DRC: Wanajeshi saba wahukumiwa kifo kwa kuonyesha 'uoga'

Askari hao wamehukumiwa kifo kwa kuonyesha 'uoga mbele ya adui' na kusababisha hofu kubwa waliwapokimbia waasi wa M23.

Moja kwa moja

  1. Na kufikia hapo tunatamatisha matangazo haya ya moja kwa moja. Hadi kesho kwaheri.

  2. Shughuli ya kutafuta manusura yaendelea Uturuki karibu saa 150 baada ya tetemeko

    Waokoaji wakimbeba Cudie mwenye umri wa miaka 12 kutoka kwenye kifusi cha jengo lililoporomoka, huko Hatay, kusini mwa Uturuki, saa 147 baada ya tetemeko hilo.

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelezo ya picha, Waokoaji wakimbeba Cudie mwenye umri wa miaka 12 kutoka kwenye kifusi cha jengo lililoporomoka, huko Hatay, kusini mwa Uturuki, saa 147 baada ya tetemeko hilo.

    Waokoaji wamemtoa mtoto wa miezi saba kwenye vifusi vya jengo huko Hatay, kusini mwa Uturuki, saa 139 baada ya tetemeko kubwa la ardhi lililokumba Uturuki siku ya Jumatatu.

    Huku hayo yakijiri, msichana mwenye umri wa miaka 12, Cudie, aliokolewa baada ya kunaswa kwa saa 147 chini ya vifusi huko Hatay.

    Vyombo vya habari vya serikali pia viliripoti mtoto wa miaka 13 aliyeokolewa huko Gaziantep siku ya Jumapili huku waokoaji wakisema: "Wewe ni muujiza."

    Idadi ya watu waliothibitishwa kufariki Uturuki na Syria imeongezeka na kufikia zaidi ya 28,000.

    Syria haijaripoti idadi ya vifo tangu Ijumaa.

    Matumaini ya kupata manusura zaidi yanaendelea kudidimia, na huenda oparesheni ya uokoaji ya uokoaji ikakamilishwa hivi karibuni.

    Kikosi cha Ulinzi wa Raia cha Syria, au White Helmets, ambacho kinahudumu katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi nchini humo, kimeiambia BBC kwamba juhudi za kundi hilo za kutafuta watu zinaelekea kukamilika.

    Lakini maelfu ya waokoaji waliendelea na msako wao usiku kucha katika maeneo yaliyoathirika nchini Uturuki na Syria.

    Maelezo zaidi:

  3. Vifo vya wanajeshi wa Urusi vyaongezeka zaidi tangu kuanza kwa vita - Ukraine

    Mwanajeshi wa Ukraine anatembea Bakhmut wiki hii. Kati ya watu 50,000 walioishi katika jiji hilo kabla ya vita, ni 2,000 pekee waliosalia

    Chanzo cha picha, Reuters

    Wanajeshi wa Urusi wanakufa kwa idadi kubwa zaidi nchini Ukraine mwezi huu kuliko wakati wowote tangu wiki ya kwanza ya uvamizi, kulingana na data ya Ukraine.

    Takwimu za Ukraine zinaonyesha wanajeshi 824 wa Urusi wanakufa kwa siku mwezi Februari.

    Takwimu hizo ziliangaziwa na Wizara ya Ulinzi ya Uingereza. Takwimu haziwezi kuthibitishwa - lakini Uingereza inasema mwelekeo "huenda ni sahihi".

    Ongezeko hilo linakuja huku kukiwa na mazungumzo ya mashambulizi ya majira ya kuchipua ya vikosi vya Urusi mashariki mwa nchi hiyo.

    Wiki iliyopita, waziri wa ulinzi wa Ukraine anayemaliza muda wake, Oleksiy Reznikov, alisema walikuwa wakitarajia mashambulizi mapya ya Urusi karibu Februari 24 - siku ya kumbukumbu ya uvamizi huo kamili.

    Lakini baadhi ya wanasiasa wa eneo hilo, wakiwemo magavana wa Luhansk na Donetsk, walidai kuwa mashambulio tayari yameanza.

    Baadhi ya mapigano makali yamekuwa karibu na Bakhmut mashariki mwa nchi.

    Siku ya Jumapili, mkuu wa kikosi cha mamluki cha Wagner cha Urusi alisema kundi hilo liliteka makazi karibu na mji huo ulioharibiwa.

    Soma:

  4. Mambo 4 ambayo huenda hukuyajua kumhusu Rihanna na kurejea kwake jukwaani baada ya miaka saba

    Rihanna

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mashabiki wa Rihanna wanatazamia kwa hamu onyesho lake katika kipindi cha mapumziko cha Super Bowl, mojawapo ya matamasha makubwa zaidi ya muziki na ya kifahari.

    Mwimbaji huyo atatumbuiza wakati wa mapumziko wakati Philadelphia Eagles watakapomenyana na Wakuu wa Jiji la Kansas siku ya Jumapili.

    Rihanna hajafanya onyesho au kutoa albamu tangu mwaka 2016, hivyo matarajio ni makubwa.Hasa baada ya kujifungua mwaka jana.

    Mashabiki wanatumai onyesho la Super Bowl la msanii huyo mwenye umri wa miaka 34 litaweza kumrudisha jukwaani kimuziki baadaye mwaka huu.

    1. utajiri

    Utajiri wa nyota huyo wa pop unafikia dola bilioni 1.7. Takriban dola bilioni 1.4 hazitokani na muziki bali kutoka kwa thamani ya kampuni yake ya vipodozi, Fenty Beauty.

    2. Umaarufu

    Alizaliwa miaka 34 iliyopita huko Saint Michel, katika kisiwa cha Barbados.

    Umaarufu wake ulitokana majaribio ya muziki wa mtayarishaji wa Evan Rodgers akiwa na wanafunzi wenzake wawili wa shule mnamo 2003.

    3. Uzazi

    Mabadiliko makubwa ambayo msanii huyo amekuwa nayo kwa wakati huu ni kuwa mama, ambayo kwa mujibu wa kile alichoiambia Apple Music, imemfanya kuwa makini zaidi na miradi anayochagua kwa sababu anajua yoyote atakayochagua inaweza kumfanya awe mbali na mwanawe kwa muda mrefu.

    3. Kuvunja Rekodi

    Kando na kuwa mwimbaji wa kike mwenye kipato cha juu zaidi, au kusaini mkataba na Jay-Z akiwa na umri wa miaka 16 pekee, nyota huyo amevunja rekodi za kila aina. Kwa mfano, Rihanna ana vibao 40 bora zaidi kuliko Beatles.

    4. Ataimba nini

    Hakuna anayejua kwa hakika ni nyimbo gani atakazoimba. Orodha za onyesho la mapumziko na wageni maalum wa wasanii huwa siri ili kuhakikisha mashabiki wanafuatilia kwa hamu onyesho hilo.

  5. Burundi yatuma kundi la waokoaji nchini Uturuki

    Burundi

    Chanzo cha picha, Serkali ya Burundi

    Serikali ya Burundi imetuma timu ya "waokoaji maalum" 10 nchini Uturuki kama hatua ya "mshikamano na watu wa Uturuki" waliokumbwa na matetemeko makubwa ya ardhi, mamlaka zilisema.

    "Wakati wa kuwasili timu itatumwa na mamlaka ya Uturuki katika maeneo ambayo wanaihitaji zaidi", waziri wa mambo ya nje wa Burundi Albert Shingiro aliiambia BBC Idhaa ya Maziwa Makuu siku ya Jumapili.

    Zaidi ya watu 28,000 wamefariki nchini Uturuki na Syria baada ya matetemeko ya ardhi Jumatatu.

    Hakuna raia wa Burundi aliyeathiriwa, na Bi Sabria Samir Kaze ambaye alikuwa katika mji wa Gaziantep - uliokumbwa vibaya na tetemeko la kwanza - alihamishwa hadi Ankara, Bw Shingiro alisema.

    Burundi haikutuma waokoaji Syria kwa sababu “ ni vigumu kufikia maeneo yaliyoathiriwa.

    Hata hivyo, tunawahurumia watu ndugu wanaoteseka wa Syria”, waziri alisema.

  6. Uturuki yatoa vibali 113 vya kukamatwa waliohusika na majengo yaliyoporomoka

    Mashirika ya misaada yameonya kuwa huenda idadi ya waliofariki ikaongezeka huku juhudi za uokoaji zikiendelea

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelezo ya picha, Mashirika ya misaada yameonya kuwa huenda idadi ya waliofariki ikaongezeka huku juhudi za uokoaji zikiendelea

    Maafisa nchini Uturuki wanasema vibali 113 vya kukamatwa vimetolewa kuhusiana na ujenzi wa majengo yaliyoporomoka katika tetemeko la ardhi la Jumatatu wiki iliopita.

    Polisi wa Uturuki tayari wamewaweka chini ya ulinzi watu wasiopungua 12, wakiwemo wakandarasi wa ujenzi.

    Wakati huo huo, machafuko kusini mwa Uturuki yametatiza juhudi za uokoaji katika baadhi ya maeneo.

    Idadi ya watu waliothibitishwa kufariki Uturuki na Syria imeongezeka na kufikia zaidi ya 28,000.

    Watu zaidi kunatarajiwa kukamawa - lakini hatua hiyo inaonekana na baadi ya watu kama jaribio la kugeuza lawama kwa ujumla kwa janga hilo.

    Kwa miaka mingi, wataalam walionya kuwa majengo mengi mapya nchini Uturuki hayakuwa salama kutokana na ufisadi uliokithiri na sera za serikali.

    Sera hizo ziliruhusu kile kinachojulikana kama msamaha kwa wakandarasi waliokiuka kanuni za ujenzi, ili kuhimiza ukuaji wa ujenzi - ikiwa ni pamoja na katika maeneo yanayokumbwa na tetemeko la ardhi.

    Maelfu ya majengo yaliporomoka wakati wa tetemeko hilo la ardhi, na hivyo kuzua maswali kuhusu iwapo athari za maafa hayo ya asili zilifanywa kuwa mbaya zaidi kutokana na mapungufu ya kibinadamu.

    Maelezo zaidi:

  7. Wanawake 500 wajawazito wa Urusi watafuta uraia wa Argentina Argentina

    Ndege katika uwanja wa ndege wa Buenos Aires

    Chanzo cha picha, Reuters

    Zaidi ya wanawake 5,000 wajawazito wa Urusi wameingia Argentina katika miezi ya hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na 33 kwa ndege moja siku ya Alhamisi, maafisa wanasema.

    Waliofika hivi punde wote walikuwa katika wiki za mwisho za ujauzito, kulingana na wakala wa kitaifa wa uhamiaji.

    Inaaminika kuwa wanawake wanataka kuhakikisha watoto wao wanazaliwa nchini Argentina ili kupata uraia wa Argentina.

    Idadi ya waliowasili imeongezeka hivi karibuni,vyombo vya habari vya ndani vinaashiria hatua hiyo imetokana na vita vya Ukraine.

    Wanawake hao wa Urusi hapo awali walidai kuwa walikuwa wakitembelea Argentina kama watalii, alisema.

    "Tulibainika kuwa hawakuja hapa kufanya shughuli za utalii. Walikubali wenyewe.

    Alisema wanawake wa Urusi walitaka watoto wao wawe na uraia wa Argentina kwa sababu ilitoa uhuru zaidi kuliko pasipoti ya Urusi.

    "Tatizo ni kwamba wanakuja Argentina, kuwasajili watoto wao kama Waargetina na kuondoka. Pasipoti yetu ni salama kote duniani. Inawaruhusu [waliyo nayo] kuingia nchi 171bila visa," Bi Carignano alisema.

    Kuwa na mtoto Muargentina pia kunasaidia kuharakisha mchakato wa wazazi kupata uraia. Kwa sasa Warusi wanaweza kusafiri bila visa katika nchi 87 pekee.

    Maelezo zaidi:

  8. DRC: Wanajeshi saba wahukumiwa kifo kwa 'uoga'

    Wanajeshi

    Chanzo cha picha, Serikali ya NORD-KIVU

    Wanajeshi saba wa Congo wamehukumiwa kifo kwa kuonyesha 'uoga mbele ya adui' na kusababisha hofu kuu walipokimbia waasi wa M23.

    Siku ya Alhamisi, wanajeshi hao walipitia katikati ya Sake, kilomita 25 magharibi mwa mji mkuu wa mashariki mwa Kongo wa Goma, "wakipiga risasi kiholelea, walipokuwa wakiwakimbia adui kutoka mstari wa mbele", mwendesha mashtaka wa kijeshi alisema katika mahakama ikiendelea siku ya Jumamosi huko Sake.

    Wanajeshi hao walikanusha mashtaka na mawakili wao walisema watakata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama, mamlaka ya mkoa wa Kivu Kaskazini ilisema.

    Raia wawili waliuawa na wengine wanne kujeruhiwa vibaya wakati wa tukio hilo lililosababishwa na kitendo cha askari, mwendesha mashtaka alisema huku akiwatuhumu kuwa 'wauaji'.

    Maelfu ya watu hivi majuzi wamekimbia makazi yao hadi Goma na Minova huku waasi wa M23 wakikaribia mji huo polepole kutoka Masisi magharibi.

    Mnamo Novemba, mahakama ya kijeshi ya Goma iliwahukumu kifo askari watatu kwa "kukimbia vitani" wakati w amakabiliano dhidi ya M23 na kusababisha hofu miongoni mwa raia.

    Adhabu za kifo bado zinatolewa nchini DR Congo lakini mara ya mwisho zilitekelezwa mwaka 2003, zinabadilishwa kwa utaratibu na kuwa kifungo cha maisha.

  9. Hujambo na karibu.