Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mapenzi ya jinsia moja yanalazimishwa kwetu na nchi za Magharibi" - Museveni
Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema kuwa nchi za Magharibi hazipaswi kulazimisha desturi zao kwa Waafrika kwa kuhalalisha mapenzi ya jinsia moja.
Moja kwa moja
Mapenzi ya jinsia moja yanalazimishwa kwetu na nchi za Magharibi" - Museveni
Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema kuwa nchi za Magharibi hazipaswi kulazimisha desturi zao kwa Waafrika kwa kuhalalisha mapenzi ya jinsia moja.
Katika hotuba yake maalum kwa Bunge siku ya Alhamisi, rais aliongeza kuwa mapenzi ya jinsi moja ni kupotoka au kuondokana na kile kilicho cha kawaida.
“Tunahitaji kuuliza swali; 'ni kwa asili au kwa malezi'," Bw. Museveni aliongeza.
"Kufanya mapenzi nchini Uganda na maeneo mengine ya Afrika ni siri. Hata kwa wapenzi wa jinsia tofauti. Tutajuaje kuwa wewe unashiriki mapenzi ya jinsia moja, labda utangaze?” Aliendelea kusema.
Maoni yake yanakuja wakati ambapo kuna wimbi la chuki dhidi ya wapenzi wa jinsia moja linaloenea kote nchini humo na ukanda wa Afrika mashariki.
Wanaharakati wa LGBTQ wanasema jumuiya yao imekabiliwa na unyanyasaji wa kimwili na mtandaoni katika wiki za hivi karibuni.
Mswada wa kupinga mapenzi ya jinsia moja uliwasilishwa katika bunge la Uganda mapema mwezi huu.
Unatafuta kuifanya kuwa haramu kwa mtu yeyote kujitambulisha kama anayeshiriki mapenzi ya jinsia moja.
Pia unaagiza kifungo cha miaka kumi jela kwa kujihusisha na mahusiano au ndoa ya jinsia moja, pamoja na kukuza shughuli zinazohusiana na mapenzi ya jinsia moja au uanaharakati.
Mswada huo kwa sasa unachunguzwa na kamati ya bunge kuhusu masuala ya sheria.
Prof. Sylvia Tamale, msomi mashuhuri ambaye alifika mbele ya kamati siku ya Alhamisi ili kushirikisha maoni yake, alikosoa sheria iliyopendekezwa kwa "kujaribu kupoteza kabisa utambulisho wa sehemu ya jamii" na kwa kuchanganya uhalifu kama vile kulawiti watoto na mapenzi ya jinsia moja.
Sheria ya kupinga mapenzi ya jinsia moja, ambayo imeweka adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa kosa hilo, ilibatilishwa na mahakama ya kikatiba mwaka 2014 kwa msingi kwamba ilipitishwa bila kuwepo kwa idadi ya wabunge inayotakiwa bungeni.
Jeshi la Ukraine laorodhesha silaha za Urusi inazoweza kuzidungua
Msemaji wa Kikosi cha Wanahewa cha Wanajeshi wa Ukraine Yuriy Ignat, makombora yafuatayo kwa sasa yanaweza kupigwa kwa ufanisi:
-"Caliber" (3M14) -makombora ya baharini;
- Kh-101 / Kh-555 / Kh-55 - makombora ya kwenye anga;
- R-500 (9M728) - makombora ya ardhini ya Iskander;
- X-59 - kombora la kuongozwa la kwenye anga hadi ardhini;
- X-35 - kombora la kujikinga la angani, bahari au pwani.
Na hapa kuna orodha ya makombora ambayo ulinzi wa anga wa Ukraine bado hauwezi kuyadungua:
- 9M723 – makombora ya Iskander;
- Roketi za MLRS, kama vile "Smerch";
- X-22 - kombora la masafa marefu la kulinda meli za kivita;
- R-800 - kombora la pwani "Onyx";
- X-47 – makombora ya hypersonic "Dagger";
- X-31P - kombora la kuzuia rada;
- S-300 makombora ya kulinda ndege yanayoongozwa.
Pia unaweza kusoma:
Maelfu ya watu wanawakimbia waasi wa Kiislamu nchini DR Congo
Wafanyakazi wa kutoa misaada katika jimbo la Ituri mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wanasema maelfu ya watu waliotoroka makazi yao wamekuwa wakiwasili katika mji mkuu wa eneo hilo, Beni.
Wanatoroka mfululizo wa mashambulizi ya waasi wa Kiislamu wa Allied Democratic Forces (ADF) katika jimbo hilo.
Zaidi ya watu 90 wameuawa katika muda wa wiki moja iliyopita katika mashambulizi dhidi ya vijiji 18.
Majaribio ya majeshi ya DR Congo na Uganda kuwaangamiza waasi yamepiga hatua kidogo.
Pia unaweza kusoma:
Urusi inajaribu kuinua mabaki ya MQ-9 Reaper kutoka chini ya Bahari Nyeusi huku Marekani ikidai hakuna kitu cha thamani tena
Mamlaka ya Urusi imethibitisha kuwa operesheni inaendelea katika Bahari Nyeusi, wakati ambapo wanajeshi wanajaribu kuinua kutoka chini mabaki ya ndege isiyo na rubani ya MQ-9 Reaper ya Marekani iliyoanguka siku moja kabla.
Maafisa wa utawala wa Marekani wanasema itakuwa vigumu sana kufanya hivyo na kusisitiza kuwa taarifa zote muhimu zilizomo kwenye ndege hiyo isiyo na rubani zimeharibiwa.
Hapo awali, Marekani ilisema ndege yake isiyo na rubani ya MQ-9 Reaper siku ya Jumanne iligongana na ndege ya kivita ya Urusi aina ya Su-27 ikiwa angani juu ya sehemu isiyo na vita upande wa Bahari Nyeusi na kuanguka majini.
Hata hivyo, Wizara ya Ulinzi ya Urusi inakanusha mgongano huo na inadai kuwa ndege hiyo isiyo na rubani iliruka na kifaa cha kupokea mawimbi kikiwa kimezimwa kuelekea Crimea iliyotwaliwa.
Siku ya Jumatano, mazungumzo ya simu mara mbili kati ya wawakilishi wa ngazi za juu wa idara ya kijeshi ya Marekani na Urusi yalifanyika kwa tukio hilo la Bahari Nyeusi.
Mazungumzo hayo yalifanywa na Mawaziri wa Ulinzi wa nchi hizo mbili Lloyd Austin na Sergei Shoigu, pamoja na Wakuu wa Majeshi Mark Milli na Valery Gerasimov.
soma zaidi:
TikTok kupigwa marufuku kwenye simu za serikali ya Uingereza
Programu ya mtandao wa kijamii inayomilikiwa na China ya TikTok imetazamiwa kupigwa marufuku kwa simu na vifaa vingine vinavyotumiwa na mawaziri wa serikali na watumishi wa umma kwa misingi ya usalama.
Waziri wa Ofisi ya Baraza la Mawaziri Oliver Dowden atatoa taarifa kwa wabunge baadaye.
Hakuna taarifa yoyote rasmi iliyotolewa hadi kufikia sasa - lakini Waziri wa Usalama Tom Tugendhat alikuwa ameuliza Kituo cha Usalama cha Mtandao cha Kitaifa kuhakiki suala hilo.
TikTok imekanusha vikali madai kwamba inakabidhi data za watumiaji kwa serikali ya Uchina.
Serikali imekuwa chini ya shinikizo kutoka kwa wabunge waandamizi kufuata mkondo wa Marekani na Tume ya Ulaya katika kupiga marufuku programu hiyo.
Marekani ilipiga marufuku TikTok kutoka kwa vifaa rasmi mnamo Desemba, na Tume ikafuata mkondo huo mwezi uliopita.
Canada na Ubelgiji zimechukua hatua sawa na hiyo.
China imeishutumu Marekani kwa kueneza habari potofu na kukandamiza TikTok huku kukiwa na ripoti kwamba Ikulu ya White House inataka wamiliki wake wa China kuuza hisa zao katika kampuni hiyo.
Mapema wiki hii, waziri mkuu alisema Uingereza "itaangalia kile washirika wetu wanafanya".
Soma zaidi:
Manchester City: Erling Haaland anasema alisajiliwa kushinda Ligi ya Mabingwa
Erling Haaland anasema aliletwa Manchester City ili kuwasaidia kushinda Ligi ya Mabingwa kwa sababu "tayari wanajua" jinsi ya kushinda Ligi ya Premia.
Haaland, 22, alifunga mabao matano katika ushindi wa 7-0 wa City dhidi ya RB Leipzig siku ya Jumanne na kujihakikishia nafasi ya kufuzu kwa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa.
Utendaji bora wa City katika shindano hili ni kumaliza washindi wa pili kwa Chelsea mnamo 2021.
"Bila shaka klabu inataka kushinda Ligi ya Mabingwa," alisema Haaland.
"Wameshinda mataji manne kati ya matano ya mwisho ya Ligi Kuu. Hawakunileta kushinda Ligi Kuu kwa sababu tayari wanajua jinsi ya kushinda.
"Kwa hivyo, unaweza kutafuta maana hasa ya hii. Niko hapa kujaribu kusaidia klabu kujiendeleza zaidi na kushinda Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza."
Kushindwa kwa City kunyanyua Ligi ya Mabingwa ni tofauti na mafanikio yao ya hivi majuzi ya nyumbani.
Wameshinda mataji 17 tangu mmiliki Sheikh Mansour kutwaa klabu hiyo mwaka 2008, ikiwa ni pamoja na mataji sita ya Ligi Kuu ya Uingereza - manne kati ya hayo yamepatikana tangu meneja Pep Guardiola alipoteuliwa mwaka 2016.
pia unaweza kusoma:
SpiceJet: Marubani wa ndege wasimamishwa kazi baada kikombe cha kahawa kuonekana ndani ya chumba cha rubani
Tukio hilo lilitokea ndani ya ndege ya SpiceJet
Shirika la ndege la kibinafsi la Indialimewazuia marubani wake wawaili kutoendesha ndege kwa madai ya kuwa na kahawa na peremende ndani ya chumba cha rubaniili hali ndege ikiwa safarini angani
Tukio hilo lilijulikana baada ya picha ya kikombe kilichokuwa kimewekwa kwenyemtambo wa uongozaji wa ndege ya SpiceJet kusambaa kwenye mitandao ya kijamii mapema wiki hii.
Taarifa zilisema kuwa ndege hiyo ilikuwa ikisafiri umbali wa futi 37,000wakati picha hiyo ilipochukuliwa.
Picha hiyo iliibua malalamiko , yaliyosababisha taasisi ya udhibiti wa safari za anga ya India kutoa onyo kwa ndege.
Jumatano SpiceJet ilisema kuwa inachunguza suala hilo, na imewasimamisha kazi marubani wanne, ambao wanadaiwa kuchukua picha hiyo, wakiwa mapumzikoni.
"Hatua inayostahiki zitachukuliwa dhisi yao baada ya kukamilika kwa uchunguzi," alisema msemaji wa kampuni hiyo katika mazungumzo na gazeti la The Times la India.
Kenya: Ruto amuonya Odinga dhidi ya maandamano ya umma,
Rais wa Kenya William Ruto amemuonya kiongozi mkuu wa upinzani Raila Odinga dhidi ya kufanya maandamano ya umma yaliyopangwa na muungano wa upinzani wa Azimio Jumatatu ijayo 20,Machi,2023.
Rais Ruto amesema hatamruhusu Bwana Odinga kufanya maandamano yatakayohatarisha maisha ya Wakenya,uharibifu wa mali au kulemaza shughuli za biashara nchini akiongeza kuwa Kenya ni nchi inayoongozwa kwa misingi ya sheria na hakuna mtu ambaye yuko juu ya sheria hizo.
Mapema wiki hii, Bwana Odinga alitangaza kuwa tarehe 20 Machi itakuwa siku ya mapumziko Kenya ili kuruhusu raia kushiriki maandamano ya kupinga utawala wa Rais Ruto na kuongezeka kwa gharama ya maisha nchini humo.
Waziri kiongozi Musalia Mudavadi hata hivyo amekosoa tangazo hilo la Bwana Odinga akilitaja linalokiuka katiba ya nchi kwani hana mamlaka ya kutangaza siku ya kitaifa wala ya mapumziko
Kiongozi huyo wa upinzani ameendelea kusisitiza hatambui uongozi wa Bwana Ruto tangu alipotangazwa mshindi wa uchaguzi wa Rais uliofanyika Agosti mwaka jana,akidai kulikuwa na udanganyifu wa kura na kutaka Tume huru ya uchaguzi kutathminiwa upya licha ya mahakama ya juu kuthibitisha ushindi wa Bwana Ruto.
Tayari,kaunti kadhaa nchini Kenya katika kipindi cha siku chache zilizopita,zimeshuhudia maandamano ya umma kuitikia wito wa Bwana Odinga kwa wananchi kuipinga serikali. Miongoni mwa kaunti hizo ni Migori na Kisumu ambazo ni ngome za kisiasa za kiongozi huyo mkuu wa upinzani.
Viongozi wa muungano wa Azimio wakiongozwa na kinara wao wamekuwa wakifanya msururu wa mikutano ya hadhara kote nchini katika wiki chache zilizopita kuwashawishi wafuasi wao kugoma na kuipinga serikali kwa kile wanachokitaja kushindwa kushughulikia masuala muhimu yanayowaathiri Wakenya kama ugumu wa Maisha,kupanda kwa bei ya bidhaa muhimu,ajira na ufisadi.
Maelezo zaidi:
Muhoozi Kainerugaba: Nitagombea urais 2026, mwana wa kiume wa Museveni atangaza
Mtoto wa kiume wa rais wa Uganda Yoweri Museveni, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, sasa anasema atagombea iti cha urais mwaka 2026.
Muhoozi, Jeneral mwenye utata ambaye mara kwa mara amekuwa akiibua mijadala kwenye mitandao ya kijamii kutokana na kauli zake, ametoa tangazo hili katika ujumbe wake wa TwitterJumatano, akisema kuwa watu wamekuwa wakimtaka atoe tangazo hilo.
“Mumenitaka mimi kulisema daima! Sawa, kwa jina la Yesu Mungu wangu, kwa jina la vijana wote wa Uganda na dunia na kwa jina la mageuzi bora, nitagombea Urais katika mwaka 2026!” alituma ujumbe wa Twitter.
Unaweza pia kusoma:
- Muhoozi Kainerugaba: Kutoka ‘kumposa’ Waziri Mkuu wa Italia hadi kutishia kuivamia Kenya
- Jenerali Muhoozi Kainerugaba wa Uganda ni nani?
Kimbunga Freddy: Rais wa Malawi atangaza maombolezo ya kitaifa ya siku 14
Rais wa Malawi Lazarus Chakwera ametangaza siku kumi na nne za maombolezo ya kitaifa baada ya zaidi ya watu mia mbili ishirini kufariki dunia katika mafuriko na maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na kimbunga Freddy.
Rais Chakwera ameomba msaada wa kimataifa kusaidia katika shughuli za uokozi na kulijenga upya taifa hilo baada ya mvua kubwa iliyonyesha kwa siku sita kusababisha maafa makubwa nchini humo.
"Malawi iko katika hali ya janga,kile kimbunga Freddy imefanya ni kuturudisha nyuma ilhali tulikuwa tunajijenga upya kutokana na majanga ya kipindi cha nyuma.Naiomba jumuiya ya kimataifa kutuangalia kwa jicho la huruma kwasababu tunahitaji msaada,tunahitaji msaada wa kuwashughulikia manusura ambao wamepoteza kila kitu.Wanahitaji vitu vya msingi,makazi,mavazi,chakula."
Mamlaka inasema takriban watu 41 bado hawajulikani walipo kufuatia mvua kubwa iliyonyesha na kusababisha mafuriko na maporomoko ya udongo kusomba nyumba zao.
Zaidi ya 4000 wameyahama makazi yao na kwa sasa wanahifadhiwa katika majengo ya muda kote nchini.
Rais pia alisema mkutano wa dharura wa baraza la mawaziri uliidhinisha kutolewa kwa dola milioni 1.5 kusaidia maelfu ya Wamalawi walioathiriwa na dhoruba.
Rais Chakwera alisema fedha hizo hazitatosha.
“Hali ya uharibifu tunayokabiliana nayo hapa ni kubwa kuliko rasilimali tulizonazo.
Marekani yatishia kuipiga marufuku TikTok iwapo haitauzwa – ripoti
Serikali ya Marekani inasema TikTok lazima iuzwe la sivyo ikabiliwe na uwezekano wa kupigwa marufuku nchini humo, kwa mujibu wa ripoti.
Programu (app) hiyo ya kushirikisha video, inayomilikiwa na kampuni ya KichinaByteDance, inashutumiwa kwa kusababisha hatari ya usalam wa taifa kwa kukusanya data kutoka data za mamilioni ya watumiaji.
Ombi la kubadili umiliki, kwa mara ya kwanza liliripotiwa katika jarida la Wall Street Journal (WSJ), lilithibitishwa kwa BBC na TikTok.
Kampuni hiyo inasema mauzo ya kulazimishwa hayatabadili usambaaji wa data au upatikanaji wa programu ya TikTok.
Ikulu ya White House bado haijajibu ombi la BBC News la kutaka kauli yake.
Kwa miaka maafisa wa Marekani wamekuwa wakielezea hofu zai kwamba taarifa(data) kutoka kwa app hiyo maarufu zinaweza kuangukia mikononi mwa serikali ya Uchina.
Korea Kaskazini yarusha kombora la masafa marefu kabla ya mazungumzo ya Japan na Korea Kusini
Korea Kaskazini imerusha kombora la masafa marefu (ICBM) saa chache kabla ya viongozi wa Korea Kusini na Japan kukutana kwa ajili ya mkutano wa kilele.
Maafisa wa Japan na Korea Kusini walithibitisha kurushwa kwa kombora hilo la masafa marefu siku ya Alhamisi asubuhi.
Iliruka takribani kilomita 1,000 (maili 620) ikitua kwenye maji magharibi mwa Japani. Ni mara ya nne kurusha kombora kutoka Pyongyang wiki ingawa nyingine zilikuwa za masafa mafupi.
Shughuli hiyo inajiri huku kukiwa na mazoezi ya majini yanayoendelea kati ya Marekani na Korea Kusini kuzunguka peninsula ya Korea - nchi washirika kubwa zaidi katika kipindi cha miaka mitano.
Korea Kaskazini imesema mara kwa mara kwamba inaona mazoezi kama hayo kuwa uchochezi.
Wizara ya ulinzi ya Japani ilithibitisha kuwa ni aina ya ICBM na kusema iliruka juu zaidi ya kilomita 6,000 kwa takribani dakika 70.
Kufuatia tukio hilo la Alhamisi, Rais wa Korea Kusini Yoon Suk Yeol aliamuru jeshi la nchi yake kuendelea na mazoezi ya pamoja ya Marekani kama ilivyopangwa.
Aliongeza kuwa Pyongyang italipia "vitendo vyake vya uchokozi". Korea Kaskazini mara ya mwisho iliifuta kazi ICBM chini ya mwezi mmoja uliopita- kitendo ambacho kilisababisha mkutano wa dharura wa Umoja wa Mataifa na kulaaniwa na nchi za G7.
NASA yazindua mavazi mapya ya anga yanayowafaa wanawake
NASA imewasilisha kizazi kipya cha mavazi ya safari za anga kwa ambao wanataka kurejea Mwezini.
Muundo wake una vipengele maalumu vya kuwasaidia wanaanga wakati wa kufanya majaribio ya kisayansi mwezini.
NASA inatarajia kuwa na suti iliyosasishwa tayari kwa misheni ya mwezi ya Artemis III, iliyopangwa mwaka 2025. Suti za anga za juu zinazovaliwa na wanaanga wa Marekani hazijaundwa upya kabisa tangu 1981.
Mavazi kwa ajili ya wanaanga wanawake
Mfano huu uliundwa ili kuwafaa zaidi wanawake. Wakati NASA ilitangaza kwamba misheni itarudi mwezini baada ya miongo mitano, iliahidi kutuma mwanamke wa kwanza na mtu wa kwanza wa rangi kwenye uso wa mwezi.
Hata hivyo, mipango ya kutuma wanaanga wa kike angani ilitatizwa na ukosefu wa suti za angani zenye ukubwa unaofaa.
Suti inayofaa ni muhimu ili kuepuka uchovu mwingi na, katika hali mbaya zaidi, uharibifu wa mwili.
Mnamo 2021, NASA ilipanga kutuma timu ya wanawake wote ya wanaanga kwenye Kituo cha Kimataifa cha Anga ili kukamilisha safari ya anga.
Unaweza pia kusoma;
FIFA yazindua rasmi Uwanja wa michezo wa Pele mjini Kigali
Uliokuwa ukiitwa Uwanja wa michezo wa Nyamirambo mjini Kigali sasa umepewa jina jipyala Kigali Pele Stadium baada ya uwanja huo kufunguliwa rasmi na Rais wa shirikisho la soka duniani (FIFA) Gianni Infantino pamoja na Rais wa Rwanda Paul Kagame.
Uwanja huu umefunguliwa kongamano la FIFA la 73 linalowajumuisha wajumbe 2,000, likitarajiwa kuanza rasmi hii leo mjini Kigali leo.
Ni katika kongamano hili ambapo uchaguzi wa FIFA utafanyika. Rais wa sasa wa FIFA Infantino ndiyo mgombea pekee wa kiti hicho baada ya kutokuwa na mpinzani.
Baada ya uzinduzi wa Uwanja wa Pele wa Kigali washiriki wa Kongamano hilo walicheza mechi ya soka, timu moja ikiongozwa na Rais wa Rwanda Paul kagame huku timu nyingine ikiongozwa na Rais wa FIFAGianni Infantino.
Rais Kagame ambaye anafahamika kama shabiki wa mpira wa migu hususan wa timu ya Uingereza ya Arsenal – ambaye hucheza mchezo wa tenesi, aliwashangaza wengi alipojitokeza uwanjani kucheza soka.
Upande wa timu ya Kagame alikuwemo Jay Jay Okocha wa Nigeria, Patrice Motsepe mkuu wa CAF, Jimmy Mulisa, Kalekezi Olivier, Kayiranga Baptiste, Eric Nshimiyimana bakanyijijeho wa Rwanda ubu bambaye kwa sasa ni kocha, Grace Nyinawumuntu kocha wa timu ya wanawake ya Rwanda, rais wa Shirikisho la soka la Rwanda FERWAFA Olivier Nizeyimana.
Upande wa timu ya Infantino ilikuw ana wachezaji kama Youri Djorkaeff aliyewahi kuchezea timu za Paris Saint Germain na Monaco uambaye kwa sasa ni mshauri mkuu wa FIFA na Gilberto Silva aliyekuwa mchezaji maarufu wa Arsenal.
Timu ya Perezida Kagame iliifunga timu ya Gianni Infantino 3-2, katika mchezo uliosimamiwa na mwamuzi wa kimataifa Salma Mukansanga.
Mwezi January, wakati wa mazishi ya Pele,Infantino, ambaye anamuelezea Pele kama“mwanamichezo wa mfano wa kuigwa”, alliahidi kuiomba kila nchi duniani kuupatia jina la Pelé uwanja, kwa heshima ya Mchezaji bora wa Brazil na dunia. Rwanda, ambayo inapokea kongamano la 73 la FIFA ni miongoni mwa nchi ambazo zimetekeleza ombi hilo.
Mtandao wa majasusi wa Urusi wanaoshutumiwa kufanya hujuma wakamatwa nchini Poland
Kikundi cha raia wa kigeni kimekamatwa baada ya kushukiwa kuifanyia ujasusi Urusi, maafisa wawili wa serikali ya Poland wameiambia BBC.
Kituo cha redio RMF FM kiliripoti kwamba huduma za usalama za Poland zimevunja mtandao unaoifayika kazi Urusi.
Watu sita walikamatwa kwa kushukiwakuweka kamera za siri kupiga picha za video muundo mbinu wa usafiri unaotumiwa kusafirisha misaada nchini Ukraine , iliripoti
RMF FM ilisema kuwa kikundi hicho kilikuwa kimeandaa mipango ya hujuma.
Mzozo wa ujasusi wa muda mrefu baina ya Urusi na Magharibi umeimarika tangu vianze vita vya Ukraine.
Poland ni mojawapo ya washirika wakuu na vikosi vyake vimemekuwa vikiwakamata watu kadhaa wanaoshukiwa kufanya ujasusi kwa ajili ya Urusi tangu ianze uvamizi Februari mwaka jana.
Kulingana na kituo hicho cha redio, kikundi hicho cha majasusi kilikuwa kimeweka kamera za video CCTV kando ya makutano ya njia ya leri na barabara muhimu ya usafirishaji iliyopo katika jimbo la Poland la Podkarpackie , inayopakana na Ukraine, ilisema
Baadhi ya kamera hizo zilipatikana a zimewekwa karibu na kiwanja kidogo cha mkoa cha ndege ambacho kimegeuzwa kuwa cha kimataifakwa ajili ya kusafirisha misaada ya kijeshi na ya kibinadamu kwa Ukraine.
Vita vya Ukraine: Mengi zaidi
- YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
- UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
- UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
- KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
- ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
- PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
Hujambo, karibu kwa matangazo yetu ya moja kwa moja leo tarehe 16.03.2023