Mongolia inalazimika kumkamata Putin ikiwa atazuru nchini humo - ICC
Maafisa wa Mongolia "wana wajibu" wa kumkamata Vladimir Putin ikiwa atazuru nchi hiyo wiki ijayo, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) imesema.
Safari hiyo, inayotarajiwa kufanyika Jumanne, itakuwa mara ya kwanza kwa kiongozi huyo wa Urusi kutembelea nchi wanachama wa ICC tangu mahakama hiyo iamuru akamatwe Machi 2023.
Mahakama inadai Bw Putin anahusika na uhalifu wa kivita, ikisema alishindwa kuzuia ufurushwaji kinyume cha sheria wa watoto kutoka Ukraine hadi Urusi tangu mzozo huo uanze.
Licha ya maafisa nchini Ukraine kutaka Mongolia wamkamate Bw Putin mara tu atakapowasili nchini humo, Kremlin ilisema "haina wasiwasi" kuhusu ziara hiyo.
"Tuna uhusiano mzuri na washirika wetu kutoka Mongolia," msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov aliwaambia waandishi wa habari huko Moscow. "Bila shaka, vipengele vyote vya ziara ya Rais vimetayarishwa kwa makini." Dkt Fadi el-Abdallah, msemaji wa ICC, aliambia BBC siku ya Ijumaa kwamba mahakama hiyo inategemea Nchi Wanachama wake, ikiwa ni pamoja na Mongolia, "kutekeleza maamuzi yake".
Alisema Mongolia, kama watia saini wengine wa ICC, ina "wajibu wa kushirikiana". Hii ni pamoja na kufuata vibali vya kukamatwa kama vile mahakama ilivyotoa kukamatwa kwa Bw Putin mnamo 2023.
Mahakama hiyo ilidai kuwa rais wa Urusi anahusika na uhalifu wa kivita, ikilenga kuwafukuza kinyume cha sheria watoto kutoka Ukraine hadi Urusi.
Pia imetoa kibali cha kukamatwa kwa kamishna wa haki za watoto wa Urusi, Maria Lvova-Belova, kwa uhalifu huohuo.
Ilisema uhalifu huo ulifanyika nchini Ukraine kuanzia tarehe 24 Februari 2022, wakati Urusi ilipoanzisha uvamizi wake.
Hapo awali Moscow ilikanusha madai hayo na kutaja hati hizo kuwa za "kuudhi". Dk Abdallah alisema majaji wa ICC watachunguza kesi za "kutoshirikiana" na watia saini wake na kuliarifu Bunge la Nchi Wanachama, ambalo linaweza "kuchukua hatua yoyote inayoona inafaa".
ICC haina mamlaka ya kuwakamata washukiwa, na inaweza tu kutumia mamlaka ndani ya nchi wanachama wake.