Wanakijiji wa Sudan wanachimba kwa mikono ili kuwafikia wahanga wa maporomoko ya ardhi

Chanzo cha picha, Sudan Liberation Movement/Army
Wanakijiji katika eneo la mbali la jimbo la Darfur magharibi mwa Sudan wanajaribu kuwafikia waathiriwa waliozikwa na udongo kwa mikono baada ya maporomoko ya Jumapili, shirika la misaada la Save the Children linasema.
"Watu wanachimba kwa mikono kuokoa miili ya jamaa zao kwa vile hakuna zana au mashine", Francesco Lanino, naibu mkurugenzi wa shirika la mipango na uendeshaji wa Sudan alisema.
Haijulikani ni watu wangapi walikufa - takwimu kutoka kwa wizara ya afya ya kitaifa inasema kuwa ni miili miwili pekee iliyopatikana, lakini kundi lenye silaha linalosimamia eneo hilo linatoa idadi ya watu kuwa 1,000.
Shirika la Save the Children limesema takriban miili 373 imepatikana, kulingana na mkuu wa Mamlaka ya Kiraia.







