikiwa zaidi Afrika Mashariki.

    Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 30 ndiye mwanamuziki wa kwanza wa kike katika Afrika Mashariki kupata wafuasi milioni moja katika mtandao wa YouTube, kwa kipindi cha mwaka mmoja.

    Yeye pia ni mwanamuziki wa kwanza wa kike Afrika Mashariki na ni msanii wa tano pekee wa kike barani humo kuzidi mara milioni 500 kutazamwa kwenye YouTube, kulingana na lebo yake ya WCB Wasafi.

  14. Watu sita wafariki kutokana na mafuriko nchini Malawi

    Zaidi ya watu 14,000 wamekimbia makazi yao kutokana na mafuriko ya wiki iliyopita nchini Malawi

    Chanzo cha picha, Idara ya Kudhibiti Majanga Malawi

    Mamlaka ya Malawi inasema watu sita wamefariki na wanne kujeruhiwa kutokana na mafuriko ya wiki iliyopita katikati mwa nchi.

    Zaidi ya watu 14,000 wamelazimika kuyahama makazi yao, huku wengi wao wakiwa wamekaa kambini, Idara ya Masuala ya Kukabiliana na Majanga nchini humo ilisema katika taarifa yake Jumanne.

    Imesema maeneo mengi ambayo yameathiriwa na mafuriko hayo bado hayafikiki kutokana na uharibifu mkubwa wa barabara na miundombinu mingine.

    Hali hii imetatiza utoaji wa misaada, ilisema, huku wafanyakazi wa kibinadamu wakitegemea zaidi boti kufikia maeneo yaliyoathirika.

    Shirika hilo limeomba msaada zaidi kutoka kwa watu binafsi, makampuni na mashirika ya misaada ili kuunga mkono juhudi za serikali za kutoa misaada.

    Tukio hili limetokea ikiwa ni mwaka mmoja tu baada ya mamia ya Wamalawi kupoteza maisha baada ya kimbunga Freddy kupiga kusini mwa Afrika. ​

  15. Mahakama ya Marekani yatupilia mbali kesi ya kuwatumikisha watoto katika migodi ya DRC

    Migodi

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mahakama ya rufaa ya Marekani Jumanne ilitupilia mbali kesi iliyodai kuwa kampuni tano kuu za teknolojia zilihusika katika shughuli ya ajira ya watoto kuchimba madini ya kobalti katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

    Kesi hiyo ilizitaja Apple, Microsoft, Tesla, Dell Technologies na kampuni mama ya Google Alphabet.

    Mahakama iliamua kwamba ununuzi wa cobalt na makampuni haukumaanisha kuwa walishiriki katika ajira ya watoto.

    Jaji Neomi Rao pia alisema kuwa walalamikaji walikosa kuonesha kwamba kampuni zinazoshtakiwa zilikuwa na ushawishi wa kukomesha matumizi ya watoto katika migodi.

    Kesi hiyo iliwasilishwa kwa mara ya kwanza mnamo 2019 na shirika la haki za binadamu la International Rights Advocates, ambalo lilikuwa likiwakilisha watoto walionusurika ambao walipata majeraha wakifanya kazi katika migodi ya kobalti ya Congo na familia za watoto waliokufa kwenye migodi.

    Ilitupiliwa mbali na mahakama ya chini mwaka wa 2021, na kusababisha kukata rufaa.

    DR Congo inazalisha 60% ya cobalt duniani, madini muhimu yanayotumika katika utengenezaji wa vifaa vingi vya kielektroniki.

    Takribani watoto 25,000 wanafanya kazi kwenye migodi ya kobalti nchini DR Congo, kulingana na Idara ya Kazi ya Marekani, mara nyingi katika mazingira hatari. ​

  16. Waziri Mkuu wa Haiti atua Puerto Rico baada ya kuzuiwa kurejea nchini mwake

    Polisi waliokuwa na silaha nzito walikuwa wakilinda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Luis Muñoz Marin huko San Juan wakati Bw Henry alipotua

    Chanzo cha picha, Reuters

    Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry ametua Puerto Rico baada ya kushindwa kurejea nchini mwake.

    Kulingana na vyombo vya habari vya ndani, aliwasili katika mji mkuu wa San Juan siku ya Jumanne baada ya kuruka kutoka jimbo la New Jersey nchini Marekani.

    Kwa siku chache zilizopita, Bw Henry alikuwa hajulikani aliko kufuatia ziara yake nchini Kenya.

    Ghasia nchini Haiti zimeongezeka bila kuwepo kwake, huku magenge yenye silaha yakijaribu kuuteka uwanja wa ndege wa kimataifa ili kumzuia kutua.

    Kiongozi wao, Jimmy "Barbecue" Chérizier, amemtaka waziri mkuu kujiuzulu, akionya kwamba nchi hiyo inaelekea "moja kwa moja kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vitasababisha mauaji ya halaiki".

    Bw Henry kugeuza njia kutoka kwa taifa analoongoza ni ishara ya jinsi Haiti imekuwa na hali duni katika siku za hivi karibuni.

    Haiti sasa inakaribia kuwa taifa lililoshindwa. Ndege ya Ariel Henry ililazimika kuelekezwa Puerto Rico , eneo la Marekani , baada ya kuzuiwa kuingia Haiti na Jamhuri ya Dominika, tovuti za habari za ndani ziliripoti.

    Jamhuri ya Dominika Jumanne ilitangaza kuwa inafunga anga yake na nchi jirani ya Haiti, ambayo inashiriki kisiwa cha Hispaniola.

    Kiongozi wa nchi hiyo, Luis Abinader, hivi karibuni alisema hatua zitachukuliwa ili kuhakikisha kiwango cha "amani na udhibiti" kinadumishwa katika mpaka wake wa ardhini.

    Sababu kadhaa zinaweza kueleza kwa nini ndege ya Bw Henry haikuruhusiwa kutua Haiti, huenda ikawa ilikuwa hatua ya utaratibu.

    Tangu hali ya hatari kuwekwa Jumapili, safari zote za ndege zimekatishwa hadi ilani nyingine itakapotolea na uwanja wa ndege katika mji mkuu Port-au-Prince, kimsingi, umefungwa.

    Sababu nyingine inaweza kuwa kwa usalama wake mwenyewe. Bw Henry alikuwa shabaha ya wazi kwa magenge ambayo yanamtaka aondoke madarakani, na kurejea kwake katika hatua hii kunaweza kuonekana kuwa kikwazo zaidi kwa utulivu wa taifa, kuliko msaada.

    Hofu kubwa kwa waziri mkuu na wafuasi wake, ikiwa ni pamoja na huko Washington, ni kwamba jaribio lake lisilofanikiwa la kurudi nyumbani linamdhoofisha zaidi.

    Inatoa hisia kwamba mamlaka zilizo chini yake zinabatilisha nia yake ya kurejea katika ardhi ya Haiti.

    Badala yake, ameketi Puerto Rico kutokana na hilo lazima atambue hatua yake inayofuata wakati nchi yake inashuka zaidi kwenye machafuko. ​

    Unaweza kusoma;

  17. Tazama: wanaanga wakikumbatiana muda mfupi baada ya kutua kwenye kituo cha anga za juu

    Maelezo ya video, Wanaanga wakikumbatiana walipofika kwenye kituo cha anga za juu

    Kikosi cha SpaceX cha wanaanga watatu wa Marekani na mwanaanga mmoja wa Urusi wamefanikiwa kufika kwenye kituo cha Kimataifa cha Anga za Juu (ISS).

    Walikaribishwa na wafanyakazi saba wa hapo awali.

    Chombo cha anga za juu cha Endeavor kilitia nanga n katika ISS baada ya kuondoka kwa mlipuko kutoka Florida.

    Ujumbe wa Crew-8 utakuwa angani kwa miezi sita. Eneo hilo la anga za juu ni mojawapo ya maeneo machache ambapo Marekani na Urusi zinaendelea kushirikiana kwa ukaribu katika uvumbuzi wa anga za juu licha ya vita nchini Ukraine.

  18. ICC yatoa waranti ya kukamatwa kwa makamanda wakuu wa Urusi

    Viktor Sokolov ni mmoja wa watu waliotajwa na ICC

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) imetoa waranti wa kukamatwa kwa makamanda wakuu wa Urusi kwa tuhuma za uhalifu wa kivita nchini Ukraine.

    Sergei Kobylash na Viktor Sokolov, luteni jenerali wa jeshi na amiri wa jeshi la wanamaji, ni watu wawili waliotajwa na ICC.

    Hii ni awamu ya pili ya waranti kwa maafisa wa Urusi kuhusiana na vita nchini Ukraine.

    Ya kwanza ilikuwa ya Rais Vladimir Putin na mjumbe wake wa haki za watoto.

    Urusi haiitambui mahakama ya ICC, na hivyo kufanya kusiwe na uwezekano mkubwa wa kupelekwa kujibu mashtaka.

    ICC ilisema hatua ya hivi punde ilitokana na kuwa na sababu za kuridhisha za kuamini kwamba washukiwa hao wawili walihusika na "mashambulio ya makombora yaliyofanywa na vikosi vilivyo chini ya amri yao dhidi ya miundombinu ya umeme ya Ukraine".

    Uhalifu unaodaiwa ulifanyika kati ya Oktoba 2022 na Machi 2023, ICC ilisema.

    Mahakama ilisema kuwa mashambulizi hayo yalisababisha madhara kwa raia.

    Wanaume hao wawili "kila mmoja anadaiwa kuhusika na uhalifu wa kivita wa kuelekeza mashambulizi kwenye vitu vya kiraia" na pia wanatuhumiwa kwa "uhalifu dhidi ya ubinadamu wa vitendo visivyo vya kibinadamu", mahakama ilisema.

    Bw Kobylash, 58, alikuwa kamanda wa safari za anga za masafa marefu wa jeshi la anga la Urusi wakati wa madai ya uhalifu.

    Bw Sokolov, 61, alikuwa amiri katika jeshi la wanamaji la Urusi ambaye aliongoza Meli ya Bahari Nyeusi.

    Moscow hapo awali ilikanusha kulenga miundombinu ya kiraia nchini Ukraine.

  19. FBI yaonya kuhusu jasusi wa Iran anayedaiwa kupanga njama ya kuwaua maafisa wa Marekani

    Onyo hilo la FBI lilijumuisha picha za Bw Farahani

    Chanzo cha picha, FBI

    FBI inamsaka mtu anayedaiwa kuwa jasusi wa Iran ambaye inaamini anahusika katika njama za kuwaua maafisa wa sasa na wa zamani wa serikali ya Marekani.

    Shirika hilo linamtuhumu Majid Farahani, 42, kwa kupanga njama ya kulipiza kisasi mauaji ya jenerali wa Iran Qasem Soleimani.

    Soleimani, kamanda wa kikosi cha Quds cha Iran, aliuawa katika shambulio la ndege isiyo na rubani ya Marekani nchini Iraq mnamo Januari 2020.

    FBI inasema Bw Farahani amechukua hatua kwa niaba ya Wizara ya Ujasusi ya Iran.

    Katika notisi iliyotumwa Ijumaa, FBI ilisema inamtaka Majid Dastjani Farahani kuhojiwa kuhusiana na kuajiri watu binafsi kwa ajili ya operesheni nchini Marekani.

    Maafisa wanasema Bw Farahani husafiri kati ya Iran na Venezuela na pia amewaajiri washirika kwa "shughuli za uchunguzi zinazolenga maeneo ya kidini, biashara na vituo vingine" nchini Marekani.

    Mnamo Desemba 2023, Bw Farahani na afisa mwingine anayedaiwa kuwa wa ujasusi waliwekewa vikwazo na hazina ya Marekani.

    BBC imewasiliana na maafisa wa Iran huko Washington na New York kwa maoni.

    Maafisa wa Iran wameapa kulipiza kisasi kwa mauaji ya Soleimani, ambaye alionekana na watu wengi kama mtu wa pili kwa nguvu zaidi nchini Iran wakati wa kifo chake. Aliuawa katika uwanja wa ndege wa Baghdad pamoja na Wairani wengine kadhaa kwa amri ya Rais wa wakati huo Donald Trump.

    Kikosi cha Quds ambacho Soleimani alikiongoza ni tawi la Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ambalo limebobea katika vita visivyo vya kawaida na ujasusi wa kijeshi.

    Inafanya kazi nje ya Iran na kuunga mkono vikundi vikiwemo Hamas, Hezbollah na Houthis nchini Yemen. Marekani inaichukulia jeshi la Quds kuwa ni kundi la kigaidi.

    Unaweza kusoma;

  20. Biden na Trump wajizolea kura za awali za mchujo za majimbo katika ‘Super Tuesday’

    f

    Chanzo cha picha, Je ‘Super Tuesday’ ni nini na kwanini ni muhimu?

    Nani ameshinda nini hadi sasa?

    Rais Joe Biden na Donald Trump kila mmoja anakadiriwa kuwa ameshinda katika kinyang'anyiro cha uteuzi wa vyama vyao katika majimbo kadhaa usiku wa kuamkia leo. Hiyo inatokana na taarifa kutoka kwa mtandao washirika wa BBC nchini Marekani, CBS News.

    Wote wawili watatunukiwa wajumbe. Kadiri wanavyopata wajumbe wengi zaidi, ndivyo kila mshindani anavyokaribia kupata kibali rasmi kutoka kwa chama chao ili kuwania uchaguzi wa urais baadaye mwakani.

    Kwa Democtrats :

    ·Biden hadi sasa anatarajiwa kushinda katika kinyang’anyiro cha uteuzi katika majimbo 11 ambayo yalipiga kura Jumanne: Alabama, Arkansas, Colorado, Maine, Massachusetts, North Carolina, Oklahoma, Tennessee, Texas, Vermont na Virginia.

    ·Pia amethibitishwa usiku wa kuamkia leo na chama chake kuwa ameshinda jimbo la 12 , Iowa, ambapo watu wameweza kupiga kura katika kikao kwa njia ya posta tangu Januari.

    Kwa Republican :

    ·Trump hadi sasa anatarajiwa na CBS inasema kuwa ameshinda mashindano ya uteuzi katika majimbo tisa : Alabama, Arkansas, Colorado, Maine, North Carolina, Oklahoma, Tennessee, Texas na Virginia.

    ·Jimbo moja - Massachusetts - limeainishwa kama "linalompendelea" Trump

    Unaweza pia kusoma:

    • Je ‘Super Tuesday’ ni nini na kwanini ni muhimu?