Rais wa Burkina Faso Roch Kaboré anadaiwa kuzuiliwa na jeshi

Roch Kabore

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, President Kaboré katika picha katika mkutano wa amani mjini paris mwezi Novemba

Rais wa Burkina Faso, Roch Kaboré, ameripotiwa kuzuiliwa na wanajeshi waasi.

Baadhi ya wanajeshi katika taifa hilo la Afrika Magharibi wametaka kufutwa kazi kwa wakuu wa kijeshi na rasilimali zaidi ili kupambana na wanamgambo wa Kiislamu.

Milio ya risasi ilikuwa imesikika usiku kucha karibu na ikulu ya rais na kwenye kambi katika mji mkuu, Ouagadougou.

Serikali siku ya Jumapili ilikanusha mapendekezo ya mapinduzi ya kijeshi au kwamba rais alikuwa amekamatwa.

Rais Kaboré alizuiliwa katika kambi ya kijeshi na wanajeshi walioasi, ripoti za vyombo vya habari vya kigeni vinasema.

Video kutoka mji mkuu inaonekana kuonyesha magari ya kivita - yanayoripotiwa kutumiwa na rais - yakiwa na matundu ya risasi na kutelekezwa mitaani.

Huduma za mtandao wa simu za mkononi zimekatizwa, ingawa mtandao wa laini zisizobadilika na wi-fi ya nyumbani zinafanya kazi. Wanajeshi pia wamezingira makao makuu ya televisheni ya serikali na hakujakuwa na vipindi vya moja kwa moja Jumatatu.

Mwandishi wa BBC Simon Gongo ana kwamba "hisia ya hali ya kawaida" imerejea mitaani. Hakuna upigaji risasi zaidi unaoweza kusikika, na watu na magari yanasonga katikati ya jiji.

Umati umekusanyika mbele ya makazi ya kibinafsi ya rais, anasema, "wakitaka kuelewa kilichotokea wakati wa usiku".

"Bila maoni rasmi kutoka kwa jeshi au serikali, watu wanasubiri kwa hamu taarifa rasmi kuhusu hali hiyo."

Siku ya Jumapili, mamia ya watu walijitokeza kuwaunga mkono wanajeshi hao na baadhi yao walichoma moto makao makuu ya chama tawala. Amri ya kutotoka nje wakati wa usiku imewekwa.

Mahali alipo rais hapajulikani, lakini shirika la habari la AFP lilinukuu vyanzo vya usalama vikisema kuwa yeye na mawaziri wengine wa serikali wako katika kambi ya Sangoule Lamizana katika mji mkuu.

Hakujakuwa na mawasiliano kutoka kwa Rais Kaboré mwenyewe tangu Jumapili usiku, alipotuma kwenye mitandao ya kijamii akipongeza timu ya taifa ya kandanda kwa ushindi wao katika mechi ya Kombe la Mataifa ya Afrika.

2px presentational grey line

Burkina faso - cha msingi

  • Iliyokuwa koloni ya Ufaransa, Burkina Faso imekumbwa na misukosuko ya ukosefu wa udhabiti tangu ilipopata uhuru mwaka 1960, ikijumuisha mapinduzi kadhaa.
  • Jina la nchi hiyo, linalomaanisha "ardhi ya watu waaminifu" lilichaguliwa na afisa mwanamapinduzi Thomas Sankara ambaye alichukua mamlaka mwaka wa 1983. Alipinduliwa na kuuawa mwaka wa 1987.
  • Tangu mwaka wa 2015, nchi hiyo imekuwa ikipambana na waasi wa Kiislamu waliosambaa kutoka nchi jirani ya Mali. Hii imechochea hasira katika jeshi na kuharibu tasnia muhimu ya utalii nchini humo.
2px presentational grey line

Machafuko hayo yanajiri wiki moja baada ya wanajeshi 11 kukamatwa kwa madai ya kupanga mapinduzi.

Lakini kutoridhika kumeongezeka nchini Burkina Faso kutokana na kushindwa kwa serikali kuwashinda waasi wa Kiislamu nchini humo tangu mwaka 2015.

Hali hiyo iliongezeka hadi kufikia hali mpya mwezi Novemba, wakati watu 53, hasa wanachama wa vikosi vya usalama, waliuawa na watu wanaoshukiwa kuwa wanajihadi. Na siku ya Jumamosi, maandamano yaliyopigwa marufuku ya kupinga kushindwa kwa serikali ilisababisha watu wengi kukamatwa.

Matatizo kama hayo katika nchi jirani ya Mali yalisababisha mapinduzi ya kijeshi mwezi Mei 2021 - ambayo yalipokelewa kwa furaha na umma.

Magari kadhaa ya rais mapema leo alfajiri yalipatikana yakiwa na matundu ya risasi

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Magari kadhaa ya rais mapema leo alfajiri yalipatikana yakiwa na matundu ya risasi

Nchini Burkina Faso, askari waasi walitoa masharti kadhaa, ikiwa ni pamoja na kuondolewa kwa mkuu wa majeshi na mkuu wa idara ya upelelezi; askari zaidi kupelekwa mstari wa mbele; na hali bora kwa familia zilizojeruhiwa na askari.

Siku ya Jumapili, Waziri wa Ulinzi Jenerali Barthelemy Simpore alipuuza uvumi wa hapo awali wa kukamatwa kwa rais, na asili ya machafuko kwa ujumla.

Televisheni ya serikali, wakati huo huo, ilibainisha milio ya risasi kwenye kambi za kijeshi kama vitendo vya wanajeshi wachache waliochukizwa badala ya mapigano yaliyoenea au jaribio la mapinduzi.

Map: The location of Burkina Faso in West Africe