Kesi ya Thomas Sankara yaahirishwa kwasababu ya mapinduzi
Mahakama nchini Burkinafaso imeahirisha kesi ya watu wanaodaiwa kumuua kiongozi mwana mapinduzi, Thomas Sankara, ambaye aliuawa mwaka 1987.
Moja kwa moja
Mwanajihadi wa Kitanzania auawa Msumbiji - Polisi
Chanzo cha picha, AFP
LinkMtu anayeshukiwa kuwa kiongozi wa wanajihadi kutoka Tanzania ameuawa nchini Msumbiji, wiki mbili baada ya kiongozi mwingine wa wanamgambo kutoka nchi hiyo ya Afrika Mashariki kukamatwa na wanajeshi.
Tuahil Muhidim anatuhumiwa kuongoza oparesheni za wanajihadi Mocimboa da Praia kwenye pwani ya kaskazini ya jimbo la Cabo Delgado mwaka 2020.
Kifo hicho kilitangazwa Jumapili na mkuu wa polisi Bernardino Rafael wakati wa gwaride la kijeshi huko Magoma, takriban kilomita 11 kutoka Naquitungue, ambapo Muhidim aliuawa pamoja na mmoja wa washirika wake siku ya Jumamosi.
Mkuu huyo wa polisi alisema kiongozi huyo wa wanajihadi aliongoza operesheni ya kuwateka nyara watawa wawili wa Brazil na "amewaadhibu" kabla ya kuokolewa.
Bw Rafael pia alitangaza kurejesha kwa vikosi vya pamoja vya Msumbiji na Rwanda silaha mbili za mashambulizi aina ya AKM na magazine nane.
Alisema vikosi vya pamoja vinavyofanya kazi nchini Msumbiji vimewaua kwa risasi zaidi ya viongozi saba wa wanajihadi katika muda wa siku 60 zilizopita.
Mwanamuziki Rihanna na mpenziwe wanatarajia mtoto wao wa kwanza
Chanzo cha picha, BET Twitter
Mwimbaji nyota wa muziki Rihanna na mpenzi wake msanii A$AP Rocky wanatarajia mtoto wao wa kwanza wakiwa pamoja, wanandoa hao walithibitisha kwenye picha zilizopatikana na kwenye mtandao wa E! News.
Katika picha hizo, zilizopigwa jijini New York mwishoni mwa wiki na kuchapishwa Jumatatu, Januari 31, Rihanna anaonekana akionesha tumbo lake huku A$AP akimbusu paji la uso.
Habari hii ya ujauzito inakuja miaka miwili baada ya marafiki wa muda mrefu kuhusishwa na taarifa kuwa ni wapenzi, tetesi zilizokuwepo muda mfupi baada ya kutengana na Hassan Jameel.
Uhusiano ulianza baada ya nyota hao kuonekana wakiwa pamoja huko New York.
Hatahivyo, wakati huo, Rihanna hakutafuta uhusiano wa dhati. Kama chanzo E! News ilieleza mwaka 2020.
"Rihanna hana mwenza. Ametoka kwenye uhusiano wa muda mrefu na Hassan. Anataka kuwa mwenyewe Anatembea na ASAP Rocky, lakini si mpenzi wake. "
Baada ya muda, mahusiano kati ya Rihanna, 33, na A$AP, pia 33, yakawa vigumu kukanusha.
Kesi ya Thomas Sankara yaahirishwa kwasababu ya mapinduzi
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Familia ya kiongozi mwanamapinduzi yaliomba kuahirishwa kwa kesi mpaka hali ya utulivu itakaporejeshwa nchini Burkina Faso
Mahakama nchini Burkina Faso imeahirisha kesi
ya watu wanaodaiwa kumuua kiongozi mwana mapinduzi, Thomas Sankara, ambaye aliuawa
mwaka 1987.
Familia ya Sankara iliomba
kuahirishwa kwa kesi hiyo kufuatia mapinduzi ya wiki iliyopita.
Walisema wanataka kuifufua
kesi hiyo mara hali ya kikatiba itakaporejeshwa.
Muungano wa Afrika
Jumatatu uliisitisha Burkina Faso uanachama, siku tatu baada ya shirika la
kikanda na Magharibi mwa Afrika, Ecowas.
Ujumbe wa pamoja wa Umoja wa mataifa na Ecowas uko mjini Ouagadougou kwa ajili ya kufanya mazungumzo na
viongozi wapya wa kijeshi.
Simba amwua mlinzi wa bustani ya wanyama Iran
Chanzo cha picha, Getty Images
Simba jike mmoja amemuua mlinzi aliyekuwa akimlisha katika bustani ya
wanyama katikati mwa Iran, vyombo vya habari vya taifa hilo vimeeleza.
Tukio hilo lilitokea siku ya Jumapili huko Arak, kusini mwa Tehran, Shirika
la Habari la Jamhuri ya Kiislamu (Irna) liliripoti.
Irna lilisema simba jike huyo alitoroka kwenye boma lake na kuzurura kwenye
bustani ya wanyama akiwa na simba mwingine aliyetoroka kwa saa kadhaa.
Wawili hao walikamatwa tena baada ya polisi, wa zima moto na maafisa wa
serikali ya mtaa kuanzisha operesheni, meya wa Arak alisema.
"Mchana wa leo mmoja wa waangalizi aliingia kwenye banda kumlisha simba
huyo na kw bahati mbaya alipoteza maisha baada ya kushambuliwa na
kuzidiwa,"
Meya Alireza Karimi alinukuliwa na Irna akisema.
Irna limesema simba jike alikuwa amesukuma nguzo ya chuma ili kufungua
mlango wa boma, akijiachia na kumshambulia mwangalizi huyo.
Haijulikani ikiwa bustani ya wanyama ilikuwa wazi kwa ajili ya Umma wakati
huo.
Mtoto wa miaka 9, mmoja wa mabilionea duniani
Chanzo cha picha, Mompha Junior/Facebook
Maelezo ya picha, Mompha Junior, bilionea mwenye umri wa miaka 9
Mtoto
mwenye umri wa miaka 9 ni mmoja wa mabilionea mwenye umri mdogo zaidi duniani huku
akimiliki nyumba yake binafsi na ndege.
Mtoto huyu ni mwana wa kike wa mmiliki wa kampuni kubwa ya inteneti ya Nigeria Ismailia Mustafa, ambaye pia anafahamika kwa
jina Momfa.
Mvulana huyu mwenye umri wa miaka 9-, kwa jina Mompha Junior, alipewa nyumba yake ya kwanza
akiwa na umri wa miaka 6.
Mompha Junior, mara kwa mara hutuma picha zake nzuri kwenye mtandao wake wa
kijamii wa Instagram, akionyesha mtindo
wake wa maisha ya kifahari.
Awali aliushirikisha umma picha ya ndege yake aina ya jet, ambapo akiandika "Usimdharau yeyote bure, na fanya kazi kwa
bidii. Mungu
awabariki watu ."
Baba yake Willkan Bw
Mompha, ambaye ni meneja mkuu wa kituo
cha kubadili pesa-Lagos Bureau De
Change, anashutumiwa kwa ubadhilifu wa pesa wa zaidi ya dola milioni 10.
Mapea mwezi huu,
mahakama ya Nigeria ilisikiliza kesi iliyowasilishwa na tume ya Nigeria ya
kupambana na ufisadi dhidi ya Bw Ismail, iliyodai kuwa alikuwa amefanya
ubadhilifu wa pesa kutoka katika biashara yake ya nyumba, ingawa Bw Ismael
anakanusha madai hayo.
Frank Lampard awa kocha wa Everton
Chanzo cha picha, Getty Images
Kiungo wa kati wa zamani wa Uingereza Frank Lampard
ameteuliwa kuwa kocha wa Everton kwa mkataba wa miaka miwili na nusu.
Mchezaji huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 43 anachukua
nafasi ya Rafael Benitez, ambaye alitimuliwa mapema mwezi huu baada ya kushinda
mchezo mmoja katika michezo 13.
Ni kazi ya kwanza kwa Lampard tangu alipotimuliwa Chelsea
mwaka mmoja uliopita huku Thomas Tuchel akichukua nafasi yake.
"Ni heshima kubwa kwangu kuwakilisha na kusimamia klabu yenye ukubwa na utamaduni wa Everton," alisema Lampard.
"Nina hamu sana ya kuanza."Mechi ya kwanza ya Lampard kutawala itakuwa ni mechi ya Jumamosi ya raundi ya nne ya Kombe la FA dhidi ya Brentford kwenye Uwanja wa Goodison Park.
Usajili wake wa kwanza Everton anatarajiwa kuwa kiungo wa kati wa Manchester United Donny van de Beek, ambaye anatazamiwa kujiunga na Toffees kwa mkopo kwa muda wote uliosalia.
Mchezaji wa zamani wa Chelsea na Manchester City Lampard, ambaye aliichezea Uingereza mechi 106, ana jukumu la kuiweka Everton kwenye msimamo wa ligi kwani klabu hiyo iko katika nafasi ya 16 na pointi nne pekee juu ya eneo la kushushwa daraja.
Lampard alisema anaona "shauku na matarajio" ya mmiliki Farhad Moshiri, mwenyekiti Bill Kenwright na bodi ya Everton katika mazungumzo juu ya jukumu hilo.
"Natumai walijua azma yangu na jinsi ninavyotaka kufanya bidii," aliongeza.
"Unaweza kuhisi shauku ya mashabiki wa Everton kwa klabu yao - hiyo itakuwa muhimu sana."Kama timu - kiwango cha ushindani kinacholetwa na Ligi Kuu na nafasi tuliyopo kwenye jedwali - hakika tunahitaji hilo. Ni jambo la pande mbili."
Everton ni klabu ya kipekee kwa kuwa unaweza kuelewa kile mashabiki wanataka kuona.
Kitu cha kwanza wanachotaka ni kupigana na kutamani na hiyo lazima uwe msingi wetu kila wakati."Ujumbe wangu wa kwanza kwa wachezaji ni kwamba tunapaswa kufanya hili pamoja.
''Tutajaribu kufanya kazi yetu na najua mashabiki watakuwa pale kutuunga mkono."
Lampard alikuwa mmoja wa wagombea watatu waliohojiwa kwa nafasi ya ukocha huku Vitor Pereira na kocha wa muda Duncan Ferguson pia wakiwania nafasi hiyo.
Kocha wa Derby na mshambuliaji wa zamani wa Everton na Manchester United Wayne Rooney alithibitisha pia kuuliziwa kuhusu kazi hiyo lakini alikataa.
Ferguson, ambaye alikuwa meneja msaidizi chini ya Benitez, na kocha wa makipa Alan Kelly watasalia kama sehemu ya benchi la Lampard.
Joe Edwards amejiunga kama kocha msaidizi, huku Paul Clement akiwa kocha wa kikosi cha kwanza na Chris Jones kama kocha wa kikosi cha kwanza na mkuu wa utendaji.
Lampard alifutwa kazi na Chelsea baada ya kuifundisha kwa miezi 18. Katika mwaka wake wa kwanza katika nafasi hiyo aliiongoza klabu hiyo kumaliza ligi ikiwa nafasi ya nne na fainali ya Kombe la FA.
Lakini wakati mgumu katika msimu wake wa pili, akiwa na vichapo vitano kwenye ligi katika mechi nane, kulimfanya afukuzwe na Blues.
Kabla ya kuchukua mikoba ya Chelsea alikuwa Derby kwa msimu mmoja.
Aliwaongoza kwenye fainali ya kuwania Ubingwa lakini wakashindwa na Aston Villa.
“Nimefurahi sana kwamba Frank amejiunga nasi,” alisema Moshiri."Alituvutia sote sana wakati wa mchakato wa mahojiano ya kina na sote tuko tayari kumpa msaada wetu wote anapotaka kuipa timu nguvu mara moja."
Jinsi mwanamke wa Ghana alivyojifungulia ndani ya ndege
Chanzo cha picha, NANCY ADOBEA ANAN
Safari ya ndege iliyotarajiwa kuwa yenye utulivu kutoka Accra
Ghana kuelekea Marekani iligeuka kuwa uzoefu ambao mwanamke mmoja mjamzito
kutoka Ghana hatausahau maishani mwake, pamoja na wasafiri waliokuwemo ndani ya
ndege ya Marekani United Airlines chapa UA
977.
Mwanamke mjamzito alipata uchungu wa uzazi,bila kutarajiwa na
ikabidi rubani na wahudumu wa ndege kushugulikia suala hilo.
Mwanamke huyo ambaye alitarajiwa kujifungua mwishoni mwa mwezi
wa Februari alishitushwa na kwamba mtoto wake mchanga aliamua kuzaliwa mapema.
Aliyeshuhudia tukio hilo, Nancy Adobea Anane ambaye alikuwa
ndani ya ndege hiyo aliiambia BBC Idhaa ya Kipidgin kuwa tangu marubani
walipotangaza watu walikuwa hawajafahamu kilichotokea.
"Wengi wao
walisikia tangazo la kuomba usaidizi kutoka kwa daktari, lakini hawakujuani nini kilichokuwa kinaendelea" Nancy Adobea Anane aliiambia BBC
Pidgin.
Hali ya mshituko na shangwe
Chanzo cha picha, NANCY ADOBEA ANAN
Maelezo ya picha, Dokta Ansah-Addo daktarin Mghana anayefanya kazi Marekani alijitokeza baada ya rubani kuomba usaidizi ndani ya ndege.
Akielezea hali iliyokuwa ndani ya ndege hiyo, Nancy alisema lilikuwa ni jambo la " mshituko na shangwe."
"Kujifungua kwake kulikuwa kwa haraka, kama dakika 30 hadi 45…kelele na kilio cha mtoto mchanga kikasikika… lilikuwa ni jambo la kufurahisha sana" anasema.
Chanzo cha picha, NANCY ADOBEA ANAN
Maelezo ya picha, Madaktari wakiingia kwenye ndege wakati ilipowasili katika Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Dallas.
Shuhuda mmoja aliwaelezea waandishi wa habari jinsi sehemu ya ndege hiyo ilivyogeuzwa kuwa wodi ya kumpokea mtoto mchanga.
Dr Ansah-Addo ambaye ni Mghana anayefanyika kazi nchini Marekani alijitokeza kusaidia baada ya rubani kuomba usaidizi wa kimatibabu ndani ya ndege hiyo.
Burkina Faso yasimamishwa na AU kwa sababu ya mapinduzi
Chanzo cha picha, AFP
Umoja wa Afrika (AU) umeisimamisha Burkina Faso wiki moja baada ya jeshi kunyakua mamlaka.
Ilisema nchi hiyo itazuiwa kujihusisha shughuli zote za AU hadi utaratibu wa kikatiba urejeshwe.
Jumuiya ya kanda ya Afrika Magharibi, Ecowas, ambayo ilisimamisha Burkina Faso wiki iliyopita, imetuma ujumbe katika mji mkuu Ouagadougou.
Itaungana na timu kutoka Umoja wa Mataifa kwa mazungumzo na viongozi hao wapya wa kijeshi.
Kimbunga Ana chagharimu maisha na riziki nchini Malawi
Mazao ya mahindi, mashamba yaliyojaa maji na madaraja yaliyoporomoka ndivyo vinavyotukaribisha huko Chikwawa, mwendo wa saa moja kwa gari kusini mwa Blantyre.
Magari ya ujenzi yakiwa yamejipanga pembezoni mwa barabara ambapo daraja kuu linalounganisha wilaya ya Blantyre na Chikwawa lilisombwa na mafuriko siku chache zilizopita.
Kuna msururu usio wa kawaida wa polisi hapa, kwa sababu Rais Lazarus Chakwera anatarajiwa kukagua uharibifu huo.
Mazao ya mahindi ya Aisha Anubi, yenye ukubwa wa uwanja wa mpira, yote yaliharibiwa na mafuriko.
Msichana huyo mwenye umri wa miaka 20 aliambia BBC kwamba amepoteza chanzo chake pekee cha mapato.
Hili ni mojawapo ya magari mengi ambayo yalikumbwa na kimbunga na kusombwa na mafuriko:
Haijulikani ikiwa watu waliokuwa kwenye gari hilo walifanikiwa kutoka bila kujeruhiwa.
Takriban watu 36 wamefariki nchini Malawi huku wengine wengi wakiwa bado hawajulikani waliko.
Huku mvua zaidi ikitarajiwa katika siku chache zijazo, watu hapa wana wasiwasi kuhusu kupoteza nyumba zao.
Harakati ndogo mpakani mwa Rwanda na Uganda baada ya kufunguliwa tena
Kuna harakati kidogo kwenye mpaka wa Gatuna wa Rwanda na Uganda, ambao umefunguliwa tena baada ya karibu miaka mitatu ya kufungwa.
Mpaka huo ulifungwa mwaka 2019 kufuatia mvutano kati ya nchi hizo mbili za Afrika Mashariki.
Mwandishi wa BBC Patience Atuhaire yuko upande wa mpaka wa Uganda na ametuma picha hizi:
Kwa upande wa Uganda, ujenzi wa ofisi za forodha - ambazo ni sehemu ya mfumo wa mpaka mmoja unaotekelezwa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki - unaendelea:
Timu ya BBC ya huduma ya Gahuza imeshiriki picha za jinsi upande wa Rwanda unavyoonekana, saa chache baada ya kufunguliwa tena:
Kufunguliwa kwa mpaka kulitangazwa wiki iliyopita baada ya mkutano kati ya Rais wa Rwanda Paul Kagame na Luteni Jenerali Muhoozi Kainerugaba wa Uganda, ambaye ni mtoto wa Rais Yoweri Museveni.
Rwanda ilikuwa imeishutumu Uganda kwa kuwazuia na kuwatesa raia wake huku Uganda ikiishutumu Rwanda kwa kupenyeza ujasusi wake wa kijeshi. Nchi zote mbili zilikanusha tuhuma hizo.
Hadi wanamgambo 60 waliuawa Burkina Faso - Ufaransa
Chanzo cha picha, AFP
Ufaransa imesma makumi ya wanamgambo wameuawa nchini Burkina Faso katika operesheni zinazohusisha wanajeshi wa ndani na wa Ufaransa.
Mashambulizi hayo yalifanywa kama sehemu ya Operesheni ya Barkhane inayoongozwa na Ufaransa dhidi ya makundi ya kijihadi katika eneo la Sahel barani Afrika - kabla ya mapinduzi ya Januari 23.
Jeshi la Ufaransa linasema lilishiriki katika operesheni nne pamoja na wanajeshi wa Burkinabè kati ya 16 na 23 Januari.
Ilisema lengo la mashambulizi haya - kwa kutumia ndege za kivita, helikopta za mashambulizi na ndege zisizo na rubani - lilikuwa kutafuta makundi ya "kigaidi" katika ngome zao, kwenye mpaka wa kaskazini na Mali.
Mamlaka ya Ufaransa ilisema hadi wanamgambo 60 waliuawa, huku takriban pikipiki 20 na lori kadhaa zilizokuwa na silaha zikiharibiwa.
Takriban watu 2,000 wamekufa katika mashambulizi ya wanajihadi nchini Burkina Faso tangu mwaka wa 2015, wakati wanamgambo wenye uhusiano na al-Qaeda na kundi la Islamic State walipoanza kufanya kuanza kufanya uvamizi kutoka Mali.
Habari za hivi punde, Gari la umma lalengwa katika shambulio la bomu kaskazini mwa Kenya
Gari la uchukuzi wa umma limekumbwa na shambulizi la bomu kaskazini mwa Kenya, karibu na mpaka wa Somalia.
Waandishi wa habari wa eneo hilo wanasema takriban watu tisa wamefariki na wengine kadhaa kujeruhiwa. Gari hilo lilikuwa likisafiri kuelekea Mandera, mji ulio katika eneo la mpakani, ambao umekuwa ukiathiriwa mara kwa mara na mashambulizi ya wanamgambo.
Picha kutoka kwa wanahabari wa eneo hilo zinazoshirikishwa katika mitandao ya kijamii zinaonesha mabaki ya gari la umma, linalojulikana kama matatu, ambalo lilipuliwa baada ya kukanyaga kilipuzi kilichokuwa kimetegwa barabarani.
Hakuna aliyedai kuhusika, lakini waasi wa Al Shabaab wamekuwa wakiwalenga polisi na raia ndani na karibu na Mandera na vifo kadhaa katika miaka ya hivi karibuni, na kuifanya Mandera kuwa moja ya maeneo hatari zaidi ya Kenya kuishi.
Shambulio hilo limetokea wiki moja tu baada ya balozi kadhaa za kigeni nchini Kenya, zikiwemo Marekani na Ufaransa, kuwaonya raia wake kuhusu uwezekano wa kutokea mashambulizi ya kigaidi nchini humo.
Polisi wa Kenya wametoa taarifa kuwahakikishia wananchi usalama wao.
Je wapiganaji wa al-Shabab kutoka Somalia wana malengo gani?
Ujumbe wa Ecowas na UN kutathmini hali ya Burkina Faso
Chanzo cha picha, AFP
Kundi la ujumbe kutoka Jumuiya ya kiuchumi ya mataifa ya Afrika magharibi Ecowas watazuru mji mkuu wa Burkina Fas, Ouagadougou, leo Jumatatu kutathmini hali ilivyo nchini humo.
Haya yanajiri wiki moja baada ya jeshi kupindua serikali ya Rais aliyechaguliwa Roch Kaboré.
Ujumbe huo wa ngazi ya mawaziri wa Ecowas utaunganishwa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa ukiongozwa na mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Afrika Magharibi na Sahel, Mahamat Saleh Annadif.
Ujumbe huo wa pamoja utafanya mazungumzo na kiongozi wa kijeshi Luteni Kanali Paul-Henri Damiba, pamoja na wadau mbalimbali wa Burkina Faso.
Mkutano wa ana kwa ana wa Ecowas umepangwa kufanyika Alhamisi nchini Ghana kwa mashauriano zaidi kuhusu hali hiyo.
Viongozi wa baraza la kikanda walifanya mkutano wa dharura wa mtandaoni Ijumaa iliyopita ambapo walisimamisha uanachama wa nchi hiyo kutoka kwa jumuia hiyo ya kikanda.
Nchi za Afrika Magharibi zimeshuhudia mapinduzi mawili ya kijeshi, huku Burkina Faso ikiwa nchi ya tatu baada ya Mali na Guinea katika mwaka uliopita.
Mapinduzi Burkina Faso: Fahamu kwa nini wanajeshi wamempindua Rais Kaboré
Paul-Henri Sandaogo Damiba : Kanali wa jeshi aliyeongoza mapinduzi Burkina Faso
Mapinduzi ya Burkina Faso: Kurejea kwa wababe wa kijeshi Afrika Magharibi
Rais wa Malawi awaonya mawaziri dhidi ya ufisadi
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Rais Lazarus Chakwera alifuta baraza lake la mawaziri wiki iliyopita
Rais wa Malawi amewaonya mawaziri dhidi ya ufisadi baada ya kuapisha baraza jipya la mawaziri siku ya Jumapili.
Rais Lazarus Chakwera alisema hatamkinga mtu yeyote dhidi ya mashtaka iwapo atajihusisha na vitendo vya ufisadi.
"Usikubali zawadi kwa kutumia ofisi yako kumpendelea mtu katika usimamizi wa utumishi wa umma. Huo ni ufisadi," alisema.
Rais alifuta baraza lake lote la mawaziri wiki jana lakini mawaziri wengi waliteuliwa tena katika safu mpya iliyotangazwa siku chache baadaye.
Maandamano ya kuipinga serikali yamefanyika tangu Novemba mwaka jana kulaani kupanda kwa gharama ya maisha na madai ya upendeleo na ufisadi.
Mason Greenwood: Mchezaji wa Man Utd akamatwa kwa madai ya ubakaji
Chanzo cha picha, Getty Images
Mchezaji wa Manchester United Mason Greenwood amekamatwa kwa tuhuma za ubakaji na shambulio kufuatia madai kwenye mitandao ya kijamii.
Polisi wa Greater Manchester walisema ilifahamishwa kuhusu "picha na video za mitandao ya kijamii zilizotumwa na mwanamke akiripoti matukio ya unyansaji wa kingono".
Iliongeza "tunaweza kuthibitisha kuwa mwanamume mwenye umri wa miaka 20 amekamatwa kwa tuhuma za ubakaji na shambulio".
Anaendelea kuzuiliwa kwa mahojiano na uchunguzi unaendelea.
Manchester United hapo awali ilisema mchezaji huyo hatarejea kwenye mazoezi au mechi hadi ilani nyingine.
Klabu hiyo ilisema "haikubaliani na vurugu za aina yoyote" na imefahamishwa kuhusu madai hayo kwenye mitandao ya kijamii lakini haitatoa maoni yoyote zaidi hadi "ukweli utakapothibitishwa".
Mason Greenwood hajajibu madai hayo ya mitandao ya kijamii.
Mchezaji kandanda huyo mwenye umri wa miaka 20, ambaye aliichezea klabu hiyo kwa mara ya kwanza Machi 2019, alisaini mkataba wa miaka minne Februari 2021 baada ya kupanda katika safu ya akademi ya United.
Kundi la vijana nchini Nigeria, chini ya mwamvuli wa Bunge la Vijana wa Kaskazini, limetoa wito kwa mfanyabishara tajiri zaidi Afrika Aliko Dangote, viongozi wengine wa wafanyabiashara na wataalamu kuingilia kati uchaguzi wa rais wa 2023.
Vijana hao wanasema kuwa uzoefu wao itasaidia kuleta maendeleo Nigeria.Katika taarifa kundi hilo ambalo lilifadhiliwa na Katibu Mkuu wake Desmond Minakaro na Baraza la Wawakilishi, Mohammed Salihu Danlami alisema watu kama Dangote, Femi Otedola, Mike Adenuga, Akinwumi Adesina, Herbert Wigwe, Ngozi Okonjo Iweala na kadhalika wana uwezo wa kuchukua nafasi ya rais wa Nigeria.
Wanasema wafanyabiashara wanaojua jinsi ya kupata faida sasa wanapaswa kuitawala Nigeria.
Hata hivyo seneta Shehu Sani amesema haoni
haja ya Bw. Dangote kuingilia siasa na kwamba anamtakaaendelee kuwa maarufu
kutokana na utajiri wake.
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya nje
Mwisho wa X ujumbe
Kauli ya Seneta huyo imezua gumzo mitandaoni:
Isha Fola, Joshua Obera, Jibra'eel na @Sirdotskill walisema kwenye akaunti yao ya Twitter kwamba Dangote na vigogo hawa wa biashara huenda wasiweze kuingia katika vituo vyao vya kupigia kura.
Wana mtazamo tofauti sana wa kisiasa kwa biashara kwa sababu mara nyingi hulinganishwa na kila mmoja.
@jibsunnah aliandika: Biashara na siasa ni vitu viwili tofauti, anaweza akafanikiwa kwenye biashara lakini hatujui anaweza kufanikiwa kwenye siasa, bora ajikite tu kwenye biashara yake.