Jeshi
nchini Uganda limekanusha ripoti kwamba linajaribu kuivuruga Ethiopia kwa kutoa
mafunzo na kutoa msaada kwa chama cha Tigray People's Liberation Front - TPLF,
ambacho kimekuwa na vita na serikali ya Ethiopia tangu 2020.
Ripoti hizo zilionekana
kuibuka mara ya kwanza mnamo Meikatika mitandao ya habari ya nchini Ethiopia.
Msemaji
wa Jeshi la Uganda Brigedia Felix Kulayigye alisema kupitia Twitter siku ya Jumapili kwamba madai ya majaribio ya Uganda
kuyumbisha Ethiopia ni uzushi mtupu.
Makala
ya kina ilionekana wiki iliyopita katika kituo cha mtandaoni kilichoko New
Zealand, pamoja na orodha ya maafisa wakuu wa jeshi la Uganda na wengine kutoka
katika vikosi vya usalama, ambao wanadaiwa kuongoza operesheni ya mafunzo
katika wilaya ya kati ya Uganda ya Masaka.
Stakabadhi
hiyo inaonyesha kuwa zaidi ya wanajeshi 4000 wa Tigray walipaswa kupewa mafunzo
katika vituo vinne tofauti nchini Uganda.
Ripoti
hiyo inadai zaidi kwamba shughuli ya mafunzo inaungwa mkono na Marekani na
Misri.
Mmoja wa
maafisa wakuu waliotajwa kwenye ripoti hiyo ni mtoto wa Rais na kamanda wa
jeshi la nchi kavu la Uganda Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ambaye alituma
ujumbe kwenye Twitter akiunga mkono vikosi vya Tigray, akiwataja kama
"ndugu", mnamo 2021.
Bado
haijabainika stakabadhi hiyo ni ya kweli
au ni sehemu ya kampeni ya habari ghushi. Tovuti ya New Zealand, inayojulikana
kama Scoop, ilisema haikuweza kuthibitisha chanzo au ikiwa maelezo hayo yalikuwa sahihi au la.
Lakini
kuna baadhi ya vitu visivyoeleweka -Inamtaja
James Kabarebe kuwa Waziri wa Ulinzi wa zamani nchini Uganda, lakini nchi hiyo
haijawahi kuwa na waziri kwa jina hilo katika nafasi hiyo.
Brigedia
Kulayigye pia alisema katika Twitter kwamba madai ya ushirikiano kati ya Uganda na
Sudan Kusini katika operesheni hiyo si ya kweli, kwa sababu balozi wa Uganda
nchini Sudan Kusini, ambaye anatajwa kuwa mratibu wa sehemu ya operesheni hiyo,
hajawahi kukutana na jenerali wa Sudan Kusini aliyetajwa katika ripoti.