Kiungo wa kati wa zamani wa Uingereza Frank Lampard
ameteuliwa kuwa kocha wa Everton kwa mkataba wa miaka miwili na nusu.
Mchezaji huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 43 anachukua
nafasi ya Rafael Benitez, ambaye alitimuliwa mapema mwezi huu baada ya kushinda
mchezo mmoja katika michezo 13.
Ni kazi ya kwanza kwa Lampard tangu alipotimuliwa Chelsea
mwaka mmoja uliopita huku Thomas Tuchel akichukua nafasi yake.
"Ni heshima kubwa kwangu kuwakilisha na kusimamia klabu yenye ukubwa na utamaduni wa Everton," alisema Lampard.
"Nina hamu sana ya kuanza."Mechi ya kwanza ya Lampard kutawala itakuwa ni mechi ya Jumamosi ya raundi ya nne ya Kombe la FA dhidi ya Brentford kwenye Uwanja wa Goodison Park.
Usajili wake wa kwanza Everton anatarajiwa kuwa kiungo wa kati wa Manchester United Donny van de Beek, ambaye anatazamiwa kujiunga na Toffees kwa mkopo kwa muda wote uliosalia.
Mchezaji wa zamani wa Chelsea na Manchester City Lampard, ambaye aliichezea Uingereza mechi 106, ana jukumu la kuiweka Everton kwenye msimamo wa ligi kwani klabu hiyo iko katika nafasi ya 16 na pointi nne pekee juu ya eneo la kushushwa daraja.
Lampard alisema anaona "shauku na matarajio" ya mmiliki Farhad Moshiri, mwenyekiti Bill Kenwright na bodi ya Everton katika mazungumzo juu ya jukumu hilo.
"Natumai walijua azma yangu na jinsi ninavyotaka kufanya bidii," aliongeza.
"Unaweza kuhisi shauku ya mashabiki wa Everton kwa klabu yao - hiyo itakuwa muhimu sana."Kama timu - kiwango cha ushindani kinacholetwa na Ligi Kuu na nafasi tuliyopo kwenye jedwali - hakika tunahitaji hilo. Ni jambo la pande mbili."
Everton ni klabu ya kipekee kwa kuwa unaweza kuelewa kile mashabiki wanataka kuona.
Kitu cha kwanza wanachotaka ni kupigana na kutamani na hiyo lazima uwe msingi wetu kila wakati."Ujumbe wangu wa kwanza kwa wachezaji ni kwamba tunapaswa kufanya hili pamoja.
''Tutajaribu kufanya kazi yetu na najua mashabiki watakuwa pale kutuunga mkono."
Lampard alikuwa mmoja wa wagombea watatu waliohojiwa kwa nafasi ya ukocha huku Vitor Pereira na kocha wa muda Duncan Ferguson pia wakiwania nafasi hiyo.
Kocha wa Derby na mshambuliaji wa zamani wa Everton na Manchester United Wayne Rooney alithibitisha pia kuuliziwa kuhusu kazi hiyo lakini alikataa.
Ferguson, ambaye alikuwa meneja msaidizi chini ya Benitez, na kocha wa makipa Alan Kelly watasalia kama sehemu ya benchi la Lampard.
Joe Edwards amejiunga kama kocha msaidizi, huku Paul Clement akiwa kocha wa kikosi cha kwanza na Chris Jones kama kocha wa kikosi cha kwanza na mkuu wa utendaji.
Lampard alifutwa kazi na Chelsea baada ya kuifundisha kwa miezi 18. Katika mwaka wake wa kwanza katika nafasi hiyo aliiongoza klabu hiyo kumaliza ligi ikiwa nafasi ya nne na fainali ya Kombe la FA.
Lakini wakati mgumu katika msimu wake wa pili, akiwa na vichapo vitano kwenye ligi katika mechi nane, kulimfanya afukuzwe na Blues.
Kabla ya kuchukua mikoba ya Chelsea alikuwa Derby kwa msimu mmoja.
Aliwaongoza kwenye fainali ya kuwania Ubingwa lakini wakashindwa na Aston Villa.
“Nimefurahi sana kwamba Frank amejiunga nasi,” alisema Moshiri."Alituvutia sote sana wakati wa mchakato wa mahojiano ya kina na sote tuko tayari kumpa msaada wetu wote anapotaka kuipa timu nguvu mara moja."