Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Waasi wa M23 wauteka mji muhimu nchini DR Congo
Vikosi vya waasi vinavyoungwa mkono na Rwanda vimeuteka mji wa Masisi ulioko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Muhtasari
- Marekani Theluji Yaanguka na kutatiza usafiri Marekani,Uingereza
- Ukraine yazindua mashambulizi mapya katika eneo la Kursk nchini Urusi
- DRC Waasi wa M23 wauteka mji muhimu nchini DR Congo
- Gaza Makumi wauawa katika Ukanda wa Gaza huku mazungumzo mapya ya kusitisha mapigano yakianza
- Kandanda Man Utd 'wana wasiwasi sana, wanaogopa sana' – Amorim
- Haiti Vikosi vya Guatemala vyawasili Haiti kupambana na magenge ya uhalifu
- Marekani Biden kutuma shehena ya silaha kwa Israel
Moja kwa moja
Martha Saranga na Munira Hussein
Theluji Yaanguka na kutatiza usafiri Marekani,Uingereza
Mamilioni ya Wamarekani wanatazamia majira ya baridi kali ambayo inaweza kusababisha kushuhudiwa kiwango kikubwa cha theluji katika kipindi cha muongo mmoja.
Baridi kali ilianza katikati mwa nchi, na itasonga mashariki katika siku chache zijazo, idara ya hali ya hewa nchini humo NWS inasema.
Hali ya hatari imetangazwa katika Majimbo ya Kentucky, Virginia, Kansas, Arkansas na Missouri.
Katikati mwa Marekani, kutakuwa na "mvurugiko mkubwa wa shughuli za kila siku" na "hali ya hatari au isiyoruhusu uendeshaji wa magari na hivyo kufungwa kwa kiasi kikubwa" hadi Jumapili, kwa mujibu wa mamlaka ya hali ya hewa NWS.
Mtangazaji wa BBC wa masuala ya hali ya hewa Elizabeth Rizzini anaonya kuhusu "hali mbaya ya kusafiri" siku nzima ya Jumapili huku theluji kubwa ikinyesha, haswa katika maeneo ya kaskazini yaliyokumbwa na dhoruba.
Jumla ya majimbo 30 yamewekwa chini ya tahadhari ya hali ya hewa huku dhoruba hiyo ikitarajiwa kusafiri kuelekea mashariki mwa nchi.
Zaidi ya safari 2,000 za ndege zimechelewa na 1,500 kughairishwa kuingia na kutoka Marekani leo, kwa mujibu wa tovuti inayofuatilia safari za anga.
Hali kama hiyo imeshuhudiwa pia nchini Uingereza ambako abiria wanakabiliwa na kuahirishwa na kucheleweshwa kwa safari baada ya viwanja vya ndege kadhaa nchini humo kulazimika kufunga njia zake za ndege huku theluji na mvua ikinyesha sehemu kadhaa za Uingereza.
Unaweza kusoma;
Ukraine yazindua mashambulizi mapya katika eneo la Kursk nchini Urusi
Ukraine imeanzisha mashambulizi mapya katika eneo la Kursk nchini Urusi, wizara ya ulinzi ya Urusi imesema.
Katika taarifa, wizara hiyo ilisema juhudi za kuangamiza makundi ya mashambulizi ya Ukraine zinaendelea. Maafisa nchini Ukraine pia wamesema operesheni inaendelea.
Ukraine ilizindua kwa mara ya kwanza uvamizi wake katika eneo la Kursk nchini Urusi mwezi Agosti mwaka jana, na kutwaa sehemu ya eneo hilo.
Katika miezi ya hivi karibuni, vikosi vya Urusi vimepata mafanikio makubwa katika eneo hilo, na kuvirudisha nyuma vikosi vya Ukraine, lakini vimeshindwa kuwaondoa kabisa.
Katika taarifa iliyotumwa kwenye mtandao wa Telegram siku ya Jumapili, wizara ya ulinzi ya Urusi ilisema: "Mnamo saa 9 asubuhi kwa saa za Moscow, katika kuzima mashambulizi ya wanajeshi wa Urusi katika mwelekeo wa Kursk, adui alianzisha mashambulizi ya kukabiliana na kikosi cha mashambulizi cha watu wawili, mizinga, gari moja la kuzuia vizuizi, na magari 12 ya kivita."
Waandishi wa mitandao kadhaa ya kijeshi wa Urusi walitoa maelezo zaidi kuhusu shambulio hilo, wakisema kuwa lilizinduliwa kutoka kambi ya vikosi vya Ukraine huko Sudzha kuelekea vijiji vya Berdin na Bolshoye Soldatskoye, kwenye njia ya kuelekea mji wa Kursk.
Mkuu wa ofisi ya rais wa Ukraine, Andriy Yermak, alisema "kulikuwa na habari njema kutoka Mkoa wa Kursk" na kwamba Urusi "inapata kile inachostahili".
Afisa wa Ukraine Andriy Kovalenko alisema katika chapisho la Telegram siku ya Jumapili: "Warusi huko Kursk wanakabiliwa na wasiwasi mkubwa kwa sababu walishambuliwa ghafla kutoka pande kadhaa."
Haijulikani ikiwa shambulio hilo ni kubwa kiasi cha kusababisha madhara yoyote katika mstari wa mbele.
Mwandishi wa Blogu ya Urusi Yury Podolyaka alisema operesheni hiyo inaweza kuwa ya upotoshaji, wakati mwingine, Alexander Kots, hakuondoa kwamba shambulio kuu linaweza kuanzishwa mahali pengine.
Vikosi vya Kyiv vinaripotiwa kukabiliwa na uhaba wa wafanyakazi na vimekuwa vikipoteza nguvu mashariki mwa Ukraine katika miezi ya hivi karibuni, huku wanajeshi wa Urusi wakisonga mbele.
Haya yanajiri wakati Jeshi la anga la Ukraine likisema Urusi ilizindua shambulio lingine la ndege isiyo na rubani dhidi ya Ukraine usiku kucha.
Unaweza kusoma;
Waasi wa M23 wauteka mji muhimu nchini DR Congo
Vikosi vya waasi vinavyoungwa mkono na Rwanda vimeuteka mji wa Masisi ulioko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kwa mujibu wa ripoti mbalimbali.
Huu ni mji wa pili kutekwa na kundi la M23 kwa siku nyingi katika jimbo la Kivu Kaskazini lenye utajiri wa madini.
Kundi hilo limechukua udhibiti wa maeneo makubwa ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo tangu 2021, na kulazimisha mamia kwa maelfu ya watu kukimbia makazi yao.
Angola imekuwa ikijaribu kupatanisha mazungumzo kati ya Rais Félix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda, Paul Kagame.
Lakini jitihda hizi ziligonga mwamba mwezi uliopita.
"Inasikitisha kwamba tunapata habari kuhusu kutekwa kwa eneo la Masisi na M23," Alexis Bahunga, mjumbe wa bunge la jimbo la Kivu Kaskazini, aliliambia shirika la habari la AFP.
Alisema hii "inaliingiza eneo hilo katika janga kubwa la kibinadamu" na kuitaka serikali kuimarisha uwezo wa jeshi katika eneo hilo.
Mkazi mmoja aliliambia shirika la habari la AFP kwamba kundi la M23 lilikuwa na mkutano wa wakaazi wa mji huo, wakisema "walikuja kuikomboa nchi".
Mamlaka ya Congo bado haijatoa kauli yoyote kuhusu kudhibitiwa kwa mji huo Masisi, ambayo ina wakazi wapatao 40,000.
Ni takriban kilomita 80 (maili 50) kaskazini mwa mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini Goma, ambao M23 waliumiliki kwa muda mfupi mwaka wa 2012.
Siku ya Ijumaa, M23 waliteka mji wa karibu wa Katale.
Mwaka jana, kulikuwa na hofu kwamba M23 wangeandamana tena hadi Goma, jiji lenye takribani watu milioni mbili.
Hata hivyo, wakati huo kulikuwa na utulivu,hadi mapema Desemba wakati mapigano yalipoanza tena. Mwezi Julai, Rwanda haikukanusha ripoti ya Umoja wa Mataifa ikisema ina takribani wanajeshi 4,000 wanaopigana pamoja na M23 nchini DR Congo.
Iliishutumu serikali ya Congo kwa kutofanya vya kutosha kukabiliana na miongo kadhaa ya migogoro mashariki mwa nchi hiyo.
Rwanda imesema hapo awali mamlaka nchini DR Congo walikuwa wanashirikiana na baadhi ya watu waliohusika na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 dhidi ya Watutsi wa kikabila na Wahutu wenye msimamo wa wastani.
Kundi la M23, lililoundwa kama chipukizi la kundi lingine la waasi, lilianza kufanya kazi mwaka 2012 ili kulinda jamii ya Kitutsi mashariki mwa DR Congo ambao kwa muda mrefu walikuwa wakilalamikia mateso na ubaguzi.
Unaweza kusoma pia;
Makumi wauawa katika Ukanda wa Gaza huku mazungumzo mapya ya kusitisha mapigano yakianza
Mashambulizi ya kijeshi ya Israel katika Ukanda wa Gaza yamesababisha vifo vya takriban watu 70 katika siku ya mwisho, matabibu wa Palestina walisema Jumamosi, wakati wapatanishi wakizindua msukumo mpya wa kusitisha mapigano ili kumaliza vita vilivyodumu kwa miezi 15.
Takriban watu 17 kati ya waliofariki waliuawa katika mashambulizi ya anga dhidi ya nyumba mbili katika Jiji la Gaza, la kwanza likiwa limeharibu nyumba ya familia ya Al-Ghoula saa za mapema, madaktari na wakaazi walisema.
"Mnamo saa 2 asubuhi tuliamshwa na sauti ya mlipuko mkubwa," alisema Ahmed Ayyan, jirani, na kuongeza kuwa watu 14 au 15 walikuwa wakiishi ndani ya nyumba hiyo.
Wengi wao ni wanawake na watoto, wote ni raia, hakuna mtu aliyerusha makombora, au kutoka kwa upinzani," Ayyan aliambia shirika la habari la Reuters.
Watu walitafuta vifusi kwa ajili ya manusura walionaswa chini ya vifusi hivyo na walisema watoto kadhaa walikuwa miongoni mwa waliouawa.
Jeshi la Israel limesema wale wote "waliolengwa katika shambulio hilo walihusika katika shughuli za kigaidi, ambazo ni pamoja na kutumia njia za misaada ya kibinadamu" na kwamba shambulio hilo lilifanyika mbali na "malori ya misaada na halikuathiri kuendelea kuingia kwa misaada ya kibinadamu."
Unaweza kusoma;
Man Utd 'wana wasiwasi sana, wanaogopa sana' – Amorim
Kocha wa Manchester United, Ruben Amorim anasema wachezaji wake "wana wasiwasi sana, wanaogopa sana" na kwamba mwenendo mbaya wa timu yake umemletea madhara.
United itawakabili vinara Liverpool siku ya Jumapili (16:30 GMT) baada ya kushindwa mara nne mfululizo katika michuano yote - ikiwa ni pamoja na tatu katika Ligi ya mabingwa.
Wameshinda mechi mbili pekee za ligi kuu tangu Amorim achukue usukani mwezi Novemba na kupata alama saba pekee.
“Unaweza kuniona usoni mwangu, unaweza kulinganisha kipindi nilipowasili na sasa,” alisema Amorim, ambaye amepoteza mechi tano kati ya nane za Ligi Kuu England.
"Bila shaka kuna shinikizo nyingi. Kwangu mimi, ni fahari na pia kupata matokeo mazuri.
"Ni vigumu zaidi wakati hatufanyi vizuri."
United ilifungwa 3-0 nyumbani na Bournemouth, 2-0 na Wolves kabla ya kulala 2-0 nyumbani dhidi ya Newcastle katika muda wa siku nane katika kipindi cha sikukuu.
Hawajapoteza mechi nne mfululizo za ligi kwa msimu mmoja tangu kati ya Desemba na Februari 1979, huku mara ya mwisho walipokea vipigo vinne mfululizo bila kufunga tena Aprili 1909.
"Wana wasiwasi, wakati mwingine wanaogopa uwanjani," Amorim alisema kuhusu wachezaji wake. "Tunapaswa kukabiliana na hilo."
Siku ya Ijumaa, kocha wa United Mreno alisema "tuna njaa ya kuongoza uwanjani" huku akimsifu beki Harry Maguire kwa kurejea kutoka katika kipindi kigumu.
"Tunahitaji viongozi wajitokeze kuwasaidia vijana wengine na mimi ndiye ninayewajibika zaidi hapa kuboresha utekelezaji," aliongeza.
"Unaweza kuona wachezaji wanafanya jitihada, wakati mwingine wana wasiwasi sana, wanaogopa sana kucheza mpira kwa sababu huu ni wakati mgumu na tutawasaidia wachezaji kuwa bora."
Unaweza kusoma;
Vikosi vya Guatemala vyawasili Haiti kupambana na magenge ya uhalifu
Kikosi cha wanajeshi 150 wa Guatemala kimewasili Haiti, kikiwa na jukumu la kusaidia kurejesha utulivu huku kukiwa na machafuko yanayotekelezwa na magenge yenye silaha.
Kundi la kwanza la wanajeshi 75 liliwasili siku ya Ijumaa na wengine 75 Jumamosi, wote wakiwa wamesajiliwa kutoka Wizara ya polisi wa kijeshi, kulingana na serikali ya Guatemala.
Hali ya hatari imekuwa ikitanda katika taifa hilo la Caribean kwa miezi kadhaa huku serikali ikipambana na magenge ya kikatili ambayo yamedhibiti sehemu kubwa ya mji mkuu wa Port-au-Prince.
Vikosi hivyo viko nchini Haiti ili kuimarisha kikosi cha usalama kinachoungwa mkono na Umoja wa Mataifa kinachoongozwa na Kenya ambacho hadi sasa kimeshindwa kuzuia ghasia.
Kenya ilituma karibu maafisa 400 wa polisi mwezi Juni na Julai mwaka jana kusaidia kupambana na magenge hayo.
Hiki kilikuwa ni awamu ya kwanza ya kikosi cha kimataifa kilichoidhinishwa na Umoja wa Mataifa ambacho kitaundwa na maafisa 2,500 kutoka nchi mbalimbali.
Idadi ndogo ya vikosi kutoka Jamaica, Belize na El Salvador pia viko Haiti kama sehemu ya mpango huo ambao mfadhili mkuu ni Marekani.
Mnamo Machi 2024, magenge yenye silaha yalivamia magereza makubwa mawili ya Haiti, na kuwaachia huru wafungwa 3,700.
Eneo la Ouest - ikiwa ni pamoja na Port-au-Prince - awali ziliwekwa chini ya hali ya hatari tarehe 3 Machi, baada ya ghasia zinazozidi kushika mji mkuu.
Unaweza kusoma;
Biden kutuma shehena ya silaha kwa Israel
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imearifu Bunge la Congress kuhusu mpango wa kuiuzia Israel silaha kwa thamani ya $8bn (£6.4bn), afisa wa Marekani ameithibitishia BBC.
Shehena ya silaha, ambayo inahitaji idhini kutoka kwa kamati za Bunge na Seneti, inajumuisha makombora na silaha nyingine.
Hatua hiyo inajiri takribani wiki mbili kabla ya Rais Joe Biden kuondoka madarakani.
Washington imekataa wito wa kusitisha msaada wa kijeshi kwa Israel kwa sababu ya idadi ya raia waliouawa wakati wa vita huko Gaza.
Mwezi Agosti, Marekani iliidhinisha uuzaji wa ndege za kivita zenye thamani ya $20bn na vifaa vingine vya kijeshi kwa Israel.
Mpango wa Shehena ya hivi karibuni ina makombora ya kutoka angani na mabomu, afisa huyo wa Marekani alisema.
Chanzo kimoja kinachofahamu mauzo hayo kiliiambia BBC siku ya Jumamosi: "Rais ameweka wazi kuwa Israel ina haki ya kutetea raia wake, kwa kuzingatia sheria za kimataifa za kibinadamu, na kuzuia uchokozi kutoka kwa Iran na washirika wake.
"Tutaendelea kuwezesha kila msaada unaohitajika kwa ulinzi wa Israel."
Biden mara nyingi ameelezea kuhusu kuiunga mkono Israel bila kutetereka.
Marekani ndiyo muuzaji mkuu zaidi wa silaha kwa Israel, baada ya kuisaidia kujenga mojawapo ya jeshi lililobobea zaidi kiteknolojia duniani.
Kwa mujibu wa Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm (SIPRI), Marekani ilichangia 69% ya silaha kuu za Israeli kati ya 2019 na 2023.
Unaweza kusoma;