Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mwanaharakati wa Tanzania aliyetekwa nyara nchini Kenya aachiwa huru
Maria Sarungi amethibitisha kuachiwa kwake kwenye mtandao wa X na kuongeza kuwa atatoa maelezo zaidi kuhusu tukio hilo Jumatatu.
Muhtasari
- Waziri nchini Kenya ashutumu serikali kwa visa vya utekaji nyara
- Meli ya 'kisiri' ya Urusi imekwama katika Bahari ya Baltic- Ujerumani
- Takriban wakazi 35,000 Los Angeles hawana umeme
- Mjumbe wa Trump akutana na Netanyahu huku wanajeshi wa Israel wakiuawa
- Upepo mkali waanza tena huku idadi ya waliofariki ikiongezeka
- Jeshi la Sudan ladai kuukomboa mji muhimu wa mashariki kutoka kwa waasi
- Wanajeshi wawili wa Korea Kaskazini wakamatwa Urusi - Ukraine
Moja kwa moja
Na Ambia Hirsi & Peter Mwangangi
Habari za hivi punde, Mwanaharakati wa Tanzania aliyetekwa nyara nchini Kenya aachiwa huru
Mwanaharakati wa Tanzania Maria Tsehai Sarungi ameachiwa huru baada ya ripoti kuibuka kuwa ametekwa nyara na watu watatu waliokuwa na silaha jijini Nairobi, Kenya.
Alichapisha kwenye akaunti yake ya X kuwa yuko salama na hiyo ingetoa maelezo zaidi juu ya kutekwa kwake siku ya Jumatatu.
Maria Tsehai, mkosoaji mkubwa wa utawala wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu, alikimbilia Kenya mwaka 2020, akiomba hifadhi baada ya kukabiliwa na vitisho vilivyoongezeka chini ya serikali ya hayati Rais John Magufuli.
Katika miezi ya hivi karibuni, alielezea wasiwasi wake kwa Amnesty International kuhusu usalama wake, akiripoti tukio ambapo wanaume wawili wasiojulikana walionekana wakimtafuta nyumbani kwake alipokuwa hayupo.
Idara ya upelelezi wa jinai ya Kenya (DCI) yamuomba Muturi kuandikisha taarifa
Idara ya upelelezi wa jinai ya Kenya (DCI) imejibu kauli ya Muturi na kusema kwamba uchunguzi wa kesi ya mwanawe bado inaendelea katika ofisi za DCI Kilimani mjini Nairobi.
Idara hio pia imemualika Waziri Muturi ‘'na mtu mwingine yeyote aliye na taarifa kuhusu kisa hicho’' kuwasilisha taarifa rasmi, ikisema kwamba ni mwanawe Muturi tu ambaye alijitolea kuandikisha taarifa kufikia sasa.
“Tunahakikishia umma kuhusu azma yetu ya kuhakikisha kwamba visa vyote vya utekaji nyara vinachunguzwa kikamilifu na kwamba wahalifu wanachukuliwa hatua,” DCI iliongeza katika taarifa Jumapili jioni.
Maelezo zaidi:
Amnesty: Maria Sarungi ametekwa nyara nchini Kenya
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International linasema kwamba mwanaharakati na mhariri wa kujitegemea kutoka Tanzania Maria Sarungi ametekwa nyara akiwa nchini Kenya.
Katika taarifa kupitia mtandao wa X, shirika hilo limesema kwamba Maria alitekwa na wanaume watatu waliokuwa na silaha na ambao walikuwa na gari nyeusi aina ya Noah.
Aidha limeongeza kuwa kisa hicho kimetokea mwendo wa saa tisa na robo mchana katika eneo la Chaka Place, mtaa wa Kilimani mjini Nairobi.
Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Irungu Houghton ameiambia BBC kuwa wako katika eneo la tukio wakijaribu kupata taarifa zaidi.
Hii si mara ya kwanza raia wa kigeni kutenkwa nchini Kenya.
Mwezi Novemba mwaka jana mwanasiasa wa upinzani wa Uganda Kizza Besigye alitekwa mjini Nairobi na watu wasiojulikana na kurejeshwa nyumbani.
Wakimbizi wannne Wa Kituruki pia walitekwa na kutimuliwa kwa lazima hadi Ankara, ambako walikabiliwa na tuhuma za kula njama dhidi ya Rais Recep Tayyip Erdogan.
Endelea kuwa nasi kwa maelezo zaidi kuhusiana na taarifa hii.
Waziri wa Kenya ashutumu serikali kwa visa vya utekaji nyara
Waziri wa huduma za umma nchini Kenya Justin Muturi ameshutumu utekaji nyara unaoendelea kushuhudiwa na kuitaka serikali kuwakamata wahusika na kuachilia vijana wanaozuiliwa kinyume cha sheria.
Akizungumza na wanahabari, Muturi amesema amechukua ‘hatua isiyo ya kawaida’, alitaja kisa cha mwanawe aliyetekwa nyara mnamo Juni 2024 ambacho kilisababibishia familia yake huzuni kubwa.
Muturi amesema kwamba licha ya kuwa Mwanasheria Mkuu wa Kenya wakati huo, juhudi zake za kumtafuta kijana wake hazikufua dafu, na hadi kufikia sasa (zaidi ya miezi sita baada ya mwanawe kuachiliwa) hawajapata majibu ya nini kilichotokea, na wala hajafikishwa kortini kushtakiwa.
“Wajibu mkuu wa serikali ni kulinda maisha ya wananchi wake na haiwezi kudai kwamba haifahamu kuhusu visa vya ukiukaji wa haki za raia wake ambazo ni kuwazuilia kinyume cha sheria na kuwanyima haki yao ya kuishi,” amesema Muturi.
Kenya imekumbwa na wimbi la watu kutoweka, huku shirika la kutetea haki za binadamu linalofadhiliwa na serikali likisema kuwa zaidi ya watu 80 wametekwa nyara katika muda wa miezi sita iliyopita.
Mnamo Januari 2, 2025, vijana watano waliotoweka kabla ya sikukuu ya Krismasi walipatikana wakiwa hai katika sehemu tofauti za Kenya.
Takriban watu 24 bado hawajulikani walipo.
Pia unaweza kusoma:
Meli ya 'kisiri' ya Urusi imekwama katika Bahari ya Baltic- Ujerumani
Mamlaka ya Ujerumani imesema meli ya mafuta iliyokwama kwenye maji ya Ujerumani ni ''inamilikiwa kisiri'' na Urusi na natumika kukwepa vikwazo.
Mamlaka ya majini ya Ujerumani (CCME) ilisema Ijumaa kuwa meli hiyo yenye bendera ya Panama, inayojulikana kama Eventin, imepoteza muelekeo, ikimaanisha kuwa boti za kuvuta zilitumwa kulinda meli hiyo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock aliilaumu Moscow, akimshutumu Rais wa Urusi Vladimir Putin kwa "kukwepa" vikwazo na kutishia usalama wa Ulaya kwa "kutumia kinyemela meli" zisizo katika hali nzuri.
Urusi, ambayo hapo awali ilikataa kujibu tuhuma kwamba inatumia meli za mataifa mengine kinyemela bado haijatoa kauli yoyote kuhusu tukio hili.
Marekani, Uingereza na Umoja wa Ulaya zimeweka vikwazo dhidi ya sekta ya mafuta ya Urusi kufuatia uvamizi wake wa Ukraine mwaka 2022.
Katika taarifa yake ya kwanza ya meli ya mafuta kukwama katika maji ya Ujerumani, CCME ilisema meli hiyo ilikuwa na urefu wa mita 274 (futi 898) na upana wa 48m (157ft) na imebeba takriban tani 99,000 za mafuta.
Takriban wakazi 35,000 Los Angeles hawana umeme
Takriban nyumba na biashara 35,000 hazina umeme katika mji wa Los Angeles, nchini Marekani kulingana na tovuti inayofuatilia kukatika kwa umeme.
Makadirio ya hivi punde kutoka Poweroutage.us yanaonyesha kuwa takriban wateja 17,500 wa kampuni inayotoa huduma ya umeme ya Southern California Edison hawana nishati.
Wateja wapatao 17,700 wa Idara ya Maji na Kawi ya Los Angeles na wateja 100 wa Pasadena hawana umeme.
Katika taarifa iliyochapishwa saa chache zilizopita, Idara ya Maji na Kawi ya LA inasema tangu moto uanze Jumanne, wahudumu wao wamerejesha huduma za umeme kwa zaidi ya wateja 350,000, huku zaidi ya wafanyakazi 100 wakielekeza juhudi zaidi katika ukarabati milingoti iliyoangushwa na upepo mkali.
Mjumbe wa Trump akutana na Netanyahu huku wanajeshi wa Israel wakiuawa Gaza
Mjumbe wa Rais mteule wa Marekani Donald Trump wa Mashariki ya Kati Steve Witkoff amekutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu siku ya Jumamosi huku kukiwa na msukumo wa kutaka kusitishwa kwa mapigano huko Gaza, ofisi ya Netanyahu ilisema.
Baada ya mkutano huo, Netanyahu alituma ujumbe wa ngazi ya juu ambao ulijumuisha mkuu wa shirika la kijasusi la Israel Mossad kwenda Qatar ili "kuendeleza" mazungumzo ya kuwarudisha mateka waliokuwa wanashikiliwa na Hamas huko Gaza, taarifa kutoka ofisi ya Netanyahu ilisema.
Mapema siku ya Jumamosi, afisa wa Israel alisema baadhi ya mafanikio yamepatikana katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Israel na kundi la Palestina la Hamas, linalopatanishwa na Misri, Qatar na Marekani, ili kufikia makubaliano huko Gaza.
Wakati huo huo, jeshi la Israel lilisema siku ya Jumamosi jioni kwamba wanajeshi wake wanne waliuawa kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, na afisa mmoja na mwanajeshi mmoja "walijeruhiwa vibaya" katika eneo hilo hilo.
Gazeti la The Times la Israel limeripoti kuwa wanajeshi sita wa Israel wamejeruhiwa, huku uchunguzi wa awali wa jeshi ukionyesha kuwa wanajeshi hao walipigwa risasi na kujeruhiwa na kilipuzi katika mji wa Beit Hanoun.
Awali, Wizara ya Afya ilisema Wapalestina 32 waliuawa na wengine 193 walijeruhiwa katika uvamizi wa Israeli siku mbili zilizopita.
Soma zaidi:
LA: Idadi ya waliofariki katika moto wa nyika yaongezeka
Idadi ya vifo kutokana na moto wa nyika huko Los Angeles imeongezeka hadi 16, mchunguzi wa matibabu wa LA amesema.
Kumi na mmoja wamefariki katika moto wa Eaton karibu na Pasadena na watano katika moto wa Palisades huku wafanyakazi wakihangaika kuzuia kuendelea kuenea kuzunguka jiji hilo.
Ndege za kumwaga maji zimekuwa zikifanya kazi usiku kucha kujaribu kudhibiti maeneo ya moto, huku upepo mkali ukirejea ambao ulisababisha uharibifu mkubwa wiki iliyopita.
Ni moto gani unaowaka sasa hivi?
Mamlaka huko Los Angeles kwa sasa wanadhibiti miako minne kuzunguka jiji hilo.
Mkubwa zaidi ni moto wa Palisades, ambao ni 11% na unawaka kwa kipande cha ekari 23,654, kulingana na Cal Fire. Moto huu unatishia eneo la watu matajiri la Brentwood na maeneo mengine mashuhuri.
Wa pili kwa ukubwa ni moto wa Eaton kaskazini mwa jiji karibu na Pasadena, unaofunika ekari 14,118 ambapo 15% umedhibitiwa.
Moto wa Kenneth umeenea ukubwa wa ekari 1,052 na 90% tayari umedhibitiwa, wakati moto wa Hurst ukienea ukubwa wa ekari 799 huku 76% ukidhibitiwa.
Soma zaidi:
Jeshi la Sudan ladai kuchukuwa mji muhimu mikononi kwa waasi
Jeshi nchini Sudan linasema kuwa limeukomboa mji muhimu mashariki mwa nchi hiyo, katika hatua ambayo inaashiria mafanikio yake makubwa katika vita vya karibu miaka miwili dhidi ya vikosi vya waasi.
Picha kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha watu wakisherehekea barabarani huku wanajeshi wakiingia katika mji wa Wad Madani.
Kiongozi wa kundi la wanamgambo la Rapid Support Forces (RSF), Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana pia kama Hemedti, alikiri tukio hilo katika ujumbe wa sauti.
Kiongozi huyo wa RSF alisema vikosi vyake vilishindwa kukabiliana na mashambulizi ya angani kupitia ndege zisizo na rubani zilizotengenezwa na Iran.
Lakini ameapa kuendelea kupigana hadi apate ushindi, hata kama itachukua zaidi ya miaka 20.
Wad Madani ni mji mkuu wa jimbo la Al Jazira, uliopo kilo mita 140km kusini mwa mji mkuu wa Sudan, Khartoum.
Wanajeshi wawili wa Korea Kaskazini wakamatwa Urusi - Ukraine
Wanajeshi wawili wa Korea Kaskazini waliojeruhiwa wamekamatwa kama wafungwa wa kivita na wanajeshi wa Ukraine katika Jimbo la Kursk nchini Urusi, Rais Volodymyr Zelensky amesema siku ya Jumamosi.
Wawili hao wanapokea "msaada muhimu wa matibabu" na wako chini ya ulinzi wa Huduma ya Usalama ya Ukraine huko Kyiv, kulingana na Zelensky.
Rais alisema "anawashukuru" wanajeshi wanaoruka kwa miamvuli wa Ukraine na wanajeshi wa Kikosi Maalum cha Operesheni kwa kuwakamata Wakorea Kaskazini.
Aliongeza kuwa "hii haikuwa kazi rahisi", akidai kwamba wanajeshi wa Urusi na Korea Kaskazini huwa wanawanyonga Wakorea Kaskazini waliojeruhiwa "ili kufuta ushahidi wowote wa kuhusika kwa Korea Kaskazini katika vita dhidi ya Ukraine".
Idara ya ujasusi ya Ukraine ilisema katika taarifa yake kwamba wafungwa hao walikamatwa tarehe 9 Januari na mara baada ya "kupewa huduma zote muhimu za matibabu kama ilivyoainishwa na Mkataba wa Geneva" walipelekwa Kyiv.
"Wanazuiliwa katika mazingira yanayofaa yenye kukidhi matakwa ya sheria za kimataifa," taarifa ya idara ya upelelezi ilisoma.
Katika taarifa iliyotumwa kwenye mtandao wa Telegram na X, Zelensky alisema wanajeshi hao "wanazungumza na wachunguzi wa Huduma ya Usalama ya Ukraine" na ameagiza Huduma hiyo kuruhusu waandishi wa habari kuwafikia.
"Ulimwengu unahitaji kujua ukweli kuhusu kile kinachoendelea," aliongeza.
Zelensky pia alichapisha picha nne pamoja na taarifa yake. Mbili zinaonyesha wanajeshi waliojeruhiwa huku moja ya picha ikionyesha kadi nyekundu ya kijeshi ya Urusi.
Mwaka jana, Rais Vladimir Putin alipoulizwa kuhusu Urusi kutumia wanajeshi wa Korea Kaskazini katika vita vyake dhidi ya Ukraine, hakukanusha. Alisema ni "uamuzi huru" wa Urusi.
Huduma ya Usalama ya Ukraine ilisema "kwa sasa inaendesha hatua muhimu za uchunguzi ili kubaini hali zote za ushiriki wa jeshi la Korea Kaskazini katika vita vya Urusi dhidi ya Ukraine".
Soma zaidi:
Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja.